Uhuru wa habari au uhuru wa viongozi mafisadi?

January 25, 2007 at 1:43 pm 4 comments

Nianze kwa kukumbuka moja ya masharti ambayo, nchi zilizotia saini Mkataba wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, zinatakiwa kuyatimiza, ambalo ni lile la nchi hizo kuhakikisha kuwa kila sheria inayotungwa (katika nchi husika), inakuwa ni yenye uelekeo wa kuzilinda na kuzitetea zaidi haki za binadamu na si kuzikandamiza kwa namna yoyote ile” Hivi Tanzania si moja kati ya nchi hizo?

Nimeanza kwa kumbukumbu na swali hilo hapo juu, wakati nikiwa naelekea kutimiza ahadi niliyowapatia wasomaji wangu katika makala iliyotangulia, ahadi ya kuzama kwa undani kidogo (na kwa mtazamo wangu), katika kujadili hiki kinachoitwa Muswada wa Sheria ya Uhuru wa Habari wa 2006, nchini Tanzania.

Baada ya kuupitia, kuusoma na kuujadili kwa kiwango changu, jambo la mwisho kabisa nililoweza kujiwa nalo kichwani mwangu ni kuwa muswada huu kwakweli umekaa vibaya tena vibaya sana. Haufai, haustahili kuwepo nchini Tanzania katika zama hizi na huenda haustahili kuwepo sehenmu yoyote ile duniani. Labda Ujerumani ya enzi za Hitler, na Uganda ya Idd Amin.

Ni muswada ambao umejaa mapungufu mengi kuliko mazuri yake, muswada ambao hauhitaji mtaalamu wa aina yoyote ile kujua kuwa umekaa vibaya, isipokuwa wanafiki wachache ambao mwandishi mmoja aliandika katika makala yake kuwa, baada ya kuona wamehodhi siasa na akili za baadhi ya watawala, sasa wanataka kuhodhi na akili za Watanzania wote.

Ni muswada ambao kwakweli ulinifanya nijiulize kama kweli walioshiriki kuishauri serikali ili kuuandaa, kuuandika na sasa kufikiria kuwa unastahili kuwasilishwa bungeni muswada huo wanaelewa kweli maana ya kitu UHURU? Kwasababu muswada huu hauna chembe yoyote ile ya hicho kitu kinaitwa uhuru ndani yake.

Labda nianze kwa kuangalia kile kinachoitwa Uhuru ndani ya muswada huo kama kweli kipo, na wakati tukiwa tunajadili hili, ningependa tuwe na mambo mawili ya muhumu sana katika fikra zetu, la kwanza likiwa ni Ibara ya 18, ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo inazungumzia juu ya haki ya kila mwananchi kupata na kutoa habari, bila kuingiliwa uhuru wake wa kufanya hivyo.

Jambo la pili ni kuwa, Tanzania ikipitisha muswada huu, itakuwa nchi ya nne ya kiafrika kuwa na sheria ya namna hii baada ya nchi za Afrika Kusini, Zimbabwe (ambako imeshaleta matatizo makubwa sana), na jirani zetu Uganda, ambako hivi karibuni kulikuwa na kesi ya aina yake kuhusu hiki kinachoitwa uhuru wa habari.

Kwa taarifa tu ni kuwa kesi hii ya watendaji wawili wa ngazi ya juu katika gazeti la The Monitor, Mhariri (Charles Onyango)na Mwandishi mwandamizi (Andrew Mujuni), dhidi ya serikali ya Uganda, iliamuliwa na Mahakama ya Rufaa ya Uganda (Supreme Court), kwa kauli au ufafanuzi ufuatao:-

” Haki ya uhuru wa kujieleza na utangazaji wa habari hauishii kwa mawazo, maoni au habari za kweli tu, bali unahusu pia habari zisizo za kweli au zisizo sahihi kwani kile ambacho kinaweza kuonekana si cha kweli kinaweza kugeuka ukweli iwapo patatolewa nafasi ya kusikilizwa “

Nikirejea katika muswada wenyewe sasa, ni kwamba muswada huu umejaa vipengele ambavyo vinalenga zaidi katika kulinda mafisadi, wala rushwa, viongozi wabovu, waongo na walafi wakubwa wa mali za umma, kuliko kuimarisha Tanzania kama nchi ambayo inakubaliana na mfumo wa Demokrasia kama nguzo muhimu ya kuleta maendeleo endelevu.

