Archive for February, 2007

Ni kwa maslahi ya UMMA au maslahi ya NYUMA?

SAKATA la ununuzi wa rada iliyonunuliwa na Serikali ya awamu ya tatu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika mazingira ya utatanishi mwaka 2002, lingali likichanja mbuga kama moto wa nyikani nyakati za kiangazi. Wengi wetu ambao tulikuwa hatujui kwa undani nini hasa kilikuwa ama kingali kimejificha ndani ya sakata hili, hivi sasa tunayajua, baada ya ukweli wake kuanza kuanikwa hadharani.
Teknolojia imetuwezesha kufunguliwa macho, Teknolojia imeonyesha tena umuhimu wake katika mchakato wa maendeleo, mchakato wa kuleta ukombozi, mchakato wa kupambana na ulafi wa baadhi ya viongozi wetu na uozo uliomo ndani ya baadhi ya serikali zetu, sio tu za kiafrika bali duniani kwa ujumla. Si hata serikali ya Uingereza ilichangia katika hili? unadhani sio uozo huo?
Bunge la Uingereza limejadili suala hili, na kukiri kuwa rushwa ilikuwemo katika manunuzi hayo, Rais wetu, mhe. Jakaya M. Kikwete, kaomba arejeshewe chenchi (cha juu kama wanavyosema vijana wa kizazi cha sasa), kutoka katika mabilioni yaliyokuwa yametolewa kwa ajili ya kununua rada hiyo. Ni kizungumkuti na mshike mshike kila kona kwa ujumla hivi sasa.
Si mimi au wewe msomaji wangu, ambao tuna uhakika kuwa nini kitajiri mwishoni mwa sakata hili, lakini naamini sote tuna uhakika kuwa huu ni mwanzo tu wa uvundo mkubwa, wakutisha, kuogofya na hata kukatisha tamaa, ambao umekuwa ukiwatafuna Watanzania na kuwaacha katika lindi kubwa la umasikini huku wale wanaojiita viongozi, waliochaguliwa na wananchi hao, wakiwa wanazidi kunenepeana kila uchao.

Naam! Kimsingi bado ningali niko katika mfululizo wa makala zangu kuhusiana na zile karatasi 85 zenye maandishi ya kuchefua ambayo yamepewa kichwa cha habari cha Muswada wa Uhuru wa Habari, na leo hii niko katika vipengele vile vinavyodaiwa kuwa si halali kuandikwa eti kwakuwa vinagusa maslahi ya Umma. Hivi ni umma upi unaozungumziwa hapa? Huu huu wa Watanzania watakaokuwa chini ya sheria hiyo au Umma wa wakubwa na vitegemezi vyao katika mahekalu yao?

Sehemu ya muswada huo inaainisha baadhi ya mambo ambayo eti yatakuwa ni siri ambazo hazitakiwi kuandikwa (bilashaka na kuhojiwa pia), ikiwa ni pamoja na biashara za nje, michakato ya kutunga sera, mijadala ya baraza la mawaziri na hata maamuzi yao pamoja na masuala yenye kuhusiana na Jeshi, tena hili hili linaloitwa Jeshi la Wananchi.

Hapa kidogo ndipo pananipa utata kwakweli, kwasababu kitu kinaitwa cha wananchi lakini hawatakiwi kukijadili, hawatakiwi kujua kinahitaji nini, hawatakiwi kujua kinasema nini, hawatakiwi kujua kinafikiria nini, hawatakiwi kujua kinataka kuwafanyia nini. hawatakiwi kuuliza, kuhoji utendaji wake, hawatakiwi kujulishwa kuwa kimefanyaje nk.

Hebu tutizame japo kwa juu juu tu kuhusu Jeshi. Hili ni Jeshi ambalo linaitwa la Wananchi wa Tanzania, kwa mantiki ya kuwa linawajibika kwa Watanzania, linatakiwa kuhudumiwa na Watanzania na masuala mengine ya namna hiyo. Watanzania wanatakiwa kujua uwezo wa Jeshi lao kwa mfano, ili waweze kutoa maamuzi ya kipi kifanyike kuliboresha, kuliongeza nguvu, na hata kuwaongeza marupurupyu ikiwa wanaona wazi kile wanafanya ni kikubwa kuliko kile wanachopata.

