Serikali ya Viwango na ‘hang-over’ ya Mapanki

August 11, 2006 at 12:18 pm 11 comments

22438th
> Mhe. JK, Ukweli huwa haupingwi bali hukabiliwa
SINA hakika kama Bw. Miruko huko aliko amekaa kimya kwasababu ya kutingwa na majukumu mapya makubwa zaidi au laa. Sina hakika kama Bw. Macha naye huko aliko kakaa kimya kwakuwa hataki kusema kitu au laa, lakini kwa ujumla naamini wana-Magazeti Tando wote wamesikia na hili.
Nazungumzia hotuba aliyoitoa Bw. Jakaya Mrisho Kikwete (almaarufu JK), rais wa Sirikali ya awamu ya nne katika Jamhuri ya Muungano wa nchi yetu hii ya Wadanganyika (Tanzania?!). Sirikali ya KASI na VIWANGO. Sirikali ya ARI, KASI NA NGUVU, vyote vikiwa vipya.
Naam, hotuba aliyoitoa kwa wananchi wake, kupitia kwa wazee wa jiji la Mwanza. Ilkuwa ndefu kiasi japo haikuwa ya kuchusha japo kwa hakika nathubutu kusema kuwa haikuwa hotuba ambayo mimi (naamini wapo kondoo wenzangu katika mkumbo huu), hatukuitarajia kutoka kwa mkuu wa kaya hii ya Wadanganyika milioni kazaa na ushee hivi.
Haikuwa hotuba ambayo niliitarajia kwakuwa ilizusha maswali kichwani mwangu zaidi kuliko kuielewa kama ambavyo nilitarajia na swali kubwa ambalo lilinijia kichwani mwangu ni kama kweli huyu mkuu wa kaya anajua ukubwa wa nyumba anayoongoza, na kuvijua vyema vyumba vilivyopo katika kaya yake.
Naam, nilijiuliza kwa hakika kama kweli Bw. JK, anaijua Tanzania anayoiongoza au anaijua Tanzania ile ambayo vyombo vya habari vya kiingereza siku hizi vimeamua kuiita Dar es salaam. Kama kweli jamaa anaijua mitaa ya Tanangozi (Iringa), Kelema (Kondoa), Matai (Sumbawanga)au anaijua Tanzania ile ya Masaki, Oyster bay, Mbezi, Mnazi mmoja na Magogoni.
Kwasababu kama kweli angalikuwa anaijua Tanzania halisi anayoiongoza, angekwepa kabisa kuizungumzia Filamu ya Darwins Nightmare, iliyoandaliwa na Bw Hubert Sauper katika hotuba yake. Na naamini ndio maana hata alipokuwa akiizungumzia pengine wazee wale waliamua kukaa kimya kwakuwa hawakuwa wakimwelewa.
Naomba nizame kabisa kwenye hoja yangu ya msingi leo hii. Filamu ya Filamu ya Darwins Nightmare ya Bw. Hubert Sauper ambayo inahusisha biashara ya samaki katika ukanda wa ziwa Victoria na biashara ya silaha, Umasikini uliokithiri miongoni mwa wananchi wanaozunguka ziwa hilo hususan upande wa Tanzania na biashara ya ukahaba katika jiji la Mwanza.
Hapa ndipo ambapo bw. JK, alitumia muda wake mwingi kupazungumzia wakati alipokutana na wazee wale kule jijini Mwanza. Akaipinga filamu hiyo, akatoa kila aina ya kebehi aliyoweza kuitoa kwa aliyehusika kuiandaa picha hiyo ingawa sijui kama ilifikia kwa kiwango alichoweza kuridhika, maana naamini angetamani hata kumla nyama. Sawa.
