Posts filed under ‘Michezo & Burudani’

Tangulia Dube, duniani hapakukustahili!!

 Ni vigumu kuamini lakini ndivyo ilivyo, kuwa mmoja kati ya watu ambao huwa naamini ni wateule walioletwa duniani kwa ajili ya kuifanya dunia kuwa sehemu inayofaa kuishi na hata kupewa hadhi ya dunia, hatunaye tena. 

Namzungumzia msanii, mwanamapinduzi, mpinga ubaguzi na mtetezi wa haki za watu ambao daima wamekuwa wakionekana wanyonge. Namzungumzia Lucky Philip Dube, ambaye alifariki dunia Alhamisi ya Oktoba 18, mwaka huu wa 2007, baada ya kupigwa risasi, akiwa na wanae wawili ndani ya gari lake. 

Nasita kusema kuwa hili limekuwa ni pigo kubwa sana kwa wanamapinduzi, kwani naamini kuwa hili ni zaidi ya ambavyo neno pigo kubwa linaweza kumaanisha sit u kwa wapenzi wa muziki wa rege, na wafuasi wa imani za kirasta, bali kwa wale wote ambao wamekuwa wakiamini katika usawa wa mwanadamu. 

Wengi wetu tutamkumbuka kwa nyimbo zake ambazo kama ilivyo ada ya nyimbo nyingi za rege zenye kuimbwa na wafuasi wa imani za kirasta, zilikuwa ni zenye kubeba ujumbe ambao ni lazima ungeweza kumgusa mtu kwa namna moja ama nyingine. 

Nani asiyezikumbuka nyimbo zake kama Think about the children (1985), Slave (1987), Together as one (1988), Prisoner (1989), Captured Live (1990), House of exile (1991), na nyingine nyingi ambazo zilikuwa zimebeba ujumbe ambao uliweza kuwatoa machozi baadhi ya watu waliokuwa wakizikiliza kwa umakini? 

Lucky Dube, ametutoka duniani akiwa na umri mdogo tu wa miaka 43, huku albam yake ya mwisho kuitoa ikiwa ile ya Respect ambayo ilitoka mwaka jana (2006), ambayo ilikuwa albam yake ya 21 zikiwemo albam 6 alizozitoa katika lugha ya Mbaqanga, na mojaaliyoiimba katika lugha ya kiafrikana. 

Dube, kama walivyo watu wengine wengi mashuhuri duniani, alizaliwa katika mazingira magumu baada ya baba na mama yake kutengana kabla hajazaliwa. Alikulia kwa mama yake ambaye alikuwa akiishi na nyanya wa Dube, katika kitongoji cha Ermelo mashariki mwa Transvaal, eneo ambalo kama ilivyo sehemu kubwa ya Afrika Kusini, lilikuwa limetawaliwa na ubaguzi wa hali ya juu wa rangi. 

Aliwahi kufanya kazi za kutunza bustani enzi za udogo wake na katika umri huo huo wakati akiwa shuleni, yeye na marafiki zake kadhaa walijiunga na kikundi cha kwaya na kuunda bendi iliyojulikana kwa jina la Skyway band. 

Katika umri wa miaka 18, Dube alijiunga na bendi ya binamu yake iliyokuwa ikijulikana kwa jina la The love Brothers, alikokuwa akipenda kupiga muziki wa kitamaduni wa kizulu uliokuwa ukijulikana zaidi kwa jina la Mbaqanga. Katika bendi hii alikuwa akifanya kazi zaidi wakati wa likizo kwani wakati huo Dube bado alikuwa ni mwanafunzi. 

Albam zake za awali mbili alizitoa katika kipindi ambapo lugha ya kiingereza bado ilikuwa ikimpa shida kidogo na baada ya albam hizo (Lucky Dube & Super soul), Dube aliamua kwenda kujifunza zaidi lugha ya kiingereza, bila shaka baada ya kuona kuwa mafanikio yake yako katika muziki na hivyo inabidi awe msanii wa kimataifa, na hilo linamlazimu kujua lugha za kimataifa. 

Ingawa albam yake ya mwaka 1984 aliyoipa jina la Rasta never die, ilielezwa kuwa haikuwa na ubora wa kutosha katika kuirekodi, alifanikiwa kuwakamata mashabiki wa kutosha kutokana na ujumbe uliokuwa unapatikana ndani ya nyimbo zilizokuwa katika albam hiyo. 

Alifanikiwa kutwaa tuzo zaidi ya 20, ikiwa ni pamoja na ile ya World Music Awards, aliyoipaya mwaka 1996 kupitia albam yake ya Serious reggae Business, albam ambayo pia ilimfanya atajwe na watathmini wa mauzo ya muziki huo wa rege kama msanii muuzaji bora wa muziki wa rege barani Afrika. 

Wengi wetu pia tutamkumbuka Dube kama mmoja kati ya wafuasi wachache sana humu duniani wa madhehebu ya kirastafarian ambao walikuwa hawavuti sigara, hawavuti bangi na hawanywi pombe. Mbali ya muziki, Dube pia aliwahi kucheza filamu ya Getting Lucky na pia kushirikishwa na msanii wa filamu John Savage, katika filamu ya Voice in the Dark.

