moto haufunikwi kwa makaratasi

January 22, 2007 at 6:55 pm Leave a comment

IKIWA imetimiza mwaka mmoja na mwezi mmoja kamili toka ilipoingia madarakani kufuatia uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, Serikali ya awamu ya nne ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya kamanda wake mkuu mheshimiwa JK, imekuwa na kipindi kilicho kigumu zaidi kuliko wengi wetu tulivyo na tunavyodhani.

Achilia mbali matukio ya kutisha ya ujambazi na uporaji wa fedha yaliyoukaribisha utawala huu katika zama zake za kuingia Ikulu, achilia mbali tatizo la umeme, maji, njaa, ukame na mengine kadha wa kadha; haya kwangu yanaweza kuwa yalikuwa ni kama rasharasha tu za mvua ambazo sasa tunaanza kuziona. Mvua za kutokujiamini, mvua za kusahau historia, kukimbia vivuli vyetu sisi wenyewe na kuanza kujikataa kule tulikotoka.

Ni katika kipindi hiki ambapo tumesikia viongozi wetu wakitueleza kuwa matatizo yanayowakabili waliyarithi kwahiyo wasitupiwe lawama sana. Ni katika kipindi hiki tumesikia hadithi ile ile ya kuwa majina ya wala rushwa na vigogo wauza unga yako miononi mwa amirijeshi wetu mkuu, lakini hayawekwi wazi. Na nzuri au pale mchezo unapokuwa mtamu ni pale unapokumbuka kuwa wakati serikali hii inaingia ilijinadi kuyafanya yote hayo kwa kasi, ari na nguvu mpya.

Kulikuwa na kauli mbiu za ‘Kasi na Viwango’, kulikuwa na kauli mbiu za Ari mpya, Nguvu mpya na Kasi mpya’, ambazo zote hizi zilisherehesha usimikwaji wa serikali hii madarakani. Hivi sasa tukiwa tunamaliza mwaka na mwezi mmoja, hivi ni tatizo lipi hasa lililokubwa ambalo limeshughulikiwa kwa vishereheshaji hivyo?

Matatizo ya wafugaji karibu kila kona ya nchi yameendelea kuitafuna serikali hii kwa muda wote huo, huku tukiendelea kuambulia matamko ambayo uzoefu wetu huko nyuma unaonyesha kuwa kufanyiwa kwake kazi ni jambo gumu sana kuliko kuyapatia sababu na visingizio vya kutokuyatimiza. Suala la umeme linaweza kuonekana kama limefikia tamati kwasababu unasemekana kuwa upo wa kutosha, lakini kwangu mimi tatizo limekuwa kubwa zaidi kwasababu bei imezidi kupanda, licha ya kuwa hata iliyokuwepo ilikuwa inalalamikiwa kuwa kubwa.

Bado wala rushwa wanaendelea kuitesa nchi hii huku wakisababisha walalahoi kukosa haki zao za msingi kwa kukosa ‘mashati ya mikono mirefu’, watoto wetu wangali wamelundikana mitaani maana hawana ajira, mitaji wala fedha za kujissomeshea achilia mbali wale ambao licha ya kuumiza akili zao kwa ajili ya kujiandalia maisha ya baadae, wamekosa nafasi hata ya kuingia sekondari.

Biashara ya madawa ya kulevya bado ni tatizo kubwa sana, urasimu katika baadhi ya sehemu na hali ya uchumi wa nchi kuendelea kuwa ya kusuasua ni changamoto ambazo bado tunazo na kwakweli jitihada za kuyafanyia kazi zikiwa zinaonekana kuwa za maneno zaidi kuliko uhalisia wenyewe.

Kati ya haya yote, hakuna hata moja ambalo uongozi wa sasa haukuwa ukiyajua toka ulipokuwa unafanya jitihada za kuingia madarakani. Na ni haya na mengine kadha wa kadha ambayo yalitumiwa kama chambo cha kuuwezesha kuingia madarakani. Ni haya na mengine mengi ambayo tulikuwa tunaahidiwa kuwa yatafanyiwa kazi kwa ari, nguvu na kasi mpya tena kwa viwango. Na ndio ahadi hizo hizo ambazo tulitarajia kuwa zitakuwa zimeshaanza kuzaa matunda katika kipindi hiki.

Kimsingi sina nia ya kusema kuwa utawala uliopo haujafanya lolote lile, laa. Isipokuwa kile walichokitenda ni KWA UWEZO WAO na sio kulingana na AHADI ZAO na namna walivyozitoa, kwasababu walipokuwa wakizitoa walikuwa wakizitoa katika namna ambayo iliwafanya mamilioni ya Watanzania kuamini kuwa sasa Yesu, anarejea kuwaokoa Watanzania ndani ya muda mfupi sana.

Hili lilikuwa moja kati ya makosa makubwa sana kuwahi kufanywa na viongozi hawa wakati walipokuwa wanajinadi. Sidhani kama walikuwa wanatambua kuwa wananchi waliokuwa wakiwaahidi mambo hayo, wangekuja kuwahukumu kulingana na staili yao ya utoaji ahadi na kile watakachokuwa wakikifanya.

Kwa hakika nashawishika kuamini kuwa hili walikuwa ama hawalitambui au walikuwa wakilitambua lakini walidhania kuwa Watanzania pengine hawana uwezo wa kutumia zile ahadi zao kama kigezo cha kuwapima. Na hili bilashaka ndilo linalojitokeza hivi sasa ambapo tunaona baada ya wao kuanza kuona hali hiyo, juhudi zimekuwa kuanza kutafuta njia za kujinasua.

Makala yangu hii, ni sehemu ya kwanza ya mfululizo wa makala kadhaa ambazo nitakuwa nikiwaletea mahususi kwa ajili ya kujadili hiki kinachoitwa Muswada wa Sheria ya Uhuru wa habari nchini. Sina hakika kama upo kwenye mtandao fulani kwa sasa kiasi cha wengi wa wasomaji wangu kuweza kuusoma, na pia sidhani kama wengi wetu tumeshauona na kuupitia, lakini nitajitahidi sana kwa kadiri niwezavyo kuuelezea vile nilivyouona na tuupitie kwa pamoja.

MOTO HAUFUNIKWI KWA MAKARATASI ILI USIENEE

Entry filed under: maskani.

wanablogu wanapoifufua JUWATA Uhuru wa habari au uhuru wa viongozi mafisadi?

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Trackback this post  |  Subscribe to the comments via RSS Feed


Blog Stats

  • 35,058 hits
January 2007
M T W T F S S
1234567
891011121314
15161718192021
22232425262728
293031