Archive for September 3, 2006

TANZANIA: Tumechoshwa na mnavyowafanyia raia wetu

HATIMAYE mgogoro uliodumu kwa siku takriban mbili mpakani mwa Tanzania na Zambia umemalizika huku serikali ya Tanzania ikiwaonya jirani zao hao kutorudia tena vitendo vya kuwanyanyasa raia wake.

Mgogoro huo ambao ulisababisha kujeruhiwa kwa watu kadhaa wa pande zote mbili sanjari na hasara ya mamilioni ya fedha, ulimalizika baada ya mkutano baina ya wawakilishi wa serikali za pande zote mbili.

Akiwahutubia wananchi waliokuwa wamefurika nje ya kituo cha Polisi cha Tunduma kufuatilia hatma ya sakata hilo, mkuu wa mkoa wa Mbeya, ambaye aliongoza ujumbe toka Tanzania, alisema kuwa mkutano baina yao ulikuwa wa mafanikio baada ya pande husika kukubaliana masharti waliyowekeana.

Alisema kuwa, katika mkutano huo yeye kwa niaba ya serikali ya Tanzania, aliwasilisha malalamiko mawili makubwa ambayo ujumbe wa Zambia uliyakubali nha kuahidi kuyafanyia kazi.

Aliyataja malalamiko hayo kuwa ni kupigwa risasi kwa raia wa Tanzania pamoja na kuuawa kwa mfanyibiashara Lucas Msuya, ambaye kifo chake ndicho kilisababisha machafyuko mpakani hapo.

Mkuu wa mkoa ambaye alikuwa ameambatana na Inspekta jenerali wa Polisi nchini, Bw. Said Mwema, alisema kuwa baada ya kuwasilisha malalamiko hayo, ujumbe wa Zambia ulikiri kuwepo kwa mapungufu yaliyosababisha hali hiyo, na kuahidi kulifanyia kazi tatizo hilo kwa kuanza kukichunguza kituo cha Polisi cha Nakonde.

Aliongeza kuwa, upande wa Zambia pia ulikubali kutuma wataalamu wake wa upasuaji kwa ajili ya kuja eneo la Nakonde kwa ajili ya kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu Msuya, ambaye inasadikika kuwa kifo chake kilitokana na mateso makali.

Ujumbe huo ambao utatoka katika jiji la Lusaka, utashirikiana na wataalamu kutoka serikali ya Tanzania, ambao wataongozwa na Bw. Robert Manumba, ambaye ni Mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai nchini.

Hata hivyo, mkuu wa mkoa aliongeza kuwa, licha ya kufikia makubaliano hayo, ujumbe wa Tanzania pia uliwaeleza wazi kuwa umechoshwa na vitendo vya uonevu ambavyo wamekuwa wakifanyiwa raia wake pindi wanapokuwa upande wa Zambia, na wakawatahadharisha kuwa ikiwa vitaendelea subira huenda ikawashinda Watanzania.

“Niliwaeleza wazi kuwa hali hii imetuchosha na kwamba ikiwa watarudia…….., mnajua” alisema mkuu wa mkoa huku akishangiliwa na maelfu ya wakazi waliokuwa eneo hilo.

Kwa upande wake Inspekta jenerali Mwema, akiongea na wananchi wa eneo hilo, alisema kuwa ujio wake ulikuwa ni kudhihirisha jinsi ambavyo serikali yao imekuwa ikiwajali, na akawashukuru sana kwa kufuata maelekezo ya mkuu wa mkoa pale alipowataka kuwa watulivu kwakuwa serikali inalifanyia kazi tatizo hilo.

“Wakazi wa Tunduma mmeonyesha jinsi gani Tanzania inastahili kuwa nchi ya kuigwa, uvumilivu, uelewa na subira yenu yamekuwa mambo ya muhimu sana katika kumaliza tatizo hili, na kwa niaba ya jeshi la Polisi na serikali kwa ujumla, nawaahidi kuwa matatizo kama haya yataendelea kudhibitiwa” alisema

Katika tamko hilo, serikali pia ilikanusha kuwepo kwa raia wa Tanzania waliiofanyiwa vitendo vya uonevu nchini Zambia, na ikaruhusu rasmi kufunguliwa kwa mpaka baina ya nchi hizi mbili, ambao jana ulikuwa umefungwa japo haikuwa rasmi.

Mara baada ya tamko hilo, wananchi waliokuwa wamefurika eneo hilo, walitawanyika huku wakiwa wanashangilia, na muda mfupi baadae makundi ya raia wa Zambia yalionekana yakivuka mpaka kuingia Tanzania kwa ajili ya kujipatia mahitaji yao, huku wakikaribishwa na Watanzania katika maeneo yao ya biashara.

