UTANDAWAZI: tatizo ni mfumo, sera, sisi au nini?

November 3, 2006 at 10:12 am 2 comments

Hivi karibuni nilibahatika kukaa mahali na baadhi ya marafiki zangu ambao ni wanafunzi wa vyuo mbalimbali vya elimu ya juu mkoani hapa. (Tuna tawi la Mzumbe, T.I.A na Chuo Huria), na katika hali ambayo haikuwa rasmi, tulijikuta tukiingia katika mjadala kuhusiana na hiki kitu UTANDAWAZI.

Kwa muda wakati maongezi hayo yanaanza, nilijikuta nikikaa kimya kiasi kwa lengo la kutaka kuwapa nafasi wataalamu hao kujimwaga nione umahiri wao katika kulijadili suala hili ambalo licha ya kuwa limeshakuwa la kawaida masikioni na akilini mwetu, bado limeshindikana kuzoeleka kwa jamii mbalimbali duniani.

Hoja kubwa waliyokuwa wakiipa msisitizo katika majadiliano yao, na ambayo karibu sehemu zote linakojadiliwa suala hilo utakuta watu wakiizungumzia, ilikuwa ni ile ya kumezwa kwa baadhi ya mataifa, Tanzania ikiwa mojawapo katika mfumo huo na hivyo kuwepo kwa hali ya kunufaisha baadhi ya mataifa hususan yaliyo matajiri, ambayo ndio yenye kuonekana kuwa yalianzisha mfumo huo wa kiuchumi.

Hata hivyo, ilifikia wakati nikalazimika kuwauliza jamaa zangu maswali kadhaa, kubwa kabisa likiwa ni “Kwanini wanadhani kuwa Tanzania haina uwezo wa kuendana na hali ya ushindani katika mfumo huo?, Nini kifanyike katika wakati huu tuliopo kuhusiana na mfumo huu?”

Cha kushangaza sana, narudia tena, “chakunishangaza sana” ni kuwa, wapo waliosema kuwa Tanzania haiwezi kushindana kwasababu haina uwezo huo na hivyo wakashauri kuwa ni vyema ikajitoa katika mfumo huo. Nikajiuliza, KUJITOA? HATUNA UWEZO? kweli ndivyo ilivyo?

Hali hii ilinifanya nianze kuwaza mambo kadhaa kichwani mwangu ikiwa ni pamoja na uelewa tulionao Watanzania katika mifumo inayotawala dunia, namna inavyoweza kujitokeza, mchango wa mwanadamu katika kuibuka kwa mifumo hiyo na mchango wake vile vile katika kuidhibiti.

Sanjari na hayo, nilianza kuwaza na kuwazua pia juu ya hii hali ambayo imekuwa sugu kati yetu Watanzania ya kuamini kuwa kuna baadhi ya mambo ambayo hatuyawezi na kwamba hata kama tutathubutu, basi sisi ni watu wa kushindwa tu. Nitaanza kujadili hilo la juu kwanza (kulingana na ufahamu wangu na sio kulingana na hoja za waliokuwa washiriki wa mjadala huo wa kwenye viti vya plastiki, vikao ambavyo awali viliitwa vya kwenye stuli ndefu)

Biashara ya Utumwa, mfumo wa Ukoloni, Ubaguzi wa rangi na mingine mingi ambayo wengi wetu tumekuwa tukijifunza katika somo la Historia, ni miongoni mwa mifumo ambayo kwa nyakati mbalimbali iliendesha dunia kwa vipindi tofauti tofauti huku ikimalizika kutokana na kuibuka kwa mfumo mwingine.

Kwa bahati mbaya sana, katika uelewa wangu, sijawahi kuona kwa hakika na nikathibitisha kuwa mifumo hiyo au mfumo fulani mmoja wapo ulitokana na jitihada za mwanadamu kama yeye, bali mazingira halisi yanayomzunguka na mabadiliko ya kimaendeleo katika nyanja za Uchumi, sayansi & teknolojia, utamaduni na nyingine kadhaa wa kadhaa.

