Archive for December 2, 2006

Siku ya UKIMWI duniani na uzinduzi wa kondomu zeny…

Siku ya UKIMWI duniani na uzinduzi wa kondomu zenye harufu ya ndizi!!!

Jana ilikuwa SIKU YA UKIMWI duniani, siku ambayo mamilioni ya watu duniani huungana katika kutafakari, kutathmini, kupanga na kupangua masuala mbalimbali yenye kuhusiana na ugonjwa huu.
Ni siku ambayo hata hivyo ushiriki wa wale wenye kuishi na gonjwa hili umekuwa duni kulinganisha na umuhimu wa ushiriki wao.
Na pale ilipotokea wachache wakashiriki hasa kwa nchi kama yangu ya Tanzania, basi imekuwa si kwa lengo la kuwafanya watoe kilio chao kwa ajili ya dunia kuweza kuwasaidia, bali imekuwa ni kwa lengo la kuwawezesha baadhi ya wahuni fulani fulani kuwatumia kwa lengo la kujipatia fedha za kununulia mashangingi mapya kwa kisingizio eti kuweza kufika vijijini kuwafikia haathirika zaidi ambao si rahisi kufikiwa (mlishawafikia wangapi mbona hamtuambii?)
Ni siku ambayo imekuwa ikiadhimishwa kwa miaka kadhaa sasa, lakini hali halisi haionyeshi kuwa imekuwa ikiboreka kwa maana ya kuwa walau na afueni dhidi ya madhara ya ugonjwa huu.
Soma takwimu zenye kuhusiana na ugonjwa huu na athari zake Duniani kwa ujumla hapa, huku pia takwimu za ugonjwa na madhara yatokanayo na ugonjwa huu katika nchi za Afrika hususan zilizoko kusini mwa jangwa la Sahara zikiwa si zenye kuonyesha matumaini ya kuridhisha. Taarifa zingali zikionyesha kuwa sehemu hii ya Dunia ndio ambayo imeendelea kuathirika zaidi pengine kuliko sehemu nyingine za Dunia.
Naam, nilikaa mahali, nikifuatilia kwa ukaribu sana karibu kila kilichokuwa kikifanyika katika siku hiyo, iwe kwa kuona ana kwa ana, kwa kusikia au hata kusoma na kwakweli kulikuwa na juhudi kubwa sana zilifanyika na zikawa na matunda katika kupashana habari kuhusiana na matukio hayo, lakini unajua nini ndugu yangu!!
Kama nilivyotarajia, longolongo zilikuwa nyingi zaidi kuliko ukweli. Yaliandaliwa matamasha ya kila aina, kuanzia ya kuzindua kondomu mpya mpaka yale ya kuonyesha ugonjwa huo unavyoenea. Zikachezwa na picha kibao kuhusiana na siku hiyo (Samahani sana dada Chemi, utanisamehe, najua lengo lako lilikuwa zuri tu kupitia filamu yenu) lakini kwangu mimi sijui kama kuna lililoniingia hapo.
Kwanza kabisa ni jina la siku yenyewe SIKU YA UKIMWI. Ni jina ambalo wenye lugha zao wangesema kuwa liko “so general”. Lilitakiwa kuwa wazi zaidi kuwa ni siku ama ya kupambana na ongezeko la maambukizi ya ugonjwa huo, siku ya kukaa pamoja na yatima watokanao na janga hilo au vingine vyovyote ilimradi ijulikane wazi kuwa ni siku kwa ajili ya nini. Lakini kwa SIKU YA UKIMWI tu!! hapana haitoshi
Hivi mnajua kuwa kuna watu ambao huitumia siku hii kwa ajili ya kufanya maambukizi mapya, ndio! Ni siku ya UKIMWI, iwe unasambaza au unaelimisha watu kuepuka maambukizi mapya haijalishi, nyote ni siku yenu hiyo, midhali tu mnajihusisha na gonjwa hilo.
Wapo vigogo ambao naamini kabisa hiyo jana walizungumza mpaka mishipa ikawatoka, jasho likawatiririka wakijitahidi kuonyesha wanavyopata uchungu kuona yatima wakiongezeka, lakini walipotoka hapo wakakimbilia mahali kwenda kuongeza idadi ya wanaoambukizwa, tena baada ya kuwahonga hela walizopewa kwenye bahasha ya khaki baada ya risala yake ndeeeefu na ya kinafiki. Mchana ana uchungu na usiku ndio hivyo tena.
