TANZANIA nchi ya akili kumkichwa

May 21, 2007 at 11:11 am 2 comments

KATIKA muda wiote amnbao nilikuwa kimya, si kwamba nilikuwa nimejifungia mahali nikibarizi na mavitabu asubuhi hadi jioni, laa. mara moja moja nilikuwa nafanya shughuli za hapa na pale ikiwa ni pamoja na kusafiri kwa shughuli mbalimbali nyingi zikiwa za kikazi kulingana na maelekezo ya ofisi (mwajiri) yangu.

Patika moja wapo ya safari hizo, siku moja nilibahatika kufanya safari ya kwenda wilayani Kyela, na ingawa haikuwa kwa mara yangu ya kwanza kufanya safari ya namna hiyo, lakini safari hii kwakweli ilikuwa ya aina yake na ambayo matukio yake niliona kuna umuhiumu tukashirikiana kuyatafakari na kuyafanyia uchambuzi.

Pengine ni kwasababu hata siku yenyewe ilianza kwa staili ya aina yake, baada ya kushuhudia Askari mmoja wa Kikosi cha Uhasama (au usalama?), barabarani akikaribia kupewa mkong’oto na mwendesha daladala mmoja, mbele ya geti la Hospitali ya Rufaa jijini Mbeya.

Nilikuwa ndio kwanza nimetoka kwangu naelekea mzigoni wakati nilipokutana na zogo hilo, ambapo dereva huyo alikuwa kafura kwa hasira anaongea mpaka mate yanamdondoka kwa hasira (sio kama wale wanasiasa aliowasema JK lakini alipohojiwa na BBC), akimwambia huyo “njagu” kuwa amechoshwa na unyanyasaji wake na chochote kiwacho na kiwe maana yeye hana hasara yoyote ile.

Nitamnukuu dereva huyo kidogo ili tushirikiane uhondo huo:- “Hivi hamtosheki na hizo ‘buku buku’ (shilingi alfu moja ya kitanzania) tunazowapa kila mkitusimamisha huko barabarani hadi unifuate hapa nilipo? Unaona sina abiria hata mmoja hapa, unaona huyo mzee anashushwa hapo hajiwezi hata kusimama, yaani mimi kumpa msaada babu wa watu hadi hapa getini sababu anaumwa hawezi kutembea imekuwa nongwa,

“Mie nimeshakueleza kuwa mi,emsaidia huyu mgonjwa wa watu maana hawezi kutembea ndio maana nilishusha abiria wote pale kituoni nimekuja naye yeye tu na ndugu zake, kama hunielewi basi bwana, nimechoka na unavyotunyanyasa na hapa gari haiendi kituoni wala wapi, kama unataka chukua funguo hizi hapa, washa nenda nalo mwenyewe kituoni atakuja tajiri mwenye gari mtamalizana naye, mmezoea na naweza hata kukuumua kichwa hapa kisha nikalala zangu mbele na usijue pa kunipata, mtashikilia gari na atakuja mwenyewe na kesho mie naendesha jingine, ebo, binadamu gani hamna utu nyie” mwisho wa kunukuu.

Unajua chanzo cha sakata hili ni nini? Kijana huyo dereva, naambiwa alikuwa amepakia abiria mmoja mzee wa makamo ambaye alikuwa anumwa na anaelekea hospitali ya rufaa. Hali yake ilikuwa mbaya kiasi kwamba alikuwa hawezi hata kutembea mwenyewe isipokuwa kwa kushikiliwa na ndugu zake waliokuwa wameongozana naye, sasa huyo kijana kuona hivyo akaona ampe msaada wa kumfikisha walau kwenye geti la hospitali.

Hata hivyo, kwa kujua kuwa katika geti hilo hamna kituo, na kwakuwa alikuwa kabeba abiria, kijana huyo aliwasili katika kituo cha abiria cha rufaa (kiko karibu kabisa na geti la hospitali yenyewe, kwa wale wanaoulijua jiji la Mbeya, nadhani watakuwa wanaelewa), na kushusha abiria wengine wote kama sheria inavyomtaka na kisha akageuza gari hilo na kuelekea usawa wa hospitali.

Kwa bahati mbaya sana wakati anatoka kulikuwa na Askari mmoja wa Uhasama (ah, wa usalama), barabarani alikuwa karibu sana na eneo hilo, na aliposimama tu usawa wa geti la Rufaa, jamaa akawasili kwa kasi ya ajabu na kuanza maswali kama ilivyo kawaida yao. Miongoni mwa maswali ambayo kijana wa watu aliulizwa naambiwa ni pamoja na kwanini alikuwa kasimamisha gari pale, wakati hamna kituo, naye bila hiyana akaonyeshea mgonjwa aliyekuwa kambeba na kumweleza yule askari kuwa amefanya kumpa msaada.

Kusikia hivyo nasikia askari yule akamkatalia katakata, akidai kuwa wamezoea, na ndipo mabishano yakaanza huku kijana yule akijitahidi kufafanua kuwa alitoa tu msaada na hakuwa na lengo la kuweka kituo pale ndio maana hata alishusha wale abiria wengine wote na kubakia na mgonjwa na jamaa zake, lakini naambiwa askarui yule alifura na kuanza kumghasi kijana yule huku akimtisha na kumtaka kuwasha gari kisha alipeleke kituoni, ambako watajuana huko.

