Archive for December 29, 2006

Tuna UHURU lakini mbona hatuko Huru

Uzuri wa maisha na hasa kwa watu kama mimi ni kuwa falsafa ya KUCHELEWA huwa inatupitia mbali sana ndio maana hatuoni taabu kuanza kuzungumzia mambo ambayo kwa wengine tunaweza kuonekana tulishachelewa kuyazungumzia. Kwanza kuchelewa katika maisha ni nini hasa? Unawahi kwenda wapi katika maisha kwani? Anyway, tuyaache hayo tuingie katika somo la leo.

Hivi karibuni, Tanzania ilisherehekea (Sio kuadhimisha), kutimiza kwake miaka 45 toka ilipojikomboa katika ukoloni wa mwingereza. Kwakweli sherehe za mwaka huu zilifana sana na atakayekataa kwakweli hatunabudi kumwangalia kwa jicho la umakini maana hatutakii mema.

Ndege zilizungyuka angali kwa mbwembwe nyingi tofauti na hata siku tulipopata uhuru. Kulikuwa na idadi ya kutosha tu ya waliohudhuria sherehe zile pengine kuliko hata siku tuliyoutwaa uhuru huo na kwa kweli kulikuwa na kila kitu ambacho hakika kilijiri kwa mara ya kwanza. Hata maandalizi yake yalikuwa tofauti na miaka iliyopita.

Watu safari hii walishirikishwa (sio kushurutishwa?) kuchangia sherehe za miaka 45 ya uhuru wao (ah!! si ajabu lakini maana siku hizi miongoni mwa pati zinazoongoza kwa kuchangiwa michango mikubwa ni zile za kuizaliwa akina fulani) Na watu walichanga, wakachanga weee, hadi mafanikio yale tuliyoyashuhudia kwenye luninga siku ile. Kwa walioweza kuhudhuria au kuona mambo makubwa yaliyojiri siku ile, sinashaka waliondoka na picha ambayo haielezeki kwa ubora na uzuri wake. lakini Je, ni kweli tulionyesha picha yetu halisi?

Hayati baba wa taifa hili ambaye pia ndiye aliyetutoa huko mikononi mwa wakoloni na leo hii tukijiita kuwa tuko huru, Mwl. J. K. Nyerere, alikuwa akiamini kuwa “Uhuru wa mwanadamu ni uhuru ikiwa mtu huyo anakuwa huru dhidi ya Umasikini, Uonevu, Ukandamizaji, Maradhi, Ujinga huku akiwa na fikra za Umoja” Naam, ni imani hii ya mwalimu ambayo leo hii ilinisukuma kukaa na kuanza kutafakari juu ya mbwembwe za Disemba 9 2006 na hatma yetu.

Sote tunajua wazi kuwa kipindi kile Tanzania inapata Uhuru, mbali ya kuwa kwa ujumla nchi ilikuwa masikini sana, hali ya uchumi haikuwa mbaya kama ilivyo sasa ambapo tumekuwa tukishuhudia kuporomoka (Mrema anasema kuserereka) kwa fedha yetu dhidi ya fedha za nje ikiwemo hata Kenya tu ambayo wakati ule wa uhuru shilingi yao ilikuwa sawa na yetu.

Kasi ya umasikini imekuwa ikizidi kuongezeka kwa Watanzania kila uchao na hadi leo hii idadi ya wananchi wanaoendelea kuwa masikini ni zaidi ya mara tatu ya wale wanaoonyesha dalili za kunyanyuka, ukiachilia mbali lile genge la wateule fulani fulani ambao nisingelipenda kuwazungumzia hapa sababu hoja ya kujieleza walikotoa utajiri wao haijajibika mpaka sasa.

Masimulizi ya kukua kwa pato la Mtanzania ambayo yameendelea kuwa wimbo wa kila kiongozi yameendelea kutokuwa na uwiano halisi na maisha ya hao wanaoambiwa pato lao kwa mwaka limekua. Bado wangali wakilala na njaa wengi wao, bado wanaendelea kufa kutokana na kukosa huduma sababu ya kukosa fedha, wapo wanaoendelea kuwa wajinga sababu wameshindwa kulipia masomo yao na wapo ambao ah!! acha tu.

Hivi Mtanzania huyu kwa falsafa ya Nyerere juu ya Uhuru, alikuwa na kipi cha kujivunia katika siku ile, tena cha kusherehekea? Rushwa, amekuwa mdudu ambaye kila anayeingia madarakani anauimba lakini akashindwa kuucheza.

