Archive for January, 2007

Kazi ni Kazi tu bora mkono kwenda kinywani 

January 30, 2007 at 12:04 pm Leave a comment

KWANINI SIUPENDI MUSWADA HUO?

“Democracy needs more free speech, for even the speech of foolish people is valuable if it serves to guarantee the right of wise to talk”
– David Cushman Coyle –
==== xxx ====xxx ==== xxx ====

Baada ya kuuelezea kwa ufupi jinsi maudhui yake yalivyo katika makala zangu mbili zilizotangulia, (zisome kwa kubonyeza hapa na hapa, kwa wale waliozikosa), leo hii nimeona kwanza kabla sijaendelea na kuuchambua muswada wenyewe, basi niseme wazi kwanini siupendi huu muswada. na Zifuatazo ndio sababu kuu na za msingi kwangu, zinazonifanya nisiupende muswada wenyewe;-

1. Muswada unampa Waziri mamlaka ya kuchagua sura au vifungu ambavyo anataka vitumike kwa wakati fulani. Kwanini vifungu vyoter visitumike kwa pamoja?

2. Kipengele cha usiri katika muswada huu kinavunja kanuni za utawala bora kuruhusu serikali na taasisi zake kutotoa habari bila vikwazo, mfano shughuli za baraza la mawaziri na michakato ya utungaji sera.

3. Muswada huu unajumuisha sheria za kikandamizaji ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kwa muda mrefu ikiwemo sheria ya magazeti (1976) na ile ya utangazaji (1993)

4. Muswada unampa Waziri mamlaka ya kuzuia habari kwa kisingizio cha kuathiri maslahi ya umma, ulinzi na usalama wa taifa bila kuweka bayana mambo hayo.

5. Uhuru wa habari uliomo katika muswada huo hauendani na kanuni za kimataifa za uhuru wa kupata habari.

6. Muswada huu unaruhusu kuibuka kwa genge la mafisadi kwa kasi mpya, nguvu mpya na ari mpya pia.

7. Unazuia habari muhimu za maendeleo ya jamii, sanjari na zile za utawala mbovu na ulaji wa fedha za wananchi kinyume na makusudo ya wanaotozwa kodi.

8. Utaratibu unaotamkwa hapa haumsaidii, kumhakikishia na kumlinda mwananchi wa kawaida katika kupata taarifa.

9. Muswada huu haumjali mwananchi wa kawaida kama mdau na sehemu muhimu ya habari.

10. Muswada huu unaiweka rehani taaluma ya habari kwani hauwahakikishii wanahabari na hususan waandishi usalama na uhuru wa kufanya kazi zao.

11. Muswada huu unakataza kuandikwa kwa habari zozote zenye kuhusiana na biashara za kimataifa.

January 29, 2007 at 3:29 pm 3 comments

Uhuru wa habari au uhuru wa viongozi mafisadi?

Nianze kwa kukumbuka moja ya masharti ambayo, nchi zilizotia saini Mkataba wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, zinatakiwa kuyatimiza, ambalo ni lile la nchi hizo kuhakikisha kuwa kila sheria inayotungwa (katika nchi husika), inakuwa ni yenye uelekeo wa kuzilinda na kuzitetea zaidi haki za binadamu na si kuzikandamiza kwa namna yoyote ile” Hivi Tanzania si moja kati ya nchi hizo?

Nimeanza kwa kumbukumbu na swali hilo hapo juu, wakati nikiwa naelekea kutimiza ahadi niliyowapatia wasomaji wangu katika makala iliyotangulia, ahadi ya kuzama kwa undani kidogo (na kwa mtazamo wangu), katika kujadili hiki kinachoitwa Muswada wa Sheria ya Uhuru wa Habari wa 2006, nchini Tanzania.

Baada ya kuupitia, kuusoma na kuujadili kwa kiwango changu, jambo la mwisho kabisa nililoweza kujiwa nalo kichwani mwangu ni kuwa muswada huu kwakweli umekaa vibaya tena vibaya sana. Haufai, haustahili kuwepo nchini Tanzania katika zama hizi na huenda haustahili kuwepo sehenmu yoyote ile duniani. Labda Ujerumani ya enzi za Hitler, na Uganda ya Idd Amin.