Linapokuja suala kwamfano la ununuzi wa rada nililoligusia katika aya za mwanzo wa makala yangu, hivi serikali inadhani kuwa inajua zaidi kilichobora kwa jeshi la wananchi wake kuliko wananchi wenyewe? na kama ni hivyo si kwasababu tayari mlishawaficha juu ya utendaji, matatizo na mahitaji ya jeshi lao? Watanzania kwamfano walioko maeneo ya mipakani walitakiwa kujulishwa juu ya kile kinataka kufanywa kwa ajili ya kuimarisha Jeshi lao, waseme kuwa kuna hali gani huko na kuwe na mtambo gani ambao utawasaidia hadi wao kule waliko, lakini haikuwa hivyo. sasa hili ni Jeshi la Wananchi au Jeshi la Serikali?

Watanzania wana haki na wajibu wa kujua, kufahamishwa na kujulishwa juu ya Jeshi lao ili waweze kulifikiria, walijadili na kisha watoe maamuzi kama ni kuliboresha lipewe nini na nini na kwa wakati gani, kwasababu wanajua umuhimu wa Jeshi lao na ndio walipa kodi ambao wanaweza hata kuamua kuwa waongezwe makato kwa ajili ya kuimarisha Jeshi ama laa. Kuweka sheria ya kuwazuia kupata habari kuhusu jeshi lao ni wizi wa haki yao ya kimsingi.

Muswada huu unawazuia Watanzania kujua kuwa Tanzania inapata faida kiasi gani kutokana na biashara baina yake na mataifa ya nje. Almasi zetu ambazo hivi sasa tunapunjwa mgao wetu, hatutatakiwa kujua kuwa baada ya mapitio ya mikataba hii zinaliingizia taifa kiasi gani, Tanzanite yetu hatutatakiwa kujua kuwa imeleta kiasi gani nchini, mauzo ya minofu ya samaki wanaovuliwa ziwa Victoria kule Mwanza, hatutakiwi kujua kuwa imetuingizia kiasi gani.

Mtanzania huyu huyu ambaye anaongozwa na viongozi aliowachagua yeye na wanaolipwa mishahara na marupurupu ya safari zao kutokana na kodi anayokamuliwa kila uchao, huenda kuanzia mwezi Aprili mwaka huu, asiwe tena na haki ya kufahamishwa kuwa serikali imeamua kuagiza chakula cha kiasi gani kutokana na kukabiliwa na uhaba wa chakula, hatatakiwa kujua serikali itatumia kiasi gani kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la ukame lililosababisha upungufu wa uzalishaji umeme, hatatakiwa kujua kuwa serikali inasafirisha nini na nini nje na inaingiza nini na nini.

Ndio hali ilivyo!! hakuna kuandika kuhusu masuala yanayogusa usalama wa taifa, hakuna kuandika kuhusu michakato ya uandaaji wa sera, majadiliano na maamuzi ya baraza la mawaziri, biashara za nje. Hivi haya mambo ni kwa manufaa ya nani? Usalama huu ni kwa ajili ya nani? Biashara hizi ni kwa faida ya nani? Sera hizo ni kwa ajili ya nani? Baraza hilo la Mawaziri ni kwa ajili ya nani?

Huu sio tu kuwa ni usanii unaotaka kufanywa na viongozi wetu kwa ajili ya kuwaibia wananchi waliowapa dhamana. Bali ni usaliti na wizi wa haki, wajibu na maslahi yao. Huku ni kujijengeea mazingira ya wizi huku wakijua kuwa hakuna wa kuwauliza maana siri zao si haziwezi kutoka?

Kutanunuliwa rada zingine sijui ngapi na jamaa kugawana bilioni 12 zingine kimya kimya bila sisi kujua. Kutanunuliwa Gulfstream 550, zingine na jamaa wagawane cha juu sisi hatujui, iko siku mtanunua hata silaha feki na kulikabidhi jeshi letu mtuweke hatarini sababu tu mnajua kuwa yakiibuka ya kuibuka hapa mna Gulfstream 550, zenu na mnaweza kwenda kupata hifadhi kwa mliogawana nao commision zilizotokana na manunuzi hayo.

Hapana. Hayo sio maslahi mnayodai ya Umma, bali ni maslahi mnayotaka kujiingizia nyie wenyewe kupitia milango ya Nyuma, lakini hala hala ndugu zetu. Watanzania wanaweza kuwa wajinga sana lakini sio kwa kiwango mnachodhania. isitoshe, inaweza kuwa kweli wamekuwa wajinga kwa muda mrefu sana, lakini hawako tayari kufanywa wapumbavu, jambo ambalo ndio mnataka kulifanya kupitia muswada huo.