Hali hizi ingawa tunawezaq kupingana kutokana na mitazamo tofauti tofauti, bado kwangu mimi naamini kabisa kuwa ni hali au mabadiliko ya kiasilia (wenye lugha zao huita nature), na kwa mujibu wa uelewa wangu, hizi ni halui ambazo haziko ndani ya uwezo wa binadamu kuzidhibiti. Binadamu anaweza akadhibiti kwamfano kutokuharibu mazingira sababu hilo sio suala la kiasilia, lakini hawezi kuzuia kubadilika kwa hali ya hewa na hata misimu sababu hilo ni suala la kiasilia zaidi.

Naam, tukirejea katika mada yangu leo hii, baada ya kuona hivyo hapo ndipo tunapokuja kuona kuwa kumbe hata kutoka katika zama za ubeberu, ubepari, ukoloni, utumwa na mifumo mingine mingi, hayakuwa mabadiliko yaliyowekwa na mwanadamu (man made changes) kama ambavyo tunataka kujiaminisha, bali yalikuwa mabadilikoya kiasilia. Na ni kutokana na iman hiyo mimi naamini hata katika suala la Utandawazi na mifumo mingine tunayoiona leo hii kuwa haifai, ni suala asilia.

Wanafalsafa mbalimbali walioishi miaka ya nyuma na kujihusisha na falsafa za kiuchumi au mifumo ya maendeleo ya kiuchumi, kwa nyakati mbalimbali waliwahi kugusia suala la mabadiliko ya mifumo ya kiuchumi duniani, mingi kati ya hiyo mifumo ikiwa imeelezewa kwanini itatokea na pengine wakati gani, hivyo basi suala hili halikuwa la jana wala juzi.

Kwa kuzingatia maelezo yangu hayo mafupi (kumbuka yanatokana na mtazamo wangu), ni wazi kabisa kuwa Tanzania kama nchi au kama kitu chochote kile kilichoko humu duniani, ni vigumu kwake kujadili suala la kujitoa katika mfumo huu, kama ambavyo ni vigumu kwa nchi au mtu yeyote katika dunia hii.

Suala la mifumo ya kiuchumi ingawa ni suala ambalo limekuwa la kawaida kutokana na kusomwa sana na kujadiliwa pengine sana tu, bahati mbaya sana halijawahi kuwa suala la kawaida na la kuzoeleka masikioni mwa watu na hususan sio tulioko nchi za ulimwengu wa tatu au zinazoendelea.

Na kwa mtazamo wangu ni kuwa penye matatizo ni kuwa watu hatu[pendi kukubaliana na ukweli kuwa ndivyo ulivyo badala yaker tunaupinga ukweli. Ni vyema tukaelewa kuwa, katika falsafa ya jkawaida kabisa ya maisha ya kila siku, moja kati ya mambo yanayoweza kukuwezesha kukabiliana na mazingira fulani yaliyokuzunguka ni kwa kuyakubali kwanza na si vinginevyo.

Sijui wachumi waliobobea kama wanaweza kunithibitishia hili au laa, lakini kwangu mimi, kwa kile ambacho nimekuwa nacho kichwani, sijawahi kusikia kama kuna mfumo ambao uliwahi kuibuka au kuibuliwa na kisha ukafurahiwa na jamii kwa ujumla kuwa uko sahihi kabisa. Sijawahi na sijui kama upo, labda kama nilivyoomba wanauchumi waliobobea wanieleze.

Kile ambacho kimekuwa kikiendelea duniani, ni kwa wanauchumi hao kubobea katika kuweka kile wanachokiita mikakati ya kuingia mfumo fulani, mikakati ambayo mara nyingi imekuwa ikizidiwa na nguvu ya uhalisia wa soko na mahitaji ya soko la dunia kwa ujumla. Lakini pengine licha ya kutambua hili, ingali inanishangaza sana kuwa wataaluma wetu wa aina hii, hawajawahi pia kukaa na kuweka mkakati wa kuiwezesha dunia kukubaliana na hali halisi hivyo inapoibuka hali fulani wakakubaliana kuendana nayo.