Siwezi kuzungumzia sana juu ya suala la silaha kwakuwa suala hilo sio tu kuwa ni nyeti bali sikuwahi kulifanyia kazi kwa wakati wowote ule, bali nitazama zaidi katika kile kilichokaribia kumtoa uvumilivu bw. JK, alipokutana na Bw. Sauper. Biashara ya ukahaba na ulaji wa mabaki ya samaki (MAPANKI) yaliyooza katika jiji la Mwanza.
Mwaka 2003, nilibahatika kukanyaga ardhi ya Mwanza kwa mara ya kwanza baada ya kupata nafasi ya kwenda kupata mafunzo ya Uandishi wa habari za Mazingira katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine ndani ya jiji la Mwanza. Na ni katika kipindi hicho niliweza kuzunguka sehemu kadhaa wakati wa kufanya kile tulikuwa tunaita mafunzo kwa vitendo.
Ndio kipindi hicho nilibahatika kufika maeneo ya Nyabuhororo, Kabangaja soko kuu (au ni kubwa?) la pale Mwanza jijini na mengine mengi. Hata hivyo, eneo ambalo kwa hakika sitaweza kulisahau ni lile ambalo mimi na wanafunzi wenzangu, tulilibatiza Soweto ya Tanzania. Sio kwasababu ya yale yanayojiri Soweto ile ya Afrika Kusini, bali kwasababu ya kile tulichokishuhudia siku hiyo. Na hapa namaanisha eneo la KANYAMA.
Kanyama ni moja kati ya vitongoji vya Mwanza, likiwa kandokando ya barabara ya Mwanza kwenda Musoma katika wilaya ya Magu, takriban umbali wa kama nusu saa hivi toka katikati ya jiji la Mwanza. Hapa ni mahali ambapo tulitakiwa kwenda kushuhudia na kisha kuandika kuhusu uharibifu wa mazingira unavyotendeka katika eneo hilo.
Kwanza hatukuamini kuwa kuna watu katika sehemu hiyo wakati tulipoanza kukumbana na harufu ambayo ni zaidi ya mbaya. Haikushangaza baadhi yetu walianza kuharibikiwa na mazingira ya tumboni kwa kadiri tulivyokuwa tunaelekea mahali husika, na hadi tunafika waliokuwa wakutapika walishatapika mara kadhaa na wale wa chafya walishazipiga nyingi sana.
Hapa ni mahali ambapo tuliambiwa kuwa wenye viwanda vya minofu hutupa mabaki ya samaki baada ya kuondoa minofu yao. Na mabaki hayo ndio wenyeji huyaita MAPANKI. Sehemu kubwa ya mabaki hayo yalikuwa yameshaoza vya kutosha na ndio chanzo cha ile harufu.
Sehemu kubwa ya eneo hilo ilijaa funza, sehemu kubwa ya eneo hilo ilikuwa ikitiririka majimaji yenye mchanganyiko wa kila uchafu unaodhania wewe.
Naam, hiyo ndio ilikuwa Kanyama. Ambayo licha ya kuwa wengi wetu tulikuwa na wakati mgumu sana katika kushuka tu mahali pale, bado tulishuhudia eneo lililochangamshwa na wakazi kadhaa wa eneo hilo ambao walikuwa wakizunguka huku na kule kwa ajili ya kukausha hayohayo mapanki ambayo sisi tulikuwa tunaona yana funza.
Kulikuwa kumejaa moshi kila mahali, na watu kuanzia watoto wa miaka 2 hadi wazee kila mmoja alikuwa akikazana kujishughulisha na yake (nadhani kwa mujibu wa ratiba zao za kila siku) Wapo waliokuwa wakikausha kwa kutumia kuni, lakini wengi wao walikuwa wakaushaji wa kutumia pumba, na kila lilipowasili gari kwa ajili ya kushusha hayo mabaki ya samaki walioondolewa minofu, watu walikuwa wakijazana katika gari husika wakigombea MALI MPYA. Sawa na ndege ambao wao walikuwa wanaweza hata kutua ndani ya gari kabla hajaruhusiwa akabeba kipande chake cha PANKI akaanza kwa kwenda mbele.
