Posts filed under ‘maskani’

Happy Maadili Day

siku ya maadili

Hivi ilikuwa siku ya Maadili au Madili? Anyway, si mbaya lakini, naamini mliifurahia

December 11, 2007 at 10:39 am Leave a comment

Hivi ni nini hasa kinaendelea ndani ya TAKUKURU?

Hivi ni nini hasa kinaendelea ndani ya TAKUKURU? Hili ndilo swali la kwanza kabisa nililojiuliza baada ya kusoma ujumbe huu. Lakini haijaishia hapo, nikasoma na kutumiwa tena ujumbe huu hapa. Na mambo yote haya yanakuja katika kipindi ambacho kumekuwa na kelele nyingi sana kuhusiana na TAKUKURU.

Madai,  tuhuma, minong’ono na mambo mengine kama hayo ambayo yamekuwa yakielekezwa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), ni miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakifukuta chini kwa chini na kusikika mitaani katika siku za karibuni. Bahati mbaya sana ni kuwa hakuna taarifa zozote ambazo zimekuwa zikitoka zenye kueleza hasa nini kinachoendelea.

Waswahili husema kuwa lisemwalo lipo na kama halipo laja. TAKUKURU, ikiwa moja ya Taasisi ambazo Watanzania wamekuwa wakizitolea macho wakiamini kuwa ndio mkombozi wao, haitakiwi kukaa tu kimya bila kusema lolote kuhusiana na masuala hayo yanayosemekana mitaani.

Lakini sio tu kuwa ifungue midomo na kupayuka kukanusha, hapana. Tunataka kupata maelezo ya kina, yenye kueleweka na ambayo yataandaliwa katika mazingira ya kuelewa kuwa Watanzania wamesoma na wanajua kile kinachosemwa kuwa ni uongo au laa.

Nikiwa mmoja wa Watanzania ambao tunaamini kuwa TAKUKURU ina nafasi kubwa sana katika maendeleo ya taifa hili, napenda kusema wazi kuwa TUMECHOSHWA NA HAYA MAMBO NA TUNATAKA MAELEZO YA KUTOSHA KUTOKA TAKUKURU NA SI BLAH BLAH.

December 11, 2007 at 10:13 am 1 comment

Waraka wa Butiku kwa Mkapa huu hapa

“Mali imeanza kuchukua nafasi ya uzalendo na kutumiwa na viongozi wengi wa CCM kama nyenzo ya uongozi bora wa kisasa. CCM imeanza hata kutoona haya, na viongozi wakuu, chini ya uongozi wako sasa wamenyamaza, wanaona haya kukemea uovu” – Hiyo ni sehemu ya maneno yaliyoko katika waraka wa Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, aliomuandikia mwenyekiti mstaafu wa CCM, taifa, Benjamin William Mkapa.

Inawezekana kweli kuwa mzee Butiku, akiwa kama mmoja wa viongozi wa ngazi mbalimbali za juu za kiserikali na chama enzi zake, hakufanya jambo lolote la maana kuhakikisha hali haifikii katika kiwango tunachokisoma katika waraka huu, kama alivyosema mchangiaji mmoja kule kwa kaka yangu Jeff wa harakati, lakini sidhani kama hicho kinaweza kuwa kigezo cha kukosoa haya anayosema kwasababu yana mantiki ndani yake na hali ndivyo ilivyo.

Soma waraka huo ambao wiki kadhaa zilizopita ulizua majibizano baina yake na viongozi kadhaa walioko madarakani hivi sasa. Bonyeza hapa kuusoma.

November 7, 2007 at 12:35 pm 1 comment

Hawa wamepona, wangapi wamekufa?

muhimbiliNi habari ambayo ilinisikitisha sana kama si kunistua sana kwakweli. Mgonjwa wa kichwa anapasuliwa mguuni na yule wa mguu anapasuliwa kichwani. Sijui nishangae au nijiulize au.

Ikiwa hukukutana na habari hiyo ambayo ilitoka katika gazeti la Mwananchi la siku ya Jumatatu ya Novemba 5, basi bofya hapa uisome habari hiyo kikamilifu na kisha bofya hapa kujua kilichofuatia baada ya habari ile.

