Archive for November, 2006

Karibu Dar Mjomba

Hivi karibuni, nilibahatika kutembelea ‘Tanzania’, nikimaanisha jiji la Dar es salaam (mnashangaa!! shauri lenu, si hata vyombo vya habari husema sijui Joji Kichaka kamwaga misaada Dar, wakimaanisha Bongo au Tanzania? Shauri lenu), Basi bwana, ile kuwasili nikapata mapokezi makuuuuubwa kama nanihii vile (utajaza mwenyewe).

Makaribisho hayo yaliambatana na risala niliyosomewa na ka-mjomba kangu kamoja kati ya vi-mjomba vyangu lukuki vilivyozamia jijini humo. Risala ya kamjomba kangu hako ilikuwa kama ifuatavyo:-

KARIBU DAAS’LAM MJOMBA.
Mjomba tunapenda kukukaribisha sana ndani ya jiji hili la Daas’lam, aka Bongo. Na tunakupa pole kwa safari ndeeefu ya kutoka huko madongo poromoka ulikotokea.

Mjomba, uliposhuka tu uliniuliza kama pale tuliposhukia ni stendi au shule na ikiwa ni shule, ni shule gain ambayo ina yunifomu mchanganyiko? Sikutaka kukujibu swali lako maana nilitaka uje nikueleze kwa utuo tukiwa nyumbani.

Mjomba hapa jijini ni vigumu sana kujua kiwango cha shule tulizonazo kwa kuangalia yunifomu, maana zipo za kila aina. Kuanzia makahaba, wezi, vibaka, waganga wa kienyeji, wauza bar, wauza mikaa na kila mtu ana yunifomu yake. Kifupi ni kuwa hapa jijini yunifomu ni vazi la kawaida kabisa na wala halimaanishi kuwa mwenye nayo anasoma au laa, chunga sana anaweza kuwa kahaba pia.

Mjomba pia uliposhuka nilikutahadharisha juu ya matumizi ya simu sasa nikueleze kwa utuo. Ndani ya jiji hili mjomba, watu huamini kuwa wao ndio wanaojua sana matumizi ya simu, na nyie wakuja toka huko madongo kwikwikwi hamjui matumizi yake.

Inakubidi ukipigiwa simu au ukitaka kusoma meseji basi uangalie kwanza mazingira yaliyokuzunguka, angalia kushoto na kulia kwanza kama unataka kuvuka barabara vile kasha ndio ufikie uamuzi.

Mjomba, ukiwa ndani ya Dar, maisha si magumu kama watu wanavyodhania, kwasababu unachotakiwa kuwa nacho kichwani ni kipaji cha Usanii, Uongo, Utapeli, kwa maana hayo humfanya mtu kuishi atakavyo jijini hapa. Zaidi ya asilimia 80 ya wakazi wa hapa huo ndio mfumo unaowaweka hapa mjini.

Kingine ambacho kinaweza kukuacha midomo wazi mjomba, ni kuwa ingawa inaaminika kuwa Dar ina wajanja kibao, lakini ukweli ni kuwa kasi ya ongezeko la wajanja inaenda sambamba kabisa na kasi ya ongezeko la wapuuzi, wajinga, wapumbavu na washamba wa kila aina.

Akiongezeka mjanja mmoja leo, jua kuna mahali kaongezeka pia mjinga mjinga mmoja huko kona Fulani Fulani. Wenyewe sisi wa mjini tunawaita Walugaluga. Fikiria ule mchezo wa karata tatu mjomba uliokuwa unatuhadithia wakati sisi wadogo kuwa mliucheza enzi hizo mko vijana? Basi wapo jamaa wanaliwa hadi leo hii.

Jambo zuri sana kwako wewe, maana nimesikia una mpango wa kutafuta Chombo cha kukurahisishia usafiri (na ni vyema ukajua kuna magari na vyombo vya kurahisisha usafiri mjomba), ni kuwa, ukiwa na gari unatakiwa tu uwe unajua unakoenda, kunyoosha gari barabarani na kukata kona. Si lazima kujua sheria za barabara, maana si mahali pa kuzi-apply hapa mjomba.

Dah!! naona ushaanza kusinzia mjomba, kutokana na uchovu. Nilikuwa na salamu kutoka kwa wajomba zako wengine, lakini nadhani watakutumia salamu zao kupitia sanduku la maoni maana hawataweza kuonana nawe laivu, na pia siwezi kuziwasilisha kwako maana ushaanza kusinzia.

