Archive for July 23, 2007

Ukaguzi wa Leseni si suluhisho, ondoeni kwanza wala rushwa

TAKRIBAN wiki tatu na zaidi kidogo, Jeshi la Polisi nchini, kupitia kitengo chake cha usalama barabarani, limekuwa likiuendesha zoezi la kukagua na kubaini leseni feki na zenye matatizo mbalimbali, ambazo baadhi ya madereva wamekuwa wakizitumia kuendeshea magari barabarani.

Tunalipongeza sana jeshi kwa hatua hii muhimu ambayo imelenga kuhakikisha kuwa tatizo la ajali za barabarani linadhibitiwa na hivyo kupunguza idadi ya mamia ya Watanzania wasio na hatia ambao wamekuwa wakipoteza maisha yao kutokana na ajali ambazo nyingi zingeweza kuzuilika.

Sifa hizo haziishii tu hapo, bali pia ni vyema zikatolewa kwa kutambua kitendo cha jeshi letu la Polisi kuonyesha dhamira ya waziwazi katika kukabiliana na kero hii ambayo imedumu kwa muda mrefu sana huku ikichukua roho za mamia ya watu ambao walikuwa nguvu kazi muhimu katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya taifa lao.

Hata hivyo, licha ya kulipongeza jeshi la Polisi kwa hatua hiyo, binafsi bado naona kuwa hatua hiyo haiwezi kuwa suluhisho au tiba ya kutosha kupunguza maumivu tuliyokwisha kuyapata Watanzania kutokana na ajali za barabarani.

Siamini kama hatua hiyo ni kidonge cha kupunguza maumivu tuliyonayo katika tatizo hilo sugu la ajali za barabarani, na imani yangu hiyo inatokana na sababu kubwa mbili, ambazo ni ile ya kimaadili ndani askari wenye kuhusika na masuala ya usalama wa barabarani na sababu ya pili ikiwa ni ya kitaalamu au kiufundi zaidi.

Wakati zoezi la ukaguzi wa leseni likiwa linaendelea (na nimesikia litakuwa la kudumu), tayari yameibuka matatizo mengi ambayo yamekuwa yakinishangaza kwa kiasi kikubwa sana. Kukamatwa kwa madereva wenye leseni feki, leseni zisizokaguliwa, kukamatwa kwa madereva wanaoendesha magari wakiwa hata hawana leseni zenyewe na mengineyo kadha wa kadha ni miongoni tu mwa yale yaliyojitokeza ambayo yameamsha upya maswali vichwani mwa Watanzania juu ya uadilifu ulioko ndani ya jeshi letu.

Katika hili mtu unajiuliza, hivi ilikuwaje mtu akaendesha basi la abiria toka sehemu moja hadi nyingine akiwa hana leseni, amefanya hivi kwa muda gani, amewahi kusababisha ajali ngapi na katika mazingira gani na alikuwa anapita barabara zipi wakati wote huo? Hizo leseni feki zilizokamatwa leo, zimetumika kwa kipindi gani hadi zinapokamatwa sasa, walizitoa wapi, kwa njia gani, kwa nani na huo ufeki wake umeanza majuzi baada ya zoezi la kuzikagua kuanza au ilikuwa toka zamani?

Nionavyo mimi, suala la uadilifu lilistahili kuwa hatua ya kwanza kabisa katika kuhakikisha kuwa ajali za barabarani zinashikiwa bango na kupunguzwa kwa kiasi kikubwa kama sio kutokomezwa kabisa. Malalamiko ya leseni feki si kilio ambacho kilihitaji wanaolia kutumia vipaza sauti ili kuweza kusikiwa sababu Watanzania wamelia kilio hiki mpaka wakatoa machozi ya damu na si kuwa wahusika hawakuyaona.

Niliwahi kunusurika ajali wakati fulani nasafiri kutoka Dar es salaam, kuelekea Dodoma na dereva wa basi tulilokuwa tunasafiria akasema (nanukuu) “Haya ndio matatizo ya leseni za mtu kupelekewa ndani ya bahasha akiambiwa tumetumwa tukuletee mzigo wako” (mwisho wa kunukuu). Alichomaanisha ni kuwa kulikuwa na tatizo la ugawaji wa leseni pasipo mtu anayepewa leseni hiyo, kujulikana walau hata kama anajua kuendesha gari yenyewe au laa, kwamba anajua sheria za barabarani au laa.