Uzembe huu katika Taasisi ya mifupa ya Muhimbili, ni wa aina yake kwakweli, na kwakuwa inaelezwa kuwa yanatokea mambo haya mara kwa mara, tunajiuliza ni wangapi wamepoteza maisha kutokana na uzembe huu?

November 6, 2007 at 12:01 pm 3 comments

Mtukufu Mwalimu, wanafunzi wako wamekuwa watukutu

the late mwalimu Nyerwrw

Oktoba 14, mwaka 1999, ilikuwa siku ambayo Watanzania hawatoisahau maishani mwao. Siku hii ilikuwa siku ya majonzi pengine kuliko siku zote katika historia ya taifa hili. Ilikuwa siku ambayo tulimpoteza muasisi na baba wa taifa hili tukufu, hayati mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

 Nakumbuka wakati taarifa za msiba huo mkubwa zilitolewa na rais wa awamu ya tatu, Bw. Benjamin William Mkapa, nilikuwa maeneo ya stendi kuu ya mabasi ya Ngamiani, jijini Tanga.

Ilikuwa ni kama vile maisha yalisimama kwa muda. Ndege waliojazana katika miti iliyoko katika kituo hicho waliacha kulia, mabasi yaliacha kupiga honi na resi, kila mtu alisimama pale alipokuwa kama kagandishwa, na ninaamini hata mzunguko wa dunia ulisimama kwa muda vichwani mwa Watanzania. Hakika ulikuwa mtu wa pekee. 

Miaka nane baadae, leo hii Watanzania tungali tukibubujikwa na machozi kutokana taifa letu tukufu kuondokewa na kiongozi wake mtukufu, na kubakiwa na viongozi watukutu. Ingawa maisha yangali yakiendelea, ukweli ni kuwa haiyumkiniki mambo si shwari atika mwenendo tulio nao. 

Na hasa katika zama hizi ambapo tumekuwa tukiishi kwa mwendo, ari na kasi mpya, Tanzania inazidi kuwa kama daladala lenye kuendeshwa dereva ambaye kwake yeye mahesabu ya tajiri ndio kitu kikubwa kuliko uhai wa abiria aliowabeba. 

Maisha ya Watanzania hivi sasa yamekuwa yanaandikika zaidi kuliko kutekelezeka. Maisha ya Watanzania hivi sasa yamekuwa ni siasa. Siasa kuanzia kuzaliwa kwa mtu, kukua kwake, kula yake, uhai wake na kila kitu kuhmusu. Maisha ya Watanzania yanazidi kuwa ya maigizo, kuanzia elimu, kilimo, afya na kila kitu.

Uchumi wetu ambao hayati mwalimu Nyerere ulitueleza kuwa hautakiwi kukua katika makaratasi bali uendane na maisha halisi ya wananchi, bado haujaweza kuendana na Mtanzania wa kweli. Kwa kadiri ambavyo takwimu za kukua uchumi zimekuwa zikizidi ndivyo ambavyo maisha nayo yameendelea kuwa magumu kwa kila hali.

Kifupi uchumi wetu bado haujaweza kuwa wa kujivunia kwa wananchi wa kawaida, zaidi ya kwa wale wateule wachache sana ambao wameamua kuishi maisha ya peponi wakiwa hapa hapa duniani. Maisha ya wakulima bado ni duni, wakiendelea na kilimo kile kile cha mwaka 1961, wakati hayati mwalimu Nyerere alipofanikiwa kutupatia uhuru wetu ambao ulikuwa mikononi mwa wakoloni wa Kiingereza. Kilimo chetu bado ni kile kile cha kutoa udongo uliposimama na kuurushia nyuma. Na haionyeshi kama kuna juhudi za kukiboresha zaidi ya hapo. 

Ingawa kuna watu ambao naamini wangekuwa na uwezo wangemwomba Mungu amrejeshe Mwalimu Nyerere, duniani, binafsi siwezi kuombea hilo hata siku moja, maana akija leo hii hatutaweza kumfaidi kamwe. Atazimia na kurejea huko kwa muumba muda mfupi tu baada ya kufika na kushuhudia maovu wanayoyafanya wanae.