Ni muswada ambao umejaa mapungufu mengi kuliko mazuri yake, muswada ambao hauhitaji mtaalamu wa aina yoyote ile kujua kuwa umekaa vibaya, isipokuwa wanafiki wachache ambao mwandishi mmoja aliandika katika makala yake kuwa, baada ya kuona wamehodhi siasa na akili za baadhi ya watawala, sasa wanataka kuhodhi na akili za Watanzania wote.

Ni muswada ambao kwakweli ulinifanya nijiulize kama kweli walioshiriki kuishauri serikali ili kuuandaa, kuuandika na sasa kufikiria kuwa unastahili kuwasilishwa bungeni muswada huo wanaelewa kweli maana ya kitu UHURU? Kwasababu muswada huu hauna chembe yoyote ile ya hicho kitu kinaitwa uhuru ndani yake.

Labda nianze kwa kuangalia kile kinachoitwa Uhuru ndani ya muswada huo kama kweli kipo, na wakati tukiwa tunajadili hili, ningependa tuwe na mambo mawili ya muhumu sana katika fikra zetu, la kwanza likiwa ni Ibara ya 18, ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo inazungumzia juu ya haki ya kila mwananchi kupata na kutoa habari, bila kuingiliwa uhuru wake wa kufanya hivyo.

Jambo la pili ni kuwa, Tanzania ikipitisha muswada huu, itakuwa nchi ya nne ya kiafrika kuwa na sheria ya namna hii baada ya nchi za Afrika Kusini, Zimbabwe (ambako imeshaleta matatizo makubwa sana), na jirani zetu Uganda, ambako hivi karibuni kulikuwa na kesi ya aina yake kuhusu hiki kinachoitwa uhuru wa habari.

Kwa taarifa tu ni kuwa kesi hii ya watendaji wawili wa ngazi ya juu katika gazeti la The Monitor, Mhariri (Charles Onyango)na Mwandishi mwandamizi (Andrew Mujuni), dhidi ya serikali ya Uganda, iliamuliwa na Mahakama ya Rufaa ya Uganda (Supreme Court), kwa kauli au ufafanuzi ufuatao:-

” Haki ya uhuru wa kujieleza na utangazaji wa habari hauishii kwa mawazo, maoni au habari za kweli tu, bali unahusu pia habari zisizo za kweli au zisizo sahihi kwani kile ambacho kinaweza kuonekana si cha kweli kinaweza kugeuka ukweli iwapo patatolewa nafasi ya kusikilizwa “

Nikirejea katika muswada wenyewe sasa, ni kwamba muswada huu umejaa vipengele ambavyo vinalenga zaidi katika kulinda mafisadi, wala rushwa, viongozi wabovu, waongo na walafi wakubwa wa mali za umma, kuliko kuimarisha Tanzania kama nchi ambayo inakubaliana na mfumo wa Demokrasia kama nguzo muhimu ya kuleta maendeleo endelevu.

Muswada huu unaainisha kuwa kile kitakachostahili kuitwa habari na kustahili kupewa ama kuchukuliwa na mwandishi wa habari, ni makabrasha au nyaraka zilizoko katika masijala ya wazi au ambayo yameandaliwa na taasisi husika kwa ajili ya kuuzwa ama kusambazwa kwa wanajamii (mnaelewa vitu vinaitwa vipeperushi?). na baada ya hapo, mwandishi kuandika kile kilichomo ndani ya makabrasha hayo tu na si zaidi ya hapo.

Ikiwa nimeletewa taarifa kuwa barabara ya kwenda kwetu upareni imejengwa kwa kiwango cha lami kwa mujibu wa kabrasha la wizara, sitakiwi kusema zaidi ya hapo, hata kama wakati nasoma taarifa hiyo nitakuwa nimekwama pale Kikweni kwasababu ya matope barabarani. Na nikiandika hivyo ni kosa, tena la jinai. Huo uhuru hapa ni upi tunaomaanisha? Uhuru wa Viongozi kusema uongo kisha tuwakubalie tu? Hapana.

