Archive for September 25, 2007

Kwa haya ya Buzwagi, Tanzania tunaelekea Ukombozi wa kifikra

Yalianza kama utani na wenye nguvu zao bilashaka walidhania ulikuwa ni moto wa kifuu, lakini kumbe haikuwa hivyo. Huu wa sasa kama twaweza kuuita moto basi ni wa nyikani na ambao unawaka katika nyika yenye nyasi kavu.

Nazungumzia hili sakata la Mkataba wa Buzwagi, ambalo lilianzishwa kule mjini Dodoma, wakati wa kikao cha bajeti cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. na ambalo kwa siku za hivi karibuni limekuwa kinara wa mambo ambayo yanalitikisa Taifa la Tanzania.

Pengine si busara sana kuuzungumzia kwa kina mkataba huo kwasababu naamini wengi wetu tumeshasikiliza masimulizi ya kila aina kuuhusu na wengine tumefanikiwa kuuona kabisa na kuupitia mstari hadi mstari, kifungu hadi kifungu. Kwa wale ambao watakuwa hawajabahatika kuusoma au kusikia lolote kuuhusu wanaweza kupata fursa hiyo kwa kubonyeza hapa.

Mkataba huu ambao uliibuliwa rasmi Bungeni na Bw. Zitto Kabwe, umeibua mambo mengine mengi huku mara leo ukisikia limeibuka hili, kesho limeibuka lile na ni wazi kuwa kwa mwenendo huu yapo mengi ambayo yataibuka kutokana na Mkataba wa Buzwagi

Vuguvugu kuhusiana na Mkataba huu limekuwa likisambaa nchini kama vile moto unavyosambaa katika sehemu iliyomwagwa petroli, na bila shaka hili ndilo msingi wa makala yangu ya leo. Tunajifunza nini kutokana na sakata la Mkataba huu?

 Kwa zaidi ya miaka 40 toka Tanzania kupata uhuru wake uliokuwa mikononi mwa wakoloni wa Kiingereza, nchi hii imekuwa ikitajwa kuwa moja ya nchi zilizo masikini sana duniani. Hili limekuwa likijitokeza licha ya uongo (sababu umekuwa hauendani na taarifa za wachunguzi) ambao tumekuwa tukishurutishwa kuukubali toka kwa viongozi wetu kuwa nchi inaendelea kukua kiuchumi.

Kwa muda wote huo, wimbo wa wale tunaowapa jukumu la kututawala, umekuwa ni ule ule wa mipango mingi ya kiuchumi na hasa ile ya kuwakwamua wananchi kutoka katika lindi la umasikini inashindwa kutekelezeka kutokana na uhaba wa bajeti. Bajeti hiyo hiyo ambayo kila mwaka imekuwa ikisomwa inaambatana na vibwagizo vya kukua kwa uchumi.

Mwananchi wa kawaida kabisa nchini Tanzania, ameendelea kuwa masikini wa kutupwa kila uchao huku akiwa katika ardhi ambayo imejaaliwa madini ya kila aina. Ardhi ambayo imejaaliwa rutuba ya kila namna.

Haya yamekuwa yakiendelea kutokea wakati mwananchi huyo huyo akishuhudia jinsi ambavyo daraja baina ya yeye mwenye kukabiliana na machungu ya umasikini huo na yule ambaye amekuwa akimtetea kuwa hana njaa, likiendelea kukua kila uchao.

Ni katika mazingira haya haya ambapo mwananchi huyo huyo mwenye kuishi katika kiwango cha chini ya shilingi 100 kwa siku, amekuwa akishuhudia pia wale anaowategemea wamtetee jinsi ambavyo wanazidi kumtoa kabali za kimaisha badala ya kile alichowachagulia.

Yapo mengi sana ambayo yamekuwa yakitokea na ambayo mara jkadhaa yamekuwa yakinifanya nifikirie Busara, Uwezo na Utashi walionao hawa tunaowaita viongozi wetu. Viongozi wetu wengi wangekuwa waliosoma sana huenda ningeamini kuwa kusoma sana kuna matatizo tena makubwa sana, lakini laa, wengi wao ni wa elimu ya kawaida tu mbona.

Tunaweza kujadili mengi sana hapa, mengi yasiyo na ukomo sababu wanayotutendea ni mengi sana, lakini jambo moja tu ambalo ningependa sana walifahamu, kulijua na kuliweka akilini mwao ni kuwa kuna kitu huitwa ishara za nyakati.

jambo pekee ambalo ningependa kuwafahamisha viongozi wangu hawa ambao nawapenda sana ni kuwa haya yanayoendelea kujiri hivi sasa kuhusiana na mkataba wa Buzwagi,  hayaji kwasababu ya upumbavu wa Watanzania. Yanakuja kwasababu Watanzania tumechoshwa na hali hii.

Ikiwa hamtaweza kusoma ishara za nyakati, ikiwa hamtakuwa tayari kukiri kuwa kama ni kula mmekula na sasa mmevimbiwa matumbo, ikiwa hamtataka kuwa wakweli na kutambua kuwa Watanzania sio wapumbavu kwa kiwango mnachodhania, hakika ipo siku mtajuta na kujutia matendo yenu. Mtajutia kuziba masikio yenu.

….itaendelea…

September 25, 2007 at 6:16 pm Leave a comment


Blog Stats

  • 35,061 hits
September 2007
M T W T F S S
 12
3456789
10111213141516
17181920212223
24252627282930