Wangali wapo Watanzania wanaokosa haki zao za msingi sababu ya rushwa, wapo wanaopoteza maisha yao sababu ya ufisadi, wapo wanaokosa hata sauti za kusemea sababu ya rushwa. Uonevu bado ungalipo, Leo hii Watanzania wangali wanachapwa bakora sababu ya kuuliza kiongozi swali. Uhuru uliopo hapo wa kusherehekea ulikuwa upi ikiwa bado uonevu unatawala hapa nchini?

Najua wapo watakaonyoosha vodole na kuhoji huyu mwandikaji wa hapa ana akili kweli? Anyway, hilo si suala langu maana madaktari ndio watakaoweza kusema kuwa ninazo au laa, lakini uwezo wa kufikiri ninao. Hivi tunajua kuwa siku ile wakati mamilioni wakiwa wanasherehekea siku ile, kulikuwa na mamilioni wengine wangapi wako kwenye njaa na mateso makubwa kutokana na kukosa huduma za msingi?

Tunajua kuwa wakati wengine walikuwa kule Uwanja wa Taifa kuna vijana wetu ambao walikuwa hata hawajui cha kufanya sababu ndoto zao za kuendelea na masomo zimekufa baada ya kukosa fedha za kujiendeleza?

Yaani ilikuwa falsafa ile ile ya uswahilini ambayo wanahabari wameipigia kelele weeee mpaka sasa wameamua kujiunga nao baada ya kushindwa kujitenga na kuwarekebisha. Nazungumzia falsafa ya kuchangishana, kuonyeshana ufahari wa shereheni lakini si katika masuala ya maendeleo, mbona walipotoswa wanafunzi pale mlimani sababu serikali haina fedha hatukutangaziwa kuchangishana kidogo kidogo ili kuweza kuwakusanyia fedha za kuwawezesha kusoma?

Ni kweli kuwa tulielezwa mambo meeeeengi sana siku ile ambayo tulitakiwa kujivunia, lakini je yanaendana na umri huo kweli? Na hawa walioko sasa wana mikakati ipi kwa ajili ya baadae maana sio suala la miaka mingine 45 ijayo tuje kuendelea kuambiwa eti taifa letu bado changa, ni kweli lakini hata watoto huwa na ndoto zao na ndoto zao wao huzitekeleza kwa matendo sio kwa maneno na porojo nyingi.

Vifo vitokanavyo na uzazi vingali vikimaliza maisha ya mama zetu, milipuko ya magonjwa ingali ikitesa wananchi wetu tena hata hapo Dar ambapo ndio kila mtu anataka kukaa hapo, kasi ya wasiokuwa na ajira nayo imekuwa ikiongezeka kila siku kutokana na sera mbovu katika mfumo wa elimu na mfumo mbovu katika kuandaa vijana kwa ujumla na kuwapa uwezo wa kulitumikia taifa lao. Huo uhuru wetu katika hali kama hii tunaweza kuuthamanisha kwa kiasi gani?

Nijuavyo mimi ni kuwa thamani ya kitu chochote ni pale kinapoonyesha matunda mazuri kama ambavyo nilitarajia kwa upande wa thamani ya uhuru wetu. Kwamba kwa kadiri ambavyo nchi ingekuwa ikipiga hatua za haraka haraka kimaendeleo kwakuwa tuna kila kinachohitajika kwa ajili ya kuendelea, basi ndio na uhuru wetu pia unazidi kuwa na thamani. LAkini tunachokifanya sasa ni kushusha thamani kama tulivyofanya kwenye fedha yetu.

Badala ya kuendelea tumekuwa ama tumesimama palepale au tunarudi nyyuma zaidi. Uhuru wetu umekuwa ni kwa manufaa ya wachache kuwaibia wengi, wachache kuwaonea wengi, wachache kudhulimu haki, fursa na maslahi ya wengi. Uhuru wa namna hii si uhuru, Uhuru wa namna hii hauna manufaa na wala hauwezi kusherehekewa kwa dhati na mbwembwe za kila aina na badala yake siku hiyo pengine ilitakiwa kutumiwa kwa ajili ya kuhitimisha labda zoezi la kukusanya kura za maoni za wananchi kuhusu mfumo bora wa elimu, mfumo bora wa kutokomeza rushwa na kadhalika.

Wakati mvi zikiwa hazijatapakaa vichwani mwetu sababu ya uzee, ni vyema basi sisi tukajipanga vyema na kikamilifu kwa ajili ya kuhakikisha kuwa tunauthaminisha uhuru wetu kwa kuufanya uendane na mamilioni ya Watanzania na sio genge la wateule wachache na vibaraka wao.

Alamsiki

December 29, 2006 at 2:38 pm 2 comments


Blog Stats

  • 35,058 hits
December 2006
M T W T F S S
 123
45678910
11121314151617
18192021222324
25262728293031