Sababu nakupenda rais wangu

December 22, 2006 at 3:17 pm Leave a comment

Ni kwasababu ninakupenda mheshimiwa Raisi wangu ndio maana kwakweli nilijitahidi sana kukaa kando ya karedio kangu nikisikiliza jinsi ulivyokuwa “unachemka” kushusha mistari iliyokuwa imejaa vina juu ya kile kilichojiri ndani ya siku zako miatatu sitini na ushee hivi ukiwa katika makazi yako ya Magogoni.

Inawezekana sikukuelewa sana au kuendana na kile ulichokuwa ukituambia kwa maana ya kuwa na mtazamo wa kile hasa kilichokuwa nafsini mwako ulipokuwa ukichemka pale Kilimani, lakini kwasababu nakupenda Rais wangu, angalau niliambulia maneno mawili matatu hasa pale mwishoni mwishoni uliposema “Tukiwaunga mtazidi kuchemka” na kisha wakati unatoka ndani ya jumba lile, nasikia Vijana au skauti wa Chama wakawa wanakuimbia kawimbo kazuuuri, eti “Tukupambe maua”

Inawezekana usinielewe kwakweli, lakini kwasababu nakupenda sana mheshimiwa Rais wangu, nisingelipenda “Tukupambe” maana tutakuumiza sana. Ndio, tutakupamba kwa lipi mheshimiwa? Kwa shada la maua yaliyojaa miiba ya dhiki na ufukara unaoendelea kututesa? Kwanini tukupambe kwa mapambo ya kukuumiza mheshimiwa?

Na ukumbuke pia kuwa shada hili utavishwa ukiwa kizani, hali ambayo huenda ikakuumiza sana kwasababu lenyewe tayari lina miiba ambayo ni hatari na yenye sumu, akikosea mtu na kukuvisha vibaya sababu ya kiza huoni kuwa tutakuwa tumesababisha mengine?

Ni kwasababu nakupenda sana mheshimiwa raisi wangu ndio maana nimeona nikupongeze kwa kutaka “Tuwaunge mkono ili mzidi KUCHEMKA” sababu umekuwa mkweli zaidi ya tulivyotarajia kwakweli. yaani mmechemka kweli kweli katika kipindi hiki, lakini sidhani kama uungwaji mkono mnaotaka utakuwa makini kama mlivyotarajia.

Tutawaungaje mkono mheshimiwa Rais tukiwa gizani, operesheni hiyo haiwezi kuwa na matunda mazuri kabisa, sana sana itakuwa ya kuwaumiza maana hamna atakayekuwa anajua afanyacho huko kwenye giza zaidi ya kuwa tu naye kachomeka mkono wake hujui una sindano yenye dawa nzuri ya kutibu au laa.

Na kwakweli mheshimiwa Rais, kwasababu nakupenda kiongozi wangu ninaona ni vyema nikueleze kuwa ikiwa hali itaendelea kuwa hivi, mtazidi “Kuchemka” zaidi ya hapo hasa mlioko katika jiji la Dar es salaam, maana mtapoozwa na nini ikiwa hata nguvu ya kusababisha viyoyozi viwapooze mnapochemka haipo?

Ni kwasababu ninakupenda kiongozi wangu niliyekupigia kura (au kukupikia kula?), ndio maana ningelipenda kwakweli ikiwezekana tujiulize pamoja mambo machache sana yafuatayo:-

Kweli unania tukuunge mkono kwa ajili uzidi kutusokomeza kizani kwa kisingizio cha kuwa tulishawekwa uelekeo wa kusukumiwa huko toka nyuma? Yale makali yako wapi mheshimiwa? Ya kutowaonea aibu wale wote ambao wana nia ya kuturejesha enzi za kutawaliwa? Inamaana mkono umevunjika ndio maana kweli umeshindwa kuwakamata hawa jamaa zetu wa Richmond, ambao kila kukicha wamekuwa wakikuchokonoa kwenye macho?

Inamaana kuwa mikono imevunjika ndio maana mnashindwa kuidaka shilingi yetu kiasi kwamba kila kukicha inazidi kuserereka, kama alivyotamka mzee wa Nji hii, Bw. Mrema? Ina uzito gani shilingi yetu kiasi cha kushindwa kuishikilia walau pale ilipokuwa hadi kuiacha iendelee kuzama?

Kilimo chetu badi kimeendelea kuwa kile kile cha kuchimba udongo hapa na kurudisha nyuma, kilimo cha miaka nenda miaka rudi, kile kile ambacho ulikipigia kelele sana kuwa utakifanyia maboresho na nilitarajia kwakweli hiki nacho kingepewa semina elekezi ili kibadilike kiende mbele kwa kasi, nguvu na ari yako, sasa mbona bado tuko pale pale? Au kime-tuchemsha tumeshindwa kukigusa?

Inawezekana kabisa kuwa umesahau kidogo baadhi ya ahadi zako, na kwakuwa nakupenda sana mheshimiwa Rais wangu, nitaomba nikukumbushe juu ya ahadi yako wakati ule wa kampeni, ahadi ya kupambana na rushwa. Mbona sijawasikia wale vigogo waliotajwa katika makabrasha mbalimbali kuwa japo wameopandishwa kizimbani na kusomewa tu mashitaka?

Na wale wauza unga ambao walizua mjadala mkubwa sana Bungeni hivi wameishioa wapi? Si ninakumbuka kuwa ulituambia umeshapewa majina yao mheshimiwa? Maana hatujatajiwa hata kutajiwa kuwa ni akina fulani na fulani. Au kutoka awamu ya tatu mlirithi tu tatizo la umeme na ile sera ya Uwazi na Ukweli hamkuona umuhimu wake?

Ni kwasababu ninakupenda kwakweli mheshimiwa Rais wangu, ndio maana napenda nikukumbushe juu ya kurejesha kale kautaratibu ka awamu iliyopita, kautaratibu ka kila mwezi kutuambia walau kuwa mmekusanya nini mwezi huo na mkatumia katika nini na nini.
Na ni kwasababu ninakupenda mheshimiwa Rais wangu, ndio maana nimeona niishie hapa leo ila nikaribishe wananchi wako wengine nao waelezee mapenzi yao kwako.

Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Tubariki sisi sote

Entry filed under: maskani.

Siku chache baada ya Moto wa Mwanjelwa KUMRADHI……KUMRADHI……KUMRADHI

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Trackback this post  |  Subscribe to the comments via RSS Feed


Blog Stats

  • 35,058 hits
December 2006
M T W T F S S
 123
45678910
11121314151617
18192021222324
25262728293031