Archive for October 12, 2007

Athman Idd ‘Chuji’; Laana ya Simba au?

Kiungo wa kimataifa wa Tanzania, Athumani Idd, almaarufu kwa jina la Chuji, ambaye alizua tafrani ya aina yake mwanzoni mwa mwaka huu wa 2007, wakati wa usajili baada ya kuvigonganisha vilabu viwili vya Simba na Yanga, bado anaendelea kukumbwa na balaa linalohatarisha uhai wa kipaji chake cha uchezaji soka.

 Mchezaji huyo ambaye alichipukia katika klabu ya Polisi Dodoma, ambaye baada ya sakata lake kuamuliwa na shirikisho la soka la Tanzania (TFF), hivi sasa atalazimika kukaa nje ya uwanja kwa muda wa miezi mitatu baada ya kutaka kumshushia kipigo mwamuzi wakati klabu yake ya Yanga ilipopambana na Coastal Union ya Tanga.

 Ikumbukwe kuwa, toka mchezaji huyo atoke klabu ya Simba na kuhamia kwa watani wao Yanga, hajawahi kufanya jambo lolote la maana kwasababu kipindi hicho chote amekuwa akikumbwa na mikasa ya hapa na pale, mingine ya kujitakia na mingine yenye kuzua uyaya.

Katika moja ya mechi chache sana alizoweza kuichezea Yanga, Athuman Idd, alijikuta matatizoni baada ya kuwanyooshea kidole cha kati mashabiki waliokuwa wakimzomea katika uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.

Hiyo ilikuwa ni siku chache sana baada ya TFF, kuingilia kati na kuuvunja mkataba baina yake na Simba, na hivyo kumuidhinisha kwenda Yanga, baada ya mvutano wa muda mrefu uliomkosesha mechi nyingi kiasi cha kutemwa katika tumi ya Taifa (Taifa Stars).

Ilionekana kama vile kiungo huyo mkabaji na mwenye mapafu yenye kujitosheleza, angerejea katika timu yake kutokana na kile kilichoonekana kutulia kwake, na washabiki kudhania kuwa amekua na amejua nini maana ya kuwa mchezaji maarufu, lakini kumbe haikuwa hivyo.

Siku tatu tu baada ya taarifa za TFF kusomeka magazetini kuwa ametulia, kiungo huyo kumbe alikuwa na yake mambo, na akajikuta tena akiingia katika tuhuma za kumpiga mwamuzi na sasa atakaa tena nje ya uwanja kwa miezi mitatu.

Swali ni kuwa, hivi huyu kijana ana matatizo gani? Ni laana ya kuondoka Simba na kuhamia Yanga inayomtafuna (maana huwa wanasema vilabu hivi ukitoka kimoja kwenda kingine ndio umekwisha), au ni nini hasa kinamkumba?

October 12, 2007 at 9:41 pm 4 comments


Blog Stats

  • 34,787 hits
October 2007
M T W T F S S
1234567
891011121314
15161718192021
22232425262728
293031