Siku ya UKIMWI duniani na uzinduzi wa kondomu zeny…

December 2, 2006 at 10:05 am 2 comments

Siku ya UKIMWI duniani na uzinduzi wa kondomu zenye harufu ya ndizi!!!

Jana ilikuwa SIKU YA UKIMWI duniani, siku ambayo mamilioni ya watu duniani huungana katika kutafakari, kutathmini, kupanga na kupangua masuala mbalimbali yenye kuhusiana na ugonjwa huu.
Ni siku ambayo hata hivyo ushiriki wa wale wenye kuishi na gonjwa hili umekuwa duni kulinganisha na umuhimu wa ushiriki wao.
Na pale ilipotokea wachache wakashiriki hasa kwa nchi kama yangu ya Tanzania, basi imekuwa si kwa lengo la kuwafanya watoe kilio chao kwa ajili ya dunia kuweza kuwasaidia, bali imekuwa ni kwa lengo la kuwawezesha baadhi ya wahuni fulani fulani kuwatumia kwa lengo la kujipatia fedha za kununulia mashangingi mapya kwa kisingizio eti kuweza kufika vijijini kuwafikia haathirika zaidi ambao si rahisi kufikiwa (mlishawafikia wangapi mbona hamtuambii?)
Ni siku ambayo imekuwa ikiadhimishwa kwa miaka kadhaa sasa, lakini hali halisi haionyeshi kuwa imekuwa ikiboreka kwa maana ya kuwa walau na afueni dhidi ya madhara ya ugonjwa huu.
Soma takwimu zenye kuhusiana na ugonjwa huu na athari zake Duniani kwa ujumla hapa, huku pia takwimu za ugonjwa na madhara yatokanayo na ugonjwa huu katika nchi za Afrika hususan zilizoko kusini mwa jangwa la Sahara zikiwa si zenye kuonyesha matumaini ya kuridhisha. Taarifa zingali zikionyesha kuwa sehemu hii ya Dunia ndio ambayo imeendelea kuathirika zaidi pengine kuliko sehemu nyingine za Dunia.
Naam, nilikaa mahali, nikifuatilia kwa ukaribu sana karibu kila kilichokuwa kikifanyika katika siku hiyo, iwe kwa kuona ana kwa ana, kwa kusikia au hata kusoma na kwakweli kulikuwa na juhudi kubwa sana zilifanyika na zikawa na matunda katika kupashana habari kuhusiana na matukio hayo, lakini unajua nini ndugu yangu!!
Kama nilivyotarajia, longolongo zilikuwa nyingi zaidi kuliko ukweli. Yaliandaliwa matamasha ya kila aina, kuanzia ya kuzindua kondomu mpya mpaka yale ya kuonyesha ugonjwa huo unavyoenea. Zikachezwa na picha kibao kuhusiana na siku hiyo (Samahani sana dada Chemi, utanisamehe, najua lengo lako lilikuwa zuri tu kupitia filamu yenu) lakini kwangu mimi sijui kama kuna lililoniingia hapo.
Kwanza kabisa ni jina la siku yenyewe SIKU YA UKIMWI. Ni jina ambalo wenye lugha zao wangesema kuwa liko “so general”. Lilitakiwa kuwa wazi zaidi kuwa ni siku ama ya kupambana na ongezeko la maambukizi ya ugonjwa huo, siku ya kukaa pamoja na yatima watokanao na janga hilo au vingine vyovyote ilimradi ijulikane wazi kuwa ni siku kwa ajili ya nini. Lakini kwa SIKU YA UKIMWI tu!! hapana haitoshi
Hivi mnajua kuwa kuna watu ambao huitumia siku hii kwa ajili ya kufanya maambukizi mapya, ndio! Ni siku ya UKIMWI, iwe unasambaza au unaelimisha watu kuepuka maambukizi mapya haijalishi, nyote ni siku yenu hiyo, midhali tu mnajihusisha na gonjwa hilo.
Wapo vigogo ambao naamini kabisa hiyo jana walizungumza mpaka mishipa ikawatoka, jasho likawatiririka wakijitahidi kuonyesha wanavyopata uchungu kuona yatima wakiongezeka, lakini walipotoka hapo wakakimbilia mahali kwenda kuongeza idadi ya wanaoambukizwa, tena baada ya kuwahonga hela walizopewa kwenye bahasha ya khaki baada ya risala yake ndeeeefu na ya kinafiki. Mchana ana uchungu na usiku ndio hivyo tena.
