Archive for January 9, 2007

Tunapalilia Upumbavu?

“Hapa duniani wale wanaopenda kunyoosha mistari ndio wanaokumbana na matatizo zaidi, wewe pinda tu mistari kisha utaona mambo yanavyokunyookea” – aliyenukuliwa anahifadhiwa.

Naandika makala hii takriban dakika 48 toka nitoke katika chumba cha mtihani nilipokuwa nafanya mitihani yangu ya kumaliza semister ya kwanza kwa kozi ninayosomea ya sheria. Nimetoka kufanya mtihani wa CL (Communication Skills), baada ya ule niliofanya jana wa DS (Developmental Studies).

Naikumbuka nukuu niliyoanza nayo hapo juu baada ya kushuhudia yote yaliyojiri katika siku hizi mbili za kufanya mitihani niliyokwishaitaja na wakati naikumbuka pia najiuliza hivi hayo yaliyojiri katika chumba cha mtihani ni kwa faida ya nani hasa? Ni kwa faida yetu tuliokuwa katika mitihani hiyo au kwa faifa ya nani hasa?

Muda mfupi baada ya kutoka katika chumba cha mtihani (nikiwa wa kwanza), alitoka mwanafunzi mwenzangu mmoja na tambio kadhaa wa kadha kuhusu “atakavyopasua” (akimaanisha kufaulu) mitihani hiyo. Nilimwangalia nikamtupia swali kwamba “Je, katika kupasua huko ni kwa asilimia ngapi atakuwa ametumia uwezo wake na kwa kiasi gani atakuwa alisaidiwa?”

Nilimtupia swali hilo kutokana na pilika pilika nilizokuwa nazishuhudia akizifanya yeye na baadhi ya wanafunzi wenzangu katika kupasiana vijikaratasi sijui niviite vya majibu au vya nini maana sina uhakika kama kweli yalikuwa majibu. Ingawa inawezekana kila mmoja akawa na mtazamo wake kuhusu hili, lakini nitakiri kuwa kuna wakati pilika pilika hizo zilikuwa zikinikera kwa namna moja ama nyingine. Zilikuwa zinanikera kwasababu sikujua kuwa zilikuwa zinafanyika kwa faida ya nani na kwa ajili ya kumkomoa nani hasa.

Asilimia kubwa ya ninaosoma nao ni watu wazima tu, wenye familia zao, wenye watoto wao na ambao wanawasomesha watoto hao. Inawezekana kuwa wapo kati yao hawana utamaduni wa kufuatilia maendeleo ya watoto wao lakini ukweli unabakia pale pale kuwa wote kwa ujumla wanataka kila mwisho wa mhula mtoto awe amefanya vyema katika mitihani yake.

Kwa mzazi wa aina hii anapoamua kuingia darasani, akajilipia ada yeye mwenyewe kwa lengo la kujiendeleza kielimu, ni wazi kuwa katika kiwango chake haitarajiwi awe na akili sawa na za mtoto wake. Ni wazi kuwa anatakiwa kuhakikisha kuwa kila aina ya senti aliyoitumbukiza katika kujisomesha inampa uchungu wa kuhakikisha kuwa inambadilisha kimawazo, kifikra na kimtazamo. Sasa hapa ndipo ninapojiuliza hivi hizo pilika pilika kweli zinamwelekeo wa kutupeleka huko?

Naam, ni wazi kabisa kuwa mzazi wa namna hii sio tu kuwa anazidi kujidunisha zaidi badala ya kujielimisha zaidi, na haitarajiwi kuwa mzazi wa namna hii atasimama kidete kuhakikisha kuwa mtoto wake anakuwa na utaratibu mzuri wa kumwezesha kufaulu mitihani yake. Ndio!! Kama mzazi unakosa kujua kuwa wajibu wako katika kujiendeleza ni kuhakikisha kuwa unatumia uwezo wako kwa kiwango cha hali ya juu, ni vipi utajali kuwa mwanao amefaulu ama kwa kuhonga au kwa kuibia majibu kwa mwenzake?

Na katika hali kama hii tunajenga jamii ya namna gani hasa? Ni wazi kabisa kuwa moja kati ya mambo ambayo yamekuwa yakikwamisha kuendelea kwa uchumi wa taifa letu ni pamoja na kiwango duni cha elimu tulicho nacho. Ni wananchi ambao wanalalamikia hali hii, lakini sasa ni wananchi hao hao ambao hawafanyi juhudi za kuhakikisha kuwa kiwango hicho kinaboreka zaidi kwa kila mmoja kuhakikisha anatumia kikamilifu akili yake. Tunamlalamikia nani hasa ambaye atatukomboa katika hili?

Wengi wetu tumekuwa ama tukisoma kwa ajili ya vyeti au kwa ajili ya kupandishwa cheo kazini, lakini badi hata waliofanya hivyo hawajaweza kuwa na ufanisi wa kutosha katika majukumu yao, yawe ya kiserikali au ya kwenye mashirika binafsi. Usomaji huu kwa ajili ya vyeti na kupandishwa cheop ndio ambao umekuwa ukidumaza elimu yetu. Ndio umekuwa ukizalisha kizazi cha watu wasiokuwa na uchungu na maendeleo, kwasababu kwao kila jambo ni rahisi sana kama kuibia majibu ya mitihani.

Na hata mifumo yetu ya ajira imekuwa ya namna hiyo hiyo na huenda ndio maana hata usomaji umekuwa wa uelekeo huu. Ajira zinazotolewa kwa kuangalia wingi wa vyeti ni ajira zisizokuwa na mwelekeo wa kulikomboa taifa hili katika umasikini. Ni ajira ambazo zinawafanya watu wasiokuwa na sifa kukaa maofisini na kuishia kuitisha makongamano, warsha, semina, mikutano nk, wakishania kuwa huko ndio kupambana na umasikini.

Kwakweli sijui wa kumlaumu atakuwa nani ingawa kwa asilimia kubwa sana naamini ni kwetu sisi wenyewe, sababu tungali tunaelea katika kina kirefu cha upumbavu badala ya ujinga. Tumejijengea utamaduni wa kuwa kila kitu ni rahisi sana kama kukisema tu na ndio maana hatutaki kutumia akili zetu. Tumejidumaza kutokana na mifumo ambayo tuliikuta ambayo kama tukiwa na uchungu kama tunavyoilalamikia kweli tunatakiwa sisi ndio tusimame kidete kuhakikisha kuwa tunaibadilisha hali hiyo.

Mtanisamehe sana ambao mtakuwa mmeguswa na hali hii lakini nimeona niseme maana ni heri kusema kuliko kukaa kimya. Kwanini tusibadilike na kuwa na mtazamo wa kuendelea katika dunia hii ya sasa ambako tunaona kabisa kuwa mambo si marahisi kama ambavyo tulikuwa tunayaona hapo awali? Tunaingie kwenye mitihani tukitarajia kurushiwa majibu na wenzetu kwa faida ya nani hasa?

January 9, 2007 at 11:40 am 4 comments


Blog Stats

  • 34,787 hits
January 2007
M T W T F S S
1234567
891011121314
15161718192021
22232425262728
293031