Kuna haja ya chaguzi katika nchi za Afrika?

January 5, 2008 at 12:57 pm 1 comment

Hili ndilo swali ambalo niliulizwa na mmoja kati ya watu niliobahatika kukutana nao na kuongea mawili matatu kuhusu kinachoendelea nchini Kenya. Na hakina hata mimi najiuliza kuna haja ya kuwa na chaguzi katika nchi zetu hizi?

Hali si shwari nchini Kenya. Hali si shwari kwa jirani zetu, hali si shwari kwa ndugu zetu, hali si shwari kwa kaka na dada zetu, …..pengine hili ndilo linaloweza kutamkwa kufuatia kinachoendelea nchini Kenya.

Pengine habari kuhusu uchaguzi wa nchini Kenya, wengi tulishazisikia toka wakati wa maandalizi na hata siku ile yenyewe ya uchaguzi. Lakini sidhani kama habari hizo zina umuhimu sana masikioni mwetu kwa sasa, kuliko zilivyo habari za matukio yatokanayo na uchaguzi huo.

Ni zaidi ya wiki sasa toka yalipotangazwa matokeo ya uchaguzi ule, na katika kipindi hiki ndugu na jirani za kenya waliokuwa wamejawa na matumaini makubwa baada ya uchaguzi, ni kama wamebakia na hakuna mikononi, mioyoni na hata katika nafsi zao. Ndio, wamebakia na hakuna.

Si tu kuwa yale matumaini waliyokuwa nayo yamefutika, bali yamefutika kwa njia isiyo ya kawaida. Njia ya kutisha, kuogofya na ambayo hakuna aliyekuwa akiiota kama ingetokea katika nchi ya Kenya, baada ya jitihada kubwa sana za taifa hilo kuwa msuluhishi wa mgogoro wa Dafur.

Damu za watoto wetu wasio na hatia zimemwagiga, wengine wamebanikwa na kuteketea kwa moto kama inavyochomwa mishikaki, wengine wengi wameachwa na majeraha na vilema vya maisha. Watu wazima wameuawa, wamechomwa moto, wameumizwa vibaya na na kuachiwa machungu makubwa katika vipindi vilivyosalia vya maisha yao.

Damu ya mtu kwa ajili ya kuingia Ikulu? Kibaki na Odinga, mnahitaji damu za watu kwa ajili ya kuingia Ikulu? Hapana. Sitaki kuamini. Natamani iwe tamthilia tu, ambayo haina ukweli. Mtu aliyekuwa shujaa wa taifa katika muda wa zaidi kidogo ya miaka mitano iliyopita, hivi sasa amekuwa chanzo cha mauaji ya watu waliomuamini.

Miaka zaidi ya mitano iliyopita, alipoingia madarakani kwa kura halali – ofcourse kupitia ule ule utamaduni wa unafiki wa kisiasa uliowatawala viongozi wetu wengi wa Afrika. Kibaki alibeba dhamana kubwa sana ya kulipeleka taifa la Kenya katika nchi ya ahadi. Lakini leo hii baada ya unafiki wake kudhihirika, kwamba hakuwa amemaanisha yale aliyoahidi wakati ule, lakini akiwa bado anazitamani raha za Ikulu, ameona njia bora ya kuparejea ni kwa kusababisha vifo na umwagaji damu zisizo hatia?

Nachelea kusema kuwa kilichotokea Kenya ni wizi wa kura, kwani huo si wizi wa kura, bali ubakaji wa demokrasia na ubakaji wa maisha na haki ya msingi ya kuishi ya Wakenya.

Natamani niseme mengi sana kwakweli, lakini midhali wapo wengi ambao wanaendelea kusema kuhusu hali inavyoendelea huko, naomba nijiweke katika kundi lile la wanaokesha na kutumia muda wao mwingi kuwaombea mamilioni ya Wakenya wasio na hatia ambao wako katika hatari ya kupoteza maisha yao kutokana na tamaa za madaraka za genge la watu wachache waliowaamini na kuwaheshimu.

Jambo pekee ninaloweza kusema kwa kuhitimisha mistari yangu hii michache ni kuwaeleza ndugu, rafiki, dada, kaka, wadogo, baba, mama, babu na bibi zetu mlioko Kenya kwamba, tuko pamoja nanyi katika kipin di hiki kigumu.

Hamkutenda dhambi kubwa kwa kutumia akili zenu kufanya kile mnachoona ni bora katika nchi yenu, kiasi kwamba Mungu awaadhibu kwa njia hiyo. Naamini upande wa haki utashinda na ule wa dhuluma utaadhibiwa.

Mungu ibariki Afrika ……….Mungu ibariki Kenya
Mungu inusuru Kenya…….Mungu wanusuru wasio na hatia.

Entry filed under: maskani.

HERI YA MWAKA MPYA Una ushahidi wa yanayojiri Kenya?

1 Comment Add your own

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Trackback this post  |  Subscribe to the comments via RSS Feed


Blog Stats

  • 35,058 hits
January 2008
M T W T F S S
 123456
78910111213
14151617181920
21222324252627
28293031