Machafuko mpakani mwa Tanzania na Zambia

September 3, 2006 at 5:54 pm Leave a comment

WATANZANIA wawili wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa na askari wa Zambia kufuatia machafuko mpakani mwa Tanzania na Zambia ambayo jana yaliingia katika siku ya pili.

Sanjari na mauaji hayo, mali zenye thamani ya mamilioni ya shilingi zimeharibiwa yakiwemo magari matatu yaliyokuwa na mali mbalimbali ambayo yaliteketezwa kwa moto.

Waandishi wa habari walipokuwa njiani kuelekea eneo hilo walishuihudia raia wa Tanzanaia waliokuwa wameweka doria barabarani kukagua magari ili kuona kama yamebeba Raia wa Zambia na pindi walipowabaini waliwashusha na kuwapiga.

Katika eneo la kituo cha polisi Tunduma, maelfu ya wananchi wa mji huo walishuhudiwa wakiwa
wamefunga shughuli zao huku wakikabiliana na askari Polisi ambao walikuwa wakiwazuia kuvuka mpaka na kuingia Zambia kwa ajili ya kulipa kisasi cha kuuawa kwa Mtanzania mwenzao.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyopatikana kutoka kwa wasemaji mbalimbali wa serikali waliokuwa eneo la tukuio, chanzo cha mapigano hayo ni kuuawa kwa Mtanzania mmoja mfanyibiashara, Bw. Lucas Msuya, ambaye alikabidhiwa kwa Polisi wa upande wa Zambia kwa ajili ya mahojiano.

Ilielezwa kuwa hatua hiyo ilikuja baada ya mfanyibiashara huyo kutuhumiwa kukutwa na deki ya televisheni ambayo aliuziwa, ikidaiwa kuwa iliibiwa nchini Zambia.

Habari zaidi zilieleza kuwa mara baada ya mfanyibiashara huyo kutuhumiwa kukutwa na mali ya wizi, alijisalimisha kituo cha Polisi cha Tunduma ambapo Polisi wa upande wa Tanzania baada ya kumhoji waliamua kumkabidhi kwa askari wa upande wa Zambia kwa ajili ya kumalizana naye.

Hata hivyo, katika hali ya kushangaza, mara baada ya Askari hao wa upande wa zambia kukabidhiwa Mtanzania huyo kwa maandishi, inadaiwa kuwa walimtesa ikiwa ni pamoja na kumnyima chakula, huku wakimpa kipigo huku wakimtaka kueleza ziliko mali zingine ambazo zilidaiwa kuwa zilikuwa zimeibwa sanjari na deki aliyokutwa nayo.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo vya habari, ndugu wa marehemu waliokuwa wakimtembelea ndugu yao walithibitisha ndugu yao kuwa katika hali mbaya na hata walipotaka kumnunulia dawa kutokana na hali yake kuwa mbaya walipokea vitisho toka kwa askari wa Zambia hivyo kulazimika kuondoka.

Kutokana na mateso hayo, mfanyibiashara huyo ambaye alikuwa akijulikana kwa jina la Mangi mjini Tunduma, alipoteza maisha usiku wa kuamkia juzi na askari wa upande wa Tanzania walipotoa taarifa kwa ndugu wa marehemu kwenda kuchukua maiti, ndugu hao walikataa
wakidai kuwa ndugu yao ameuawa hivyo wanataka maelezo ya kina.

Hata hivyo, ndugu hao hawakupata maelezo hayo hali ambayo iliamsha hasira zao na za wananchi wa Tunduma kwa ujumla ambao walianza kujikusanya kwa lengo la kuvuka mpaka na kuingia Zambia kwa lengo la kulipa kisasi kutokana na kile wanachodai kuwa wamechoshwa na
uonevu wa Wazambia.

Huku wakiwa na bendera, mabango, na silaha za aina mbalimbali, wakiimba nyimbo za “tumechoshwa na uonevu huu tunataka haki” wananchi hao walianza kulipa kisasi hiccho kwa kuharibu mali za baadhi ya wakazi wa Zambia ambazo zilikuwa upande wa Tanzania, sanjari na
kuwapiga Wazambia waliokuwa upande wa Tanzania.

Mbali ya hilo, Watanzania wengine waliamua kuvuka mpaka ambapo walikutana na askari wa upande huo waliokuwa wakitumia silaha za moto ambapo hadi kufikia jana jioni Watanzania wawili walikuwa wameshajeruhiwa vibaya mmoja akiwa amepigwa risasi mbili za kifuani.

Kufuatia hali hiyo, serikali mkoani Mbeya ililazimika kuhamia mjini Tunduma kwa ajili ya kuweka hali shwari ambapo mkuu wa mkoa, kamanda wa polisi wa mkoa sanjari na vikosi kadhaa vya walinda usalama vilimwagwa katika eneo hilo.

Licha ya jitihada hizo, wananchi hao ambao waliendelea kuweka mgomo wa kurudi majumbani mwao ambapo walitanda katika njia na maeneo mbalimbali ya upande wa Tanzania huku wakivizia magari ya Wazambia kwa ajili ya kuwachukulia hatua.

Hata hivyo, wakati mkuu wa mkuu wa mkoa wa Mbeya Bw. John Mwakipesile, akiwapooza wananchi kwa kuwaeleza kuwa amewasiliana na uongozi wa mkoa wa Kasama na wale wa wilaya ya Nakonde, umbali wa km. 100, na kwamba wanakuja mpakani kwa ajili ya majadiliano, tayari
Wazambia kadhaa walishavamia nyumba za askari Polisi na kuharibu mali ambazo hazikuweza kujulikana thamani yake.

Hata hivyo kulikuwa na taarifa za kutatanisha kuhusu ujio wa viongozi wa serikali ya Zambia kwa ajili ya kufanya mazungumzo na uongozi wa Tanzania. Akielezea uatata huo Mkuu wa Mkoa alisema amefanya mawasiliano na viongozi hao lakini wamekuwa wakimapa majibu tafauti kila alipoulizwa mahali walipo.

Mbali ya nyumba za polisi, raia wengine kadhaa walikuwa wameshatawanyika katika sehemu kadhaa za Tanzania huku wakiendeleza uharibifu ikiwa ni pamoja na kuchoma nyumba, hali ambayo iliwapandisha Watanzania hasira zaidi na kuamua kuingia upande wa Zambia kwa ajili ya kufanya uharibifu.

Kwa mujibu wa mkazi mmoja wa Tunduma, Bi. Hidaya Mahamoud, hasira zao zinatokana na ukweli kuwa hii ni safari ya tatu ambapo Watanzania wanauawa na Wazambia ambapo mwaka jana Watanzania wawili waliuawa kwa kupigiliwa misalabani kwa mfano wa Yesu, likiwa ni tukio la pili baada ya jingine la miaka kadhaa iliyopita.

Hadi waandishi wa habari wanaondoka eneo la tukio, milio ya risasi ilikuwa ikiendelea kurindima
kutoka upande wa Zambia, huku askari Polisi na wale wa FFU kwa upande wa Tanzania wakiendelea kuwadhibiti wananchi wasivuke mpaka, kwa maelezo kuwa taratibu zinafuatwa ili kuliweka sawa tatizo hilo.

Entry filed under: maskani.

Siku ya Kublog Duniani TANZANIA: Tumechoshwa na mnavyowafanyia raia wetu

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Trackback this post  |  Subscribe to the comments via RSS Feed


Blog Stats

  • 34,787 hits
September 2006
M T W T F S S
 123
45678910
11121314151617
18192021222324
252627282930