Kwa kila aliyeweza kuzungumza hakuna hata mmoja aliyekanusha kuwa kile kilichokuwa kikionekana mbele si kitu chenye kufaa kwa ajili ya chakula na kwa wale walio wakazi wa Mwanza ambao tulikuwa nao darasa moja walituthibitishia hilo wakisema “Mbona mambo ya kawaida hayo, hapo mtu anakausha baadhi kwa ajili ya mlo, wengine anakwenda kuuza mjini na wengine wasiofaa kabisa ni kwa ajili kuandalia chakula cha kuku”.
Na wasingeishia hapo tu, wangeendelea kukwambia “Unashangaa? Mbona kuna watu hapa wana maisha mazuri kwa kuuza haya mapanki?,” ukiwauliza hao samaki ambao wana wadudu, wananuka na ambao ni mabaki tu ya vichwa yanauzwa na kuwapatia watu utajiri wa hata kusomesha watoto wao kweli, wenyeji wangekwambia “Nenda soko kubwa pale ukaone”
Na kweli nenda soko kuu pale utashuhudia hayo. Yapo na kwa ujumla kwa wakazi wa Mwanza, PANKI sio kitu cha ajabu. Kuna jamaa mmoja hapa Mbeya alinichekesha aliposema kwa mkazi wa Mwanza kumkataza asile panki ni sawa na kumtusi. Sina hakika na hilo lakini kwahiyo msiniulize. Nimekumbukia tu alichokisema rafiki yangu huyo ambaye huko Mwanza ndio kwao.
Naam, sijui kama Bw. JK aliwahi kufika Kanyama, sijui kama aliwahi kujua kuwa PANKI na wakazi wa Mwanza ni kama simu na chaja yake, sijui kama aliwahi kufika kule mwaloni akashuhudia yanayojiri huko, sijui kama aliwahi kufika huko soko kuu na akaona kuwa panki huuzwa kama mchicha, nyanya na bidhaa nyingine yoyote, na sijui kama aliwahi kusikia baadhi ya wenyeji wakisema “ah samaki kuwa na wadudu mbona jambo la kawaida”
Sijui kama anajua kuwa yote haya ni sehemu ya kukata tama kwa Watanzania kutokana na sera mbovu zinazohusiana na biashara hiyo ya minofu, kuwa mzungu au mwenye ngozi nyeupe ndiye mwenye haki zaidi kwa minofu ya samaki wa Mwanza kuliko mkazi wa Mwanza, ambaye hata kodi inayosemekana kutoka kwenye hiyo minofu ukimuuliza hajui kama imeshamsaidia kwa lolote.
Binafsi nilisoma makala ya mwandishi mmoja katika gazeti moja la kila wiki, kuhusu ile filamu, mwili ukanisisimka. Nilisisimkwa na mwili maana nilijiwa na kumbukumbu za hali halisi ya Kanyama na niliyoyashuhudia. Ulinisisimka baada ya kukumbuka usiku mmoja tulipokuwa tunarejea toka Bunda, na kuamua kupata chakula cha jioni katika hoteli moja hivi (siikumbuki)
Nilishuhudia vibinti hadi mibinti ya kila aina katika mitaa hiyo na kwakuwa sikuwa mtembezi wa nyakati za usiku, basi nililazimika kuuliza kuwa hao nao vipi na haraka nikajibiwa hawa ni wafanyibiashara ya mwili na wapo kila kona hapo Mwanza. Unaweza kuwapata wa kila aina kulingana na mahitaji yao na kwa idadi yoyote unayotaka.