Nazungumza tena na tena nikiwa katika nafasi ya mwananchi wa kawaida na pia kama mwana habari katika nafsi ya pili nikisema kuwa, MUSWADA WENU HUO SIO TU KUWA HAUFAI BALI PIA HATUUTAKI KAMA HAMTAUFANYIA MAREKEBISHO TUNAYOTAKA MYAFANYE.

February 16, 2007 at 10:34 am 1 comment

msimu wa mapenzi au wazinifu?

Kapteni Gadner G. Habash, yule nahodha wa Jahazi la Clouds FM analijua hili fika kuwa, Vijana wa kisasa miili yao si ya kawaida, ikitokea ukawachana kwa kisu au kiwembe sehemu yoyote ile ya miili yao, utashangaa kuona hawatoki damu, bali kopa (alama inayotumiwa kuashiria mapenzi). Ndio, “Vijana wa kisasa wamejaa mapenzi” pengine iwekwe hivyo kwa ufupi.
Naam, ni msimu wa mapenzi, msimu wa wazinifu, msimu wa wazinzi, msimu wa kudanganyana, msimu wa maambukizi mapya ya virusi vinavyosababisha upungufu wa kinga mwilini. Oh yes… Ni msimu wa Shetani kujiongezea wafuasi mamilioni kadhaa hivi. Unashangaa!!

February 14, ya kila mwaka, mamilioni ya watu Duniani huadhimisha Siku ya Wapendanao, a.k.a Valentine Day kama wanavyoiita wenye lugha yao. Kwa wengine, siku hii pia hujulikana kama Siku ya Mtakatifu Valentine, jamaa ambaye wamethubutu pia kumpachika cheo cha Patron Mtakatifu wa Wapendanao

