Archive for February 16, 2007

Ni kwa maslahi ya UMMA au maslahi ya NYUMA?

SAKATA la ununuzi wa rada iliyonunuliwa na Serikali ya awamu ya tatu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika mazingira ya utatanishi mwaka 2002, lingali likichanja mbuga kama moto wa nyikani nyakati za kiangazi. Wengi wetu ambao tulikuwa hatujui kwa undani nini hasa kilikuwa ama kingali kimejificha ndani ya sakata hili, hivi sasa tunayajua, baada ya ukweli wake kuanza kuanikwa hadharani.
Teknolojia imetuwezesha kufunguliwa macho, Teknolojia imeonyesha tena umuhimu wake katika mchakato wa maendeleo, mchakato wa kuleta ukombozi, mchakato wa kupambana na ulafi wa baadhi ya viongozi wetu na uozo uliomo ndani ya baadhi ya serikali zetu, sio tu za kiafrika bali duniani kwa ujumla. Si hata serikali ya Uingereza ilichangia katika hili? unadhani sio uozo huo?
Bunge la Uingereza limejadili suala hili, na kukiri kuwa rushwa ilikuwemo katika manunuzi hayo, Rais wetu, mhe. Jakaya M. Kikwete, kaomba arejeshewe chenchi (cha juu kama wanavyosema vijana wa kizazi cha sasa), kutoka katika mabilioni yaliyokuwa yametolewa kwa ajili ya kununua rada hiyo. Ni kizungumkuti na mshike mshike kila kona kwa ujumla hivi sasa.
Si mimi au wewe msomaji wangu, ambao tuna uhakika kuwa nini kitajiri mwishoni mwa sakata hili, lakini naamini sote tuna uhakika kuwa huu ni mwanzo tu wa uvundo mkubwa, wakutisha, kuogofya na hata kukatisha tamaa, ambao umekuwa ukiwatafuna Watanzania na kuwaacha katika lindi kubwa la umasikini huku wale wanaojiita viongozi, waliochaguliwa na wananchi hao, wakiwa wanazidi kunenepeana kila uchao.

Naam! Kimsingi bado ningali niko katika mfululizo wa makala zangu kuhusiana na zile karatasi 85 zenye maandishi ya kuchefua ambayo yamepewa kichwa cha habari cha Muswada wa Uhuru wa Habari, na leo hii niko katika vipengele vile vinavyodaiwa kuwa si halali kuandikwa eti kwakuwa vinagusa maslahi ya Umma. Hivi ni umma upi unaozungumziwa hapa? Huu huu wa Watanzania watakaokuwa chini ya sheria hiyo au Umma wa wakubwa na vitegemezi vyao katika mahekalu yao?

Sehemu ya muswada huo inaainisha baadhi ya mambo ambayo eti yatakuwa ni siri ambazo hazitakiwi kuandikwa (bilashaka na kuhojiwa pia), ikiwa ni pamoja na biashara za nje, michakato ya kutunga sera, mijadala ya baraza la mawaziri na hata maamuzi yao pamoja na masuala yenye kuhusiana na Jeshi, tena hili hili linaloitwa Jeshi la Wananchi.

Hapa kidogo ndipo pananipa utata kwakweli, kwasababu kitu kinaitwa cha wananchi lakini hawatakiwi kukijadili, hawatakiwi kujua kinahitaji nini, hawatakiwi kujua kinasema nini, hawatakiwi kujua kinafikiria nini, hawatakiwi kujua kinataka kuwafanyia nini. hawatakiwi kuuliza, kuhoji utendaji wake, hawatakiwi kujulishwa kuwa kimefanyaje nk.

Hebu tutizame japo kwa juu juu tu kuhusu Jeshi. Hili ni Jeshi ambalo linaitwa la Wananchi wa Tanzania, kwa mantiki ya kuwa linawajibika kwa Watanzania, linatakiwa kuhudumiwa na Watanzania na masuala mengine ya namna hiyo. Watanzania wanatakiwa kujua uwezo wa Jeshi lao kwa mfano, ili waweze kutoa maamuzi ya kipi kifanyike kuliboresha, kuliongeza nguvu, na hata kuwaongeza marupurupyu ikiwa wanaona wazi kile wanafanya ni kikubwa kuliko kile wanachopata.

Linapokuja suala kwamfano la ununuzi wa rada nililoligusia katika aya za mwanzo wa makala yangu, hivi serikali inadhani kuwa inajua zaidi kilichobora kwa jeshi la wananchi wake kuliko wananchi wenyewe? na kama ni hivyo si kwasababu tayari mlishawaficha juu ya utendaji, matatizo na mahitaji ya jeshi lao? Watanzania kwamfano walioko maeneo ya mipakani walitakiwa kujulishwa juu ya kile kinataka kufanywa kwa ajili ya kuimarisha Jeshi lao, waseme kuwa kuna hali gani huko na kuwe na mtambo gani ambao utawasaidia hadi wao kule waliko, lakini haikuwa hivyo. sasa hili ni Jeshi la Wananchi au Jeshi la Serikali?