Muswada huu unamtaka mwenye kuhitaji taarifa zozote zile kutoka taasisi yoyote ile (sijaona mahali wamegusia sekta binafsi lakini), kuandika barua ya kuomba kabrasha au waraka wenye kile anachokitafuta, tena akiainisha kuwa anachokitaka kiko sehemu gani. Majibu yake yanaweza kuchukua hadi siku 21 na sio lazima yawe na kukubaliwa, kwasababu unaweza kuambiwa kuwa kile unachokitaka ni siri ya ‘Sirikali’.

na ikiwa utakuwa na bahati zaidi, basi utakaribishwa mezani kwa mheshimiwa mwenye tumbo lake kuuuubwa, akikuchekea chekea na faili ulilolitaka likiwa mbele yake, kisha atatumia nguvu yake nyingine anayopewa na sheria hii, ya kunyofoa karatasi/taarifa ambazo anaona zinagusa ‘maslahi ya umma’.

Kama ulifuata hotuba ya kiongozi fulani yenye kurasa kumi kwa mfano, jamaa anaweza (kwa mujibu wa sheria hii), akanyofoa kuanzia ukurasa wa pili hadi wa tisa, kwa kisingizio kuwa zinagusa maslahi ya umma, kisha ukapewa ukurasa wa kwanza wenye utangulizi na majina kibaaaao ya waongo waliokuwa wamehudhuria sehemu hotuba ilikosomwa, na ule wa mwisho wenye nawashukuruni kwa kunisikiliza. Uhh!!

Ikiwa ndugu yangu utabahatika kupata jalada zima kama ulivyokuwa umeliomba, lina kurasa zote, usije ukajidai kuwa ni mjanja sana, kwasababu inawezekana kabisa kuwa huenda ndio umechimbiwa kaburi lako ukiwa unajiona ili uzikwe mzima mzima, ama ujikaange mwenyewe kama samaki Pweza.

Kwasababu, sheria hii imemtega mwana habari wazi wazi kwa kumpa mamlaka mheshimiwa mwenye dhamana ya habari kuweka pia usiri katika kabrasha/waraka wowote ule ikibidi (nadhani walimaanisha akijisikia kwakweli, maana kama ni kubidi ilibidi wautupilie mbali sababu tumeshaona haufai na wameshalalamikiwa). Tujiulize, hivi kuna uadilifu katika viongozi wetu kweli?

Kwasababu hata pale walipoongea jambo leo, kesho likaripotiwa na vyombo vya habari kisha wakajiona kuwa walitafsiriwa (sio kuandikwa) na umma, wamekuwa wakikurupuka ama kukanusha na kutishia kushitaki vyombo vilivyoandika hivyo. Bahati nzuri tu ni kuwa kwa sasa kidogo sheria zetu za kuchechemea nazo zimekuwa zikisaidia, lakini kwa muswada huu kitakachojiri ni hiki.

Kwamba leo utafika na kupewa risala na kiongozi baada ya kuiombea siku zaidi ya 21 zilizopita, kisha utaenda kuandika habari kulingana na waraka ule kama sheria ilivyotangulia kubainisha, lakini kesho wananchi wakija juu kuhusu taarifa hiyo na kuanza kuhoji, Waziri anaweza kuamua tu kuwa agionge muhuri wa usiri katika lile kabrasha, na kisha mwandishi utaenda kuulizwa chanzo chako ukikutwa na waraka ule tayari uko mavini.

Ndio, si umekutwa na waraka wa siri wa serikali? Na waziri si anakwambia tu kwasababu wananchi walishaanza kuhoji kuhusu habari uliyoandika na kwamba ilishahatarisha usalama na maslahi ya umma? Ana mamlaka hayo kwa mujibu wa muswada huu ikiwa utapita na kuwa sheria. Katika mfumo huu, kila kukicha waandishi wa habari watatakiwa wawe wanaandika kile wanachopewa kimaandishi na viongozi.