September 3, 2006 at 5:56 pm 1 comment

Machafuko mpakani mwa Tanzania na Zambia

WATANZANIA wawili wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa na askari wa Zambia kufuatia machafuko mpakani mwa Tanzania na Zambia ambayo jana yaliingia katika siku ya pili.

Sanjari na mauaji hayo, mali zenye thamani ya mamilioni ya shilingi zimeharibiwa yakiwemo magari matatu yaliyokuwa na mali mbalimbali ambayo yaliteketezwa kwa moto.

Waandishi wa habari walipokuwa njiani kuelekea eneo hilo walishuihudia raia wa Tanzanaia waliokuwa wameweka doria barabarani kukagua magari ili kuona kama yamebeba Raia wa Zambia na pindi walipowabaini waliwashusha na kuwapiga.

Katika eneo la kituo cha polisi Tunduma, maelfu ya wananchi wa mji huo walishuhudiwa wakiwa
wamefunga shughuli zao huku wakikabiliana na askari Polisi ambao walikuwa wakiwazuia kuvuka mpaka na kuingia Zambia kwa ajili ya kulipa kisasi cha kuuawa kwa Mtanzania mwenzao.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyopatikana kutoka kwa wasemaji mbalimbali wa serikali waliokuwa eneo la tukuio, chanzo cha mapigano hayo ni kuuawa kwa Mtanzania mmoja mfanyibiashara, Bw. Lucas Msuya, ambaye alikabidhiwa kwa Polisi wa upande wa Zambia kwa ajili ya mahojiano.

Ilielezwa kuwa hatua hiyo ilikuja baada ya mfanyibiashara huyo kutuhumiwa kukutwa na deki ya televisheni ambayo aliuziwa, ikidaiwa kuwa iliibiwa nchini Zambia.

Habari zaidi zilieleza kuwa mara baada ya mfanyibiashara huyo kutuhumiwa kukutwa na mali ya wizi, alijisalimisha kituo cha Polisi cha Tunduma ambapo Polisi wa upande wa Tanzania baada ya kumhoji waliamua kumkabidhi kwa askari wa upande wa Zambia kwa ajili ya kumalizana naye.

Hata hivyo, katika hali ya kushangaza, mara baada ya Askari hao wa upande wa zambia kukabidhiwa Mtanzania huyo kwa maandishi, inadaiwa kuwa walimtesa ikiwa ni pamoja na kumnyima chakula, huku wakimpa kipigo huku wakimtaka kueleza ziliko mali zingine ambazo zilidaiwa kuwa zilikuwa zimeibwa sanjari na deki aliyokutwa nayo.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo vya habari, ndugu wa marehemu waliokuwa wakimtembelea ndugu yao walithibitisha ndugu yao kuwa katika hali mbaya na hata walipotaka kumnunulia dawa kutokana na hali yake kuwa mbaya walipokea vitisho toka kwa askari wa Zambia hivyo kulazimika kuondoka.

Kutokana na mateso hayo, mfanyibiashara huyo ambaye alikuwa akijulikana kwa jina la Mangi mjini Tunduma, alipoteza maisha usiku wa kuamkia juzi na askari wa upande wa Tanzania walipotoa taarifa kwa ndugu wa marehemu kwenda kuchukua maiti, ndugu hao walikataa
wakidai kuwa ndugu yao ameuawa hivyo wanataka maelezo ya kina.

Hata hivyo, ndugu hao hawakupata maelezo hayo hali ambayo iliamsha hasira zao na za wananchi wa Tunduma kwa ujumla ambao walianza kujikusanya kwa lengo la kuvuka mpaka na kuingia Zambia kwa lengo la kulipa kisasi kutokana na kile wanachodai kuwa wamechoshwa na
uonevu wa Wazambia.

Huku wakiwa na bendera, mabango, na silaha za aina mbalimbali, wakiimba nyimbo za “tumechoshwa na uonevu huu tunataka haki” wananchi hao walianza kulipa kisasi hiccho kwa kuharibu mali za baadhi ya wakazi wa Zambia ambazo zilikuwa upande wa Tanzania, sanjari na
kuwapiga Wazambia waliokuwa upande wa Tanzania.

Mbali ya hilo, Watanzania wengine waliamua kuvuka mpaka ambapo walikutana na askari wa upande huo waliokuwa wakitumia silaha za moto ambapo hadi kufikia jana jioni Watanzania wawili walikuwa wameshajeruhiwa vibaya mmoja akiwa amepigwa risasi mbili za kifuani.

Kufuatia hali hiyo, serikali mkoani Mbeya ililazimika kuhamia mjini Tunduma kwa ajili ya kuweka hali shwari ambapo mkuu wa mkoa, kamanda wa polisi wa mkoa sanjari na vikosi kadhaa vya walinda usalama vilimwagwa katika eneo hilo.

