Archive for May, 2007

Taifa Stars, uchaguzi CCM & Uchaguzi wetu.

Kwa kweli najivunia Utanzania wangu, najivunia kuwa Mtanzania na ni mmoja kati ya tunaoombea ifikapo Juni 02, 2007, katika uwanja wa CCM Kirumba kule Mwanza, Mungu awe upande wetu ili maajabu yatokee kwa timu yetu ya taifa (Taifa Stars A.K.A JK Boyz), iliyowahi kuitwa kichwa cha mwendawazimu, kuwachinga Simba wa Teranga (Timu ya taifa ya Senegali). Inshaalah, kama wao wameweza kwanini sisi tushindwe bwana!! Ebo, wakitushinda uwanjani basi hata kwa mdomo pia!!

Kwa wale wanaofuatilia masuala ya kisiasa humu nchini mwetu, iwe ukiwa humu humu ndani, au ukiwa uko ughaibini, naamini kuwa kwa kipindi cha wiki kadhaa sasa, wamekuwa wakikutana na habari za Vigogo mbalimbali kutoka hiki chama kilichoshikilia kila kilicho kitamu nchini Tanzania (huku pia kikijitahidi kunyakua na zile chache , kama zipo, zilizobakia kwa wengine), kuumana makoo katika kuwania ulaji zaidi kupitia chama chao hicho. Habari za fulani kaibukia mkoa fulani, huyu kachukua huku, yule naye kafufukia NEC, sijui fulani kazindukia ujumbe wa CCM nk, ndizo ambazo nimekuwa nikikutana nazo katika kipindi hiki. Ah!! bwana wee, si tunaambiwa “majina makubwa yanamaanisha habari kubwa?”

Nyie ambao vichanga vyenu vunatupiwa mochwari vikiwa bado hai, nyie mnaolalamikia kuhujumiwa matokeo ya mitihani na akina kalagabaho wengine, kwakweli mlie tu. Kwa sasa nyie kurasa zenu zimefunikwa kwa muda katika tuvyombo twetu twa habari hapa nyumbani. Anyway, hali ndivyo ilivyo mwanawane, tuendelee kukandamiza maumivu yetu ndani yetu tukisubiri habari za wakubwa kuwania ulaji mkubwa zipite kwanza.

Tuyaache hayo, eeeh ni hivi; mwanane, nimejitokeza kugombea likiti la uenyekiti katika lijuiya letu la wana blogi, nawania linafasi la uenyekiti mwanawame kwahiyo naomba wajameni mnikandamizie mikura yenu ya kutosha tu, kusudi niweze kuliongoza lijumuiya hili changa. Kimsingi hakutakuwa na masufuria ya wali, wala sitawarestisha in pisi wanyama wa watu ili niwaandalie mapilau, lakini nadhani mtanikandamizia tu bila wasiwasi.

Lakini mwanawane, ukitaka kupata mitaarifa ya kutosha kuhusu lijumuiya letu lilikotoka, malengo na lilipo kwa sasa, unaweza tu kujimuvuzisha mwenyewe kwa kulitembelea liblogi la jumuiya kwa kukong’oli hapa, kisha mwenyewe utakuwa umeingia huko mwanawani ujionee mwenyewe lijuiya linavyozidi kuserereka kwa kwenda mbele. Halkafu mwanawame, ufuatilie limuchakato la uchaguzi wa hili lichama linalotawala nchini mwetu na ule wa lijumuiya letu.

Waveja mwanawani, neksti wiki lile lihabari la akili kumkichwa litakujia sehemu ya pili yake na ya mwisho kabisa.

May 31, 2007 at 11:44 am Leave a comment

TANZANIA nchi ya akili kumkichwa

KATIKA muda wiote amnbao nilikuwa kimya, si kwamba nilikuwa nimejifungia mahali nikibarizi na mavitabu asubuhi hadi jioni, laa. mara moja moja nilikuwa nafanya shughuli za hapa na pale ikiwa ni pamoja na kusafiri kwa shughuli mbalimbali nyingi zikiwa za kikazi kulingana na maelekezo ya ofisi (mwajiri) yangu.