 Waliokuwa wakijidai kuwa wafuasi wake wazuri enzi za uhai wake. Wafuasi wake hao hivi sasa wananuka rushwa, wananuka uozo wa maovu na uonevu kwa wananchi waliowapa kura zao ili wawaongoze, wao wakazigeuza kula. Wafuasi wake hao wamegeuka kuwa mabepari wa kutupwa, wenye kutaka sifa za kijinga toka kwa wazungu waliowahi kututawala huku wakiwatesa wananchi wao. 

Chama ambacho hayati mwalimu Nyerere alikiacha kiwe mwanga na kiongozi wa kila kitu katika nchi hii, hivi sasa kimekuwa kinara wa maovu. Kimekuwa chama kinachowaongoza Watanzania kugawanyika makundi kwa makundi. Kimekuwa chama cha kuwagawa wananchi kwa dhana za ukabila na matabaka ya matajiri na masikini. 

CCM aliyotuachia mwalimu, naamini kabisa kuwa kwa sasa haipo na kama ipo basi hii ni remix ya ile CCM ya hayati. Hii ni CCM isiyojali kelele za wananchi walio wengi, wakati ile ya mwalimu ilikuwa inasikiliza hata za wachache. Hii ya sasa ni ya kuwapuuzia Watanzania na kuwaona wote ni wapumbavu na wala si wajinga. 

Kwa hakika yapo mengi, mengi mabaya sana ambayo yamejitokeza katika kipindi hiki kifupi sana. Chui waliokuwa wamevaa ngozi za kondoo wamejionyesha waziwazi. Rushwa hivi sasa watu wanakula bila soni wala aibu. Maisha yamekuwa ailimradi kunakucha na kuchwa tu. 

Kwa ujumla yapo mengi ambayo tunakabiliana nayo hivi sasa ambayo yanatufanya tukukumbuke mwalimi, na kama kuna ambalo unaweza kutusaidia, basi ni kusimama nyuma ya wale wote ambao wameonyesha nia ya wazi sasa ya kuleta mabadiliko kwa taifa letu. 

RIP mwalimu.

October 14, 2007 at 4:19 pm 1 comment

Athman Idd ‘Chuji’; Laana ya Simba au?

Kiungo wa kimataifa wa Tanzania, Athumani Idd, almaarufu kwa jina la Chuji, ambaye alizua tafrani ya aina yake mwanzoni mwa mwaka huu wa 2007, wakati wa usajili baada ya kuvigonganisha vilabu viwili vya Simba na Yanga, bado anaendelea kukumbwa na balaa linalohatarisha uhai wa kipaji chake cha uchezaji soka.

 Mchezaji huyo ambaye alichipukia katika klabu ya Polisi Dodoma, ambaye baada ya sakata lake kuamuliwa na shirikisho la soka la Tanzania (TFF), hivi sasa atalazimika kukaa nje ya uwanja kwa muda wa miezi mitatu baada ya kutaka kumshushia kipigo mwamuzi wakati klabu yake ya Yanga ilipopambana na Coastal Union ya Tanga.

 Ikumbukwe kuwa, toka mchezaji huyo atoke klabu ya Simba na kuhamia kwa watani wao Yanga, hajawahi kufanya jambo lolote la maana kwasababu kipindi hicho chote amekuwa akikumbwa na mikasa ya hapa na pale, mingine ya kujitakia na mingine yenye kuzua uyaya.

Katika moja ya mechi chache sana alizoweza kuichezea Yanga, Athuman Idd, alijikuta matatizoni baada ya kuwanyooshea kidole cha kati mashabiki waliokuwa wakimzomea katika uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.

Hiyo ilikuwa ni siku chache sana baada ya TFF, kuingilia kati na kuuvunja mkataba baina yake na Simba, na hivyo kumuidhinisha kwenda Yanga, baada ya mvutano wa muda mrefu uliomkosesha mechi nyingi kiasi cha kutemwa katika tumi ya Taifa (Taifa Stars).

Ilionekana kama vile kiungo huyo mkabaji na mwenye mapafu yenye kujitosheleza, angerejea katika timu yake kutokana na kile kilichoonekana kutulia kwake, na washabiki kudhania kuwa amekua na amejua nini maana ya kuwa mchezaji maarufu, lakini kumbe haikuwa hivyo.