Karibu Daa’slam Mjomba.

November 30, 2006 at 3:04 pm Leave a comment

Wasamaria wetu na usamaria wa vyombo vya habari

“Sadaka ni SIRI, kama umetoa kwa mkono wa kushoto, basi hata ule wa kulia usijue kuwa umetoa nini, sio jambo la kutangaza kwa maana unapotoa unamtolea Mungu, naye anakuona, ukitoa kwa ajili ya kujipatia ufahari basi haiwezi kubarikiwa sadaka yako
=======================

Kwa muda wa kutosha tu nimekuwa nikiendelea kufuatilia hali ya kuongezeka kwa Wasamaria wema na Usamaria wema wao hapa nchini kwetu. Watu wenye moyo wa kusaidia yatima, wasio jiweza, wanaoishi katika mazingira magumu na hata hawa ndugu zetu ambao wanaishi na VVU.

Kwa wale ambao wamekuwa wakiyaona bila shaka wataungana nami kukiri kuwa hali hii imezidi kushamiri zaidi hasa katika kipindi hiki ambapo teknolojia pia imekuwa ikiwezesha usambazwaji na upatikanaji wa habari katika kona mbalimbali ndani na hata nje ya nji yetu hii.

Hata hivyo (sijui kwasababu nilizaliwa kuona mambo kinyume au vipi), kuna jambo ambalo nimekuwa kila nikilitafakari, basi limekuwa likinisukuma kuhoji uhalali wa misaada hiyo na watoaji wake. Hivi MSAADA sio sawa tu na SADAKA? Sasa kuna haja gani kwa mtoaji kuhanikiza “Jamani kesho naenda kutoa misaada mahali fulani mje mnione” au Leo nimetoa msaada kwa akina fulani jamani oneni”

Kwa wafuatiliaji wa taarifa zetu za habari katika vyombo vyetu mbalimbali, limekuwa jambo la kawaida kila siku (Narudia tena KILA SIKU), kukutana na habari za ama fulani kesho atatoa msaada sehemu fulani, au fulani leo katoa misaada sehemu fulani, na habari hizo hufuatiwa na mlolongo wa maelezo kibaaaaaaao yote yakimsifia mtoa msaada huyo kufikia hata hatua ya kupachikwa uheshimiwa.

Ukisoma kwa undani au kusikiliza kwa undani maelezo ya mhusika huyo, mengine huweza hata kukuletea maswali mengi sana kuliko uhalisia wa wasifu wake, na ukweli ndio uko hivyo. Kuwa wengi wa “Waheshimiwa Matajiri” watoa misaada, ni wale ambao utajiri wao huo una maswali mengi zaidi juu ya upatikanaji wake kuliko ukweli wa mambo ambao wananchi wanatakiwa kuuamini.

Ni watu ambao wamewageuza binadamu wenzao “migodi” kwa ajili ya kusakia fedha zao hizo na pia wamewageuza binadamu wenzao “majosho” kwa ajili ya kusafishia fedha zao chafu (Dirty money).

Wakati fulani nilipokuwa bado mdogo, nakumbuka maneno niliyoyanukuu hapo juu, kuhusiana na kitu msaada (unadhani ni tofauti na sadaka?) Sasa hawa jamaa zetu ambao wanatoa sadaka, ubani sijui, misaada nk, huku wakiwa wameitisha maluninga na magazeti kwa ajili wawatangaze kwa kile walichotoa, wao wanatoa kwa ajili ya kusaidia kweli au kwa lengo la kupewa sifa za duniani?

Hivi ikitokea tukachachamaa na kumkaba mmoja wao na kisha tukamwambia ashike kitabu kitakatifu na akiri kuhusu utajiri wake, ambao ana tusaidia, ni wangaopi watathubutu kufanya hivyo? Hivi msaada ukitolewa kimya kimya, kwa mtu kujiendea zake akatoa msaada na kisha akajirudia dukani au ofisini na hata nyumbani kwake, huo msaada hautakuwa msaada kweli? Hivi ni wangapi wanapowanunulia watoto wao nguo au kuwatoa out hujitangaza? Ebo! ukiwa na utajiri kusaidia wasio nacho si wajibu wako kwani?