Hivi, katika mfumo huu ni lini tunatarajia kuwa tutaambiwa fulani kala fedha za umma? Unajua tatizo kubwa la mifumo ya kiutendaji katika utawala ni kwamba ni ya kimuingiliano zaidi kuliko sehemu nyingine. Kwa maana ya kwamba hata inapotokea ulaji rushwa katika jambo fulani, si wizara husika tu ambayo itakuwa imeshiriki, bali karibu kila wizara kwasababu suala la matumizi ya fedha za umma ni suala la Baraza la Mawaziri.

Kwa maana hii ni kwamba hatutarajii kuwa wizara fulani siku moja itatoa tamko la kuituhumu wizara fulani kwasababu ya ufisadi, rushwa na wizi unaofanywa na viongozi wake. Kwa mantiki hii, Watanzania wanatakiwa kuwa watu wa kuambiwa leo tumekusanya shilingi 20 waseme ndio wazee. Na katika hizo 20 tumetumia 55 zingine zikiwa tumekopa kwahiyo deni letu limekua nje, nao waitikie tawile wazee. Huu ni uhuni, wizi na upuuzi wa hali ya juu.

Huu ni ujenzi wa genge la viongozi matapeli, wezi, wala rushwa na madikteta, kwakuwa wanajua kuwa hakuna wa kuanika siri zao zikajulikana kwa wananchi na hakuna atakayewezesha mabaya yao kujulikana kwa jamii inayowazunguka hivyo wataendelea tu kula raha, huku wakijibadilishia hata sheria waendelee kuwepo madarakani kinyemela bila wananchi kujua.

Hii ni rasharasha tu ya utapeli unaoandaliwa kupitia muswada huu, hii ni mwendelezo tu wa makala kadhaa nilizoahidi kuziandika kwa ajili ya kuujadili muswada huu. Wakati tukiwa tunajiandaa kwa ajili ya kuendelea kuona mapungufu nmengine, ni vyema tukashiriki kujadili haya na ikiwezekana kuyatolea tamko.

January 25, 2007 at 1:43 pm 4 comments

moto haufunikwi kwa makaratasi

IKIWA imetimiza mwaka mmoja na mwezi mmoja kamili toka ilipoingia madarakani kufuatia uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, Serikali ya awamu ya nne ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya kamanda wake mkuu mheshimiwa JK, imekuwa na kipindi kilicho kigumu zaidi kuliko wengi wetu tulivyo na tunavyodhani.

Achilia mbali matukio ya kutisha ya ujambazi na uporaji wa fedha yaliyoukaribisha utawala huu katika zama zake za kuingia Ikulu, achilia mbali tatizo la umeme, maji, njaa, ukame na mengine kadha wa kadha; haya kwangu yanaweza kuwa yalikuwa ni kama rasharasha tu za mvua ambazo sasa tunaanza kuziona. Mvua za kutokujiamini, mvua za kusahau historia, kukimbia vivuli vyetu sisi wenyewe na kuanza kujikataa kule tulikotoka.

Ni katika kipindi hiki ambapo tumesikia viongozi wetu wakitueleza kuwa matatizo yanayowakabili waliyarithi kwahiyo wasitupiwe lawama sana. Ni katika kipindi hiki tumesikia hadithi ile ile ya kuwa majina ya wala rushwa na vigogo wauza unga yako miononi mwa amirijeshi wetu mkuu, lakini hayawekwi wazi. Na nzuri au pale mchezo unapokuwa mtamu ni pale unapokumbuka kuwa wakati serikali hii inaingia ilijinadi kuyafanya yote hayo kwa kasi, ari na nguvu mpya.

Kulikuwa na kauli mbiu za ‘Kasi na Viwango’, kulikuwa na kauli mbiu za Ari mpya, Nguvu mpya na Kasi mpya’, ambazo zote hizi zilisherehesha usimikwaji wa serikali hii madarakani. Hivi sasa tukiwa tunamaliza mwaka na mwezi mmoja, hivi ni tatizo lipi hasa lililokubwa ambalo limeshughulikiwa kwa vishereheshaji hivyo?

