msimu wa mapenzi au wazinifu?

February 13, 2007 at 9:25 am 3 comments

Kapteni Gadner G. Habash, yule nahodha wa Jahazi la Clouds FM analijua hili fika kuwa, Vijana wa kisasa miili yao si ya kawaida, ikitokea ukawachana kwa kisu au kiwembe sehemu yoyote ile ya miili yao, utashangaa kuona hawatoki damu, bali kopa (alama inayotumiwa kuashiria mapenzi). Ndio, “Vijana wa kisasa wamejaa mapenzi” pengine iwekwe hivyo kwa ufupi.
Naam, ni msimu wa mapenzi, msimu wa wazinifu, msimu wa wazinzi, msimu wa kudanganyana, msimu wa maambukizi mapya ya virusi vinavyosababisha upungufu wa kinga mwilini. Oh yes… Ni msimu wa Shetani kujiongezea wafuasi mamilioni kadhaa hivi. Unashangaa!!

February 14, ya kila mwaka, mamilioni ya watu Duniani huadhimisha Siku ya Wapendanao, a.k.a Valentine Day kama wanavyoiita wenye lugha yao. Kwa wengine, siku hii pia hujulikana kama Siku ya Mtakatifu Valentine, jamaa ambaye wamethubutu pia kumpachika cheo cha Patron Mtakatifu wa Wapendanao

Siku hii ambayo katika Bara la Afrika imekuwa ikizidi kuongezeka umaarufu wake kila kukicha, sio tu kuwa ina historia ndefu na pana kupita maelezo, bali pia imejaa historia zenye kupishana kutoka kwa mtu mmoja anayeisimulia hadi mwingine. lakini yote kwa yote, historia hizo haziibadili siku hii au maana yake. SIKU YA WAPENDANAO sio ya WANAOPENDANA?
Licha ya tofauti zinazojitokeza kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine, wote wanaosimulia kuhusu siku hii wanakubaliana kuwa ni siku ambayo ilitengwa mahususi kwa Wapendanao, yaani Likizo ya Wapenzi na Mapenzi, kwa maana ya kuthamini uwepo wa masuala hayo mawili. Ni siku ambayo watu walitarajiwa kuwa wanapeana (au kubadilishana vile?), zawadi mbalimbali, kuwa karibu sana na wapenzi wao (maana siku zingine hawako nao sio?), na mambo mengine ya namna hiyo.
Hata hivyo sijui ni kutokana na mabadiliko tunayoyaita ya lazima yanayojiri duniani au kutokana na kuwa BUSY, wataalamu wanakiri wazi kuwa siku hii imepoteza mvuto wake katika siku za hivi karibuni. Naamini kabisa kuwa kama ingewezekana huyo Patron Mtakatifu wa Wapendanao (st Valentine), akarejea Duniani na kuona siku ya kumkumbuka inavyosherehekewa, angeweza kuzimia kwa mshtuko.
Katika kipindi changu choooote cha kuijua siku hii, sikuwahi kumsikia mtu akimtumia mama yake, dadake, babake, shangaziye, nyanya yake, mdogo wake au mkubwa wake zawadi iwe ya maua, kadi au hata ujumbe mfupi kwa ajili ya kuwatakia kila lakheri katika siku hii, huo ndio upande mmoja wa shilingi ninayoijua mimi ya Siku ya Valentine. Upande ambao wengi wetu hatutaki kuuangalia maana tunahisi haukustahili kuwepo katika ‘sarafu’ ya Valentine Day.
Na kwa upande wa pili wa shilingi hii, upande ambao wengi wetu ndio tunapenda kuuangalia, tunakutana na picha ya waongo waliokubuhu katika kufanya uharibifu kimapenzi wakiitumia siku hii kwa ajili ya kufanikisha uovu wao. Nitakupa kisa kimoja nilikishuhudia mahali
Siku moja katika pita pita yangu, nilikutana na jamaa mmoja hivi ambaye alikuwa akinunua kadi katika duka moja la kuuza vitu vya namna hiyo. Alinunua kadi nzuri, kubwa na maua kadhaa kiasi kwamba nikasema kwakweli jamaa ameonyesha kuwa anamjali mwenzie. Masaa mawili baada nilibahatika kukutana na yule jamaa katika mkahawa fulani wa chakula, alikuwa na binti mzuri na wa haja tu, huku akimwambia kuwa anataka wakitoka hapo wapitie dukani akamnunulie zawadi kwa ajili ya siku ya wapendanao, moyoni nikasema “Ama!! zile za kwanza zilienda wapi?”
Naam, huu ndio upande ambao tumekuwa tukijitahidi kuufanya uonekane mzuri sana katika sarafu hii ijapokuwa ni upande mchafu kupita maelezo. Ukiwatizama vijana wanayoyafanya katika siku hiyo unaweza ni wazi utajiuliza kama kweli kulikuwa na haja ya kumkumbuka mtu ambaye alikuwa akifanya yale wanayoyafanya, maana ukiwauliza bila haya wala soni wanakwambia tunamkumbuka mfalme na masiah wa wapendanao. Je, ndio alikuwa anafanya hayo mnayofanya?
Siku hii imekuwa ikitumiwa na vijana hadi wazee kama siku ya kuwaingiza mkenge mabinti wa watu, ambao nao kwa bahati mbaya sana wamekuwa hawana nafasi japo kidogo ya kuhangaisha akili zao katika kufikiri na kutafakari kila waambiwalo, ni siku ambayo wapo waliahidiwa kuzawadiwa viatu vua kioo, ghorofa za dhahabu, magari ya almasi na zawadi kemkem, lakini wakaishia kuzawadiwa virusi vya UKIMWI. Ndio wapo na wala usibishe.
Kuna jamaa yangu aliwahi kuniambia kuwa shetani huwa anaishi katika mabara mengine na huku Afrika na hususan Tanzania, huwa anakuja kwa mapumziko ya siku moja moja hasa nyakati za sikukuu, na kwakweli kwa kuangalia yale yanayofanyika katika siku hii, ni wazi kuwa shetani anakuwa yuko mapumzikoni Tanzania katika siku hii. Tizama magazeti na hasa yale wanayoyaita ya ‘Udaku’, siku chache baada ya siku hiyo, kama hutakumbana na picha za vijana kwa wazee wakiwa wako uchi wa mnyama.
Hivi kupendana ni hadi mkacheze uchi, au mkalewe na kujisahau hadi mnafumaniwa na ama wake za watu au watoto wa watu? Hivi kupendana ni lazima kuwa na mademu zenu tu? Hamuwezi kupendana na wazazi, ndugu jamaa na marafiki zenu wa kawaida hadi mpendane mabinti au wake za watu? Hivi kupendana ni hadi mkalale gesti mkiwa na mipombe yenu kichwani na kujisahau kiasi cha kushiriki ngono zembe na kuambukizana maradhi?
Hivi hatuwezi kupendana na watoto wetu na siku hiyo tukatona nao pamoja na mama zao tukiwa tumeulamba suti zetu nyekundu (kuna jamaa watasema wanaogopa radi najua hapa), na tukaenda mahali tukabarizi nao hadi mida mida hivi na kurejea majumbani mwetu tukiwa wapya?
Hatuwezi kupendana kwa kuhuisha upya ndoa zetu kwa wake zetu tuliowaoa miaka kadhaa iliyopita, hali ambayo itawafanya nao kujisikia wapya nafsini mwetu na hivyo kuendelea kututhamini? Hivi…… hivi…, ah nashindwa hata niseme nini kwakweli, maana hii hali tunakoelekea naamini itakuja kufikia wakati kuwa siku hii itageuka kutoka Siku ya Wapendanao hadi Siku ya Kulia, kwa kukumbukia yale yaliyotutokea katika siku hiyo.
HAPPY VALENTINE DAY wandugu wapendwa