Naam, hayo ndio niliyoyashuhudia jijini Mwanza mwaka huo wa 2003. mambo ambayo niliyakumbuka wakati nilipokuwa nasoma makala ya RAI iliyokuwa inachambua filamu ya Bw. Sauper. Ni mambo ambayo pia niliyakumbuka wakati nilipomsikia Bw. JK akiongelea filamu hiyo.
Na nililazimika kumpigia simu mtu tuliyesoma naye ile kozi ya uandishi wa habari za mazingira, ambaye anaishi Mwanza na kumuuliza “Hivi Kanyama imebadilika siku hizi?” na akanambia wakuibadili nani. Nilitamani sana nimpigie Bw. JK simu nimwambie kuna mahali kama unaweza uende wakati ukishamaliza hiyo hotuba yako, lakini sikuwa na namba ya simu ya mkuu wa kaya. Lakini nilihofia pia kuwa huenda hoja yangu ikatakiwa kusubiri hadi mheshimiwa atakapopanga tena ziara ya kwenda kuongea na wazee jijini Mwanza.
Lakini nilishikwa pia na mshangao wa aina yake kutokana na kile alichokuwa akikiongelea Bw. JK. Nilishindwa kumwelewa kuwa kosa la yule bwana lilikuwa kupiga ile picha au nini hasa? Kuwa Bw. Sauper alizungumza uongo au vipi? Kuwa hakuwa na haki ya kuonyesha yale kwakuwa tu Ulaya nako kuna masikini na makahaba? Hapana, hapana mheshimiwa Raisi. Nadhani sikukusikia vizuri.
Kuwa eti Ulaya makahaba wapo na wanafanya biashara hiyo kwa kulipia? Kwahiyo? Watanzania nasi tuweke utaratibu kuwa walipie na wakatiwe leseni sio? Kwamba eti kwasababu Marekani wapo masikini basi si ajabu Tanzania nako wakawepo? Hapana mheshimiwa. Kwa hapa nitaomba tutofautiane.
Nadhani kulikuwa na mkinzano wa hoja za Bw. JK katika hili. Sidhani kama kulikuwa na mantiki katika yeye kuilinganisha Ulaya, eti tu kwakuwa kuna masikini basi adai Bw. Sauper hakutenda haki katika kuanika umasikini wetu. Sidhani kama kwakuwa Ulaya kuna makahaba tena wanaolipia shughuli hiyo, basi Bw. Sauper alifanya kosa katika kuanika ukahaba unavyofanywa Mwanza.
Kwa mantiki hii itafika wakati mheshimiwa Rais atatuambia kwakuwa Marekani kuna wasiosoma basi hata huku si muhimu kusoma na mengi yakafuata baada ya hapo. Si ndio maana yake? Alichokifanya mheshimiwa rais, ilikuwa ni kupingana na ukweli, tena basi mbele ya watu wanaoujua huo ukweli wenyewe.
Na haikunishangaza sana kuwa hata pale alipokuwa akizungumza hata wale wazee baadhi walionekana kwenye TV wakigeukiana kuonyesha ishara za mshangao labda, nadhani walikuwa wakijiuliza kama kweli rais wao anajua kile anachokiongelea. Yapo mengi ambayo kwakweli ningeweza kuongelea, lakini kwa leo nadhani niweke kituo hapa kwa kumkumbusha tu mheshimiwa rais kuwa……………….
“NI KWELI KUNA MAENEO YENYE MAKOSA (KAMA TUTAYAITA HIVYO) KATIKA FILAMU HIYO LAKINI KISIWE KIGEZO CHA KUKWEPA UKWELI NA KUTOKUWAJIBIKA”