Licha ya jitihada hizo, wananchi hao ambao waliendelea kuweka mgomo wa kurudi majumbani mwao ambapo walitanda katika njia na maeneo mbalimbali ya upande wa Tanzania huku wakivizia magari ya Wazambia kwa ajili ya kuwachukulia hatua.

Hata hivyo, wakati mkuu wa mkuu wa mkoa wa Mbeya Bw. John Mwakipesile, akiwapooza wananchi kwa kuwaeleza kuwa amewasiliana na uongozi wa mkoa wa Kasama na wale wa wilaya ya Nakonde, umbali wa km. 100, na kwamba wanakuja mpakani kwa ajili ya majadiliano, tayari
Wazambia kadhaa walishavamia nyumba za askari Polisi na kuharibu mali ambazo hazikuweza kujulikana thamani yake.

Hata hivyo kulikuwa na taarifa za kutatanisha kuhusu ujio wa viongozi wa serikali ya Zambia kwa ajili ya kufanya mazungumzo na uongozi wa Tanzania. Akielezea uatata huo Mkuu wa Mkoa alisema amefanya mawasiliano na viongozi hao lakini wamekuwa wakimapa majibu tafauti kila alipoulizwa mahali walipo.

Mbali ya nyumba za polisi, raia wengine kadhaa walikuwa wameshatawanyika katika sehemu kadhaa za Tanzania huku wakiendeleza uharibifu ikiwa ni pamoja na kuchoma nyumba, hali ambayo iliwapandisha Watanzania hasira zaidi na kuamua kuingia upande wa Zambia kwa ajili ya kufanya uharibifu.

Kwa mujibu wa mkazi mmoja wa Tunduma, Bi. Hidaya Mahamoud, hasira zao zinatokana na ukweli kuwa hii ni safari ya tatu ambapo Watanzania wanauawa na Wazambia ambapo mwaka jana Watanzania wawili waliuawa kwa kupigiliwa misalabani kwa mfano wa Yesu, likiwa ni tukio la pili baada ya jingine la miaka kadhaa iliyopita.

Hadi waandishi wa habari wanaondoka eneo la tukio, milio ya risasi ilikuwa ikiendelea kurindima
kutoka upande wa Zambia, huku askari Polisi na wale wa FFU kwa upande wa Tanzania wakiendelea kuwadhibiti wananchi wasivuke mpaka, kwa maelezo kuwa taratibu zinafuatwa ili kuliweka sawa tatizo hilo.

September 3, 2006 at 5:54 pm Leave a comment

Siku ya Kublog Duniani

==========================================

Ikiwa zipo siku za akina mama, za akina nanihii na nanihii sijui kina nani vile, kwanini nasi tusiwe na yetu? Pengine hili ndilo swali ambalo Bw. Nir Ofir, alichojiuliza na baada ya kuchanganya na ubunifu wake kidogo, basi akaibuka na wazo kuwa Agosti 31 inafaa kuwa Siku ya Blogi Duniani, kwa maana ukiamua kuingiza usanifu wa maandishi katika tarakimu 3108, zinaweza kusomeka Blog.

Leo ni Siku ya Blogi/Kublogi/Mabloga, duniani, ikiwa ni mwaka wa pili kwa siku hii kuadhimishwa. Kwa wale ambao hawajabahatika kujua nini maana ya siku hii, wanaweza kusoma hapa maana ya siku hiyo kama ilivyotafsiriwa na mwanaharakati Maitha anayemiliki blogi ya Bangaiza.

Kwa wale ambao hawakubahatika kushiriki mwaka jana, pengine itakuwa vyema wakatambua ushiriki wa wenzao, wakiwemo Watanzania kadhaa walioshiriki siku hiyo ikiwa ni pamoja na Bw. Ndesanjo Macha, ambaye katika siku hiyo aliandika makala unazoweza kuzisoma kwa kubofya hapa na hapa, na makala hiyo ikavutia watu wengi kuichangia. Soma maoni ya waliochangia makala hiyo kwa kubofya hapa.

Mwingine alikuwa kaka yangu Jeff Msangi, wa harakati, ambaye aliandika makala hii, kuhusiana na siku ya kublogi duniani, na vilevile hata mimi mwenyewe kupitia Blogi yangu nilishiriki kwa kuandika makala unayoweza kuisoma kwa kubofya hapa, na Bw. Akiey ambaye ni mmoja kati ya niliowagusia siku hiyo alinitumia ujumbe nilioufurahia kwahakika.