Siku hii ambayo katika Bara la Afrika imekuwa ikizidi kuongezeka umaarufu wake kila kukicha, sio tu kuwa ina historia ndefu na pana kupita maelezo, bali pia imejaa historia zenye kupishana kutoka kwa mtu mmoja anayeisimulia hadi mwingine. lakini yote kwa yote, historia hizo haziibadili siku hii au maana yake. SIKU YA WAPENDANAO sio ya WANAOPENDANA?
Licha ya tofauti zinazojitokeza kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine, wote wanaosimulia kuhusu siku hii wanakubaliana kuwa ni siku ambayo ilitengwa mahususi kwa Wapendanao, yaani Likizo ya Wapenzi na Mapenzi, kwa maana ya kuthamini uwepo wa masuala hayo mawili. Ni siku ambayo watu walitarajiwa kuwa wanapeana (au kubadilishana vile?), zawadi mbalimbali, kuwa karibu sana na wapenzi wao (maana siku zingine hawako nao sio?), na mambo mengine ya namna hiyo.
Hata hivyo sijui ni kutokana na mabadiliko tunayoyaita ya lazima yanayojiri duniani au kutokana na kuwa BUSY, wataalamu wanakiri wazi kuwa siku hii imepoteza mvuto wake katika siku za hivi karibuni. Naamini kabisa kuwa kama ingewezekana huyo Patron Mtakatifu wa Wapendanao (st Valentine), akarejea Duniani na kuona siku ya kumkumbuka inavyosherehekewa, angeweza kuzimia kwa mshtuko.
Katika kipindi changu choooote cha kuijua siku hii, sikuwahi kumsikia mtu akimtumia mama yake, dadake, babake, shangaziye, nyanya yake, mdogo wake au mkubwa wake zawadi iwe ya maua, kadi au hata ujumbe mfupi kwa ajili ya kuwatakia kila lakheri katika siku hii, huo ndio upande mmoja wa shilingi ninayoijua mimi ya Siku ya Valentine. Upande ambao wengi wetu hatutaki kuuangalia maana tunahisi haukustahili kuwepo katika ‘sarafu’ ya Valentine Day.
Na kwa upande wa pili wa shilingi hii, upande ambao wengi wetu ndio tunapenda kuuangalia, tunakutana na picha ya waongo waliokubuhu katika kufanya uharibifu kimapenzi wakiitumia siku hii kwa ajili ya kufanikisha uovu wao. Nitakupa kisa kimoja nilikishuhudia mahali
Siku moja katika pita pita yangu, nilikutana na jamaa mmoja hivi ambaye alikuwa akinunua kadi katika duka moja la kuuza vitu vya namna hiyo. Alinunua kadi nzuri, kubwa na maua kadhaa kiasi kwamba nikasema kwakweli jamaa ameonyesha kuwa anamjali mwenzie. Masaa mawili baada nilibahatika kukutana na yule jamaa katika mkahawa fulani wa chakula, alikuwa na binti mzuri na wa haja tu, huku akimwambia kuwa anataka wakitoka hapo wapitie dukani akamnunulie zawadi kwa ajili ya siku ya wapendanao, moyoni nikasema “Ama!! zile za kwanza zilienda wapi?”
Naam, huu ndio upande ambao tumekuwa tukijitahidi kuufanya uonekane mzuri sana katika sarafu hii ijapokuwa ni upande mchafu kupita maelezo. Ukiwatizama vijana wanayoyafanya katika siku hiyo unaweza ni wazi utajiuliza kama kweli kulikuwa na haja ya kumkumbuka mtu ambaye alikuwa akifanya yale wanayoyafanya, maana ukiwauliza bila haya wala soni wanakwambia tunamkumbuka mfalme na masiah wa wapendanao. Je, ndio alikuwa anafanya hayo mnayofanya?
Siku hii imekuwa ikitumiwa na vijana hadi wazee kama siku ya kuwaingiza mkenge mabinti wa watu, ambao nao kwa bahati mbaya sana wamekuwa hawana nafasi japo kidogo ya kuhangaisha akili zao katika kufikiri na kutafakari kila waambiwalo, ni siku ambayo wapo waliahidiwa kuzawadiwa viatu vua kioo, ghorofa za dhahabu, magari ya almasi na zawadi kemkem, lakini wakaishia kuzawadiwa virusi vya UKIMWI. Ndio wapo na wala usibishe.
Kuna jamaa yangu aliwahi kuniambia kuwa shetani huwa anaishi katika mabara mengine na huku Afrika na hususan Tanzania, huwa anakuja kwa mapumziko ya siku moja moja hasa nyakati za sikukuu, na kwakweli kwa kuangalia yale yanayofanyika katika siku hii, ni wazi kuwa shetani anakuwa yuko mapumzikoni Tanzania katika siku hii. Tizama magazeti na hasa yale wanayoyaita ya ‘Udaku’, siku chache baada ya siku hiyo, kama hutakumbana na picha za vijana kwa wazee wakiwa wako uchi wa mnyama.
Hivi kupendana ni hadi mkacheze uchi, au mkalewe na kujisahau hadi mnafumaniwa na ama wake za watu au watoto wa watu? Hivi kupendana ni lazima kuwa na mademu zenu tu? Hamuwezi kupendana na wazazi, ndugu jamaa na marafiki zenu wa kawaida hadi mpendane mabinti au wake za watu? Hivi kupendana ni hadi mkalale gesti mkiwa na mipombe yenu kichwani na kujisahau kiasi cha kushiriki ngono zembe na kuambukizana maradhi?
Hivi hatuwezi kupendana na watoto wetu na siku hiyo tukatona nao pamoja na mama zao tukiwa tumeulamba suti zetu nyekundu (kuna jamaa watasema wanaogopa radi najua hapa), na tukaenda mahali tukabarizi nao hadi mida mida hivi na kurejea majumbani mwetu tukiwa wapya?
Hatuwezi kupendana kwa kuhuisha upya ndoa zetu kwa wake zetu tuliowaoa miaka kadhaa iliyopita, hali ambayo itawafanya nao kujisikia wapya nafsini mwetu na hivyo kuendelea kututhamini? Hivi…… hivi…, ah nashindwa hata niseme nini kwakweli, maana hii hali tunakoelekea naamini itakuja kufikia wakati kuwa siku hii itageuka kutoka Siku ya Wapendanao hadi Siku ya Kulia, kwa kukumbukia yale yaliyotutokea katika siku hiyo.
HAPPY VALENTINE DAY wandugu wapendwa

February 13, 2007 at 9:25 am 3 comments

SEMINA ELEKEZI…….Usiache ikupite

Dunia hii kweli ina watu jamani. Hebu someni ujumbe huu ambao nimetumiwa na mmoja wa marafiki zangu wa karibu sana. Nimeuweka katika blogi yangu kama nilivyoupata kusudi nisiupunguze uhondo wake.