Siku tatu tu baada ya taarifa za TFF kusomeka magazetini kuwa ametulia, kiungo huyo kumbe alikuwa na yake mambo, na akajikuta tena akiingia katika tuhuma za kumpiga mwamuzi na sasa atakaa tena nje ya uwanja kwa miezi mitatu.

Swali ni kuwa, hivi huyu kijana ana matatizo gani? Ni laana ya kuondoka Simba na kuhamia Yanga inayomtafuna (maana huwa wanasema vilabu hivi ukitoka kimoja kwenda kingine ndio umekwisha), au ni nini hasa kinamkumba?

October 12, 2007 at 9:41 pm 4 comments

Msaada jamani!!

Leo hii, asubuhi sana na mapema nilipoingia ofisini kwangu, jambo la kwanza kabisa kulifanya ilikuwa kusoma barua nilizotumiwa na wasgirika mbalimbali kama ilivyo kawaida yangu. Moja kati ya ujumbe ambao nilikutana nao ni huu hapa chini kumhusu binti aliyeko pichani, ambao nitauweka kama ambavyo niliukuta.

 

===

Ukimuona kwa sura, ni msichana mzuri mwenye macho ya kuvutia, lakini masikini hana raha ya maisha! Mtoto Sofia James Mwiga (17, pichani)mkazi wa Manispaa ya Tabora nchini Tanzania anaishi kwa mateso kufuatia ugonjwa wa ajabu wa kuvimba miguu hali iliyomfanya ajione mpweke machoni mwa jamii huku akishindwa kuanza shule.


Licha ya baba yake kumtafutia matibabu kwa zaidi ya miaka 10 bado hajafanikiwa kwani kila Daktari anayemfanyia uchunguzi hutoa maelezo kuwa hapa Tanzania hawezi kufanyiwa oparesheni isipo kuwa nje ya nchi ambako kuna Wataalam na vyombo vya kitabibu vya kisasa.

Kutokana na umasikini alionao baba mtu ameshindwa kumsaidia badala yake amebaki akisubiri miujiza ya mungu ishuke pengine atapata mfadhili atakaye weza kumsaidia kupata matibabu hivyo anawaomba wasamaria wema popote duniani waweze kumsaidia kuokoa maisha ya mtoto wake huyo.


Hivi sasa mtoto huyu yupo katika hospitali ya Lugalo, jijini Dar es salaam akisubiri atakayeweza kujitokeza na kumsadia kupata matibabu sahihi nje ya nchi, kwa mujibu wa mdaktari, anahitaji operation ya kuondoa nyama hizo zilizozidi.

cheki anavyoumia

Mungu kama amekupa, basi kumbuka na wenye shida. Naamini kunamtu hapo anaweza kubadili masiha ya msichana huyu kwa uwezo wake mola! namba ya simu ya baba mzazi wa msichana huyu ni +255 753 916690.

Akiwa na jamaa

Nilipomaliza kuusoma ujumbe huo niliwasiliana na mwenye namba hiyo ambaye alijitambulisha kwa jina la Francis Aloyce Mwiga, ambaye ni baba wa wa binti huyo na akanieleza kuwa tatizo hilo lilimuanza mwaka 1998, lakini halikuwa kubwa sana, hadi mwaka 2005 ndipo hali ilipofumuka ghafla na hadi kufikia hali aliyo nayo binti huyo kwa sasa.

Alinipa ruhusa ya kupandisha ujumbe huu katika blogi yangu na ruhusa kwa yeyote atakayeupata kujitahidi kwa kadiri awezavyo kusambaza kwa watu wengine ili binti huyu ambaye ni dada yetu na rasilimali muhimu kwa Taifa la Tanzania, aweze kusaidiwa.

KUTOA NI MOYO JAMANI. MWENYE NACHO HAKIKA NI VYEMA AKASAIDIA WASIO NACHO. MSAADA WENU UNAHITAJIKA KUSAIDIA MAISHA YA BINTI YETU HUYU.

August 11, 2007 at 10:52 am 2 comments

Older Posts Newer Posts


Blog Stats

  • 34,654 hits
February 2020
M T W T F S S
« Feb    
 12
3456789
10111213141516
17181920212223
242526272829