Kwa namna ya kipekee nitaomba ushiriki wangu wa mwaka huu uhusishe kuwatambua watu kadhaa kutokana na sababu mbalimbali nikianza na ndugu yangu, mwanaharakati, mbunifu na kinara wa mabadiliko katika blogi za Watanzania. Na hapa namaanisha ndugu yangu MK mwenye kumiliki blogi ya Vijimamboz.

Kwa wale ambao wamekuwa wasomaji wetu, nadhani watagundua kuwa blogi zetu nyingi zimekuwa na mabadiliko ya kimwonekano zikawa na sura ya kuvutia zaidi. Hii ni kazi ya huyu mheshimiwa ambaye amekuwa yuko tayari kutoa msaada wa namna yoyote ile kwa yeyote anayejihisi ana tatizo katika kusukuma gurudumu la kublogi duniani.

Ameshafanya kazi kadhaa zikiwemo za kuleta viungo kwa ajili ya kuwezesha mambo mbalimbali kwenda kwa urahisi na kwa namna ya kupendeza, amenishawishi nami nikajiingiza katika ujenzi (ona jumba nililolijenga hapa), lakini zaidi ya yote yuko huru kumsaidia mtu kwa lolote lile. Kwa wale wenye kuwa na maswali mbalimbali kuhusu ku-blogi, wanaweza kumtembelea katika blogi yake kwa kubofya hapa.

Ninaye mwana-Blogi mwingine ambaye kazi zake ukizisoma zinaweza kukufanya ujiulize mara kadhaa, hivi kwanini watu wa namna hii hawapewi nafasi za kuongoza nchi, na hapa namzungumzia dada yangu Hawra Shamte. Unaweza kuona kile anachokiandika ambacho kinanivutia kwa kutembelea blogi yake ya Mnyonge Mnyongeni.

Ukiachilia mbali ndugu zangu weeeeengi ambao nimekuwa nikiwazungumzia mara nyingi kama Ndesanjo, Reginald, Jeff nakadhalika kuna Watanzania wengine ambao kwa hakika nitapenda kutambua kuwepo kwao katika siku hii ikiwa ni pamoja na jamaa zangu wa Kijijini (Ulaya kuna Vijiji?) ambao unaweza kuwapata kwa kuingia hapa.

Na….oh!! Nitamsahau dadangu na mpishi wetu Miriam? Hapana, mchango wako ni mkubwa sana dada, tumekuwa tukitangaza lugha, tumekuwa tukitangaza amani tuliyonayo, utulivu na kila kitu, lakini ni nani aliyekumbuka kuwa hata mapishi ya Kitanzania ni muhimu yakatangazwa kwa kuwa ni ya aina yake kama sio wewe? Kwa wasio au wanaotatizwa kiasi na namna ya kukorofisha masuala ya jikoni nadhani mkitembelea hapa, mtakutana na mtaalamu wa mapishi, dada Miriam.

Na kwa wale ambao wamekuwa na imani sawa na ile ya Ndesanjo, kuwa baadhi ya nyakati ni vyema kuwasikiliza wenye kukuponda zaidi kuliko wale wanaokuunga mkono kwa kila hoja, nadhani itakuwa vyema nikiwaambia kuwa ushiriki wangu katika siku hii ya kublogi duniani, utahusisha pia kutambua uwepo wa blogi inayozungumzia filamu ambayo imekuwa gumzo kubwa nchini Tanzania, namaanisha filamu ya Darwins Nightmare iliyotengenezwa na Bw. Hubert Sauper. Unaweza kuitembelea (na ukaiona vipande vipande filamu yenyewe) kwa kubofya hapa, na kasha ukashiriki mjadala kuhusu filamu hiyo kama unavyoendelea kwa Wanakijiji wa Tanzania walioko Ulaya, walau ukiwa unajua jambo kuihusu.

Wapo wengi ambao natambua mchango wao kwa ujumla, na ni wazi kuwa siwezi kuwataja wote, kwa maana hiyo naomba niwaeleze kuwa kwa ujumla wenu natambua mchango, ushiriki na umuhimu wenu katika kazi hii tuliyoamua kuifanya. Yapo mambo kadhaa ambayo tutatakiwa kuyajadili kwa kina hasa kwetu sisi tulio Watanzania, na naamini wapo ambao wataongoza mijadala hiyo kulingana na jinsi tutavyojipanga nikiamini kuwa mwaka ujao kwa wale tutaobahatika bilashaka tutakuwa na mengi ya kuzungumza katika siku kama hii.

Unaweza kupata taarifa zaidi kuhusu siku hii kwa kuingia hapa au hapa

KILA LAKHERI WANA-BLOGI WOTE KATIKA SIKU HII

September 3, 2006 at 5:19 pm 2 comments


Blog Stats

  • 35,058 hits
September 2006
M T W T F S S
 123
45678910
11121314151617
18192021222324
252627282930