Archive for June 27, 2006

Makamba!! Yaani ni kaaazi kweli kweli

Sijui ni kwasababu sisi wengine tulizaliwa na matatizo ya kuona mambo kinyume au ni kwanini hasa lakini haya yanayoendelea kujiri katika awamu hii ya Uongo-Zii wa awamu ya nne ni kizungumkuti tu. “Yaani ni kaaaazi kweli kweli” anajisemea’ga’ Seki wa Chanel 5

Niliposikia juu ya uteuzi wake, kwakweli nilijua tu kuwa mengi yanakuja, na kwa yakini naamini hata hiki ambacho tumeshakishuhudia ni rasharasha tu, mvua zenyewe zingali zaja.

Nazungumzia uteuzi wa Mgosi, Yusuph Makamba, ambaye ndani ya muda usiozidi siku kumi amelamba ulaji wa haja tu, baada ya kuteuliwa kuwa Mbunge kupitia zile nafasi kumi ambazo mkubwa yeyote wa nchi anapewa mamlaka ya kujaza “washkaji zake” anaoona kuwa uwepo wao katika Bunge, huenda ukasaidia katika mambo fulani fulani hivi (nadhani hata kuwafanya wengi wasilale ni muhimu pia)

Katika muda huo huo, jamaa akaukwaa na ukatibu mkuu wa Chama dume, Chama kilichoshikilia Utamu….ah samahanini wajameni, Chama kilichoshika Hatamu, katika siku ambayo chama hicho kilifanya mkutano wake wa mabadiliko…ah samahani tena, mkutano wa uchaguzi wa mwenyekiti mpya.

Kwa wanaomfahamu luteni huyu mstaafu ( na ninaamini wakazi wa Dar wengi wanamfahamu), watakubaliana nami katika yafuatayo: Kuwa Makamba, ni mmoja kati ya viongozi wazuri sana tulionao hapa nchini, maana kila mmoja anavigezo vyake vya uzuri na ubaya wa kitu. Lakini pia watakubaliana nami kuwa mshkaji, ambaye ni mtoto wa mjini kweli kweli, ni mmoja kati ya viongozi wasanii ambao Tanzania imewahi kuwa nao.

Dakika chache sana baada ya kusikia uteuzi wake kupitia kituo kimoja cha redio, nilipoingia mtandaoni, nilikutana na marafiki zangu kadhaa ambao wako ughaibuni, kila mmoja alisisimkwa kusikia habari ya uteuzi huo, lakini kila mmoja alihoji: “Ulizingatia vigezo gani hasa”unajua niliwajibu nini? Niliwajibu kuwa uteuzi huo kwa dhati kabisa, umezingatia mwelekeo ule ule: Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi mpya.

Kulikuwa na maswali kadhaa ambayo wengi wa waliozungumzia juu ya uteuzi wake kuwa mbunge, waliyauliza au kuyatafakari ikiwa ni pamoja na jitihada ambazo jamaa ameweza kuzifanya ili kuhakikisha kuwa Undugu baina ya Kipindupindu na wakazi wa jiji la Dar, unaisha.

Hapo hujazungumzia ongezeko la makahaba ndani ya jiji lake, hujagusia kuenea kwa mimaji michafu, hujazungumzia kodi za ajabu ajabu wanazotozwa wafanyibiashara wa hapo na wala hujazungumzia mengine mengi tu ambayo hata kina Ndesanjo waliyaacha yakingali yanafanyiwa upembuzi yakinifu.

Uteuzi huu ndio ukanirejesha katika swali ambalo nimekuwa najiuliza mara nyingi: Hivi uteuzi wa watu wa kujaza nafasi zile kumi unazingatia vigezo gani?, au ni kwa yeyote ambaye “Mshika Utamu” mkuu akimtunuku basi anamsogeza? na kwa kasi hii si ipo siku tutakuja kukuta “Mshika Utamu” mkuu kajaza “Tu-vitegemezi Twake” kumi na kutupa usaidizi kwenye ulafi kwakuwa tu ana mamlaka ya kutumia nafasi zile apendavyo yeye?

Hivi ingekuwa vipi kama tungesikia kuwa Mshika Utamu” mkuu angemwingiza mtu kama Mbowe ndani ya uteuzi huo? na je, angemwingiza profesa Shayo ingekuwaje? Je, angetoa nafasi moja kwa mwanafunmzi toka taasisi za elimu ya juu, mmoja akatoka kwenye kundi la wanaoishi kwa matumaini, na nafasi nyingine kwa yule mkulima aliyechukua fomu ya kuwania Urais mwaka 1995, ingekuwa vipi?

Siku moja kabla sijaandika makala hii, nilipokuwa safarini mahali fulani, ndani ya gari kuna jamaa walikuwa wanajadili suala hilo hilo, na mmoja wao akadai “Nadhani JK ana mpango wa kukamilisha safu ya usanii katika serikali yake” Nilimtizama jamaa mara kadhaa lakini nilipotafakari sana nikaona alikuwa na mantiki. Alikuwa na mantiki sababu mgosi ni mmoja kati ya viongozi ambao anaweza kukupa jibu kuhusu jambo fulani, jibu ambalo ni la kisanii kweli kweli.

Na ndipo hapa ambapo najiwa na fikra kuwa pengine Mshika Utamu mkuu ameona kuwa ndani ya jumba lile jipya wanalotumia pale Dodoma, huenda waheshimiwa wakawa wanalala kwa kasi mpya, tena usingizi wa Viwango na Spidi mpya pia, kwahiyo apelekwe mtu ambaye atakuwa akiwachekesha chekesha wahishimiwa wasilale wakapitiliza. Ndio! Kwani zaidi ya hapo ni kipi kikubwa sana ambacho kimemfanya aonekane katika kujaza nafasi hiyo? Ukongwe? Utiifu? Uadilifu? Uwajibikaji? Kampeni? au nini hasa?

Na sasa unaambiwa jamaa anakuwa: Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Mbunge wa Kuteuliwa na Katibu Mkuu wa Chama kilichoshika Utamu. Ndio maana yake ati, nimeshangaa sana hata katika uteuzi wa mabalozi hakukuwa na hata ……….? Charahani labda unisaidie kwanini

Tibindiize ndima mghoshi

June 27, 2006 at 5:08 pm 3 comments


Blog Stats

  • 35,058 hits
June 2006
M T W T F S S
 1234
567891011
12131415161718
19202122232425
2627282930