Tukija katika hoja ya Watanzania kutokuwa na uwezo. Hoja hii kwakweli ndio ambayo imekuwa ikinishangaza sana. Ni hoja ambayo imekuwa ikinishangaza sana kutokana na wale wanaotoa hoja hii kuitoa kwa kiwango cha kujionyesha wazi kuwa tungali na upeo mdogo sana katika kuyachambua mazingira tuliyomo.

Hivi mwenye uwezo wa kuuthibitishia umma juu ya uwezo wako binafsi ni nani kama sio wewe, na unategemea nini ikiwa mwenyewe tu huutambui uwezo ulionao? Mwaka jana wakati naanza ku-blogi, rafiki yangu mmoja aliniambia kuwa nilikuwa ninapoteza muda wangu bure tu sababu singeweza sio tu kuiendeleza blogi yenyewe, bali kutokupata wa kunisikiliza, na alinifanya nikacheka sana pale nilipokuwa nahangaika kufungua akaunti ya blogi.

Nilicheka kwasababu kadhaa, lakini kubwa ni kuwa nilitaka kwanza kujifariji mimi mwenyewe na kutokufadhaika sababu kufanya hivyo ingekuwa hatua ya kwanza ya kuanguka kwangu, lakini pia kwanini nifadhaike kwa maoni ya mtu mwingine asiyejua kilichoko kichwani mwangu?

Nilimjibu rafiki yangu kwa kumwambia kuwa, mimi binafsi ninaamini kabisa kuwa ninajua ninachokifanya, kwahiyo huenda pale watakapoona kuwa nimeishia, ndio ulikuwa mwisho wa nilichokuwa nimefikiria kukifanya, lakini pia nilimuuliza kuwa je, ikitokea hivyo, kwani mimi nitakuwa mtu wa kwanza kuanguka au nitakuwa wa mwisho? Binadamu gani ambaye aliwahi kufurahi daima bila kukasirika kwanza?

Siwezi kusema kuwa kauli ya rafiki yangu yule ilitimia au laa, maana ninachokifanya sijajua kama kina mchango gani katika jamii, lakini pia siwezi kusema kuwa mtazamo wangu ulitimia au laa sababu pia sina uhakika kuwa ninachokifanya kiko sahihi au laa, lakini jambo pekee nililo na uhakika nalo ni kuwa najua ninafanya nini na kwa ajili ya nini.

Ndio, najua natumia fursa yangu kushirikiana na jamii ama kujadili kile ninachoona kuwa kingekuwa namna fulani kingekuwa sahihi zaidi au vibaya, na hilo ndilo lilikuwa lengo langu. Kuishirikisha jamii katika maoni yangu. na ninafanya hivyo sababu najua kuwa maoni yangu ni sehemu muhimu katika mchakato wa maisha kwa ujumla.

Turejee katika somo langu la Utandawazi na imani ya kuwa Watanzania hatuwezi. Hapa kuna maswali kadhaa ambayo pengine nivyema tukajiuliza likiwemo nililouliza awali kuwa, ni nani alisema hatuna uwezo? Mara ngapi tumethubutu na tukashindwa na ni nani alisema kuwa kushindwa jaribio hata liwe la kumi ndio kufeli kila kitu?

Ukweli uliowazi ni kuwa Tanzania na mataifa mengine yanayotajwa kuwa masikini/ya ulimwengu wa tatu/yanayoendelea ni mataifa ambayo pia yamekuwa yakitajwa kuwa na rasilimali nyingi sana za aina tofauti tofauti. Je, ni kwa kiasi gani mataifa hayo yamethubutu kutumia kikamilifu rasilimali zake, hilo ni suala ambalo mara nyingi limekuwa na utatanishi kwasababu ya kile kinachodaiwa kuzidiwa nguvu na mataifa yaliyoendelea.

Lakini katika hilo hilo, ni nani ambaye amewapa uwezo huo wa zaidi hao tunaowaita mataifa yaliyoendelea kama sio mtazamo wao kuwa wanaweza na walishathubutu kufanya kile wanachoamini kuwa wanakiweza? Kwa Tanzania kwamfano, ni Watanzania wangapi ambao tunaamini kuwa kwa kupitia kilimo tu tunaweza kuwa taifa lenye kuuhitaji mfumo wa Utandawazi kuliko mtu mwingine yeyote yule?