==================

Baada ya semina elekezi kwa viongozi na watumishi wa Serikali kule ‘A-Town’, na nyingine zilizofuata baada ya hapo kama ile ya wakuu wa mikoa kwa watendaji na viongozi mbalimbali wa mikoa yao na nyingine kama hizo, Shetani naye aliitisha semina elekezi kwa mapepo duniani. Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo alisema

“Tumeshindwa kuwazuia wakristo na Waisilamu wasiende makanisani na Misikitini, tumeshindwa kuwazuia wasisome vitabu vyao vitakatifu na kufahamu ukweli, tumeshindwa hata kuwazuia wasiwe na mapenzi ya kweli kwa Muumba wao na mara wapatapo muungano wa kweli na Muumba wao, mamlaka yetu yatakuwa yamefika mwisho, kwahiyo waacheni waende misikitini na makanisani, waacheni waendelee na karamu zao za upendo,

“Lakini waibieni muda, iliwasipate nafasi ya kudumisha mahusiano na mapenzi yakweli kwa Muumba wao, na hiki ndio ninachotaka mkifanye kwa mwanadamu” alisema Shetani kisha akatulia na kusafisha koo lake kwanza kabla ya kutoa maagizo aliyotaka mapepo wakamfanyia mwanadamu

“Wataabisheni wasipate kamwe kushikamana na Muumba wao, wao na wasifungamane naye kwa siku nzima, hakikisheni wanakuwa ‘BUSY’ (Being Under Satan’s York) katika mambo yasiyokuwa na umuhimu katika maisha yao na muanzishe mipango mingi sana isiyohesabika ili kujaza akili na ufahamu wao.

“Wapeni kutumia, na kutumia, na kutumia; na kukopa, na kukopa, na kukopa, washawishini wake zao waende kufanya kazi kila siku kushinda huko kwa masaa mengi sana kwa siku na waume zao wafanye kazi kwa siku sita hadi saba kwa wiki, na masaa 10 hadi 12 kwa siku, ili wasiweze kupata nafasi ya kutulia na kutafakari chochote kulingana na mfumo huo wa maisha. Wazuieni wasiwe na nafasi ya kukaa na watoto wao kwa maana familia zao zikiparaganyika nyumba zao hazitakwepa msongamano wa kazi na mawazo.

“Wachocheeni zaidi akili na fahamu zao ili kuhakikisha kwamba hawaiskii ile sauti ndogo, tulivu ya Mungu wao, washawishini walize radio au kaseti au muziki kwenye simu,popote wanapoendesha gari au wanapotembea kwa miguu, waache TV, VCR, CD na Computer zao zikiwa zimewashwa kama kawaida majumbani mwao na mhakikishe kwamba kila duka na mgahawa kote duniani linapiga muziki usiokuwa wa kiimani, mfululizo bila kukoma, na hii itasonga akili na fahamu zao na kuvunja ule muungano wa baina yao na Mungu wao.

“Jazeni magazeti na vijarida mbalimbali kwenye meza zao za kahawa na chai dunia kote, shindilieni habari na matukio mbalimbali ndani ya fahamu zao kwa muda wa masaa 24, ingilieni kwenye muda wao wa kuendesha barabarani kwa
kuwaonyesha mabango na matangazo.

“Kwenye masanduku ya posta na barua pepe jazeni vipeperushi na majarida na kila aina ya matangazo ya habari za vitu na hudumu yanayowapa matumaini ya uongo, wekeni wanawake warembo sana mitaani na kwenyeTV, na majarida ili kwamba wanaume walioko kwenye ndoa wadanganyike na kuamini kwamba urembo wa nje ndio muhimu, na wasiridhike na wake zao,

“Wafanye wake zao wachoke sana wasiweze kuonesha upendo kwa waume zao usiku, wapeni maumivu ya kichwa pia kwa maana kama hawatawapa waume zao upendo wanaouhitaji sana wataanza kutazama kwingine na hiyo itaparaganyisha familia zao haraka sana.

Wapeni waalimu wa uongo ili wawapotoshe wasifundishe imani ya kweli kwa watoto wao na waumini wao, wapeni zawadi na kadi za pasaka ili wasizungumzie nguvu za ufufuko kwa Kristo juu ya dhambi na mauti, hata katika karamu zao wachosheni sana kwa anasa nakuwafanya warudi wakiwa wamechoka sana.

