Archive for June 20, 2007

akili kumkichwa 2

UMBALI wa kutoka Mbeya mjini (Jijini?), hadi Kyela ni kilomita 100 na kidogo hivi. Katika mazingira ya kawaida, unatarajia kuwa safari baina ya sehemu hizi mbili (kwa kutumia usafiri wa jumuiya/basi), ikugharimu muda wa masaa mawili kwa kiwango cha juu kabisa.

Hii inatokana na ukweli kuwa njia hiyo ambayo pia huelekea ulipo mpaka baina ya Tanzania na Malawi, imejengwa katika kiwango cha lami na ni moja ya barabara ninazozikubali kwa kiasi cha kutosha sana maana mbali ya lami na uimara wake, pia ni miongoni mwa barabara chache sana ambazo alama zake za barabarani zimeendelea kudumu kwa kipindi kirefu sana.

Mbali ya hilo, barabara hii pengine ni miongoni mwa zile ambazo zina idadi kubwa ya maaskari wa Usalama (au Uhasama?), wa Barabarani, ambapo kuna sehemu (sijui ni vituo), zaidi ya sita vyenye askari wa aina hii, wanaovaa sare zenye kumeremeta mno, na baadhi yao wakinakshia na makoti makuuuuubwa hata pale jua linapowaka.

Kuna askari katika kituo kikuu cha mabasi jijini Mbeya, wapo eneo la Meta (takriban km 1.5 toka walipo wa awali), wapo katika eneo Kadege (km 1 toka meta), wapo eneo la Soweto, wapo eneo la Nanenane, wapo eneo la Igawilo, wapo km chache kabla ya kufika Tukuyu, wapo km chache baada ya kutoka Tukuyu, wapo eneo la Kiwira, wapo…..duh, yaani kifupi ni kuwa wapo kila mahali, na kwakweli mtu unaweza kusema kuwa njia hii imebahatika, kumbe loh!!!

Licha ya mlolongo huo wa askari hao, ambao ungetarajia kuwa wawe wafuatiliaji wazuri wa ratiba za magari hayo ambayo hutoka stendi kuu kwa ratiba walizopangiwa na mamlaka husika, bado nathubutu kusema kuwa kama kuna safari ambazo huwa zinanikera sana ndani ya mkoa huu wa Mbeya, basi ni ya kwenda Kyela.

Ni safari ambayo kila mara ambapo nimekuwa nikiifanya, nimekuwa najiuliza swali moja tu; “Hawa askari wanachokifanya ni nini hasa, na huyo aliyewatuma atakuwa ametajirika kiasi gani?”

Ndio, kwasababu licha ya wingi wao wote, licha ya sare zao za kupendeza, bado ni askari hawa hawa ambao wamekuwa wanaruhusu gari kuondoka stendi kuu katika muda wake kwa mujibu wa ratiba, kisha wakaliruhusu kuweka kambi kituo cha Meta kwa zaidi ya nusu saa, Soweto kwa masaa kadhaa, Uyole kwa madakika mengine mengi tu.

Si hivyo tu, bali pia ni askari hawa hawa ambao wamekuwa wakiyaruhusu magari haya kubeba abiria na mizigo kupita uwezo wake, huku wakiyaangalia tu bila kuchukua hatua zozote pindi wanapoyasimamisha. Wanawatizama abiria waliolundikwa humo ndani pamoja na mifukoya sukari kama nyanya mbovu.

Siku moja nakumbuka nilikuwa nataka haki yangu ya kupatiwa tiketi yangu baada ya kulipa nauli, nikaambiwa gari halina kitabu kimeisha ebo!! Gari halina hata kitabu cha tiketi linaruhusiwaje kusafiri barabarani?

Kibaya zaidi ni kuwa baada ya kufika katika moja ya vituo vya hao mabwana usalama wa barabarani, na kulalamikia kuhusu kunyimwa tiketi, nilishangaa nikiambiwa eti “Tiketi kitu gani bwana?” Wewe jali kufika kwako salama achana na masuala zaidi ya hapo.

Kufika salama? katika gari ambayo ilikuwa na abiria zaidi ya 50, wakati uwezo wake wa kawaida ni wa kubeba abiria 25? Usalama katika hali kama hiyo ulikuwa wapi? na kazi ya hawa mabwana ni nini hasa? Ndio kuwaambia abiria hawana haki ya kupewa tiketi au?

Hivyo ni vijambo tu, hapo hujakutana na mkasa wa kufikishwa Tukuyu na kisha ukashushwa pale ukiambiwa na wenye gari lao eti “sisi tunaishia hapa”, licha ya kuwa gari ilianza safari ikiwa na kibao cha kuelekeza kuwa inafanya safari za kwenda Kyela. jaribu kuuliza, sanasana utaishia kuambiwa “hamna biashara” au “ruti hailipi”

Utarudishiwa nauli yako, na wala hamna atakayejali kama utapata usafiri zaidi ya hapo au laa. Hizi zipo kwa karibu kila gari, hadi lile moja wanaloliita la mkuu wa mkoa (sijui ni yupi sasa huyo mkuu mwenyewe). Yanatokea mbele ya askari hao wa usalama wa barabarani waliopo eneo la stendi ya hapo Tukuyu, lalamika halafu utashangaa kile utakachojibiwa.