Watanzania wana haki na wajibu wa kujua, kufahamishwa na kujulishwa juu ya Jeshi lao ili waweze kulifikiria, walijadili na kisha watoe maamuzi kama ni kuliboresha lipewe nini na nini na kwa wakati gani, kwasababu wanajua umuhimu wa Jeshi lao na ndio walipa kodi ambao wanaweza hata kuamua kuwa waongezwe makato kwa ajili ya kuimarisha Jeshi ama laa. Kuweka sheria ya kuwazuia kupata habari kuhusu jeshi lao ni wizi wa haki yao ya kimsingi.

Muswada huu unawazuia Watanzania kujua kuwa Tanzania inapata faida kiasi gani kutokana na biashara baina yake na mataifa ya nje. Almasi zetu ambazo hivi sasa tunapunjwa mgao wetu, hatutatakiwa kujua kuwa baada ya mapitio ya mikataba hii zinaliingizia taifa kiasi gani, Tanzanite yetu hatutatakiwa kujua kuwa imeleta kiasi gani nchini, mauzo ya minofu ya samaki wanaovuliwa ziwa Victoria kule Mwanza, hatutakiwi kujua kuwa imetuingizia kiasi gani.

Mtanzania huyu huyu ambaye anaongozwa na viongozi aliowachagua yeye na wanaolipwa mishahara na marupurupu ya safari zao kutokana na kodi anayokamuliwa kila uchao, huenda kuanzia mwezi Aprili mwaka huu, asiwe tena na haki ya kufahamishwa kuwa serikali imeamua kuagiza chakula cha kiasi gani kutokana na kukabiliwa na uhaba wa chakula, hatatakiwa kujua serikali itatumia kiasi gani kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la ukame lililosababisha upungufu wa uzalishaji umeme, hatatakiwa kujua kuwa serikali inasafirisha nini na nini nje na inaingiza nini na nini.

Ndio hali ilivyo!! hakuna kuandika kuhusu masuala yanayogusa usalama wa taifa, hakuna kuandika kuhusu michakato ya uandaaji wa sera, majadiliano na maamuzi ya baraza la mawaziri, biashara za nje. Hivi haya mambo ni kwa manufaa ya nani? Usalama huu ni kwa ajili ya nani? Biashara hizi ni kwa faida ya nani? Sera hizo ni kwa ajili ya nani? Baraza hilo la Mawaziri ni kwa ajili ya nani?

Huu sio tu kuwa ni usanii unaotaka kufanywa na viongozi wetu kwa ajili ya kuwaibia wananchi waliowapa dhamana. Bali ni usaliti na wizi wa haki, wajibu na maslahi yao. Huku ni kujijengeea mazingira ya wizi huku wakijua kuwa hakuna wa kuwauliza maana siri zao si haziwezi kutoka?

Kutanunuliwa rada zingine sijui ngapi na jamaa kugawana bilioni 12 zingine kimya kimya bila sisi kujua. Kutanunuliwa Gulfstream 550, zingine na jamaa wagawane cha juu sisi hatujui, iko siku mtanunua hata silaha feki na kulikabidhi jeshi letu mtuweke hatarini sababu tu mnajua kuwa yakiibuka ya kuibuka hapa mna Gulfstream 550, zenu na mnaweza kwenda kupata hifadhi kwa mliogawana nao commision zilizotokana na manunuzi hayo.

Hapana. Hayo sio maslahi mnayodai ya Umma, bali ni maslahi mnayotaka kujiingizia nyie wenyewe kupitia milango ya Nyuma, lakini hala hala ndugu zetu. Watanzania wanaweza kuwa wajinga sana lakini sio kwa kiwango mnachodhania. isitoshe, inaweza kuwa kweli wamekuwa wajinga kwa muda mrefu sana, lakini hawako tayari kufanywa wapumbavu, jambo ambalo ndio mnataka kulifanya kupitia muswada huo.

Nazungumza tena na tena nikiwa katika nafasi ya mwananchi wa kawaida na pia kama mwana habari katika nafsi ya pili nikisema kuwa, MUSWADA WENU HUO SIO TU KUWA HAUFAI BALI PIA HATUUTAKI KAMA HAMTAUFANYIA MAREKEBISHO TUNAYOTAKA MYAFANYE.

February 16, 2007 at 10:34 am 1 comment


Blog Stats

  • 35,061 hits
February 2007
M T W T F S S
 1234
567891011
12131415161718
19202122232425
262728