Entry filed under: maskani.

Hongereni Italia lakini…………….. Siku ya Kublog Duniani

11 Comments Add your own

 • 1. Anonymous  |  August 13, 2006 at 12:16 am

  Mzee wewe ni kiboko, nakukumbuka ulipokuwa SAUT na ziara zernu za mafunzo. Ulichoeleza ni kile ambacho kwa mtu mkweli ambaye si mpenda sifa ma siasa atasema, mzee sehemu ile ndege na moshhi utafikiri kuna kiwanda cha kucoma mmatofali, JK ni mwanasiasa alafu alikuwa nafikiri watu watapiga makofi hakujua kuwa watu tunaijua Mwanza na tunaijua hiyo picha na ukweli wake.Cha ajabu waandamaji na waunga hoja hawajaiona hiyo picha alafu wanathubutu kuunga mkono hotuba, ni nini hii mzee,siasa siyo?tutafika kweli

 • 2. Ansbert Ngurumo  |  August 13, 2006 at 9:52 pm

  Nimependa mjadala wako kuhusu JK na mapanki. Bila shaka umesomam na maoni yangu katika http://www.ngurumo.blogspot.com Nadhani sasa mjadala ndo umeanza, kwani serikali imejiingiza katika malumbano na mtengeneza filamu. wabunge nao wamenisikitisha kwa msimamo wao. wanaonyesha hawaijui Tz. Kikwete naye sasa ameanzn akumtumia waziri mkuu kuwadhibiti wahariri wasichapishe makala za mapanki. Halafu CCM inaanza kutoa matamko ya kuwakosoa waandishi na kusema walipotosha hotuba ya JK. Eti alisema wananchi hawali mapanki YALIYOOZA, si kwamba hawali mapanki. lakini ukweli ni kwamba wanakula mapanki, yaliyooza na yasiyooza. Na akumbuke kuwa mkanda huo haukuctengenezwa leo. Makala yako nimeipenda, nitaomba niiediti kidogo na kuitumia katika gazeti la Jumapili wiki hii. Tafadhari.

 • 3. Anonymous  |  August 13, 2006 at 9:56 pm

  Naandika kumjibu mtoa maoni ANYONYMOUS! Hii anayofanya JK si siasa ni uchafuzi wa siasa. Ndio uchafu ambao wamekuwa wakiifanyia nchi yetu kwa miaka 40 sasa, na wanataka tuiite siasa! Kizazi hiki kina mawazo na approach tofauti. Ndiyo maana tunadhani wazee hawa wanastahili nunyang’anywa madaraka. wameuza nchi, na wanatakatunyamaze, tuwapigie makofi na kuandamana kuwashangilia wanapokosea! HATUKUBALI!

 • 4. Anonymous  |  August 13, 2006 at 10:19 pm

  Sakata la hotuba ya JK Mwanza ni dira ya tunakoenda, mgema kisifiwa tembo hutia maji na hili ni dhahili, TZ ielewe sasa ni mtu gani mabaye tunaye, tulizidi kusdifia na kupiga makofi bila hata kujua.Huu ndio UMAKIAVERI wa wanasiasa wengi ila nadhani kwake JK ni mapema mno maana sasa amedtgoa mwanga wa jinsi m,abavyo watu tunao mafahamu tunajua hivi ndivyo alivyo, hii ni sdcandal na hakuna maana kuithibiti bali aitolee ufafanuzi yeye mwenyewe kuliko kutumia uthibiti, maana ishatapakaa, la maana atoe hotuba mbadala na azuie waandamaji wanaunga mkono na hata Bunge lisiizungumzie hotuba hityo, kwani kuna ngapi maeshatoia na hawazizungumzii, waache ushabiki katika swala nyeti kama hili lililopeleka hata kuvunja protocol kwa
  kumbana mtengeneza film tena ugenini! AJABU!

 • 5. Rashid Mkwinda  |  August 15, 2006 at 12:55 pm

  Kwa upande wetu wana Fasihi ni kwamba mjadala huu utakomaa iwapo picha ya Darwing Nightmare ya Bw. Sauper Hubert itaonekana wazi tukachangia kulingana na FASIHI iliyopo ndani ya Tamthiliya hiyo kwani tunaamini kazi iliyofanyika ni ya kifasihi na ni fikra binafsi za mtunzi kwa mnasaba wa kila kilichopo katika jamii.

 • 6. James  |  August 16, 2006 at 10:17 am

  ukiangalia jinsi watu wanavyolishabikia suala hili, utabaini kuwa hata sisi wenyewe tumeshakuwa mapanki vichwani mwetu.Minofu ya kufikiri imeshatoka kabisaaa. Tupo ambao tunaishabikia bila hata kuiona, tupo ambao hata hotuba yenyewe ya raisi hatukuisikiliza siku ile, tupo ambao hata Mwanza hatupajui, lakini sote tumeingia kwenye mkumbo wa kutuhumu jambo eti kwakuwa raisi alisema. Heri yako walau umefika eneo la Kanyama. Nalijua fika eneo lile na hadi leo niandikapo maoni yangu liko kama ulivyoliacha mwaka 2003.

  Kuna watoto pale ambao kama Sauper angeliwapiga picha hekaheka zao naamini raisi angeweza kumtafuna nyama, lakini wapo pale, haijulikani kama wanaenda shule wakati gani.

  Tukae TUZUNGUMZE (nakumbuka ulishadai kuna kusema na kuzungumza), kisha tufikie muafaka kuwa hii ni changamoto na si tatizo hivyo tulikabili kwa kuukabili ukweli huu.

