Posts filed under ‘Jamii’

Kwa haya ya Buzwagi, Tanzania tunaelekea Ukombozi wa kifikra

Yalianza kama utani na wenye nguvu zao bilashaka walidhania ulikuwa ni moto wa kifuu, lakini kumbe haikuwa hivyo. Huu wa sasa kama twaweza kuuita moto basi ni wa nyikani na ambao unawaka katika nyika yenye nyasi kavu.

Nazungumzia hili sakata la Mkataba wa Buzwagi, ambalo lilianzishwa kule mjini Dodoma, wakati wa kikao cha bajeti cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. na ambalo kwa siku za hivi karibuni limekuwa kinara wa mambo ambayo yanalitikisa Taifa la Tanzania.

Pengine si busara sana kuuzungumzia kwa kina mkataba huo kwasababu naamini wengi wetu tumeshasikiliza masimulizi ya kila aina kuuhusu na wengine tumefanikiwa kuuona kabisa na kuupitia mstari hadi mstari, kifungu hadi kifungu. Kwa wale ambao watakuwa hawajabahatika kuusoma au kusikia lolote kuuhusu wanaweza kupata fursa hiyo kwa kubonyeza hapa.

Mkataba huu ambao uliibuliwa rasmi Bungeni na Bw. Zitto Kabwe, umeibua mambo mengine mengi huku mara leo ukisikia limeibuka hili, kesho limeibuka lile na ni wazi kuwa kwa mwenendo huu yapo mengi ambayo yataibuka kutokana na Mkataba wa Buzwagi

Vuguvugu kuhusiana na Mkataba huu limekuwa likisambaa nchini kama vile moto unavyosambaa katika sehemu iliyomwagwa petroli, na bila shaka hili ndilo msingi wa makala yangu ya leo. Tunajifunza nini kutokana na sakata la Mkataba huu?

 Kwa zaidi ya miaka 40 toka Tanzania kupata uhuru wake uliokuwa mikononi mwa wakoloni wa Kiingereza, nchi hii imekuwa ikitajwa kuwa moja ya nchi zilizo masikini sana duniani. Hili limekuwa likijitokeza licha ya uongo (sababu umekuwa hauendani na taarifa za wachunguzi) ambao tumekuwa tukishurutishwa kuukubali toka kwa viongozi wetu kuwa nchi inaendelea kukua kiuchumi.

Kwa muda wote huo, wimbo wa wale tunaowapa jukumu la kututawala, umekuwa ni ule ule wa mipango mingi ya kiuchumi na hasa ile ya kuwakwamua wananchi kutoka katika lindi la umasikini inashindwa kutekelezeka kutokana na uhaba wa bajeti. Bajeti hiyo hiyo ambayo kila mwaka imekuwa ikisomwa inaambatana na vibwagizo vya kukua kwa uchumi.

Mwananchi wa kawaida kabisa nchini Tanzania, ameendelea kuwa masikini wa kutupwa kila uchao huku akiwa katika ardhi ambayo imejaaliwa madini ya kila aina. Ardhi ambayo imejaaliwa rutuba ya kila namna.

Haya yamekuwa yakiendelea kutokea wakati mwananchi huyo huyo akishuhudia jinsi ambavyo daraja baina ya yeye mwenye kukabiliana na machungu ya umasikini huo na yule ambaye amekuwa akimtetea kuwa hana njaa, likiendelea kukua kila uchao.

Ni katika mazingira haya haya ambapo mwananchi huyo huyo mwenye kuishi katika kiwango cha chini ya shilingi 100 kwa siku, amekuwa akishuhudia pia wale anaowategemea wamtetee jinsi ambavyo wanazidi kumtoa kabali za kimaisha badala ya kile alichowachagulia.

Yapo mengi sana ambayo yamekuwa yakitokea na ambayo mara jkadhaa yamekuwa yakinifanya nifikirie Busara, Uwezo na Utashi walionao hawa tunaowaita viongozi wetu. Viongozi wetu wengi wangekuwa waliosoma sana huenda ningeamini kuwa kusoma sana kuna matatizo tena makubwa sana, lakini laa, wengi wao ni wa elimu ya kawaida tu mbona.