Ni katika ruti hizi ambapo huwa najiuliza pia kama kazi kubwa ya askari hawa huwa ni kukagua bima za magari au laa. Maana kila kituo, swali pekee mtaloulizwa ni “Rete bima ya gari lako” na ukishaonyesha bima basi kila kitu kinakuwa kimeishia hapo hapo.

Au jamaa wanakazana kuuliza bima sababu wanajua wazi kuwa wametengeneza mazingira ya nyie kwenda kluchinjwa mbele ya safari yenu?

Lakini hizo bima nani alishawahi kulipwa kwa mujibu wa kumbukumbu mlizonazo ninyi wasomaji? Si ajali zinajiri kila uchao na wale wahanga wa ajali hizo tunao mitaani hadi leo hii hawana kitu chochote walichoambulia kutoka kwa hao wanaoitwa matajiri ambao bima zao hukaguliwa kila siku?

Imekuwa kama jambo la kawaida kabisa, kama vile ndio wajibu wao, kuwa ukaguzi wao ni kwenye bima za magari. Sijawahi kuona wala kusikia wakikagua matairi ya gari hilo yakoje, injini ya hilo gari ilitengenezwa lini na kufanyiwa ukarabati lini, bodi ya gari hiyo ilitengenezwa wapi na kwa viwango vinavyokubalika.

Sijawahi kuona mie mwenyewe au kusikia kwa mtu kuwa gari alilokuwa anaendesha au kupakia kama abiria, lilisimamishwa na kuangaliwa kama mzigo uliobebwa ndani yake ni wa kulingana na uzito ambao hilo gari linaruhusiwa kubeba au laa.

Sijui kama kuna aliyewahi kuona gari alilopanda limesimamishwa na kisha ikaangaliwa idadi ya abiria waliomo ndani yake kama wanaendana na viwango vinavyokubaliwa kwa gari hilo kubeba au laa.

Mliwahi kusikia kuwa kuna gari ambalo lilisimamishwa kukaguliwa hata mfumo wake wa breki, taa au hata kuangalia uhalali wa leseni ya dereva wake? Au sababu wengi wao wamevaa tu sare zao basi wanaonekana kuwa wako safi hadi katika leseni zao? Mbona tunao madereva kibao ambao wanaendesha magari, tunawajua lakini hamuwakamati? Au sababu hizo leseni feki nyie ndio watoaji wakuu?

Kile kinachotokea ni kuwa kila gatri linapoona linakaribia kituo cha matrafiki au askari sijui wa usalama au uhasama barabarani, dereva na konda wake wanachokifanya ni kutafuta chenji kama walikuwa hawanazo, ili kuwa na buku au buku mbili, ambazo huambatana na ile karatasi inayoonyesha muda wa wahusika hao kufanya safari yao.

Kwa mantiki hiyo, askari anapokabidhiwa karatasi ile baada ya yeye kuuliza “Wapi timetable ya gari?”, macho yake yanatangulia kwanza kusoma ile buku au buku mbili, na baada ya hapo kinachofuatia ni kuruhusiwa tu kwa gari hilo, bila kujali limewahi kabla ya muda wake, au limechelewa baada ya muda wake.

Haya yapo, hayahitaji wakurugenzi wa PCB kuanza kulimulika Jeshi la Polisi, kwakuwa ni jambo ambalo hata Jeshi lenyewe la Polisi linajua kuwa yapo, yanatendeka na yanaendelea kutendwa. Ni kwanini basi hamna anayethubutu kulichukulia hatua hili? na msituambie kuwa hamuoni. yanatendwa hadharani tena kweupeeee kabisa.

Au mnataka wananchi waanze kuonyesha kuwa wanakerwa na hali hii mjue kuwa kitachotokea ni nini? waruhusuni tu kisha matokeo yake mtayaona muda si mrefu. Dereva akijidai kuwa anajipumzisha huku wananchi wakiungua jua ndani ya gari, turuhusuni sisi tujue cha kumfanya.

Akituchelewesha mahali na kisha akataka kufidia muda huo kwa kuendesha gari kwa mwendo ajuao yeye (wenyewe wanasema kuendesha kama limeibwa), wapeni uhuru wa kumchukulia hatua.

Askari akisimamisha barabarani gari kisha akadai kadi ya gari, wamuulize kwanini hajakagua injini au mfumo mzima wa gari hilo kuona kama linafaa kuwaendeleza na safari hiyo au laa.

Yanawezekana haya, hasa katika zama hizi ambazo ni za kidemokrasia. Wapeni wananchi uhuru wa kutimiza demokrasia yao kwa matendo, sababu wameshalalamika sana na hamna linalofanyiwa kazi.

Rushwa ndani ya Jeshi la Polisi iko wazi na wala haihitaji wataalamu kutoka nje kuja kuibainisha. wala hatuhitaji wataalamu kuja toka nje kwa ajili ya kututajia majina ya watu wanaohusika na wakawajibishwa.

Na wala huu si muda wa kuzidi kupeana miaka zaidi ya kujirekebisha sababu hawa sio watu wa kujirekebisha, sanasana labda mseme kuwa mnapeana muda wa kuchuma zaidi na kuendelea kusababisha vifo vya Watanzania ambao wanawanenepesha ninyi kutokana na kodi zao.

June 20, 2007 at 12:55 pm 4 comments


Blog Stats

  • 35,058 hits
June 2007
M T W T F S S
 123
45678910
11121314151617
18192021222324
252627282930