Tena wengine unakuta wanachangisha na kuchangisha fedha kwa ajili ya kwenda kutoa misaada hiyo, na kisha kujipangia katika fedha hizo za michango kuwa mimi nitatumia kiasi fulani kwa ajili ya kuniwezesha kupeleka misaada sehemu fulani, Ebo! ndio misingi ya misaada hiyo jamani?

Nauliza tu lakini, msije mkanitoa roho maana hapa tayari kuna watu wakisoma hapa najua wataanza kuomba kila aina ya dua ili nifie mbali maana na nimewagusa pabaya. Ninachotaka kusema hapa ni kuwa, kama unatoa kwa ajili ya kuonyesha uchungu wako, basi ni vyema uchungu huo akauona Mungu aliyekuwezesha kuupata utajiri huo, na sio binadamu mwenzio akusifu.

Samahani wote nitakaokuwa nimewagusa, japo ninaamini kuwa kwasababu nyie ni waungwana na “mnaomtolea Mungu wenu” mtakuwa mmenielewa namaanisha nini. Ni vijimambo tu, ila vinanikera kweli kweli

November 13, 2006 at 5:25 pm 2 comments

ya ditopile: tulishindwa kusoma ishara za nyakati?


Duh, ni kama vile yametimia, kwasababu tuliokuwa tukiyaona haya mambo kwa mtazamo wa kipekee, lazima tuseme kuwa tulijua kuwa hili ndilo litakalofuatia, na kwakweli naweza kukiri kuwa haikunishangaza sana niliposikia taarifa hizi jana.
Alikuwepo sijui RPC wa wapi vile nasikia aliwachapa WAPIKAKULA bakora, kama vile anaviadabisha vitegemezi vyake nyumbani. Wakaibuka sijui wale maraisi wa wilaya (DCs), sikumbuki wangapi vile nao tukasikia wamewalamba watu vibao.
Tupo ambao tulihoji, tupo ambao tulitilia mashaka kasi hii, lakini nani alisikia? Na matokeo ya kutokufungwa gavana huku tukijua wazi kuwa asilimia kubwa ya magari yaliyoko katika msafara huu hayako salama, ndio haya sasa ya kina komredi Dito.
Huyu huyu ambaye ni (au alikuwa?) mkuu wa mkoa wa Tabora, huyu huyu ambaye aliwahi kusema kuwa yeye ni Born Town, kwa maana kazaliwa Dar, kasomea shule ya msingi Dar, Sekondari Dar na kila kitu Dar. Na ndio hukohuko ambapo amefanya madudu ya hali ya juu. Soma taarifa za kuhusu ufedhuli wake alioufanya wa kuua raia (mpigakura) kisa? Eti nasikia alikwangua VX lake.
Bonyeza hapa kusoma kwa kiingereza, na hapa na hapa kwa kiswahili.
Picha kwa hisani ya kaka Michuzi

November 6, 2006 at 9:20 am 8 comments

Mkutano wa wana-blogi wa kitanzania

Tembeleeni jumba la Jeff Msangi linalokwenda kwa jina la HARAKATI kisha mupate ujumbe huu, kuhusu kichwa hapo juu.

November 3, 2006 at 11:49 am Leave a comment

UTANDAWAZI: tatizo ni mfumo, sera, sisi au nini?

Hivi karibuni nilibahatika kukaa mahali na baadhi ya marafiki zangu ambao ni wanafunzi wa vyuo mbalimbali vya elimu ya juu mkoani hapa. (Tuna tawi la Mzumbe, T.I.A na Chuo Huria), na katika hali ambayo haikuwa rasmi, tulijikuta tukiingia katika mjadala kuhusiana na hiki kitu UTANDAWAZI.

Kwa muda wakati maongezi hayo yanaanza, nilijikuta nikikaa kimya kiasi kwa lengo la kutaka kuwapa nafasi wataalamu hao kujimwaga nione umahiri wao katika kulijadili suala hili ambalo licha ya kuwa limeshakuwa la kawaida masikioni na akilini mwetu, bado limeshindikana kuzoeleka kwa jamii mbalimbali duniani.

Hoja kubwa waliyokuwa wakiipa msisitizo katika majadiliano yao, na ambayo karibu sehemu zote linakojadiliwa suala hilo utakuta watu wakiizungumzia, ilikuwa ni ile ya kumezwa kwa baadhi ya mataifa, Tanzania ikiwa mojawapo katika mfumo huo na hivyo kuwepo kwa hali ya kunufaisha baadhi ya mataifa hususan yaliyo matajiri, ambayo ndio yenye kuonekana kuwa yalianzisha mfumo huo wa kiuchumi.