Huu ulikuwa ni udhaifu mkubwa sana wa kimaadili ambao ulikuwa umemea ndani ya Jeshi la Polisi, katika kitengo chake cha usalama wa barabarani. Na ni udhaifu huu ambao leo hii unanishawishi mimi binafsi na mamia ya Watanzania, kuamini kuwa suala la ukaguzi wa leseni unaoendelea kufanywa, haliwezi kuwa suluhisho la kutosha kuokoa roho za Watanzania wanaoteketea kutokana na ajali za barabarani.

Ikiwa waliweza kutoa leseni feki, watashindwa hivi sasa kuzifumbia macho wakimkuta nayo mtu ambaye walimpatia leseni ya namna hiyo? Ndio maana naamini kabisa kuwa hatua ya kwanza ilitakiwa kwanza kusafisha uozo wa upungufu wa kimaadili ndani ya Jeshi kwanza, kabla ya kuendelea na hatua zinazofuatia za ukaguzi wa leseni na nyinginezo nyingi.

Lakini zaidi ya hapo, naona hivi sasa umefikia wakati ambapo askari wa usalama wa barabarani wanatakiwa kuwa na taaluma ya kutosha juu ya magari. Wajue mifumo ya magari ilivyo na inavyofanya kazi pia. Wajue ubora wa magari na kila kitu kuhusiana na magari. Umefikia wakati ambapo askari wa usalama wa barabara watatakiwa kupatikana kwa sifa maalum za kitaaluma ya ufundi na sio kuteuliwa tu kwa ajili ya kuwa vibaraka wa kupokea rushwa na kulichafua jeshi zima kwa ujumla wake.

Imeshatokea mara kadhaa ambapo ajali zimetokea hatua chache sana baada ya gari husika kusimamishwa na askari wa barabarani na kuruhusiwa kuendelea na safari yake. Ziumetokea ajali za magari kukosa breki, kushindwa kupiga kona na sababu zingine za kiufundi. Je, askari wangekuwa na taaluma ya magari ajali hizi zisingeweza kuepukika?

Maaskari wa usal;ama wa barabarani hivi sasa ukiwaangalia na kuwachunguza kile wanachokifanya ni sawa na kutimiza majukumu ya uwakala wa TRA na kampuni za Bima. Maana akisimamisha gari kitu cha kwanza kuanza kukagua ni bima na kipande cha kuashiria kuwa gari hiyo imelipiwa leseni. Zaidi ya hapo watauliza dereva kwanini hajafunga mkanda, apige honi na kisha gari kuruhusiwa.

Sikatai kuwa wakiwa kama wadau muhimu wa maendeleo ya taifa hili wanatakiwa kuhakikisha mambo hayo lakini pia naamini kuwa askari hawa wanatakiwa kuwa na majukumu zaidi ya hapo. Askari wa usalama wa barabarani anatakiwa anaposimamisha gari anatakiwa kusihakiki kama tairi za gari hilo zinakidhi kiwango cha kusafirisha ama abiria au mizigo husika.

Akunje mgongo na kuona kama sehemu ya chini ya gari hilo iko salama na springi za gari hilo hazikufungwa kwa kamba wala manati, askari huyo awe na utashi wa kuingia ndani ya gari na kuuliza hata abiria kama kuna mwenye tatizo lolote lile na amsaidie, ajue kuwa gari hilo mfumo wake wa breki unafanya kazi kwa usahihi, injini iliwekwa maji na mambo mengine ya kiufundi kama hayo.

Athubutu kuulizia kadi ya matengenezo ya mwisho yaliyofanywa kwa gari hiyo na aone kama kweli halijapitiliza muda wa kutakiwa kufanyiwa matengenezo mengine yanayofuatia. Haya yote yanawezekana, na ni jukumu la askari wa usalama wa barabarani ambao wameelimishwa na kubobea katika kazi hiyo.

Yapo maboresho mengi ambayo yanatakiwa kufanywa kwa kuanzia ikiwa pia ni pamoja na kuongeza vitendea kazi na mengineyo, lakini naamini kwa kuanza na hili la maadili na taaluma ya magari, tutakuwa tumepiga hatua nyingi zaidi katika kukabiliana na ajali, kuliko hata kuishia kukagua tu leseni. Tkabiliane na tatizo hili kwa kuanza kung’oa mizizi ya tatizo lenyewe badala ya kuanza kwa kukata majani.

Alamsiki…. ni mtazamo tu

July 23, 2007 at 10:32 am 1 comment


Blog Stats

  • 35,058 hits
July 2007
M T W T F S S
 1
2345678
9101112131415
16171819202122
23242526272829
3031