Muswada huu unaainisha kuwa kile kitakachostahili kuitwa habari na kustahili kupewa ama kuchukuliwa na mwandishi wa habari, ni makabrasha au nyaraka zilizoko katika masijala ya wazi au ambayo yameandaliwa na taasisi husika kwa ajili ya kuuzwa ama kusambazwa kwa wanajamii (mnaelewa vitu vinaitwa vipeperushi?). na baada ya hapo, mwandishi kuandika kile kilichomo ndani ya makabrasha hayo tu na si zaidi ya hapo.

Ikiwa nimeletewa taarifa kuwa barabara ya kwenda kwetu upareni imejengwa kwa kiwango cha lami kwa mujibu wa kabrasha la wizara, sitakiwi kusema zaidi ya hapo, hata kama wakati nasoma taarifa hiyo nitakuwa nimekwama pale Kikweni kwasababu ya matope barabarani. Na nikiandika hivyo ni kosa, tena la jinai. Huo uhuru hapa ni upi tunaomaanisha? Uhuru wa Viongozi kusema uongo kisha tuwakubalie tu? Hapana.

Muswada huu unamtaka mwenye kuhitaji taarifa zozote zile kutoka taasisi yoyote ile (sijaona mahali wamegusia sekta binafsi lakini), kuandika barua ya kuomba kabrasha au waraka wenye kile anachokitafuta, tena akiainisha kuwa anachokitaka kiko sehemu gani. Majibu yake yanaweza kuchukua hadi siku 21 na sio lazima yawe na kukubaliwa, kwasababu unaweza kuambiwa kuwa kile unachokitaka ni siri ya ‘Sirikali’.

na ikiwa utakuwa na bahati zaidi, basi utakaribishwa mezani kwa mheshimiwa mwenye tumbo lake kuuuubwa, akikuchekea chekea na faili ulilolitaka likiwa mbele yake, kisha atatumia nguvu yake nyingine anayopewa na sheria hii, ya kunyofoa karatasi/taarifa ambazo anaona zinagusa ‘maslahi ya umma’.

Kama ulifuata hotuba ya kiongozi fulani yenye kurasa kumi kwa mfano, jamaa anaweza (kwa mujibu wa sheria hii), akanyofoa kuanzia ukurasa wa pili hadi wa tisa, kwa kisingizio kuwa zinagusa maslahi ya umma, kisha ukapewa ukurasa wa kwanza wenye utangulizi na majina kibaaaao ya waongo waliokuwa wamehudhuria sehemu hotuba ilikosomwa, na ule wa mwisho wenye nawashukuruni kwa kunisikiliza. Uhh!!

Ikiwa ndugu yangu utabahatika kupata jalada zima kama ulivyokuwa umeliomba, lina kurasa zote, usije ukajidai kuwa ni mjanja sana, kwasababu inawezekana kabisa kuwa huenda ndio umechimbiwa kaburi lako ukiwa unajiona ili uzikwe mzima mzima, ama ujikaange mwenyewe kama samaki Pweza.

Kwasababu, sheria hii imemtega mwana habari wazi wazi kwa kumpa mamlaka mheshimiwa mwenye dhamana ya habari kuweka pia usiri katika kabrasha/waraka wowote ule ikibidi (nadhani walimaanisha akijisikia kwakweli, maana kama ni kubidi ilibidi wautupilie mbali sababu tumeshaona haufai na wameshalalamikiwa). Tujiulize, hivi kuna uadilifu katika viongozi wetu kweli?

Kwasababu hata pale walipoongea jambo leo, kesho likaripotiwa na vyombo vya habari kisha wakajiona kuwa walitafsiriwa (sio kuandikwa) na umma, wamekuwa wakikurupuka ama kukanusha na kutishia kushitaki vyombo vilivyoandika hivyo. Bahati nzuri tu ni kuwa kwa sasa kidogo sheria zetu za kuchechemea nazo zimekuwa zikisaidia, lakini kwa muswada huu kitakachojiri ni hiki.

