Tunapalilia Upumbavu?

January 9, 2007 at 11:40 am 4 comments

“Hapa duniani wale wanaopenda kunyoosha mistari ndio wanaokumbana na matatizo zaidi, wewe pinda tu mistari kisha utaona mambo yanavyokunyookea” – aliyenukuliwa anahifadhiwa.

Naandika makala hii takriban dakika 48 toka nitoke katika chumba cha mtihani nilipokuwa nafanya mitihani yangu ya kumaliza semister ya kwanza kwa kozi ninayosomea ya sheria. Nimetoka kufanya mtihani wa CL (Communication Skills), baada ya ule niliofanya jana wa DS (Developmental Studies).

Naikumbuka nukuu niliyoanza nayo hapo juu baada ya kushuhudia yote yaliyojiri katika siku hizi mbili za kufanya mitihani niliyokwishaitaja na wakati naikumbuka pia najiuliza hivi hayo yaliyojiri katika chumba cha mtihani ni kwa faida ya nani hasa? Ni kwa faida yetu tuliokuwa katika mitihani hiyo au kwa faifa ya nani hasa?

Muda mfupi baada ya kutoka katika chumba cha mtihani (nikiwa wa kwanza), alitoka mwanafunzi mwenzangu mmoja na tambio kadhaa wa kadha kuhusu “atakavyopasua” (akimaanisha kufaulu) mitihani hiyo. Nilimwangalia nikamtupia swali kwamba “Je, katika kupasua huko ni kwa asilimia ngapi atakuwa ametumia uwezo wake na kwa kiasi gani atakuwa alisaidiwa?”

Nilimtupia swali hilo kutokana na pilika pilika nilizokuwa nazishuhudia akizifanya yeye na baadhi ya wanafunzi wenzangu katika kupasiana vijikaratasi sijui niviite vya majibu au vya nini maana sina uhakika kama kweli yalikuwa majibu. Ingawa inawezekana kila mmoja akawa na mtazamo wake kuhusu hili, lakini nitakiri kuwa kuna wakati pilika pilika hizo zilikuwa zikinikera kwa namna moja ama nyingine. Zilikuwa zinanikera kwasababu sikujua kuwa zilikuwa zinafanyika kwa faida ya nani na kwa ajili ya kumkomoa nani hasa.

Asilimia kubwa ya ninaosoma nao ni watu wazima tu, wenye familia zao, wenye watoto wao na ambao wanawasomesha watoto hao. Inawezekana kuwa wapo kati yao hawana utamaduni wa kufuatilia maendeleo ya watoto wao lakini ukweli unabakia pale pale kuwa wote kwa ujumla wanataka kila mwisho wa mhula mtoto awe amefanya vyema katika mitihani yake.

Kwa mzazi wa aina hii anapoamua kuingia darasani, akajilipia ada yeye mwenyewe kwa lengo la kujiendeleza kielimu, ni wazi kuwa katika kiwango chake haitarajiwi awe na akili sawa na za mtoto wake. Ni wazi kuwa anatakiwa kuhakikisha kuwa kila aina ya senti aliyoitumbukiza katika kujisomesha inampa uchungu wa kuhakikisha kuwa inambadilisha kimawazo, kifikra na kimtazamo. Sasa hapa ndipo ninapojiuliza hivi hizo pilika pilika kweli zinamwelekeo wa kutupeleka huko?

Naam, ni wazi kabisa kuwa mzazi wa namna hii sio tu kuwa anazidi kujidunisha zaidi badala ya kujielimisha zaidi, na haitarajiwi kuwa mzazi wa namna hii atasimama kidete kuhakikisha kuwa mtoto wake anakuwa na utaratibu mzuri wa kumwezesha kufaulu mitihani yake. Ndio!! Kama mzazi unakosa kujua kuwa wajibu wako katika kujiendeleza ni kuhakikisha kuwa unatumia uwezo wako kwa kiwango cha hali ya juu, ni vipi utajali kuwa mwanao amefaulu ama kwa kuhonga au kwa kuibia majibu kwa mwenzake?

Na katika hali kama hii tunajenga jamii ya namna gani hasa? Ni wazi kabisa kuwa moja kati ya mambo ambayo yamekuwa yakikwamisha kuendelea kwa uchumi wa taifa letu ni pamoja na kiwango duni cha elimu tulicho nacho. Ni wananchi ambao wanalalamikia hali hii, lakini sasa ni wananchi hao hao ambao hawafanyi juhudi za kuhakikisha kuwa kiwango hicho kinaboreka zaidi kwa kila mmoja kuhakikisha anatumia kikamilifu akili yake. Tunamlalamikia nani hasa ambaye atatukomboa katika hili?

Wengi wetu tumekuwa ama tukisoma kwa ajili ya vyeti au kwa ajili ya kupandishwa cheo kazini, lakini badi hata waliofanya hivyo hawajaweza kuwa na ufanisi wa kutosha katika majukumu yao, yawe ya kiserikali au ya kwenye mashirika binafsi. Usomaji huu kwa ajili ya vyeti na kupandishwa cheop ndio ambao umekuwa ukidumaza elimu yetu. Ndio umekuwa ukizalisha kizazi cha watu wasiokuwa na uchungu na maendeleo, kwasababu kwao kila jambo ni rahisi sana kama kuibia majibu ya mitihani.