Nakumbuka katika moja ya safari nilizobahatika kuongozana na kiongozi mmoja wa ngazi ya juu katika serikali yetu, kiongozi huyo aliwaeleza wananchi wa eneo fulani kuwa ikiwa Tanzania itatumia japo nusu tu ya uwezo wake katika shughuli za kilimo, basi itakuwa nchi yenye kunufaika zaidi na Shirikisho la Afrika Mashariki, na kwakweli nilikubaliana naye maana huo ndio ukweli wenyewe. Kwamba tufanye kile tunachostahili kukifanya kisha tuone matokeo yake.

Napenda tu kuwakumbusha marafiki zangu wa vyuo mbalimbali vikuu ndani ya Mbeya na nje ya Mbeya ikiwa hata nje ya nchi yetu kwa ujumla kuwa, Ukweli au uhalisia wa mazingira yanayotukabili hatuwezi kuupinga au kupingana nao bali kuukubali ili tupate nguvu za kukabiliana na hali halisi. Tukikubali kuwa sisi ni sehemu ya dunia ambayo mifumo ya kiuchumi ndio inayoiendesha na sio kinyume chake, tutafahamu kuwa wajibu wetu ni kujenga mazingira ya kutumia kila mfumo unaojitokeza kwakuwa uwezo tunao, nguvu tunazo, rasilimali tunazo na kila kinachohitajika tunacho.

Tukijiamini, tukajenga umoja, kuwa na msimamo thabiti juu ya rasilimali zilizoko ndani yetu, hakuna litakaloshindikana, tuthubutu tuone kama hilo haliwezekani, badala ya kuulalamikia mfumo huo, sera au mazingira yoyote yaliyoambatana nao.

TATIZO NI SISI WENYEWE NA SIO SERA, MFUMO WALA CHOCHOTE KILE.

Entry filed under: maskani.

Eti nchini Libya unaweza kumpinga Mungu ila si Gaddafi Mkutano wa wana-blogi wa kitanzania

2 Comments Add your own

  • 1. luihamu  |  November 4, 2006 at 12:31 pm

    Mzee Msangi umenena,nakubaliana na wewe kabisa.Kwanza umefanya kazi nzuri ya kuelimisha wale ambao hawajiamini.Mimi ninaamini katika KILIMO na Tanzania inaweza kujitoa katika matatizo ya umaskini kupitia kilimo.Nimejaribu na nitaendelea kutetea kilimo katika nchi yangu(Tanzania)katika blogu yangu.Badhi ya wanablogu wananipinga kabisa kuhusu swala la kilimo wakidai ya kwamba teknolojia ndiyo inayoongoza.Mzee Msangi vijana wapo tena wenye nguvu,tukiweza kuwapa vitendea kazi kama jembe,mbolea,mbegu n.k watashindwa kweli?kuliko kupoteza muda vijiweni.Tukiweza kuelimishana sanasana vijana tukubali kurudi vijijini na kukamata jembe,kilimo kitatutoa kimaisha na shilingi ya Tanzania itapanda juu.Amani na Upendo,Mungu ibariki Afrika Mungu ibariki Tanzania.

    Naomba kuwakilisha.

  • 2. ASM  |  August 12, 2012 at 2:57 pm

    SI VEMA KUDANGANYA KINACHOANGAMIZA NCHI CHANGA NI SERA CHAFU ZA IMF NA WB HAIWEZEKANA NCHI ZA G8 ZIPEWE ASILIMIA 99 YA MISAADA YA UCHUMI NCHI ZA KIAFRIKA ZIKIAMBULIA ASILIMIA MOJA AMBAYO HATA HIYO INAELEKEZWA NCHI ZA KASKAZINI ZINAZOCHIMBA MAFUTA NA AFRIKA YA KUSINI TANZANIA SI AJABU HUPATA 0.00000001 ASILIMIA SIJUI WAIFANYIE NINI

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Trackback this post  |  Subscribe to the comments via RSS Feed


Blog Stats

  • 35,058 hits
November 2006
M T W T F S S
 12345
6789101112
13141516171819
20212223242526
27282930