Aidha, Dube pia alikuwa ni mshabiki mkubwa sana wa michezo ya farasi ambapo alikuwa akimiliki shamba la wanyama na mchezo huo, katika eneo la Kwazulu Natal. Yote haya hivi sasa yamekuwa historia, Dube hatunaye tena duniani, baada ya kutwangwa risasi na watu ambao bado Polisi wa Afrika Kusini wanaelezwa kuwa wanaendelea kuwatafuta. 

Aliuawa na watu hao wanaosemekana kuwa walikuwa watatu, waliokuwa katika gari aina ya VW Polo, huku yeye mwenyewe Dube akiwa ndani ya gari lake aina ya Chrysler, akiwa na wanae wawili ambao kwa kudra za mwenyezi Mungu walisalimika katika tukio hilo. 

Kwa hali ilivyo ni kuwa tukio hili lilikuwa limepangwa na kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa sana na wahusika wa uovu wa aina hii. Na wakati watu wakisikitika kuwa dunia imempoteza mtu huyu muhimu sana, binafsi ninao ujumbe kidogo ambao ningependa umsindikize. 

Kwa watu wa mataifa bila shaka tutasema kuwa Tangulia Dube. Dunia haikuwa sehemu ya wewe kuwepo kwani dunia hii si ya waungwana.  lakini kwa wafuasi wa muziki wa rege na imani ya kirastafarian tunasema Rasta Never Die

October 22, 2007 at 10:51 am 2 comments

Tangazo…tangazo…tangazo

Asubuhi hii nimepokea ujumbe huu toka kwa babkadja sankofa. Tafadhali usome kwa makini na uufanyie kazi.

Naomba ubonyeze hapa  AU www.zafaa.com halafu bonyeza link ya NOMINATE HERE. Ukifunguka huo ukurasa naomba uende kwenye category ya BEST DOCUMENTARY FEATURE, pale kuna filamu tatu, ya kwetu (ya Watanzania) ni PLAY YOUR PART – TANZANIA. Naomba uipigie kura ili ishinde tuzo za African Academy Awards. Naomba uwaambie na watu wengine wengi, ikiwezekana weka tangazo kwenye blogu yako kama unayo. SAMBAZA HABARI HII KABLA GIZA HALIJAINGIA.

Filamu ya PLAY YOUR PART inapambana na Filamu kutoka Zambia na moja kutoka Uganda. Hadi sasa PLAY YOUR PART inaongoza kwa kura. Tafadhali ongeza idadi ya kura zile ili kilio cha wakina mama na watoto wanaopoteza
maisha kwa sababu ya afya mbaya ya uzazi kisikike zaidi. PIGA KURA kwa PLAY YOUR PART

Asante sana.

To the English Speaking Friends:

Please visit www.zafaa.com or click here and on the category “BEST DOCUMENTARY FEATURE” vote for the film “PLAY YOUR PART” from Tanzania. Your vote will add to the voice of the mothers and children who are fighting for the better maternal health.

September 30, 2007 at 10:46 am Leave a comment

Msanii wa Bongo Fleva ndani ya Blogu

Wengi wetu tulitarajia na tulijua kuwa ni suala la muda tu, tungeweza kumwona Freddy Macha mtandaoni, lakini ni nani alitarajia ujio wa Ilunga Khalifa? Eh!! Kuna watu tayari wanajiuliza naye ni nani. 

Huyu jamaa ambaye anaringia simu yake ya kamera (sijui ni nzuri kama hii yangu au vipi), kwa jina anaitwa Ilunga Khalifa. ukipenda unaweza kumuita CP au Cpwaa kama vijana wanavyopenda kumwita huko mitaani na ujio wake kwakweli umenisisimua sana. Msanii kwenye Blogu!! Inashangaza eeh!!

Sasa ngoja nikwambie kitu… Ilunga Khalifa, ni mmoja kati ya wasanii kadhaa wa huu muziki wa kizazi kipya, ambao wamefanikiwa ‘kuwashika’ vijana vilivyo kutokana na nyimbo zao zenye mistari ya aina yake.

Si mpenzi sana wa aina hii ya muziki, lakini nilishawishika kusikiliza muziki wake mmoja, baada ya kuiona blogi yake na kuambiwa kuwa ni msanii. Kwa wale vijana wanaoufuatilia sana muziki huu, naamini wanaujua wimbo wake uliowakamata vilivyo, unaokwenda kwa jina la CPwaaa. 

Wakati wasanii wetu wengi hapa nchini wakiwa wanafanya kazi zao katika hali ambayo hata sisi tumekuwa tukiilalamikia kila siku, bilashaka kutokana na elimu ndogo waliyonayo wengi wao, huenda Khalifa, akawa kawafungulia milango wenzake kwa ajili ya kuweza kuchangamana na dunia inayowazunguka. 

Sijui kama wenyewe wanaweza kunielewa kwakweli, ila naamini kwa wale wenzangu na mie ambao tumeshaogelea huku, naamini mnanielewa namaanisha nini. 

Nitazungtumza zaidi kuhusu msanii huyu pindi nikishapata wasaa nikakutana naye na kuzungumza naye mawili matatu. Kwa leo, naomba niwape mwito wa kumtembelea CP, na kisha kumpa mawili matatu katika kijiwe chake. Pia muweze kushuhudia kile anachokiona kupitia kamera yake ya kwenye simu.Bonyeza hapa kumtembelea na kumkaribisha

August 24, 2007 at 12:55 pm Leave a comment


Blog Stats

  • 35,058 hits
September 2020
M T W T F S S
 123456
78910111213
14151617181920
21222324252627
282930