Archive for November 13, 2006

Wasamaria wetu na usamaria wa vyombo vya habari

“Sadaka ni SIRI, kama umetoa kwa mkono wa kushoto, basi hata ule wa kulia usijue kuwa umetoa nini, sio jambo la kutangaza kwa maana unapotoa unamtolea Mungu, naye anakuona, ukitoa kwa ajili ya kujipatia ufahari basi haiwezi kubarikiwa sadaka yako
=======================

Kwa muda wa kutosha tu nimekuwa nikiendelea kufuatilia hali ya kuongezeka kwa Wasamaria wema na Usamaria wema wao hapa nchini kwetu. Watu wenye moyo wa kusaidia yatima, wasio jiweza, wanaoishi katika mazingira magumu na hata hawa ndugu zetu ambao wanaishi na VVU.

Kwa wale ambao wamekuwa wakiyaona bila shaka wataungana nami kukiri kuwa hali hii imezidi kushamiri zaidi hasa katika kipindi hiki ambapo teknolojia pia imekuwa ikiwezesha usambazwaji na upatikanaji wa habari katika kona mbalimbali ndani na hata nje ya nji yetu hii.

Hata hivyo (sijui kwasababu nilizaliwa kuona mambo kinyume au vipi), kuna jambo ambalo nimekuwa kila nikilitafakari, basi limekuwa likinisukuma kuhoji uhalali wa misaada hiyo na watoaji wake. Hivi MSAADA sio sawa tu na SADAKA? Sasa kuna haja gani kwa mtoaji kuhanikiza “Jamani kesho naenda kutoa misaada mahali fulani mje mnione” au Leo nimetoa msaada kwa akina fulani jamani oneni”

Kwa wafuatiliaji wa taarifa zetu za habari katika vyombo vyetu mbalimbali, limekuwa jambo la kawaida kila siku (Narudia tena KILA SIKU), kukutana na habari za ama fulani kesho atatoa msaada sehemu fulani, au fulani leo katoa misaada sehemu fulani, na habari hizo hufuatiwa na mlolongo wa maelezo kibaaaaaaao yote yakimsifia mtoa msaada huyo kufikia hata hatua ya kupachikwa uheshimiwa.

Ukisoma kwa undani au kusikiliza kwa undani maelezo ya mhusika huyo, mengine huweza hata kukuletea maswali mengi sana kuliko uhalisia wa wasifu wake, na ukweli ndio uko hivyo. Kuwa wengi wa “Waheshimiwa Matajiri” watoa misaada, ni wale ambao utajiri wao huo una maswali mengi zaidi juu ya upatikanaji wake kuliko ukweli wa mambo ambao wananchi wanatakiwa kuuamini.

Ni watu ambao wamewageuza binadamu wenzao “migodi” kwa ajili ya kusakia fedha zao hizo na pia wamewageuza binadamu wenzao “majosho” kwa ajili ya kusafishia fedha zao chafu (Dirty money).

Wakati fulani nilipokuwa bado mdogo, nakumbuka maneno niliyoyanukuu hapo juu, kuhusiana na kitu msaada (unadhani ni tofauti na sadaka?) Sasa hawa jamaa zetu ambao wanatoa sadaka, ubani sijui, misaada nk, huku wakiwa wameitisha maluninga na magazeti kwa ajili wawatangaze kwa kile walichotoa, wao wanatoa kwa ajili ya kusaidia kweli au kwa lengo la kupewa sifa za duniani?

Hivi ikitokea tukachachamaa na kumkaba mmoja wao na kisha tukamwambia ashike kitabu kitakatifu na akiri kuhusu utajiri wake, ambao ana tusaidia, ni wangaopi watathubutu kufanya hivyo? Hivi msaada ukitolewa kimya kimya, kwa mtu kujiendea zake akatoa msaada na kisha akajirudia dukani au ofisini na hata nyumbani kwake, huo msaada hautakuwa msaada kweli? Hivi ni wangapi wanapowanunulia watoto wao nguo au kuwatoa out hujitangaza? Ebo! ukiwa na utajiri kusaidia wasio nacho si wajibu wako kwani?

Tena wengine unakuta wanachangisha na kuchangisha fedha kwa ajili ya kwenda kutoa misaada hiyo, na kisha kujipangia katika fedha hizo za michango kuwa mimi nitatumia kiasi fulani kwa ajili ya kuniwezesha kupeleka misaada sehemu fulani, Ebo! ndio misingi ya misaada hiyo jamani?

Nauliza tu lakini, msije mkanitoa roho maana hapa tayari kuna watu wakisoma hapa najua wataanza kuomba kila aina ya dua ili nifie mbali maana na nimewagusa pabaya. Ninachotaka kusema hapa ni kuwa, kama unatoa kwa ajili ya kuonyesha uchungu wako, basi ni vyema uchungu huo akauona Mungu aliyekuwezesha kuupata utajiri huo, na sio binadamu mwenzio akusifu.

Samahani wote nitakaokuwa nimewagusa, japo ninaamini kuwa kwasababu nyie ni waungwana na “mnaomtolea Mungu wenu” mtakuwa mmenielewa namaanisha nini. Ni vijimambo tu, ila vinanikera kweli kweli

November 13, 2006 at 5:25 pm 2 comments


Blog Stats

  • 35,058 hits
November 2006
M T W T F S S
 12345
6789101112
13141516171819
20212223242526
27282930