Matatizo ya wafugaji karibu kila kona ya nchi yameendelea kuitafuna serikali hii kwa muda wote huo, huku tukiendelea kuambulia matamko ambayo uzoefu wetu huko nyuma unaonyesha kuwa kufanyiwa kwake kazi ni jambo gumu sana kuliko kuyapatia sababu na visingizio vya kutokuyatimiza. Suala la umeme linaweza kuonekana kama limefikia tamati kwasababu unasemekana kuwa upo wa kutosha, lakini kwangu mimi tatizo limekuwa kubwa zaidi kwasababu bei imezidi kupanda, licha ya kuwa hata iliyokuwepo ilikuwa inalalamikiwa kuwa kubwa.

Bado wala rushwa wanaendelea kuitesa nchi hii huku wakisababisha walalahoi kukosa haki zao za msingi kwa kukosa ‘mashati ya mikono mirefu’, watoto wetu wangali wamelundikana mitaani maana hawana ajira, mitaji wala fedha za kujissomeshea achilia mbali wale ambao licha ya kuumiza akili zao kwa ajili ya kujiandalia maisha ya baadae, wamekosa nafasi hata ya kuingia sekondari.

Biashara ya madawa ya kulevya bado ni tatizo kubwa sana, urasimu katika baadhi ya sehemu na hali ya uchumi wa nchi kuendelea kuwa ya kusuasua ni changamoto ambazo bado tunazo na kwakweli jitihada za kuyafanyia kazi zikiwa zinaonekana kuwa za maneno zaidi kuliko uhalisia wenyewe.

Kati ya haya yote, hakuna hata moja ambalo uongozi wa sasa haukuwa ukiyajua toka ulipokuwa unafanya jitihada za kuingia madarakani. Na ni haya na mengine kadha wa kadha ambayo yalitumiwa kama chambo cha kuuwezesha kuingia madarakani. Ni haya na mengine mengi ambayo tulikuwa tunaahidiwa kuwa yatafanyiwa kazi kwa ari, nguvu na kasi mpya tena kwa viwango. Na ndio ahadi hizo hizo ambazo tulitarajia kuwa zitakuwa zimeshaanza kuzaa matunda katika kipindi hiki.

Kimsingi sina nia ya kusema kuwa utawala uliopo haujafanya lolote lile, laa. Isipokuwa kile walichokitenda ni KWA UWEZO WAO na sio kulingana na AHADI ZAO na namna walivyozitoa, kwasababu walipokuwa wakizitoa walikuwa wakizitoa katika namna ambayo iliwafanya mamilioni ya Watanzania kuamini kuwa sasa Yesu, anarejea kuwaokoa Watanzania ndani ya muda mfupi sana.

Hili lilikuwa moja kati ya makosa makubwa sana kuwahi kufanywa na viongozi hawa wakati walipokuwa wanajinadi. Sidhani kama walikuwa wanatambua kuwa wananchi waliokuwa wakiwaahidi mambo hayo, wangekuja kuwahukumu kulingana na staili yao ya utoaji ahadi na kile watakachokuwa wakikifanya.

Kwa hakika nashawishika kuamini kuwa hili walikuwa ama hawalitambui au walikuwa wakilitambua lakini walidhania kuwa Watanzania pengine hawana uwezo wa kutumia zile ahadi zao kama kigezo cha kuwapima. Na hili bilashaka ndilo linalojitokeza hivi sasa ambapo tunaona baada ya wao kuanza kuona hali hiyo, juhudi zimekuwa kuanza kutafuta njia za kujinasua.

Makala yangu hii, ni sehemu ya kwanza ya mfululizo wa makala kadhaa ambazo nitakuwa nikiwaletea mahususi kwa ajili ya kujadili hiki kinachoitwa Muswada wa Sheria ya Uhuru wa habari nchini. Sina hakika kama upo kwenye mtandao fulani kwa sasa kiasi cha wengi wa wasomaji wangu kuweza kuusoma, na pia sidhani kama wengi wetu tumeshauona na kuupitia, lakini nitajitahidi sana kwa kadiri niwezavyo kuuelezea vile nilivyouona na tuupitie kwa pamoja.