Patika moja wapo ya safari hizo, siku moja nilibahatika kufanya safari ya kwenda wilayani Kyela, na ingawa haikuwa kwa mara yangu ya kwanza kufanya safari ya namna hiyo, lakini safari hii kwakweli ilikuwa ya aina yake na ambayo matukio yake niliona kuna umuhiumu tukashirikiana kuyatafakari na kuyafanyia uchambuzi.

Pengine ni kwasababu hata siku yenyewe ilianza kwa staili ya aina yake, baada ya kushuhudia Askari mmoja wa Kikosi cha Uhasama (au usalama?), barabarani akikaribia kupewa mkong’oto na mwendesha daladala mmoja, mbele ya geti la Hospitali ya Rufaa jijini Mbeya.

Nilikuwa ndio kwanza nimetoka kwangu naelekea mzigoni wakati nilipokutana na zogo hilo, ambapo dereva huyo alikuwa kafura kwa hasira anaongea mpaka mate yanamdondoka kwa hasira (sio kama wale wanasiasa aliowasema JK lakini alipohojiwa na BBC), akimwambia huyo “njagu” kuwa amechoshwa na unyanyasaji wake na chochote kiwacho na kiwe maana yeye hana hasara yoyote ile.

Nitamnukuu dereva huyo kidogo ili tushirikiane uhondo huo:- “Hivi hamtosheki na hizo ‘buku buku’ (shilingi alfu moja ya kitanzania) tunazowapa kila mkitusimamisha huko barabarani hadi unifuate hapa nilipo? Unaona sina abiria hata mmoja hapa, unaona huyo mzee anashushwa hapo hajiwezi hata kusimama, yaani mimi kumpa msaada babu wa watu hadi hapa getini sababu anaumwa hawezi kutembea imekuwa nongwa,

“Mie nimeshakueleza kuwa mi,emsaidia huyu mgonjwa wa watu maana hawezi kutembea ndio maana nilishusha abiria wote pale kituoni nimekuja naye yeye tu na ndugu zake, kama hunielewi basi bwana, nimechoka na unavyotunyanyasa na hapa gari haiendi kituoni wala wapi, kama unataka chukua funguo hizi hapa, washa nenda nalo mwenyewe kituoni atakuja tajiri mwenye gari mtamalizana naye, mmezoea na naweza hata kukuumua kichwa hapa kisha nikalala zangu mbele na usijue pa kunipata, mtashikilia gari na atakuja mwenyewe na kesho mie naendesha jingine, ebo, binadamu gani hamna utu nyie” mwisho wa kunukuu.

Unajua chanzo cha sakata hili ni nini? Kijana huyo dereva, naambiwa alikuwa amepakia abiria mmoja mzee wa makamo ambaye alikuwa anumwa na anaelekea hospitali ya rufaa. Hali yake ilikuwa mbaya kiasi kwamba alikuwa hawezi hata kutembea mwenyewe isipokuwa kwa kushikiliwa na ndugu zake waliokuwa wameongozana naye, sasa huyo kijana kuona hivyo akaona ampe msaada wa kumfikisha walau kwenye geti la hospitali.

Hata hivyo, kwa kujua kuwa katika geti hilo hamna kituo, na kwakuwa alikuwa kabeba abiria, kijana huyo aliwasili katika kituo cha abiria cha rufaa (kiko karibu kabisa na geti la hospitali yenyewe, kwa wale wanaoulijua jiji la Mbeya, nadhani watakuwa wanaelewa), na kushusha abiria wengine wote kama sheria inavyomtaka na kisha akageuza gari hilo na kuelekea usawa wa hospitali.