“Hakikisheni wanakuwa ‘BUSY’ na kusongwa na mambo kiasi kwamba hawapati muda wa kutafakari wema wa Mungu na badala yake yake wapeni kutalii kwenye maeneo ya ajabu, matukio ya michezo, matamasha, kumbi za sinema na video. Wafanye wawe BUSY, BUSY, BUSY!!, yaani wasongwe na kusongwa na
kusongwa na kazi kwelikweli,

“Na wanapokutanika kwenye ibada zao za kiroho wafanye waingie katika umbea na fitina na kuzungumzia mambo madogo madogo ya umbea na fitina ili waondoke wakiwa na dhamira mbaya zilizochafuliwa, jazeni visababishi vingi vya mambo katika maisha yao ili wasiwe na nafasi ya kutafuta msaada na nguvu za Mungu wao, muda si mrefu watakuwa wakitegemea akili zao wenyewe,wakihatarisha afya zao na za familia zao kwa ajili ya maangamizi yao wenyewe.

“Itafanya kazi nawaambia, itafanya kazi, sababu huu ni mkakati kweli kweli” asanteni sana kwa kunisikiliza” Shetani alihitimisha hotuba yake ya ufunguzi.

Mapepo yaliondoka kwenye mkutano yakiwa na hamu kubwa sana ya kutekeleza majukumu hayo waliyopewa na kuanza kuwafanya wanadamu wanaoamini, waanze kukimbia na mambo huku na huko.wakawa na muda mdogo sana kwa ajili ya Mungu wao na familia zao, wakakosa muda wa kuwaeleza wengine kuhusu nguvu za Mungu kubadili maisha ya wanadamu.

SWALI: Je, Shetani kwa kushirikiana na kikosi chake amefanikiwa katika mipango yake hiyo? Ubize au kutingwa na kazi kunamaanisha kuwa chini ya mkataba au utumwa wa shetani?.

HAKIMU NI WEWE UNAYESOMA UJUMBE HUU.

PLEASE PASS THIS ON, IF YOU AREN’T TOO BUSY

February 10, 2007 at 10:52 am Leave a comment

TUNAJIFUNZA KUTENGENEZA SHANGA?

Kwa siku ya leo, sikuwa na nia ya kuandika chochote kile kwasababu ningali nautafakari na kuufanyia kazi muswada wa kifisadi wa habari ambao wanaoupigia debe wanauita Muswaha wa Sheria ya Uhuru wa Habari. Hata hivyo, magazeti ya leo yamenilazimisha niandike kidogo hapa ili kuwajulisha machache sana yaliyojiri katika magazeti ya nchini Tanzania kwa siku ya leo.

Magazeti mengi sana yamezungumzia juu ya Homa ya Bonde la Ufa (Rift Valley Fever) kuwa imeingia nchini Tanzania na tayari imeshachukua maisha ya Watanzania wawili huko Arusha. Magazeti ya Majira na lile la Serikali ya Habari Leo, (kwa mfano), yote yamegusia juu ya habari hiyo, ikiwa ndio habari kuu iliyotawala kurasa za mbele za magazeti husika.

Kwa upande wa Burudani ambako ndiko kidogo kuliniacha hoi, ni habari ya kuwa eti Dar es salaam kunafanyika semina ya kutengeneza shanga…. Ndio, ni SEMINA YA KUTENGENEZA SHANGA na wala hujakosea ulivyo soma, tena semina hii inaendeshwa na Wa-Ghana, waliokuja nchini kutufundisha kuzitengeneza. Soma habari hiyo zaidi kwa kubofya hapa.

Na mwisho kabisa, nasikia eti timu ya taifa ya Tanzania, yaani ile Taifa Stars, a.k.a JK Boys, ambayo iko ziarani Brazil kwa mafunzo ya mwezi mmoja, eti ilidhaniwa ni timu ya taifa ya Watoto. Soma hapa ujue kina Mwaikimba, SMG na wengineo walivyoonekana watoto huko Brazil.

NGOJA NIKAONE SEMINA YA KUTENGENEZA SHANGA KWENYE TV

February 6, 2007 at 4:33 pm Leave a comment

SAFARI YA MWISHO YA MWAIBABILE

Ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu Adam Mwaibabile wakishuhudia mwili wa mwandishi huyo aliyefariki dunia juzi, ukiingizwa kaburini tayari kwa mazishi yake, yaliyofanyika katika makaburi ya Mianzini – Nzovwe, jijini Mbeya

February 1, 2007 at 8:06 pm 3 comments


Blog Stats

  • 34,787 hits
February 2007
M T W T F S S
 1234
567891011
12131415161718
19202122232425
262728