Tunaweza kujadili mengi sana hapa, mengi yasiyo na ukomo sababu wanayotutendea ni mengi sana, lakini jambo moja tu ambalo ningependa sana walifahamu, kulijua na kuliweka akilini mwao ni kuwa kuna kitu huitwa ishara za nyakati.

jambo pekee ambalo ningependa kuwafahamisha viongozi wangu hawa ambao nawapenda sana ni kuwa haya yanayoendelea kujiri hivi sasa kuhusiana na mkataba wa Buzwagi,  hayaji kwasababu ya upumbavu wa Watanzania. Yanakuja kwasababu Watanzania tumechoshwa na hali hii.

Ikiwa hamtaweza kusoma ishara za nyakati, ikiwa hamtakuwa tayari kukiri kuwa kama ni kula mmekula na sasa mmevimbiwa matumbo, ikiwa hamtataka kuwa wakweli na kutambua kuwa Watanzania sio wapumbavu kwa kiwango mnachodhania, hakika ipo siku mtajuta na kujutia matendo yenu. Mtajutia kuziba masikio yenu.

….itaendelea…

September 25, 2007 at 6:16 pm Leave a comment

Msaada jamani!!

Leo hii, asubuhi sana na mapema nilipoingia ofisini kwangu, jambo la kwanza kabisa kulifanya ilikuwa kusoma barua nilizotumiwa na wasgirika mbalimbali kama ilivyo kawaida yangu. Moja kati ya ujumbe ambao nilikutana nao ni huu hapa chini kumhusu binti aliyeko pichani, ambao nitauweka kama ambavyo niliukuta.

 

===

Ukimuona kwa sura, ni msichana mzuri mwenye macho ya kuvutia, lakini masikini hana raha ya maisha! Mtoto Sofia James Mwiga (17, pichani)mkazi wa Manispaa ya Tabora nchini Tanzania anaishi kwa mateso kufuatia ugonjwa wa ajabu wa kuvimba miguu hali iliyomfanya ajione mpweke machoni mwa jamii huku akishindwa kuanza shule.


Licha ya baba yake kumtafutia matibabu kwa zaidi ya miaka 10 bado hajafanikiwa kwani kila Daktari anayemfanyia uchunguzi hutoa maelezo kuwa hapa Tanzania hawezi kufanyiwa oparesheni isipo kuwa nje ya nchi ambako kuna Wataalam na vyombo vya kitabibu vya kisasa.

Kutokana na umasikini alionao baba mtu ameshindwa kumsaidia badala yake amebaki akisubiri miujiza ya mungu ishuke pengine atapata mfadhili atakaye weza kumsaidia kupata matibabu hivyo anawaomba wasamaria wema popote duniani waweze kumsaidia kuokoa maisha ya mtoto wake huyo.


Hivi sasa mtoto huyu yupo katika hospitali ya Lugalo, jijini Dar es salaam akisubiri atakayeweza kujitokeza na kumsadia kupata matibabu sahihi nje ya nchi, kwa mujibu wa mdaktari, anahitaji operation ya kuondoa nyama hizo zilizozidi.

cheki anavyoumia

Mungu kama amekupa, basi kumbuka na wenye shida. Naamini kunamtu hapo anaweza kubadili masiha ya msichana huyu kwa uwezo wake mola! namba ya simu ya baba mzazi wa msichana huyu ni +255 753 916690.

Akiwa na jamaa

Nilipomaliza kuusoma ujumbe huo niliwasiliana na mwenye namba hiyo ambaye alijitambulisha kwa jina la Francis Aloyce Mwiga, ambaye ni baba wa wa binti huyo na akanieleza kuwa tatizo hilo lilimuanza mwaka 1998, lakini halikuwa kubwa sana, hadi mwaka 2005 ndipo hali ilipofumuka ghafla na hadi kufikia hali aliyo nayo binti huyo kwa sasa.

Alinipa ruhusa ya kupandisha ujumbe huu katika blogi yangu na ruhusa kwa yeyote atakayeupata kujitahidi kwa kadiri awezavyo kusambaza kwa watu wengine ili binti huyu ambaye ni dada yetu na rasilimali muhimu kwa Taifa la Tanzania, aweze kusaidiwa.

KUTOA NI MOYO JAMANI. MWENYE NACHO HAKIKA NI VYEMA AKASAIDIA WASIO NACHO. MSAADA WENU UNAHITAJIKA KUSAIDIA MAISHA YA BINTI YETU HUYU.

August 11, 2007 at 10:52 am 2 comments


Blog Stats

  • 35,058 hits
September 2020
M T W T F S S
 123456
78910111213
14151617181920
21222324252627
282930