Ukiangalia taarifa zilizokuwa zimejaa kwenye magazeti, redio, luninga siku hiyo, zote zilionyesha kiasi gani jamii nzima kwa ujumla ilivyo na udhaifu katika harakati za kukabiliana na ugonjwa huu. Nyingi zilikuwa zile za Kiongozi fulani kasema…, Asasi fulani imedai…, Waathirika waongezeka…. Yatima nao sijui wamefanya nini……. Yaani blah blah kibao.
Hiyo jana sikuona gazeti hata moja ambalo lilikuwa na kile wanaita wenye lugha zao “Exclusive Interview” labda na mgonjwa fulani aliye mahututi katika hospitali fulani au nyumbani kwake kijiji fulani akieleza kwa undani labda namna alivyorubuniwa na kiongozi fulani hadi kuambukizwa ugonjwa huo, au namna alivyorubuniwa na dereva wa lori sijui lipitalo Manyoni kwenda Burundi, hadi akamwambukiza.
Sikuona mahali au kazi fulani ya mwandishi ambaye aliandika kwa ufasaha na kwa namna ambayo aliyoyaandika yangewavuta viongozi kujitokeza kupima afya zao na kisha kuweka hadharani majibu yao. Wala hakukuwa na mahojiano na yatima wa eneo fulani wakielezea namna ambavyo fedha wanazotumiwa zinaishia kwa watendaji kadha wa kadha kabla ya kuwafikia wao.
Hivi ni chombo gani hiyo jana kiliamua kutuma japo mwandishi wake mmoja kufuatilia kama mamilioni ya asasi fulani waliyoyapata toka kwa wahisani kama yaliwafikia kweli hao walengwa na yakawanufaisha? Sana sana walichokifanya ni kile kile tulichozoea.
Asasi fulani imetoa msaada kwa yatima wa kijiji fulani au kituo fulani cha kulelea yatima watokanao na ugonjwa huo. Kwanini msifuatilie kujua kama kiasi kilichogawiwa huko kinaendana walau na kile kiasi walichochangisha au kumkamua mfadhili fulani?
Na serikali nayo ilisema nini vile katika siku hiyo zaidi ya kile watoto wa mijini wanaita longolongo (usanii uliozoeleka ambao umekuwa hautekelezwi). Walitoa matamko kadhaa ambayo ukiyaona mengine yanatia walakini na kuzua maswali kuliko majibu.
Hivi hamjasikia kilio cha wananchi kuwa wamegeuzwa migodi?
Hamjui kuwa waathirika wamekuwa wakifanywa miradi ya baadhi ya watu na wamenufaika sana kupitia migongoni mwao? na hali hii mtaiacha hadi lini? Kwanini msitoe tamko la kuwa mmeweka utaratibu wa kukagua hesabu za asasi hizo na wawe wanatoa taarifa zao za makusanyo (sio mapato ni makusanyo) na matumizi yao? Au kwasababu nanyi wengi wenu mmekuwa sehemu ya wanaowafanya waathirika miradi?
Kwa ujumla yanayofanyika katika suala hili ni mchezo wa kuigiza zaidi kuliko mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI. Na ndio maana haishangazi kuona kuwa hadi sasa kumekuwa na nguvu zinazokinzana katika matumizi ya mipira ya kondomu kama kinga dhidi ya maambukizi mapya. na wanao kinzana ni wataalamu ambao tunatarajia kuwa wawe na suluhisho muafaka katika janga hili.
Kuna mengi ambayo tunaweza kuyazungumza kwakweli, mengi kuliko vile ambavyo mtu anaweza kutarajia, lakini ni vyema tu tukaelezana kuwa, kwa mfumo huu tulio nao hivi sasa, madhara ya janga hili yataendelea kukua na kuongezeka kila kukicha kama hatutafanya juhudi za dhati na za makusudi katika kubadilisha taratibu zetu za kulikabili janga hili, ikiwa kweli tuna nia ya kukabiliana nalo.

December 2, 2006 at 10:05 am 2 comments


Blog Stats

  • 34,787 hits
December 2006
M T W T F S S
 123
45678910
11121314151617
18192021222324
25262728293031