Kwamba leo utafika na kupewa risala na kiongozi baada ya kuiombea siku zaidi ya 21 zilizopita, kisha utaenda kuandika habari kulingana na waraka ule kama sheria ilivyotangulia kubainisha, lakini kesho wananchi wakija juu kuhusu taarifa hiyo na kuanza kuhoji, Waziri anaweza kuamua tu kuwa agionge muhuri wa usiri katika lile kabrasha, na kisha mwandishi utaenda kuulizwa chanzo chako ukikutwa na waraka ule tayari uko mavini.

Ndio, si umekutwa na waraka wa siri wa serikali? Na waziri si anakwambia tu kwasababu wananchi walishaanza kuhoji kuhusu habari uliyoandika na kwamba ilishahatarisha usalama na maslahi ya umma? Ana mamlaka hayo kwa mujibu wa muswada huu ikiwa utapita na kuwa sheria. Katika mfumo huu, kila kukicha waandishi wa habari watatakiwa wawe wanaandika kile wanachopewa kimaandishi na viongozi.

Hivi, katika mfumo huu ni lini tunatarajia kuwa tutaambiwa fulani kala fedha za umma? Unajua tatizo kubwa la mifumo ya kiutendaji katika utawala ni kwamba ni ya kimuingiliano zaidi kuliko sehemu nyingine. Kwa maana ya kwamba hata inapotokea ulaji rushwa katika jambo fulani, si wizara husika tu ambayo itakuwa imeshiriki, bali karibu kila wizara kwasababu suala la matumizi ya fedha za umma ni suala la Baraza la Mawaziri.

Kwa maana hii ni kwamba hatutarajii kuwa wizara fulani siku moja itatoa tamko la kuituhumu wizara fulani kwasababu ya ufisadi, rushwa na wizi unaofanywa na viongozi wake. Kwa mantiki hii, Watanzania wanatakiwa kuwa watu wa kuambiwa leo tumekusanya shilingi 20 waseme ndio wazee. Na katika hizo 20 tumetumia 55 zingine zikiwa tumekopa kwahiyo deni letu limekua nje, nao waitikie tawile wazee. Huu ni uhuni, wizi na upuuzi wa hali ya juu.

Huu ni ujenzi wa genge la viongozi matapeli, wezi, wala rushwa na madikteta, kwakuwa wanajua kuwa hakuna wa kuanika siri zao zikajulikana kwa wananchi na hakuna atakayewezesha mabaya yao kujulikana kwa jamii inayowazunguka hivyo wataendelea tu kula raha, huku wakijibadilishia hata sheria waendelee kuwepo madarakani kinyemela bila wananchi kujua.

Hii ni rasharasha tu ya utapeli unaoandaliwa kupitia muswada huu, hii ni mwendelezo tu wa makala kadhaa nilizoahidi kuziandika kwa ajili ya kuujadili muswada huu. Wakati tukiwa tunajiandaa kwa ajili ya kuendelea kuona mapungufu nmengine, ni vyema tukashiriki kujadili haya na ikiwezekana kuyatolea tamko.

Entry filed under: maskani.

moto haufunikwi kwa makaratasi KWANINI SIUPENDI MUSWADA HUO?

4 Comments Add your own

 • 1. JaqueNgowi  |  January 25, 2007 at 3:35 pm

  Mzee Mada imetulia……..Congrats

 • 2. luihamu  |  January 25, 2007 at 7:50 pm

  uliyonena ni kweli Kamanda,huu ni ubaguzi wali ya juu,je walala hoi watalia na nani?chombo cha habari ni chombo muhimu sana kwa jamii,sasa kama hiki chombo kikibanwa sijui

 • 3. luihamu  |  January 28, 2007 at 1:59 pm

  Kamanda,tunaanda kamati yetu vipi mbona kimya?Tuchangie maoni Kamanda.

 • 4. ndesanjo  |  January 30, 2007 at 8:11 pm

  Nyanja hii inavyobadilika kwa kasi, nyanja ya enzi za Youtube badala ya CNN, sijui hawa wazandiki watatuweza?

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Trackback this post  |  Subscribe to the comments via RSS Feed


Blog Stats

 • 35,058 hits
January 2007
M T W T F S S
1234567
891011121314
15161718192021
22232425262728
293031