MOTO HAUFUNIKWI KWA MAKARATASI ILI USIENEE

January 22, 2007 at 6:55 pm Leave a comment

wanablogu wanapoifufua JUWATA

Kuna baadhi ya nyakati binadamu hukosa maneno muafaka kuweza kuelezea hisia za dhati zilizoko ndani ya nafsi yake. Nakumbwa na hali hii hivi sasa wakati ninapoona kasi ya kuelekea kuwa na Jumuiya ya Wana-Blogu Tanzania.

Furaha yangu inatokana na mambo mawili makuu la kwanza likiwa kasi yenyewe katika kulifanikisha jambo hili na vile vile ujio wa jambo lenyewe kuwa umetokea katika kipindi ambacho jamii hii ya mtandaoni huenda ikawa inaandaliwa mazingira ya kuwa mkombozi wa kweli wa Watanzania. (Kwa wanaojua kinachojiri Tanzania juu ya kizaazaa cha muswada wa Sheria ya Uhuru wa vyombo vya habari wanaelewa namaanisha nini, nitaanza kulizungumza hili muda si mrefu).

Kwa kila aliyehudhuria mkutano wetu ule wa kwanza na wa kihistoria wa Novemba 18, naamini atakuwa anakumbuka maamuzi kadhaa ambayo yalifikiwa katika mkutano ule, kubwa kabisa likiwa hili la kuunda Jumuiya yetu.

Inapendeza kuona maendeleo ya mchakato wa kuundwa kwa Jumuiya hii yanavyokwenda kwa kasi sana. Tayari tuna Blogi maalum kwa ajili ya kuendesha mijadala ya ukamilishwaji wa Jumuiya hiyo, na sio tu kuwa Blogi hiyo imeshaanza kufanya kazi, bali imeshafanikisha ajenda ya kwanza kabisa na muhimu katika kukamilisha Jumuiya yetu, ajenda ambayo ilikuwa ni JINA la Jumuiya.

Tembelea Blogi hiyo kwa kubofya hapa, soma makala ya utangulizi & mjadala wa kwanza ndani ya blogi hiyo hapa, fahamu kilichoamuliwa katika mjadala wa kuhusu jina la Jumuiya kwa kubofya hapa, na soma mjadala wa sasa ambao unaendelea na kisha kuuchangia kwa kubofya hapa. Kumbuka muda wa kujadili kila mada ni wiki moja tu, hivyo wahi kuweka maoni yako.

Shukrani, pongezi na kila aina ya dua zangu zitaelekea kwa Da’Mija (mwanamke wa shoka huyu), mtani wangu Ndesanjo na kakangu Jeff kwa juhudi ambazo wamekuwa wakizifanya katika kufanikisha hili.

Shukrani za pekee pia nazielekeza kwa Ras Luihamu (sijui yeye hatumii mishikaki au vipi maana kuna ma-Ras hapa Mbeya, wanafakamia mishikaki kama hawana akili vile), ambaye amekuwa mtu wa changamoto mara zote karibu katika kila hoja, bila kumsahau mpiganaji Gerald Shuma, kwa juhudi zenu, michango yenu na changamoto mbalimbali. Jumuiya isiyokuwa na fikra kinzani haiwezi kuwa Jumuiya ya kujivunia.

Kwa wanablogi walio hai (wenye blogi hivi sasa), wale wanaotarajia kuwa nazo (ni rahisi mkisoma hapa), na kwa wasionazo na wala wasiokuwa na mawazo ya kuwa nazo, nyote kwa ujumla mchango wenu unahitajika sana katika kufanikisha zoezi hili. Kwa niaba ya wenzagu wote walioteuliwa kuratibu (sio kuongoza) zoezi hili, napenda kuwaomba rasmi kushiriki katika mjadala huu kwa kutupa maoni yenu yatakayoweza kutusaidia kuwa na Jumuiya imara, yenye uelekeo wa kumkomboa kila Mtanzania. Shitiki kwa kubofya hapa.

January 22, 2007 at 1:07 pm Leave a comment

Tunapalilia Upumbavu?

