Archive for January 3, 2007

BENKI ZETU NA SERA KWA WALALAHOI

Katika pita pita yangu mitaani hivi karibuni, nilikuta kikundi cha wananchi ambao walikuwa wakijadili masuala mbalimbali kuhusu hali halisi za kiuchumi walizonazo. Ingawa mjadala huo mwanzoni kabisa sikuwa nimevutika nao kwa kiasi cha kutosha, nilijikuta nikivutiwa nao baada ya mmoja kati ya washiriki wake alipoanza kuzungumzia kuwa Benki ni mmoja kati ya wakombozi wa walalahoi nchini Tanzania.

Hilo pekee halikuwa tatizo, ila jamaa mmoja alipoamua kumpinga mwenzake kuhusu hoja ya benki kuwa mkombozi. Sehemu ya maongezi ilikuwa kama ifuatavyo:-

Mwananchi A: Siku hizi kuna uwezeshwaji mkubwa lakini kiasi kwamba wakijipanga (sijui kwanini anajitenga), hata benki zinakopesha siku hizi.

Mwananchi B: Benki!! Benki hivi unajua maana ya benki wewe? Hizi benki zetu tafsiri yake ni kukusanya fedha za wananchi walio walalahoi kwa kisingizio cha kuwahifadhia na kuwapatia matajiri. Ndio maana unaona hata kasi yenyewe ya ukopeshaji ni kwa walio nacho, wa kawaida (wananchi), unabembelezwa kuweka fedha zako lakini kwenye kukopa masharti kibaaaaaao, sijui hatimiliki, sijui mambo gani tena, yaani ah!!
==========

Naam, hiyo ni sehemu ambayo ilinivuta zaidi, ikanikumbusha wakati fulani nilipokuwa nasafiri kutoka Dar es salaam kwenda Moshi, nilikuwa na jamaa nao walikuwa wakilalamika eti kuna benki ukiweka fedha zako unapata faida ya asilimia mbili tu (2%) na wakati huo huo ukienda kukopa katika benki hiyo utatakiwa kurejesha mkopo huo kwa riba ya asilimia kumi (10%), nane zaidi ya faida ya kuweka fedha zako.

Tukirejea katika ukweli halisi wa maisha tuliyo nayo hivi sasa, watendaji wa ngazi mbalimbali serikalini na hata kwenye chama hiki kilichoshika hatamu (sio utamu?), wamekuwa wakihanikiza juu ya wananchi kukopeshwa, kukopa au kujitafutia mitaji kwa ujumla ili kuweza kujiajiri au kujifanyia kazi zitakazowaletea tija katika kazi zao.

Ni kweli kuwa katika mazingira ya kawaida kabisa, msingi wa kupatia mtaji ni mkopo, na ndio maana hata serikali zetu zinakopa, lakini je, benki zetu nchini zimeshiriki kwa kiasi gani kuhakikisha kuwa wananchi wananufaika nazo? Ukiachilia mbali miaka ya karibuni ambako juhudi za kuunda vyama vya ushirika wa akiba na mikopo zimekuwa zikiongezeka ili kuwafanya wananchi hao kukopesheka, bado mchango wa mabenki yetu hapa nchini katika kuinua hali za wananchi umeendelea kuwa wa chini sana.

Masharti ya kupata mikopo, urasimu katika kushughulikia maombi yaliyowasilishwa, riba inayotakiwa wakati wa kuurejesha, uhakika wa masoko, miundombinu, elimu ya ujasiriamali, mabadiliko ya hali ya hewa na matatizo mengine kadhaa ni miongoni mwa sababu ambazo zimekuwa zikiathiri suala hili kwa kiasi kikubwa.

Sina hakika ikiwa benki zetu zimejikita katika kuhakikisha zinajiimarisha kwa kuwekeza kwa wananchi walio wa kawaida sana, ambapo zitatakiwa kuhakikisha zinashirikiana nazo katika kuboresha miundombinu ya mawasiliano na uchukuzi, masoko na hata pembejeo. Kwa maana hili ni jukumu ambalo hawawezi kulikwepa.

Wadadisi wa masuala ya kibenki na mahusiano ya jamii wamekuwa wakielezea kuwa ukuaji wa benki yoyote ile umekuwa ukitegemea zaidi ukuaji wa hali ya uchumi kwa wananchi walioko karibu nayo, hivyo ni jukumu la benki husika kuhakikisha kuwa inawekeza zaidi katika rasilimali watu. Sijui kwakweli kama hili limefikiwa kwa kiasi gani hapa nchini, lakini midhali bado hali za wanaoyazunguka mabenki yaliyopo hazijaweza kuwa nzuri, huo ni uthibitisho kuwa uwekezaji wa mabenki yetu katika rasilimali watu ni wa kiwango cha chini sana.

Kwa bahati mbaya sana ni kuwa mabenki mengi yameendelea kuishi kwa dhana ya kuwa uimara wao unatokana na wateja wakubwa wachache, na asilimia kubwa ndio uwekezaji wao ulikoelekea. Hili limekuwa likinipa shida kidogo kwasababu ninavyojua mimi ni kuwa kuwekeza kwa wale wengi walio na hali za chini ni sawa na kujijengea kizazi cha wateja wengi katika miaka ijayo. Inamaana hili halionekani au?

Natambua kuwa kunaweza kukawa na maelezo mengi sana katika hili kutoka kwa watu wa kwenye mabenki mbalimbali, na bilashaka ninayapenda sana maelezo haya yaje hapa ili tuweze kuelimishana na kupeana changamoto, lakini kwa namna yoyote ile bado hali ingali inabaki kuwa kasi ya benki zetu hapa nchini katika kujenga kizazi kitakachozifanya ziwe benki kubwa sana ndani na nje ya nchi, iko chini sana na kuwa mbinu zinahitajika katika hili.

Tuwaone hawa walalahoi kama sehemu muhimu sana kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi, ukuaji wa benki hizi na ukuaji wa huduma na ubora wa maisha, kwa kuona namna ambavyo wanaweza kukopeshwa kwa masharti ambayo yanaendana na hadhi zao. Kuweka masharti ambayo ni vigumu kwa wao kuyafikia tayari ndio kunakosababisha uwepo wa dhana ya kuwa zinachukua fedha zao na kisha kuwakopesha wenye nazo.

Unaweka mashartyi kwamfano ya kuwa sijui na hatimiliki ya kiwanja wakati halmashauri zenyewe zinazotakiwa kupima viwanja hivyo zinashindwa kutimiza wajibu wake hadi kurejesha fedha za kazi hiyo serikali kuu, unadhani huyo mwananchi lini atakuwa wa kukopeshwa? Na huko si kumnyima haki yake kwa kosa au udhaifu wa mtu mwingine?

Naomba nikaribishe changamoto mbalimbali kuhusu hali hii na ikiwa watajitokeza wanataaluma ya benki kwa ajili ya kujadili mjadala huu naamiini tutafanikisha wajibu wetu katika kujenga taifa lililo na wananchi wasiolia njaa kila kukicha

Alamsiki.

tukijipanga

January 3, 2007 at 1:47 pm Leave a comment


Blog Stats

  • 35,058 hits
January 2007
M T W T F S S
1234567
891011121314
15161718192021
22232425262728
293031