Mtukufu Mwalimu, wanafunzi wako wamekuwa watukutu

October 14, 2007 at 4:19 pm 1 comment

the late mwalimu Nyerwrw

Oktoba 14, mwaka 1999, ilikuwa siku ambayo Watanzania hawatoisahau maishani mwao. Siku hii ilikuwa siku ya majonzi pengine kuliko siku zote katika historia ya taifa hili. Ilikuwa siku ambayo tulimpoteza muasisi na baba wa taifa hili tukufu, hayati mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

 Nakumbuka wakati taarifa za msiba huo mkubwa zilitolewa na rais wa awamu ya tatu, Bw. Benjamin William Mkapa, nilikuwa maeneo ya stendi kuu ya mabasi ya Ngamiani, jijini Tanga.

Ilikuwa ni kama vile maisha yalisimama kwa muda. Ndege waliojazana katika miti iliyoko katika kituo hicho waliacha kulia, mabasi yaliacha kupiga honi na resi, kila mtu alisimama pale alipokuwa kama kagandishwa, na ninaamini hata mzunguko wa dunia ulisimama kwa muda vichwani mwa Watanzania. Hakika ulikuwa mtu wa pekee. 

Miaka nane baadae, leo hii Watanzania tungali tukibubujikwa na machozi kutokana taifa letu tukufu kuondokewa na kiongozi wake mtukufu, na kubakiwa na viongozi watukutu. Ingawa maisha yangali yakiendelea, ukweli ni kuwa haiyumkiniki mambo si shwari atika mwenendo tulio nao. 

Na hasa katika zama hizi ambapo tumekuwa tukiishi kwa mwendo, ari na kasi mpya, Tanzania inazidi kuwa kama daladala lenye kuendeshwa dereva ambaye kwake yeye mahesabu ya tajiri ndio kitu kikubwa kuliko uhai wa abiria aliowabeba. 

Maisha ya Watanzania hivi sasa yamekuwa yanaandikika zaidi kuliko kutekelezeka. Maisha ya Watanzania hivi sasa yamekuwa ni siasa. Siasa kuanzia kuzaliwa kwa mtu, kukua kwake, kula yake, uhai wake na kila kitu kuhmusu. Maisha ya Watanzania yanazidi kuwa ya maigizo, kuanzia elimu, kilimo, afya na kila kitu.

Uchumi wetu ambao hayati mwalimu Nyerere ulitueleza kuwa hautakiwi kukua katika makaratasi bali uendane na maisha halisi ya wananchi, bado haujaweza kuendana na Mtanzania wa kweli. Kwa kadiri ambavyo takwimu za kukua uchumi zimekuwa zikizidi ndivyo ambavyo maisha nayo yameendelea kuwa magumu kwa kila hali.

Kifupi uchumi wetu bado haujaweza kuwa wa kujivunia kwa wananchi wa kawaida, zaidi ya kwa wale wateule wachache sana ambao wameamua kuishi maisha ya peponi wakiwa hapa hapa duniani. Maisha ya wakulima bado ni duni, wakiendelea na kilimo kile kile cha mwaka 1961, wakati hayati mwalimu Nyerere alipofanikiwa kutupatia uhuru wetu ambao ulikuwa mikononi mwa wakoloni wa Kiingereza. Kilimo chetu bado ni kile kile cha kutoa udongo uliposimama na kuurushia nyuma. Na haionyeshi kama kuna juhudi za kukiboresha zaidi ya hapo. 

Ingawa kuna watu ambao naamini wangekuwa na uwezo wangemwomba Mungu amrejeshe Mwalimu Nyerere, duniani, binafsi siwezi kuombea hilo hata siku moja, maana akija leo hii hatutaweza kumfaidi kamwe. Atazimia na kurejea huko kwa muumba muda mfupi tu baada ya kufika na kushuhudia maovu wanayoyafanya wanae.

 Waliokuwa wakijidai kuwa wafuasi wake wazuri enzi za uhai wake. Wafuasi wake hao hivi sasa wananuka rushwa, wananuka uozo wa maovu na uonevu kwa wananchi waliowapa kura zao ili wawaongoze, wao wakazigeuza kula. Wafuasi wake hao wamegeuka kuwa mabepari wa kutupwa, wenye kutaka sifa za kijinga toka kwa wazungu waliowahi kututawala huku wakiwatesa wananchi wao. 

Chama ambacho hayati mwalimu Nyerere alikiacha kiwe mwanga na kiongozi wa kila kitu katika nchi hii, hivi sasa kimekuwa kinara wa maovu. Kimekuwa chama kinachowaongoza Watanzania kugawanyika makundi kwa makundi. Kimekuwa chama cha kuwagawa wananchi kwa dhana za ukabila na matabaka ya matajiri na masikini. 

CCM aliyotuachia mwalimu, naamini kabisa kuwa kwa sasa haipo na kama ipo basi hii ni remix ya ile CCM ya hayati. Hii ni CCM isiyojali kelele za wananchi walio wengi, wakati ile ya mwalimu ilikuwa inasikiliza hata za wachache. Hii ya sasa ni ya kuwapuuzia Watanzania na kuwaona wote ni wapumbavu na wala si wajinga. 

Kwa hakika yapo mengi, mengi mabaya sana ambayo yamejitokeza katika kipindi hiki kifupi sana. Chui waliokuwa wamevaa ngozi za kondoo wamejionyesha waziwazi. Rushwa hivi sasa watu wanakula bila soni wala aibu. Maisha yamekuwa ailimradi kunakucha na kuchwa tu. 

Kwa ujumla yapo mengi ambayo tunakabiliana nayo hivi sasa ambayo yanatufanya tukukumbuke mwalimi, na kama kuna ambalo unaweza kutusaidia, basi ni kusimama nyuma ya wale wote ambao wameonyesha nia ya wazi sasa ya kuleta mabadiliko kwa taifa letu. 

RIP mwalimu.

Entry filed under: maskani.

Athman Idd ‘Chuji’; Laana ya Simba au? Tangulia Dube, duniani hapakukustahili!!

1 Comment Add your own

  • 1. luihamu  |  October 15, 2007 at 7:33 am

    Ndio mkuu hii safi sana.hongera.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Trackback this post  |  Subscribe to the comments via RSS Feed


Blog Stats

  • 35,058 hits
October 2007
M T W T F S S
1234567
891011121314
15161718192021
22232425262728
293031