 • 7. msangimdogo  |  August 20, 2006 at 4:57 pm

  kaka yangu Ngurumo nakuruhusu kutumia kile unachoona kinafaa kwakuwa lengo letu ni kuamsha akili zilizodumazwa za kutokukubali ukweli wa mambo

 • 8. Miriam  |  August 25, 2006 at 4:55 am

  Asante sana kwa kutuelimisha. sisi kuku tulio nje, tunaweza kusoma hotuba ya JK wapi?

 • 9. Innocent  |  August 28, 2006 at 6:23 pm

  Eh Bwana eh mimi nakupongeza manake watanzani CCM inatufanya kama hatuna akili vile.
  JK katurudisha kule enzi za “ZIDUMU FIKRA ZA MWENYEKITI WA CHAMA CHA……..”Yaani wananchi wa mwanza walichemsha kweli kuandamana kwa kitu wasichokijua.
  Magazeti ndio basi tena, uchuro tu wanaandika kumsifia tu.
  Ni hatari.

 • 10. SIMON KITURURU  |  August 30, 2006 at 2:31 pm

  Mimi ninamshangaa tu JK kwa kujaribu kukana jambo lililo wazi.Katika filamu ile ni swala la silaha tu naweza kuwa na wasiwasi nalo hasa ukitaka kulihusisha na Tanzania. Kama zile ndege huleta silaha Afrika, siwezi kushangaa lakini katika filamu hii hakukuwa na ushahidi wa hilo wakutosha. Lakini lazima kuna namna silaha zinafika Afrika. Na inawezekana ni kweli baadhi ya ndege hizi huzileta. Siamini kuwa hizi ndege huwa zinakuja tupu katika bara la Afrika .Pia ni ukweli kuwa ndege hizi hubeba mizigo kwa bei rahisi kuliko ndege nyingine.Kwa hilo tu mimi naweza kumpa huyu mtengeneza filamu benefit of a doubt. Kwa JK kukana TZ kuhusishwa na usambazaji wa silaha kupitia ndege hizi, naweza kuelewa ni kwanini ni jambo ambalo inabidi alifanye. Kwasababu ni jambo ambalo linaweza kuleta uharibifu wa mahusiano kati ya TZ na nchi za majirani zetu. Kuhusu Mapanki nadhani hata mwenyewe leo aanakubaliana nasi kuwa alichemsha.

 • 11. Eliya  |  May 19, 2008 at 2:39 pm

  Utafiti wa kina unahitajika katika hayo yote, lakini mashaka yangu kwa watu hawa wa filamu ni kuwa wanapenda kuremba kazi yao ionekana ilikuwa nzuri na ngumu. Nchi zetu kwakuwa ni masikini wanachukulia rahisi tu hata kuzichafua chafua na kama viongozi wetu wanakuwa walegevu basi kila ubaya ni kwetu. Najua Ulaya hawana zuri lakuongelea Afrika na Asia, ninasoma Ulaya ninajua wana mapungufiu mengi juu ya mtazamo wa Afrika kwa ujumla, nimesha wahi ombwa kuongelea juu ya Africa Mashariki huko Sweden vijana wengi wa huko walishangazwa na picha waliyokuwa nayo awali juu ya Afrika na vyombo vya habari vilivyo wadanganya mambo mengi feki. Juu ya mapank inawezekana kweli yana chukuliwa pengine kwa mlo ama kwaajili ya kulishia mifugo kama kuku, nk lakini hatuna uhakikka kama nilivyo sema utafiti wa kina unahitajika na suluhisho lake litafutwe. JK ange waamuru wahusika wafuatilie na kutoa ripoti kwa utekelezaji, ila kitendo cha kupinga mimi nimekipenda kulinda nyumba yako kama baba ni muhimu kinyume na hapo unakuwa baba usiyejua majukumu yako.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Trackback this post  |  Subscribe to the comments via RSS Feed


Blog Stats

 • 35,058 hits
August 2006
M T W T F S S
 123456
78910111213
14151617181920
21222324252627
28293031