Kufikia hapo, kijana huyo ambaye alikuwa pia akiombewa msamaha na wale ndugu wa mgonjwa aliyekuwa kamsaidia, akaona eh!! isiwe tabu (wasambaa ikifikia hatua hiyo ndio hukwambia “Kama m’mbwai, m’mbwai, bwana), maana hakuwa na jinsi.

Si ndio hapo akampasha jamaa, akamwambia hamuogopi, gari haliendi kituoni wala wapi na halipi chochote. Kama ni kituoni alipeleke mwenyewe (na alikuwa akimpa funguo), akimwambia kuwa mwenye gari atakuja wataelewana, atamkatia kidogo kama akitaka, lakini sio yeye, maana wameshazoea kumnyanyasa licha ya kuwapa bukubuku kila ruti wanayomsimamisha barabarani.

Kabla sijaingia katika kisa cha niliyoyashuhudia baadae siku hiyo wakati naelekea Kyela, pengine ni vyema nikawapa nafasi ya kutafakari simulizi hili la ufasaha na kujiuliza maswali kadhaa wa kadhaa. Miongoni mwa maswali ambayo nimekuwa najiuliza ni kuwa hivi hizi bukubuku zinazotolewa huko barabarani ni kwamba hazionekani machoni mwa wale wanaojiita watendaji wa Taasisi (au Chama, kwa mujibu wa Makene), ya kupambana na Rushwa?

Askari wangapi wa usalama barabarani ambao wameshafikishwa mahakamani kwa kupokea rushwa za namna hiyo ambazo wala hazihitaji uwe mtaalamu kuzigundua na namna wanavyopeana? makondakta na madereva wangapi wamefikishwa mahakamani kwa makosa ya kutoa mlungula kwa njia hii huku wakiishia kuua mamia ya watu wasio na hatia kupitia ajali za barabarani?

Au mnataka kutuambia kuwa hazionekani wakati wanapeana? Alaa, naambiwa kuwa kumbe ni kwasababu hao wanaojiita wapambanaji wa rushwa hutembelea magari ambayo hayasimamishwi na madereva wao kudaiwa bukubuku kila mahali. Hawatumii daladala, hawatumii mabasi, licha ya kusikia malalamiko hayo kwa siku nyingi pia, hawataki hata kupanda vyomvo hivyo vya usafiri kwa lengo la kuchunguza.

Kuna haja ya kuiangalia upya PCB, sanjari na hiki kinachoitywa sheria ya kuipambana na rushwa. Mbona rushwa zingine ziki waziwazi jamani mnachotaka ni nini kuzifanyia kazi kama sio kututafuta ubaya lakini? Tutaendelea wiki ijayo na simulizi hii

Poleni sana mliokuwa mmenikosa kwa muda nilipokuwa natafuta funguo

Entry filed under: maskani.

Natafuta funguo Taifa Stars, uchaguzi CCM & Uchaguzi wetu.

2 Comments Add your own

  • 1. ndesanjo  |  May 29, 2007 at 6:52 am

    Kama huyu askari angekuwa amesimamisha basi hilo kwakuwa anajali sana sheria, basi tungeweza kumwelewa kwa kiasi fulani (ingawa sheria haitakiwi kutufanya tuwe kama mashine). Lakini askari huyu (kuna uwezekano mkubwa alikuwa na kitambi na kama hana basi kinakuja…buku buku hizo huleta nyama choma na bia kisha kitambi…kisha anaonekana maisha yamemwendea vizuri…nchi inaendelea kubomolewa) inaonekana kuwa ni mla rushwa asiye na ubinadamu hata kidogo.

    Umegusia suala la taasisi ya kuzuia rushwa. Taasisi hii inabidi nayo iundiwe taasisi. Waafanyaje kazi wakati ambapo wakuu wenye funguo za ajira zao ndio vinara wa rushwa? Hajatokea mtu bado ambaye anaweza kusimama mbele ya umma na kusema kuwa anapinga rushwa. Wote unaowasikia, changanya Mkapa na Kikwete, ni waongo wakubwa. Rushwa ingekuwa inapigwa vita nchi nzima tungeona na kutikisa vichwa kukubali kuwa kweli rushwa inapigwa vita. Hakuna vita vyovyote. Hadi siku ile tutakapokataa kudanganywa. Tutakapojua kuwa hakuna wa kutuzuia kurejesha nchi na utawala mikononi mwa wananchi walio wengi na sio kundi dogo la watu wanaovaa mashati ya kijani.

  • 2. ngono  |  May 29, 2007 at 3:35 pm

    Haya ni mambo makubwa , siyo mchezo…

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Trackback this post  |  Subscribe to the comments via RSS Feed


Blog Stats

  • 35,058 hits
May 2007
M T W T F S S
 123456
78910111213
14151617181920
21222324252627
28293031