Hata hivyo, ilifikia wakati nikalazimika kuwauliza jamaa zangu maswali kadhaa, kubwa kabisa likiwa ni “Kwanini wanadhani kuwa Tanzania haina uwezo wa kuendana na hali ya ushindani katika mfumo huo?, Nini kifanyike katika wakati huu tuliopo kuhusiana na mfumo huu?”

Cha kushangaza sana, narudia tena, “chakunishangaza sana” ni kuwa, wapo waliosema kuwa Tanzania haiwezi kushindana kwasababu haina uwezo huo na hivyo wakashauri kuwa ni vyema ikajitoa katika mfumo huo. Nikajiuliza, KUJITOA? HATUNA UWEZO? kweli ndivyo ilivyo?

Hali hii ilinifanya nianze kuwaza mambo kadhaa kichwani mwangu ikiwa ni pamoja na uelewa tulionao Watanzania katika mifumo inayotawala dunia, namna inavyoweza kujitokeza, mchango wa mwanadamu katika kuibuka kwa mifumo hiyo na mchango wake vile vile katika kuidhibiti.

Sanjari na hayo, nilianza kuwaza na kuwazua pia juu ya hii hali ambayo imekuwa sugu kati yetu Watanzania ya kuamini kuwa kuna baadhi ya mambo ambayo hatuyawezi na kwamba hata kama tutathubutu, basi sisi ni watu wa kushindwa tu. Nitaanza kujadili hilo la juu kwanza (kulingana na ufahamu wangu na sio kulingana na hoja za waliokuwa washiriki wa mjadala huo wa kwenye viti vya plastiki, vikao ambavyo awali viliitwa vya kwenye stuli ndefu)

Biashara ya Utumwa, mfumo wa Ukoloni, Ubaguzi wa rangi na mingine mingi ambayo wengi wetu tumekuwa tukijifunza katika somo la Historia, ni miongoni mwa mifumo ambayo kwa nyakati mbalimbali iliendesha dunia kwa vipindi tofauti tofauti huku ikimalizika kutokana na kuibuka kwa mfumo mwingine.

Kwa bahati mbaya sana, katika uelewa wangu, sijawahi kuona kwa hakika na nikathibitisha kuwa mifumo hiyo au mfumo fulani mmoja wapo ulitokana na jitihada za mwanadamu kama yeye, bali mazingira halisi yanayomzunguka na mabadiliko ya kimaendeleo katika nyanja za Uchumi, sayansi & teknolojia, utamaduni na nyingine kadhaa wa kadhaa.

Hali hizi ingawa tunawezaq kupingana kutokana na mitazamo tofauti tofauti, bado kwangu mimi naamini kabisa kuwa ni hali au mabadiliko ya kiasilia (wenye lugha zao huita nature), na kwa mujibu wa uelewa wangu, hizi ni halui ambazo haziko ndani ya uwezo wa binadamu kuzidhibiti. Binadamu anaweza akadhibiti kwamfano kutokuharibu mazingira sababu hilo sio suala la kiasilia, lakini hawezi kuzuia kubadilika kwa hali ya hewa na hata misimu sababu hilo ni suala la kiasilia zaidi.

Naam, tukirejea katika mada yangu leo hii, baada ya kuona hivyo hapo ndipo tunapokuja kuona kuwa kumbe hata kutoka katika zama za ubeberu, ubepari, ukoloni, utumwa na mifumo mingine mingi, hayakuwa mabadiliko yaliyowekwa na mwanadamu (man made changes) kama ambavyo tunataka kujiaminisha, bali yalikuwa mabadilikoya kiasilia. Na ni kutokana na iman hiyo mimi naamini hata katika suala la Utandawazi na mifumo mingine tunayoiona leo hii kuwa haifai, ni suala asilia.

Wanafalsafa mbalimbali walioishi miaka ya nyuma na kujihusisha na falsafa za kiuchumi au mifumo ya maendeleo ya kiuchumi, kwa nyakati mbalimbali waliwahi kugusia suala la mabadiliko ya mifumo ya kiuchumi duniani, mingi kati ya hiyo mifumo ikiwa imeelezewa kwanini itatokea na pengine wakati gani, hivyo basi suala hili halikuwa la jana wala juzi.