Kwa bahati mbaya sana wakati anatoka kulikuwa na Askari mmoja wa Uhasama (ah, wa usalama), barabarani alikuwa karibu sana na eneo hilo, na aliposimama tu usawa wa geti la Rufaa, jamaa akawasili kwa kasi ya ajabu na kuanza maswali kama ilivyo kawaida yao. Miongoni mwa maswali ambayo kijana wa watu aliulizwa naambiwa ni pamoja na kwanini alikuwa kasimamisha gari pale, wakati hamna kituo, naye bila hiyana akaonyeshea mgonjwa aliyekuwa kambeba na kumweleza yule askari kuwa amefanya kumpa msaada.

Kusikia hivyo nasikia askari yule akamkatalia katakata, akidai kuwa wamezoea, na ndipo mabishano yakaanza huku kijana yule akijitahidi kufafanua kuwa alitoa tu msaada na hakuwa na lengo la kuweka kituo pale ndio maana hata alishusha wale abiria wengine wote na kubakia na mgonjwa na jamaa zake, lakini naambiwa askarui yule alifura na kuanza kumghasi kijana yule huku akimtisha na kumtaka kuwasha gari kisha alipeleke kituoni, ambako watajuana huko.

Kufikia hapo, kijana huyo ambaye alikuwa pia akiombewa msamaha na wale ndugu wa mgonjwa aliyekuwa kamsaidia, akaona eh!! isiwe tabu (wasambaa ikifikia hatua hiyo ndio hukwambia “Kama m’mbwai, m’mbwai, bwana), maana hakuwa na jinsi.

Si ndio hapo akampasha jamaa, akamwambia hamuogopi, gari haliendi kituoni wala wapi na halipi chochote. Kama ni kituoni alipeleke mwenyewe (na alikuwa akimpa funguo), akimwambia kuwa mwenye gari atakuja wataelewana, atamkatia kidogo kama akitaka, lakini sio yeye, maana wameshazoea kumnyanyasa licha ya kuwapa bukubuku kila ruti wanayomsimamisha barabarani.

Kabla sijaingia katika kisa cha niliyoyashuhudia baadae siku hiyo wakati naelekea Kyela, pengine ni vyema nikawapa nafasi ya kutafakari simulizi hili la ufasaha na kujiuliza maswali kadhaa wa kadhaa. Miongoni mwa maswali ambayo nimekuwa najiuliza ni kuwa hivi hizi bukubuku zinazotolewa huko barabarani ni kwamba hazionekani machoni mwa wale wanaojiita watendaji wa Taasisi (au Chama, kwa mujibu wa Makene), ya kupambana na Rushwa?

Askari wangapi wa usalama barabarani ambao wameshafikishwa mahakamani kwa kupokea rushwa za namna hiyo ambazo wala hazihitaji uwe mtaalamu kuzigundua na namna wanavyopeana? makondakta na madereva wangapi wamefikishwa mahakamani kwa makosa ya kutoa mlungula kwa njia hii huku wakiishia kuua mamia ya watu wasio na hatia kupitia ajali za barabarani?

Au mnataka kutuambia kuwa hazionekani wakati wanapeana? Alaa, naambiwa kuwa kumbe ni kwasababu hao wanaojiita wapambanaji wa rushwa hutembelea magari ambayo hayasimamishwi na madereva wao kudaiwa bukubuku kila mahali. Hawatumii daladala, hawatumii mabasi, licha ya kusikia malalamiko hayo kwa siku nyingi pia, hawataki hata kupanda vyomvo hivyo vya usafiri kwa lengo la kuchunguza.

Kuna haja ya kuiangalia upya PCB, sanjari na hiki kinachoitywa sheria ya kuipambana na rushwa. Mbona rushwa zingine ziki waziwazi jamani mnachotaka ni nini kuzifanyia kazi kama sio kututafuta ubaya lakini? Tutaendelea wiki ijayo na simulizi hii

Poleni sana mliokuwa mmenikosa kwa muda nilipokuwa natafuta funguo

May 21, 2007 at 11:11 am 2 comments


Blog Stats

  • 34,787 hits
May 2007
M T W T F S S
 123456
78910111213
14151617181920
21222324252627
28293031