“Hapa duniani wale wanaopenda kunyoosha mistari ndio wanaokumbana na matatizo zaidi, wewe pinda tu mistari kisha utaona mambo yanavyokunyookea” – aliyenukuliwa anahifadhiwa.

Naandika makala hii takriban dakika 48 toka nitoke katika chumba cha mtihani nilipokuwa nafanya mitihani yangu ya kumaliza semister ya kwanza kwa kozi ninayosomea ya sheria. Nimetoka kufanya mtihani wa CL (Communication Skills), baada ya ule niliofanya jana wa DS (Developmental Studies).

Naikumbuka nukuu niliyoanza nayo hapo juu baada ya kushuhudia yote yaliyojiri katika siku hizi mbili za kufanya mitihani niliyokwishaitaja na wakati naikumbuka pia najiuliza hivi hayo yaliyojiri katika chumba cha mtihani ni kwa faida ya nani hasa? Ni kwa faida yetu tuliokuwa katika mitihani hiyo au kwa faifa ya nani hasa?

Muda mfupi baada ya kutoka katika chumba cha mtihani (nikiwa wa kwanza), alitoka mwanafunzi mwenzangu mmoja na tambio kadhaa wa kadha kuhusu “atakavyopasua” (akimaanisha kufaulu) mitihani hiyo. Nilimwangalia nikamtupia swali kwamba “Je, katika kupasua huko ni kwa asilimia ngapi atakuwa ametumia uwezo wake na kwa kiasi gani atakuwa alisaidiwa?”

Nilimtupia swali hilo kutokana na pilika pilika nilizokuwa nazishuhudia akizifanya yeye na baadhi ya wanafunzi wenzangu katika kupasiana vijikaratasi sijui niviite vya majibu au vya nini maana sina uhakika kama kweli yalikuwa majibu. Ingawa inawezekana kila mmoja akawa na mtazamo wake kuhusu hili, lakini nitakiri kuwa kuna wakati pilika pilika hizo zilikuwa zikinikera kwa namna moja ama nyingine. Zilikuwa zinanikera kwasababu sikujua kuwa zilikuwa zinafanyika kwa faida ya nani na kwa ajili ya kumkomoa nani hasa.

Asilimia kubwa ya ninaosoma nao ni watu wazima tu, wenye familia zao, wenye watoto wao na ambao wanawasomesha watoto hao. Inawezekana kuwa wapo kati yao hawana utamaduni wa kufuatilia maendeleo ya watoto wao lakini ukweli unabakia pale pale kuwa wote kwa ujumla wanataka kila mwisho wa mhula mtoto awe amefanya vyema katika mitihani yake.

Kwa mzazi wa aina hii anapoamua kuingia darasani, akajilipia ada yeye mwenyewe kwa lengo la kujiendeleza kielimu, ni wazi kuwa katika kiwango chake haitarajiwi awe na akili sawa na za mtoto wake. Ni wazi kuwa anatakiwa kuhakikisha kuwa kila aina ya senti aliyoitumbukiza katika kujisomesha inampa uchungu wa kuhakikisha kuwa inambadilisha kimawazo, kifikra na kimtazamo. Sasa hapa ndipo ninapojiuliza hivi hizo pilika pilika kweli zinamwelekeo wa kutupeleka huko?

Naam, ni wazi kabisa kuwa mzazi wa namna hii sio tu kuwa anazidi kujidunisha zaidi badala ya kujielimisha zaidi, na haitarajiwi kuwa mzazi wa namna hii atasimama kidete kuhakikisha kuwa mtoto wake anakuwa na utaratibu mzuri wa kumwezesha kufaulu mitihani yake. Ndio!! Kama mzazi unakosa kujua kuwa wajibu wako katika kujiendeleza ni kuhakikisha kuwa unatumia uwezo wako kwa kiwango cha hali ya juu, ni vipi utajali kuwa mwanao amefaulu ama kwa kuhonga au kwa kuibia majibu kwa mwenzake?

