TANZANIA: Tumechoshwa na mnavyowafanyia raia wetu

September 3, 2006 at 5:56 pm 1 comment

HATIMAYE mgogoro uliodumu kwa siku takriban mbili mpakani mwa Tanzania na Zambia umemalizika huku serikali ya Tanzania ikiwaonya jirani zao hao kutorudia tena vitendo vya kuwanyanyasa raia wake.

Mgogoro huo ambao ulisababisha kujeruhiwa kwa watu kadhaa wa pande zote mbili sanjari na hasara ya mamilioni ya fedha, ulimalizika baada ya mkutano baina ya wawakilishi wa serikali za pande zote mbili.

Akiwahutubia wananchi waliokuwa wamefurika nje ya kituo cha Polisi cha Tunduma kufuatilia hatma ya sakata hilo, mkuu wa mkoa wa Mbeya, ambaye aliongoza ujumbe toka Tanzania, alisema kuwa mkutano baina yao ulikuwa wa mafanikio baada ya pande husika kukubaliana masharti waliyowekeana.

Alisema kuwa, katika mkutano huo yeye kwa niaba ya serikali ya Tanzania, aliwasilisha malalamiko mawili makubwa ambayo ujumbe wa Zambia uliyakubali nha kuahidi kuyafanyia kazi.

Aliyataja malalamiko hayo kuwa ni kupigwa risasi kwa raia wa Tanzania pamoja na kuuawa kwa mfanyibiashara Lucas Msuya, ambaye kifo chake ndicho kilisababisha machafyuko mpakani hapo.

Mkuu wa mkoa ambaye alikuwa ameambatana na Inspekta jenerali wa Polisi nchini, Bw. Said Mwema, alisema kuwa baada ya kuwasilisha malalamiko hayo, ujumbe wa Zambia ulikiri kuwepo kwa mapungufu yaliyosababisha hali hiyo, na kuahidi kulifanyia kazi tatizo hilo kwa kuanza kukichunguza kituo cha Polisi cha Nakonde.

Aliongeza kuwa, upande wa Zambia pia ulikubali kutuma wataalamu wake wa upasuaji kwa ajili ya kuja eneo la Nakonde kwa ajili ya kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu Msuya, ambaye inasadikika kuwa kifo chake kilitokana na mateso makali.

Ujumbe huo ambao utatoka katika jiji la Lusaka, utashirikiana na wataalamu kutoka serikali ya Tanzania, ambao wataongozwa na Bw. Robert Manumba, ambaye ni Mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai nchini.

Hata hivyo, mkuu wa mkoa aliongeza kuwa, licha ya kufikia makubaliano hayo, ujumbe wa Tanzania pia uliwaeleza wazi kuwa umechoshwa na vitendo vya uonevu ambavyo wamekuwa wakifanyiwa raia wake pindi wanapokuwa upande wa Zambia, na wakawatahadharisha kuwa ikiwa vitaendelea subira huenda ikawashinda Watanzania.

“Niliwaeleza wazi kuwa hali hii imetuchosha na kwamba ikiwa watarudia…….., mnajua” alisema mkuu wa mkoa huku akishangiliwa na maelfu ya wakazi waliokuwa eneo hilo.

Kwa upande wake Inspekta jenerali Mwema, akiongea na wananchi wa eneo hilo, alisema kuwa ujio wake ulikuwa ni kudhihirisha jinsi ambavyo serikali yao imekuwa ikiwajali, na akawashukuru sana kwa kufuata maelekezo ya mkuu wa mkoa pale alipowataka kuwa watulivu kwakuwa serikali inalifanyia kazi tatizo hilo.

“Wakazi wa Tunduma mmeonyesha jinsi gani Tanzania inastahili kuwa nchi ya kuigwa, uvumilivu, uelewa na subira yenu yamekuwa mambo ya muhimu sana katika kumaliza tatizo hili, na kwa niaba ya jeshi la Polisi na serikali kwa ujumla, nawaahidi kuwa matatizo kama haya yataendelea kudhibitiwa” alisema

Katika tamko hilo, serikali pia ilikanusha kuwepo kwa raia wa Tanzania waliiofanyiwa vitendo vya uonevu nchini Zambia, na ikaruhusu rasmi kufunguliwa kwa mpaka baina ya nchi hizi mbili, ambao jana ulikuwa umefungwa japo haikuwa rasmi.

Mara baada ya tamko hilo, wananchi waliokuwa wamefurika eneo hilo, walitawanyika huku wakiwa wanashangilia, na muda mfupi baadae makundi ya raia wa Zambia yalionekana yakivuka mpaka kuingia Tanzania kwa ajili ya kujipatia mahitaji yao, huku wakikaribishwa na Watanzania katika maeneo yao ya biashara.

Entry filed under: maskani.

Machafuko mpakani mwa Tanzania na Zambia Sauper=Mzushi……..IRINnews nao je?

1 Comment Add your own

 • 1. Merali Chawe  |  September 11, 2006 at 6:45 pm

  Kweli watanzanzatumechoka na hatutaki tena kunyanyaswa.
  Nakumbumbuka Msangi ulikuwa ni mmoja kati ya waandishi walioingia katika mji mdogo wa Tunduma mkiwa na gari inayopendwa wanaiita balloon au puto huku mkilazimika kujitambulisha kuwa nyinyi Watanzania na ni waandishi wa habari, hakika mkiwa mmenyoosha juu kwa bidii notebook zenu kiroho kikiwadunda,lakini mngefanyaje ilikuwa ni lazima muingie katika moto,lakini mtoke mkiwa wazima, kwa kuwa Muandishi wa Habari anayoifuatilia na kisha akafa vitani huyo kamwe siyo shujaa kwa kuwa wananchi wataikosa habari aliyoifuata.
  Habari ni nzuri hakika inayonyesha jinsi watanzania walivyochoka kunyanyaswa,.Kweli watanzania kuuawa na wengine kujeruhiwa si jambo na halipendezi,mbaya kwa madai ya kudhaniwa kuwa alinunua mali ya wizi.
  lakini nilikuwa najiuliza huyu Mtanzania alikamatwa na kukaa huko siku saba hadi anakufa, sijui polisi wa tanzania walikuwa wapi.Hii kweli iliwafanyawatanzania wawe na haki ya kuchukia na kutaka kulipiza kisasi kwa kile kilichotokea kwa mwenzao.
  Lakini Bwana Msangi hujasema matukio ya wizi na uchomaji wa mali zilizokuwa zinadhaniwa ni Zambia ulikuwa haki,je ni haki kutumia machafuko kufanya uhalify, hapa naona kunatatizo la kiusalama kwa kuwa waathirika wa wizi na uchomaji ule hawakuwa wazambia tu hata watanzania walipoteza mali zao.
  Nikukumbuka naona vita kweli haifai kweli amani ya Tanzania idumu daima, heko mwanajeshi wangu maana ulinidhihirishia ukamanda ingawa kuondoka ilibidi msindikizwe mkiwa chini ya ulinzi wa polisi, haya mimi nipo kwnye ya nyuma hapa na mimi ndio natoka Tunduma nawahi Mbeya kilomita 100 kutoka hapa, mji ni shwari kiasi na wazambia wameanza kuingia huku kuja kutafuta chakula na mahitaji mengine ila yule Mkongo ametaka magunia ya dagaa yalioibwa yarudishwe vinginevyo atamtoa roho, unajua nini kimetokea…

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Trackback this post  |  Subscribe to the comments via RSS Feed


Blog Stats

 • 35,058 hits
September 2006
M T W T F S S
 123
45678910
11121314151617
18192021222324
252627282930