Kwa kuzingatia maelezo yangu hayo mafupi (kumbuka yanatokana na mtazamo wangu), ni wazi kabisa kuwa Tanzania kama nchi au kama kitu chochote kile kilichoko humu duniani, ni vigumu kwake kujadili suala la kujitoa katika mfumo huu, kama ambavyo ni vigumu kwa nchi au mtu yeyote katika dunia hii.

Suala la mifumo ya kiuchumi ingawa ni suala ambalo limekuwa la kawaida kutokana na kusomwa sana na kujadiliwa pengine sana tu, bahati mbaya sana halijawahi kuwa suala la kawaida na la kuzoeleka masikioni mwa watu na hususan sio tulioko nchi za ulimwengu wa tatu au zinazoendelea.

Na kwa mtazamo wangu ni kuwa penye matatizo ni kuwa watu hatu[pendi kukubaliana na ukweli kuwa ndivyo ulivyo badala yaker tunaupinga ukweli. Ni vyema tukaelewa kuwa, katika falsafa ya jkawaida kabisa ya maisha ya kila siku, moja kati ya mambo yanayoweza kukuwezesha kukabiliana na mazingira fulani yaliyokuzunguka ni kwa kuyakubali kwanza na si vinginevyo.

Sijui wachumi waliobobea kama wanaweza kunithibitishia hili au laa, lakini kwangu mimi, kwa kile ambacho nimekuwa nacho kichwani, sijawahi kusikia kama kuna mfumo ambao uliwahi kuibuka au kuibuliwa na kisha ukafurahiwa na jamii kwa ujumla kuwa uko sahihi kabisa. Sijawahi na sijui kama upo, labda kama nilivyoomba wanauchumi waliobobea wanieleze.

Kile ambacho kimekuwa kikiendelea duniani, ni kwa wanauchumi hao kubobea katika kuweka kile wanachokiita mikakati ya kuingia mfumo fulani, mikakati ambayo mara nyingi imekuwa ikizidiwa na nguvu ya uhalisia wa soko na mahitaji ya soko la dunia kwa ujumla. Lakini pengine licha ya kutambua hili, ingali inanishangaza sana kuwa wataaluma wetu wa aina hii, hawajawahi pia kukaa na kuweka mkakati wa kuiwezesha dunia kukubaliana na hali halisi hivyo inapoibuka hali fulani wakakubaliana kuendana nayo.

Tukija katika hoja ya Watanzania kutokuwa na uwezo. Hoja hii kwakweli ndio ambayo imekuwa ikinishangaza sana. Ni hoja ambayo imekuwa ikinishangaza sana kutokana na wale wanaotoa hoja hii kuitoa kwa kiwango cha kujionyesha wazi kuwa tungali na upeo mdogo sana katika kuyachambua mazingira tuliyomo.

Hivi mwenye uwezo wa kuuthibitishia umma juu ya uwezo wako binafsi ni nani kama sio wewe, na unategemea nini ikiwa mwenyewe tu huutambui uwezo ulionao? Mwaka jana wakati naanza ku-blogi, rafiki yangu mmoja aliniambia kuwa nilikuwa ninapoteza muda wangu bure tu sababu singeweza sio tu kuiendeleza blogi yenyewe, bali kutokupata wa kunisikiliza, na alinifanya nikacheka sana pale nilipokuwa nahangaika kufungua akaunti ya blogi.

Nilicheka kwasababu kadhaa, lakini kubwa ni kuwa nilitaka kwanza kujifariji mimi mwenyewe na kutokufadhaika sababu kufanya hivyo ingekuwa hatua ya kwanza ya kuanguka kwangu, lakini pia kwanini nifadhaike kwa maoni ya mtu mwingine asiyejua kilichoko kichwani mwangu?

Nilimjibu rafiki yangu kwa kumwambia kuwa, mimi binafsi ninaamini kabisa kuwa ninajua ninachokifanya, kwahiyo huenda pale watakapoona kuwa nimeishia, ndio ulikuwa mwisho wa nilichokuwa nimefikiria kukifanya, lakini pia nilimuuliza kuwa je, ikitokea hivyo, kwani mimi nitakuwa mtu wa kwanza kuanguka au nitakuwa wa mwisho? Binadamu gani ambaye aliwahi kufurahi daima bila kukasirika kwanza?