Ukiangalia taarifa zilizokuwa zimejaa kwenye magazeti, redio, luninga siku hiyo, zote zilionyesha kiasi gani jamii nzima kwa ujumla ilivyo na udhaifu katika harakati za kukabiliana na ugonjwa huu. Nyingi zilikuwa zile za Kiongozi fulani kasema…, Asasi fulani imedai…, Waathirika waongezeka…. Yatima nao sijui wamefanya nini……. Yaani blah blah kibao.
Hiyo jana sikuona gazeti hata moja ambalo lilikuwa na kile wanaita wenye lugha zao “Exclusive Interview” labda na mgonjwa fulani aliye mahututi katika hospitali fulani au nyumbani kwake kijiji fulani akieleza kwa undani labda namna alivyorubuniwa na kiongozi fulani hadi kuambukizwa ugonjwa huo, au namna alivyorubuniwa na dereva wa lori sijui lipitalo Manyoni kwenda Burundi, hadi akamwambukiza.
Sikuona mahali au kazi fulani ya mwandishi ambaye aliandika kwa ufasaha na kwa namna ambayo aliyoyaandika yangewavuta viongozi kujitokeza kupima afya zao na kisha kuweka hadharani majibu yao. Wala hakukuwa na mahojiano na yatima wa eneo fulani wakielezea namna ambavyo fedha wanazotumiwa zinaishia kwa watendaji kadha wa kadha kabla ya kuwafikia wao.
Hivi ni chombo gani hiyo jana kiliamua kutuma japo mwandishi wake mmoja kufuatilia kama mamilioni ya asasi fulani waliyoyapata toka kwa wahisani kama yaliwafikia kweli hao walengwa na yakawanufaisha? Sana sana walichokifanya ni kile kile tulichozoea.
Asasi fulani imetoa msaada kwa yatima wa kijiji fulani au kituo fulani cha kulelea yatima watokanao na ugonjwa huo. Kwanini msifuatilie kujua kama kiasi kilichogawiwa huko kinaendana walau na kile kiasi walichochangisha au kumkamua mfadhili fulani?
Na serikali nayo ilisema nini vile katika siku hiyo zaidi ya kile watoto wa mijini wanaita longolongo (usanii uliozoeleka ambao umekuwa hautekelezwi). Walitoa matamko kadhaa ambayo ukiyaona mengine yanatia walakini na kuzua maswali kuliko majibu.
Hivi hamjasikia kilio cha wananchi kuwa wamegeuzwa migodi?
Hamjui kuwa waathirika wamekuwa wakifanywa miradi ya baadhi ya watu na wamenufaika sana kupitia migongoni mwao? na hali hii mtaiacha hadi lini? Kwanini msitoe tamko la kuwa mmeweka utaratibu wa kukagua hesabu za asasi hizo na wawe wanatoa taarifa zao za makusanyo (sio mapato ni makusanyo) na matumizi yao? Au kwasababu nanyi wengi wenu mmekuwa sehemu ya wanaowafanya waathirika miradi?
Kwa ujumla yanayofanyika katika suala hili ni mchezo wa kuigiza zaidi kuliko mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI. Na ndio maana haishangazi kuona kuwa hadi sasa kumekuwa na nguvu zinazokinzana katika matumizi ya mipira ya kondomu kama kinga dhidi ya maambukizi mapya. na wanao kinzana ni wataalamu ambao tunatarajia kuwa wawe na suluhisho muafaka katika janga hili.
Kuna mengi ambayo tunaweza kuyazungumza kwakweli, mengi kuliko vile ambavyo mtu anaweza kutarajia, lakini ni vyema tu tukaelezana kuwa, kwa mfumo huu tulio nao hivi sasa, madhara ya janga hili yataendelea kukua na kuongezeka kila kukicha kama hatutafanya juhudi za dhati na za makusudi katika kubadilisha taratibu zetu za kulikabili janga hili, ikiwa kweli tuna nia ya kukabiliana nalo.

