Archive for August 3, 2007

Washindwe na walegee!!

WAKATI mbio za kila mwaka za Mwenge wetu wa Uhuru zikiwa zinaendelea kuchanja mbuga katika mikoa mbalimbali, nikiwa kama mmoja wa Watanzania wanaoamini kuwa ni wazalendo wa kweli kwa taifa lao, nimekuwa mfuatiliaji mzuri wa yanayojiri katika sehemu unakopita.

Nimekuwa nikijitahidi kufuatilia masuala mbalimbali yanayojitokeza katika mbio hizo iwe kwa kupitia vyombo vya habari vinavyoripoti masuala hayo au hata kuwasiliana na marafiki zangu walioko sehemu ambako unapita na kwa ujumla mambo ambayo yamekuwa yakijitokeza ni yaleyale ambayo naamini yameshaanza kuzoeleka masikioni na hata machoni mwa Watanzania.

Mwenge huu umeendelea kuwa unalala sehemu za vijijini kwa kile kinachoelezwa kuwa ni katika kuamsha ari ya uzalendo na uwajibikaji kwa taifa lao miongoni mwa wananchi walioko “gizani” huku pia ukiwa unazindua miradi mbalimbali ya kimaendeleo katika sehemu husika na kuweka mawe ya msingi katika miradi kadha wa kadha.

Nakumbuka kupitia historia ambayo nilijifunza shule ya msingi (maana nilikuwa sijazaliwa wakati huo) kuwa wakati mwenge wa uhuru ulipokuwa unawashwa, mwaka 1961, hayati baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alisema kuwa mwenge huo uliwashwa ili uiangaze Tanzania ndani na hata nje ya mipaka yake. Uwamulikie Watanzania ndani na hata nje ya mipaka ya nchi yao na pia kuwamulika kusudi waweze kuonekana (bilashaka na kuchukuliwa hatua) wale wote ambao wenye nia mbaya na nchi yetu.

Kimantiki, ni wazi kabisa kuwa malengo, dhamira nia na madhumuni ya mwenge wetu wa uhuru, yalikuwa ya kipekee na ya muhimu sana kwa maendeleo ya nchi hii na hususan katika kuhakikisha kuwa Watanzania, kizazi hadi kizazi, wanaendelea kujirithisha Uzalendo wa dhati na wa kweli kwa nchi yao. Na ndio maana umaarufu wa mwenge ulikuwa ni wa aina yake pia.

Hata hivyo, katika siku za karibuni, umaarufu huo umekuwa ukizidi kupungua kwa kadiri ambavyo miaka inazidi kusonga mbele na bilashaka hii ikiwa ni kutokana na kuibuka kwa genge la watu ambao wamekuwa wakiutumia mwenge kwa manufaa yao binafsi na kuupaka matope.

Ukiachilia mbali masuala ya kisiasa ambayo yameingilia katika misafara ya mbio za mwenge na hivyo kusababisha malalamiko kutoka kwa watu wa kada mbalimbali na hususan wale wanaosemekana kuwa wapinzani, yapo matendo ambayo yamekuwa yakitendeka wakati wa hafla za kukaribisha mwenge katika maeneo mbalimbali ambayo binafsi yamekuwa yakinipa maswali mengi kuliko majibu.

Miongoni mwa matendo hayo ni pamoja na kushamiri vitendo vya ngono wakati wa mikesha ya mwenge unapokuwa mahala fulani. Ndio!! najua wapo ambao watang’aka katika hili lakini lipo na limekuwa likikua kwa kasi ya ajabu sana katika miaka ya hivi karibuni.

Nakumbuka mwaka 2005, kipindi hicho nikiishi mkoani Dodoma, niliwahi kuwa mmoja kati ya waandishi waliokuwa wakizunguka na mwenge katika wilaya mbalimbali za mkoa huo ambapo moja kati ya matukio yaliyonistaajabisha katika siku ya kwanza tu ya kuwa katika msafara huo lilikuwa la kukusanywa kwa ndoo kadhaa za kondomu katika uwanja ambako mwenge ulilala.

Lakini nilishangaa zaidi baada ya kufanya udadisi kwa baadhi ya watu na kuelezwa kuwa matukio kama hayo ni ya kawaida kabisa. Kwamba yamekuwa yakitendeka sehemu mbalimbali. Toka wakati huo tukio hilo lilinikaa kichwani mwangu na toka wakati huo ambao nimekuwa nikijitahidi kufuatilia kuona kama kuna mabadiliko katika hili au laa.

Cha kushangaza ni kuwa hakuna mabadiliko yoyote. Badala yake idadi kubwa (sio wote), ya watu wanaoshiriki katika sherehe hizo wamekuwa wakithamini zaidi pombe ambayo kuzidi kwake ndo chanzo cha matendo hayo machafu ya ngono hali inayonipa mashaka kuamini kuwa idadi hiyo kubwa hukumbuka kutumia kinga kama nilivyo shuhudia ndoo hiyo moja tu ya kondomu iliyokusanywa kwa wakati huo.

Kwa uelewa wangu pombe ikishafanya kazi kwenye ubongo wa mtu, sidhani kama ataweza kukumbuka kutumia kondomu. Na kwa sababu sherehe hizo hutumika sana pombe kama kiburudisho, hilo ndilo linalo niumiza kichwa katika fikra zangu kwamba huenda asilimia kubwa ya watu wanaoshiriki mbio hizo za mwenge huambukizwa ugonjwa huo hatari wa ukimwi baada ya kupata kileo hicho .

Kwa hali hiyo basi , huenda baada ya miaka mitano mbele kukawa na ongezeko kubwa la waathirika wa ugonjwa huu hatari wa ukimwi kama jamii haitachukua hatua kukabiliana na vitendo hivyo vya ngono zisizo salama vinavyo endekezwa wakati wa sherehe hizo za kuleta maendeleo ya nchi yetu.

Na si kwamba elimu na maonyo ya tahadhari dhidi ya maambukizo ya ugonjwa huo wa ukimwi haitolewi na viongozi mbalimbali katika sherehe hizo bali jamii imekuwa ikipuuza maagizo hayo yanayo tolewa kwa kufanya hivyo kwa kile ninacho dhani ni makusudi wakijua madhara yake .

Tumeshuhudia mara nyingi baadhi ya viongozi wa misafara hiyo ya mwenge na vikundi mbalimbali vya ngoma wakitoa nasaha kwa njia ya nyimbo na mashairi lengo lao ikiwa ni kuhakikisha jamii inachukua tahadhari dhidi ya maambukizi mapya ya gonjwa hili la ukimwi ili kunusuru maisha ya wachache waliokoswa na janga hili.

Wakati umefika sasa kwa jamii kuamua kuchana na tabia hiyo ambayo haina faida kwa maendeleo ya nchi kwa kufumbia macho vitendo hivyo vinashusha hadhi ya maadili ya taifa letu la Tanzania.Na kama tukiamua kwa dhati na moyo mmoja kubadilika nafikili tutaondokana na janga hili sugu la watoto yatima na kupoteza watu ambao ni nguvu kazi ya taifa.

Mbali ya hayo, umefika wakati sasa kwa kila Mtanzania, tukianza na wale walioko katika nafasi zenye ushawishi mkubwa, kuona kuwa umefikia wakati wa kurejesha hadhi ya mwenge wetu wa uhuru. Uwachome wale wanaoudhalilisha na kuwamulikia wale walioko gizani.

August 3, 2007 at 4:06 pm 1 comment


Blog Stats

  • 35,058 hits
August 2007
M T W T F S S
 12345
6789101112
13141516171819
20212223242526
2728293031