Na katika hali kama hii tunajenga jamii ya namna gani hasa? Ni wazi kabisa kuwa moja kati ya mambo ambayo yamekuwa yakikwamisha kuendelea kwa uchumi wa taifa letu ni pamoja na kiwango duni cha elimu tulicho nacho. Ni wananchi ambao wanalalamikia hali hii, lakini sasa ni wananchi hao hao ambao hawafanyi juhudi za kuhakikisha kuwa kiwango hicho kinaboreka zaidi kwa kila mmoja kuhakikisha anatumia kikamilifu akili yake. Tunamlalamikia nani hasa ambaye atatukomboa katika hili?

Wengi wetu tumekuwa ama tukisoma kwa ajili ya vyeti au kwa ajili ya kupandishwa cheo kazini, lakini badi hata waliofanya hivyo hawajaweza kuwa na ufanisi wa kutosha katika majukumu yao, yawe ya kiserikali au ya kwenye mashirika binafsi. Usomaji huu kwa ajili ya vyeti na kupandishwa cheop ndio ambao umekuwa ukidumaza elimu yetu. Ndio umekuwa ukizalisha kizazi cha watu wasiokuwa na uchungu na maendeleo, kwasababu kwao kila jambo ni rahisi sana kama kuibia majibu ya mitihani.

Na hata mifumo yetu ya ajira imekuwa ya namna hiyo hiyo na huenda ndio maana hata usomaji umekuwa wa uelekeo huu. Ajira zinazotolewa kwa kuangalia wingi wa vyeti ni ajira zisizokuwa na mwelekeo wa kulikomboa taifa hili katika umasikini. Ni ajira ambazo zinawafanya watu wasiokuwa na sifa kukaa maofisini na kuishia kuitisha makongamano, warsha, semina, mikutano nk, wakishania kuwa huko ndio kupambana na umasikini.

Kwakweli sijui wa kumlaumu atakuwa nani ingawa kwa asilimia kubwa sana naamini ni kwetu sisi wenyewe, sababu tungali tunaelea katika kina kirefu cha upumbavu badala ya ujinga. Tumejijengea utamaduni wa kuwa kila kitu ni rahisi sana kama kukisema tu na ndio maana hatutaki kutumia akili zetu. Tumejidumaza kutokana na mifumo ambayo tuliikuta ambayo kama tukiwa na uchungu kama tunavyoilalamikia kweli tunatakiwa sisi ndio tusimame kidete kuhakikisha kuwa tunaibadilisha hali hiyo.

Mtanisamehe sana ambao mtakuwa mmeguswa na hali hii lakini nimeona niseme maana ni heri kusema kuliko kukaa kimya. Kwanini tusibadilike na kuwa na mtazamo wa kuendelea katika dunia hii ya sasa ambako tunaona kabisa kuwa mambo si marahisi kama ambavyo tulikuwa tunayaona hapo awali? Tunaingie kwenye mitihani tukitarajia kurushiwa majibu na wenzetu kwa faida ya nani hasa?

January 9, 2007 at 11:40 am 4 comments

"Mwana wa Komba" mwenye jicho linalowaona watoto wa Mitaani

Nadhani ndio wale wale wa kule mahali hawa maana jina tu linajieleza (nadhani Ndesanjo unaelewa namaanisha wa wapi). Huyu ni dada yetu Anna Komba a.k.a Mwana wa Komba, ambaye ameamua kujiunga katika mtandao wa Wanablogi wa Kitanzania. Ilikuwa kama utani vile nilikutana naye mtandaoni siku hiyo tukaongea mambo kadhaa akaniomba nimsaidie kufungua blogi nami nikafanya hivyo, nikadhani itamchukua muda kufikiria “Atoke Vipi” lakini kumbe mwenyewe alikuwa kajipanga anasubiri tu aone njia. Dada Anna ambaye blogi yake ameiita Jicho lake Mtaani ameanza kwa kugusia tatizo sugu la watoto wa mitaani, ingawa siamini kama kuna watoto wa mitaani kweli (nitasema siku nyingine). Mtembelee na umkaribishe kwa kubofya hapa.

January 8, 2007 at 5:12 pm Leave a comment

Older Posts


Blog Stats

  • 34,787 hits
January 2007
M T W T F S S
1234567
891011121314
15161718192021
22232425262728
293031