Entry filed under: maskani.

Karibu Dar Mjomba Kuelekea nchi ya ahadi

2 Comments Add your own

 • 1. Rashid Mkwinda  |  December 3, 2006 at 2:07 pm

  Wapo wanaonufaika na siku hii, wapo wanaoumia kutokana na siku halikadhalika wapo wanaodhalilika kutokana na siku hii, nathubutu kusema kuwa huenda taasisi zinashadidia kwamba isipatikane dawa itakayotibu maradhi haya hatari ili waweze kuendelea kula fedha za yatima wa walioathirika na ugonjwa huo, waendelee kupeleka picha za waathirika wa ugonjwa huu kwa wafadhili ili waendelee kuishi kwa kutegemea kuugua kwa wenzao.

  Inataka kuthibiti kwamba hii inaweza kuwa ni laana ambayo madhara ya wengie kwa wengine ni tija, (Vita vya Panzi Furaha kwa Kunguru).

  Naamini wapo watu ambao wanapenda wengine waendelee kuugua ugonja huu ili waendelee kuvimbisha vitumbo vyao,…. ni kweli kwani uongo? (naona kuna jamaa yangu mmoja yuko karibu nami katika kmpyuta ananishangaa ninavyopandisha mada hii) ee kwani iwapo watu watapona maradhi haya taasisi za kiserikali na zile zisizo za kiserikali zitafungwa ulaji utakuwa umekwisha sijui watabuni njia ipi ya kitapeli nadhani wataomba mafua ya ndege yaje kwa kasi nchini ili waunde vikundi vya kutoa ushauri nasaha juu ya waathirika wa mafua ya ndege,eee ndiko tunakoelekea ni usanii tuu hadi siku ya kiyama inafika.

  Angalia wengine wanaanzisha vituo vya kulelea watototo yatima wanakusanya yatima hao kutoka sehemu mbalimbali za nchi kisha huwapiga picha na kupeleka kwa wafadhili mara baada ya kuletewa mafungu wanawafukuza yatima hao kama sio dhambi ni nini halafu wanajifanya ni viongozi wa dini…mnashangaa imetokea hiyo katika mji fulani na mtu fulani katika ncchi ya Tanzania namhifadhi lakini inafahamika kabisa hii.

  Kwa hilo Bw. Msangi unategemea nini zaidi ya kuweka siku maalumu ya UKIMWI duniani? na subiri utasikia imekuja siku maalumu ya watoto yatima ambao wazazi wao wameathirika kwa UKIMWI hilo si ajabu kabisa katika anga hili la Wadanganyika.

  Kabla ya siku ile inayoitwa ni SIKU YA UKIMWI, nilikwenda mahali katika taasisi ya watu ambao wanaishi na virusi vya UKIMWI, ili nipate kuongea na mmoja wa waathirika wa ugonjwa huo hatari ambaye kwa sasa anaishi kwa matumaini kwa zaidi ya miaka 12, jambo ala ajabu nilipofika pale kutaka kuongea na mtu huyo alijitokeza Ofisa mmoja wa kiserikali na kuniambia kuwa msemaji wa mambo yote ya waathirika wa UKIMWI ni Ofisa fulani ambaye si mwathirika wa UKIMWI.

  Jambo hili lilinistaaajabisha sana nilijiuliza itakuwaje mtu ambaye si muathirika anaweza kudiriki kunieleza mimi kitu ambacho hakimhusu ilhali muhusika mwenyewe wa kuzungumza yote yaliyomkuta yupo? niliondoka mahali pale nikiwa na mengi ya kujiuliza juu ya kile kinachoendelea katika medani ya waathirika wa UKIMWI.

  Kwa hiyo ndiyo hivyo Bwana tukubaliane na hali iliyopo kwa kuwanufaisha wasiohuisika na kuwadhalilisha wahitaji halisi wa misaada inayotolewa kwa ajili yao.

  Yapo mengi lakini tuachie uwanja wengine nao wadiriki kuchangia juu ya jambo hili ambalo kila uchao linaumiza vichwa vya madaktari na Maprofesa kutafutia sijui ni ufumbuzi au ugunduzi wanajua wao pia nadhani wanashindwa kufanya utafiti wa kina kwa kuchelea kwamba wakimaliza utafiti wao marupu rupu ya kazi hiyo yatakuwa yamekwisha.

  Mie simo kazi kwenu wengine

  Watabahu

 • 2. MACHWEO  |  December 17, 2006 at 8:01 pm

  Bwana Mkwinda anashangaa kuhusu watu wanaofaidika na uwepo wa ukimwi! hapa hakuna cha kushangaa wala nini kwani kila kitu kipo wazi yaani ni kama padri anavyolijua kanisa na nk.
  Ukimwi sasa umekuwa dili kubwa la kuingiza mamilioni huku kwa wasanii ‘waliojaa tele’ huku watoto yatima wakikusanywa siku hiyo tu na kupewa karanga na viatu vya mtumba, na wale wanaofaidika na ukimwi wakikazana kuvumbua kondomu zenye ladha ya ndizi!
  natamani kila mmoja angesoma kilichoandikwa humu hasa wale wote wanaowasemea wenye virusi huku wao wakiwa si wahusika.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Trackback this post  |  Subscribe to the comments via RSS Feed


Blog Stats

 • 35,058 hits
December 2006
M T W T F S S
 123
45678910
11121314151617
18192021222324
25262728293031