Tangulia Dube, duniani hapakukustahili!!

October 22, 2007 at 10:51 am 2 comments

 Ni vigumu kuamini lakini ndivyo ilivyo, kuwa mmoja kati ya watu ambao huwa naamini ni wateule walioletwa duniani kwa ajili ya kuifanya dunia kuwa sehemu inayofaa kuishi na hata kupewa hadhi ya dunia, hatunaye tena. 

Namzungumzia msanii, mwanamapinduzi, mpinga ubaguzi na mtetezi wa haki za watu ambao daima wamekuwa wakionekana wanyonge. Namzungumzia Lucky Philip Dube, ambaye alifariki dunia Alhamisi ya Oktoba 18, mwaka huu wa 2007, baada ya kupigwa risasi, akiwa na wanae wawili ndani ya gari lake. 

Nasita kusema kuwa hili limekuwa ni pigo kubwa sana kwa wanamapinduzi, kwani naamini kuwa hili ni zaidi ya ambavyo neno pigo kubwa linaweza kumaanisha sit u kwa wapenzi wa muziki wa rege, na wafuasi wa imani za kirasta, bali kwa wale wote ambao wamekuwa wakiamini katika usawa wa mwanadamu. 

Wengi wetu tutamkumbuka kwa nyimbo zake ambazo kama ilivyo ada ya nyimbo nyingi za rege zenye kuimbwa na wafuasi wa imani za kirasta, zilikuwa ni zenye kubeba ujumbe ambao ni lazima ungeweza kumgusa mtu kwa namna moja ama nyingine. 

Nani asiyezikumbuka nyimbo zake kama Think about the children (1985), Slave (1987), Together as one (1988), Prisoner (1989), Captured Live (1990), House of exile (1991), na nyingine nyingi ambazo zilikuwa zimebeba ujumbe ambao uliweza kuwatoa machozi baadhi ya watu waliokuwa wakizikiliza kwa umakini? 

Lucky Dube, ametutoka duniani akiwa na umri mdogo tu wa miaka 43, huku albam yake ya mwisho kuitoa ikiwa ile ya Respect ambayo ilitoka mwaka jana (2006), ambayo ilikuwa albam yake ya 21 zikiwemo albam 6 alizozitoa katika lugha ya Mbaqanga, na mojaaliyoiimba katika lugha ya kiafrikana. 

Dube, kama walivyo watu wengine wengi mashuhuri duniani, alizaliwa katika mazingira magumu baada ya baba na mama yake kutengana kabla hajazaliwa. Alikulia kwa mama yake ambaye alikuwa akiishi na nyanya wa Dube, katika kitongoji cha Ermelo mashariki mwa Transvaal, eneo ambalo kama ilivyo sehemu kubwa ya Afrika Kusini, lilikuwa limetawaliwa na ubaguzi wa hali ya juu wa rangi. 

Aliwahi kufanya kazi za kutunza bustani enzi za udogo wake na katika umri huo huo wakati akiwa shuleni, yeye na marafiki zake kadhaa walijiunga na kikundi cha kwaya na kuunda bendi iliyojulikana kwa jina la Skyway band. 

Katika umri wa miaka 18, Dube alijiunga na bendi ya binamu yake iliyokuwa ikijulikana kwa jina la The love Brothers, alikokuwa akipenda kupiga muziki wa kitamaduni wa kizulu uliokuwa ukijulikana zaidi kwa jina la Mbaqanga. Katika bendi hii alikuwa akifanya kazi zaidi wakati wa likizo kwani wakati huo Dube bado alikuwa ni mwanafunzi. 

Albam zake za awali mbili alizitoa katika kipindi ambapo lugha ya kiingereza bado ilikuwa ikimpa shida kidogo na baada ya albam hizo (Lucky Dube & Super soul), Dube aliamua kwenda kujifunza zaidi lugha ya kiingereza, bila shaka baada ya kuona kuwa mafanikio yake yako katika muziki na hivyo inabidi awe msanii wa kimataifa, na hilo linamlazimu kujua lugha za kimataifa. 

Ingawa albam yake ya mwaka 1984 aliyoipa jina la Rasta never die, ilielezwa kuwa haikuwa na ubora wa kutosha katika kuirekodi, alifanikiwa kuwakamata mashabiki wa kutosha kutokana na ujumbe uliokuwa unapatikana ndani ya nyimbo zilizokuwa katika albam hiyo. 

Alifanikiwa kutwaa tuzo zaidi ya 20, ikiwa ni pamoja na ile ya World Music Awards, aliyoipaya mwaka 1996 kupitia albam yake ya Serious reggae Business, albam ambayo pia ilimfanya atajwe na watathmini wa mauzo ya muziki huo wa rege kama msanii muuzaji bora wa muziki wa rege barani Afrika. 

Wengi wetu pia tutamkumbuka Dube kama mmoja kati ya wafuasi wachache sana humu duniani wa madhehebu ya kirastafarian ambao walikuwa hawavuti sigara, hawavuti bangi na hawanywi pombe. Mbali ya muziki, Dube pia aliwahi kucheza filamu ya Getting Lucky na pia kushirikishwa na msanii wa filamu John Savage, katika filamu ya Voice in the Dark.

Aidha, Dube pia alikuwa ni mshabiki mkubwa sana wa michezo ya farasi ambapo alikuwa akimiliki shamba la wanyama na mchezo huo, katika eneo la Kwazulu Natal. Yote haya hivi sasa yamekuwa historia, Dube hatunaye tena duniani, baada ya kutwangwa risasi na watu ambao bado Polisi wa Afrika Kusini wanaelezwa kuwa wanaendelea kuwatafuta. 

Aliuawa na watu hao wanaosemekana kuwa walikuwa watatu, waliokuwa katika gari aina ya VW Polo, huku yeye mwenyewe Dube akiwa ndani ya gari lake aina ya Chrysler, akiwa na wanae wawili ambao kwa kudra za mwenyezi Mungu walisalimika katika tukio hilo. 

Kwa hali ilivyo ni kuwa tukio hili lilikuwa limepangwa na kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa sana na wahusika wa uovu wa aina hii. Na wakati watu wakisikitika kuwa dunia imempoteza mtu huyu muhimu sana, binafsi ninao ujumbe kidogo ambao ningependa umsindikize. 

Kwa watu wa mataifa bila shaka tutasema kuwa Tangulia Dube. Dunia haikuwa sehemu ya wewe kuwepo kwani dunia hii si ya waungwana.  lakini kwa wafuasi wa muziki wa rege na imani ya kirastafarian tunasema Rasta Never Die

Entry filed under: Michezo & Burudani.

Mtukufu Mwalimu, wanafunzi wako wamekuwa watukutu Hawa wamepona, wangapi wamekufa?

2 Comments Add your own

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Trackback this post  |  Subscribe to the comments via RSS Feed


Blog Stats

  • 35,058 hits
October 2007
M T W T F S S
1234567
891011121314
15161718192021
22232425262728
293031