Na hata mifumo yetu ya ajira imekuwa ya namna hiyo hiyo na huenda ndio maana hata usomaji umekuwa wa uelekeo huu. Ajira zinazotolewa kwa kuangalia wingi wa vyeti ni ajira zisizokuwa na mwelekeo wa kulikomboa taifa hili katika umasikini. Ni ajira ambazo zinawafanya watu wasiokuwa na sifa kukaa maofisini na kuishia kuitisha makongamano, warsha, semina, mikutano nk, wakishania kuwa huko ndio kupambana na umasikini.

Kwakweli sijui wa kumlaumu atakuwa nani ingawa kwa asilimia kubwa sana naamini ni kwetu sisi wenyewe, sababu tungali tunaelea katika kina kirefu cha upumbavu badala ya ujinga. Tumejijengea utamaduni wa kuwa kila kitu ni rahisi sana kama kukisema tu na ndio maana hatutaki kutumia akili zetu. Tumejidumaza kutokana na mifumo ambayo tuliikuta ambayo kama tukiwa na uchungu kama tunavyoilalamikia kweli tunatakiwa sisi ndio tusimame kidete kuhakikisha kuwa tunaibadilisha hali hiyo.

Mtanisamehe sana ambao mtakuwa mmeguswa na hali hii lakini nimeona niseme maana ni heri kusema kuliko kukaa kimya. Kwanini tusibadilike na kuwa na mtazamo wa kuendelea katika dunia hii ya sasa ambako tunaona kabisa kuwa mambo si marahisi kama ambavyo tulikuwa tunayaona hapo awali? Tunaingie kwenye mitihani tukitarajia kurushiwa majibu na wenzetu kwa faida ya nani hasa?

Entry filed under: maskani.

"Mwana wa Komba" mwenye jicho linalowaona watoto wa Mitaani wanablogu wanapoifufua JUWATA

4 Comments Add your own

 • 1. SaHaRa  |  January 15, 2007 at 9:53 am

  Mtu kama huyu hata huko kazini atakuwa anachungulia tu. Sasa sijui akirudi nyumbani atamfundisha nini mtoto wake kuhusu kujitegema na ‘the values of hard work?’

 • 2. simbadeo  |  January 15, 2007 at 7:28 pm

  Namuunga mkono Sahara. Ama kwa hakika aina hiyo ya watu (waibiaji nyakati za mitihani) ndio wanaotukwamisha katika kuleta maendeleo kwenye nchi hii. Watu wa namna hiyo wanachoweza kufanya vizuri ni kutozishughulisha akili zao katika kutafuta majibu kwa changamoto na matatizo wanayokabili.
  Wazazi wa aina hii ni kikwazo katika kupata Watanzania wanaofanya vizuri katika nyanja mbalimbali, maana huwezi kujitokeza katika kiwango cha pekee katika fani fulani bila kuisugua akili yako kwa ukali unaotakiwa.
  Kuna mtu wangu mmoja wa karibu huwa ananiambia kuwa heri mtu uchakaze nguo kuliko kuchakaza akili. Akili ikichakaa matokeo yake ni shida na superficiality katika maisha. Nadhani hili ni tatizo la nne kwa ukali katika nchi ya Tanzania ukiondoa Umaskini, UKIMWI na rushwa. Hebu tubadilike jamani?
  Hivi na wale wanaowapa majibu watu wa namna hii wanakuwa wanafikiri nini? Je, rushwa hii ina malipo gani?

 • 3. SIMON KITURURU  |  January 15, 2007 at 11:56 pm

  Hili tatizo ni sugu sana!Halafu , cha kusikitisha ni kuwa watu huamini kuwa ni ujanja. Watu , hupenda njia za mkato sana. Lakini tusivyobadilika sijui itatokea nini! Lakini hii si kwa Watanzania tu. Nilisoma na Wapakistani kadhaa wakati nafanya masters ya biashara ,Sweden. Walikuwa wanatupiana vijikaratasi na kuangaliziana mpaka inakuwa noma.Wakati nilivyokuwa nasoma bongo niliona watu wanavyoigiliziana lakini hawa Wapakistani niliowashuhudia wakifanya shughuli zao walikuwa wamevuka mpaka. Sijui walio soma huko Pakistani kama wanapitia hapa watasemaje kuhusu huko kwao.Si vizuri kuwajumlisha watu, lakini nikiwa nasoma chochote , popote na Mpakistani najihami.

 • 4. mwandani  |  January 17, 2007 at 1:59 pm

  Hili ni tatizo la kimadunia, udosini ndio kabisaa, wakati nikiwa delhi kulikuwa kukiwekwa walinzi vyooni, watu wakishaingia vyumba vya mitihani, walinzi wanapeksheni matanki yote, wakikuta vijikaratasi na vitabu vyenye fomula vyote wanataifisha, na kama mwanafunzi akiingia kujisaidia basi wanasikiliza sauti ya vikaratasi…

  Njia rahisi ya kumfanya mtu asiige pengine ni kupewa mtihani ukafanye nyumbani kama insha, uweke na reference zote ulizosoma. hiyo itamfanya yoyote asome tu, hakuna ujanja.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Trackback this post  |  Subscribe to the comments via RSS Feed


Blog Stats

 • 34,787 hits
January 2007
M T W T F S S
1234567
891011121314
15161718192021
22232425262728
293031