Siwezi kusema kuwa kauli ya rafiki yangu yule ilitimia au laa, maana ninachokifanya sijajua kama kina mchango gani katika jamii, lakini pia siwezi kusema kuwa mtazamo wangu ulitimia au laa sababu pia sina uhakika kuwa ninachokifanya kiko sahihi au laa, lakini jambo pekee nililo na uhakika nalo ni kuwa najua ninafanya nini na kwa ajili ya nini.

Ndio, najua natumia fursa yangu kushirikiana na jamii ama kujadili kile ninachoona kuwa kingekuwa namna fulani kingekuwa sahihi zaidi au vibaya, na hilo ndilo lilikuwa lengo langu. Kuishirikisha jamii katika maoni yangu. na ninafanya hivyo sababu najua kuwa maoni yangu ni sehemu muhimu katika mchakato wa maisha kwa ujumla.

Turejee katika somo langu la Utandawazi na imani ya kuwa Watanzania hatuwezi. Hapa kuna maswali kadhaa ambayo pengine nivyema tukajiuliza likiwemo nililouliza awali kuwa, ni nani alisema hatuna uwezo? Mara ngapi tumethubutu na tukashindwa na ni nani alisema kuwa kushindwa jaribio hata liwe la kumi ndio kufeli kila kitu?

Ukweli uliowazi ni kuwa Tanzania na mataifa mengine yanayotajwa kuwa masikini/ya ulimwengu wa tatu/yanayoendelea ni mataifa ambayo pia yamekuwa yakitajwa kuwa na rasilimali nyingi sana za aina tofauti tofauti. Je, ni kwa kiasi gani mataifa hayo yamethubutu kutumia kikamilifu rasilimali zake, hilo ni suala ambalo mara nyingi limekuwa na utatanishi kwasababu ya kile kinachodaiwa kuzidiwa nguvu na mataifa yaliyoendelea.

Lakini katika hilo hilo, ni nani ambaye amewapa uwezo huo wa zaidi hao tunaowaita mataifa yaliyoendelea kama sio mtazamo wao kuwa wanaweza na walishathubutu kufanya kile wanachoamini kuwa wanakiweza? Kwa Tanzania kwamfano, ni Watanzania wangapi ambao tunaamini kuwa kwa kupitia kilimo tu tunaweza kuwa taifa lenye kuuhitaji mfumo wa Utandawazi kuliko mtu mwingine yeyote yule?

Nakumbuka katika moja ya safari nilizobahatika kuongozana na kiongozi mmoja wa ngazi ya juu katika serikali yetu, kiongozi huyo aliwaeleza wananchi wa eneo fulani kuwa ikiwa Tanzania itatumia japo nusu tu ya uwezo wake katika shughuli za kilimo, basi itakuwa nchi yenye kunufaika zaidi na Shirikisho la Afrika Mashariki, na kwakweli nilikubaliana naye maana huo ndio ukweli wenyewe. Kwamba tufanye kile tunachostahili kukifanya kisha tuone matokeo yake.

Napenda tu kuwakumbusha marafiki zangu wa vyuo mbalimbali vikuu ndani ya Mbeya na nje ya Mbeya ikiwa hata nje ya nchi yetu kwa ujumla kuwa, Ukweli au uhalisia wa mazingira yanayotukabili hatuwezi kuupinga au kupingana nao bali kuukubali ili tupate nguvu za kukabiliana na hali halisi. Tukikubali kuwa sisi ni sehemu ya dunia ambayo mifumo ya kiuchumi ndio inayoiendesha na sio kinyume chake, tutafahamu kuwa wajibu wetu ni kujenga mazingira ya kutumia kila mfumo unaojitokeza kwakuwa uwezo tunao, nguvu tunazo, rasilimali tunazo na kila kinachohitajika tunacho.

Tukijiamini, tukajenga umoja, kuwa na msimamo thabiti juu ya rasilimali zilizoko ndani yetu, hakuna litakaloshindikana, tuthubutu tuone kama hilo haliwezekani, badala ya kuulalamikia mfumo huo, sera au mazingira yoyote yaliyoambatana nao.

TATIZO NI SISI WENYEWE NA SIO SERA, MFUMO WALA CHOCHOTE KILE.

November 3, 2006 at 10:12 am 2 comments


Blog Stats

  • 35,058 hits
November 2006
M T W T F S S
 12345
6789101112
13141516171819
20212223242526
27282930