Entry filed under: maskani.

SEMINA ELEKEZI…….Usiache ikupite Ni kwa maslahi ya UMMA au maslahi ya NYUMA?

3 Comments Add your own

 • 1. ndesanjo  |  February 18, 2007 at 6:38 pm

  Imebidi nicheke tu kuhusu hiyo habari ya shetani kuja Tanzania mapumzikoni siku moja moja!

  Valentine: unajua mtu akionyesha kunipenda bila kujali tarehe iliyopangwa na watu ambao hata hatuwajui nitafurahi mno kuliko alifanya hivyo katika siku iliyopangwa ambayo ni mara moja kwa mwaka mzima. Mimi napenda mtu aonyeshe mapenzi kufuata hisia zake badala ya kuwa kama mashine kusubiri tarehe 14 Februari. Wajamaa zetu wanatumia neno “spontenous” (sijui nimekosea herufi, aah, tuendelee mambo ya kutazama kamusi baadaye) kuelezea ninachosema.

 • 2. Chediel Charles  |  February 22, 2007 at 4:49 pm

  Hii nami huwa inanifanya niwaze inapokuja siku moja tu kwa mwaka mzima ya kuonyesha mapendo kwa mtu.Kuna maana gani kama siku nyingine sitaweza kumwonyesha kuwa nampenda.Pendo ni la kila siku si siku moja na hii sasa imegeuzwa kuwa siku nyingine ambayo wafanyabiashara kuvuna pesa bila msingi wowote kisa umwonyeshe mwenzio unampenda Pia wengine wanaiyanya ndio siku ya kufanya mambo machafu yasiyo faa inakera

 • 3. masereka  |  March 18, 2009 at 5:17 pm

  kweli asiefundwa nawazazi hufundwa na ulimwengu,hivi nini maana ya neno valentine?nj
  inamengi yakusema lakini nipeni jibu nami nita nena nanyi maana hujafa hujaumbika wengi wame………..~~`~~ napata shida kuelezea nipeni jibu nami nitakujuzeni sawa?18/03/09

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Trackback this post  |  Subscribe to the comments via RSS Feed


Blog Stats

 • 35,058 hits
February 2007
M T W T F S S
 1234
567891011
12131415161718
19202122232425
262728