Archive for June 9, 2006

Ni kweli Prof. Charles Bwenge, lakini……….??

Sijui ni wasomaji wangu wangapi ambao ni marafiki wa Profesa Charles Bwenge, lakini naamini huenda wapo na kama wapo basi naomba wanifikishie ujumbe huu kwake, kwamba “Kijiji cha Wana-Blogi wa Kitanzania kinamhitaji sana katika makazi yao kwasababu tayari nyumba yake imeshaandaliwa ikiwa na kila kitu ndani yake, anachotakiwa kufanya yeye ni kuhamia tu basi”

Profesa Charles Bwenge, ni mmoja kati ya waandishi ambao nimekuwa nikiwahusudu sana kwa kazi zao. Amekuwa akiandika sana katika gazeti la Rai na mara nyingi, nimekuwa nikisoma kazi zake. Ingawa kuna kazi zake nyingi sana ambazo ningeliweza kuzizungumzia, kwa leo napenda niizungumzie zaidi kazi aliyoaiandika katika gazeti hilo toleo namba 661, yenye kichwa cha habari “MAKAO MAKUU YA SERIKALI YA TANZANIA YAKO WAPI, DAR ES SALAAM AU DODOMA?”

Katika makala yake hiyo, Prof. Bwenge, anachagiza makala yake kwa maelezo aliyoyakuta katika tovuti ya Tanzania, kuhusiana na kile kinaitwa MJI MKUU ambapo ananukuu maelezo toka katika tovuti hiyo yakisema “Ukiwa na idadi ya takriban wakazi 300,000 (1998), mji wa Dodoma ulioko umbali wa km 309 magharibi mwa Dar es salaam, ndio makao makuu ya siasa na utawala. Dar es salaam ni mji mkuu wa biashara na uchumi”

Maelezo hayo kutoka katika tovuti ya Serikali, yanampa prof. Bwenge maswali kadhaa kubwa likiwa “Kama ndivyo mheshimiwa Kikwete na Serikali yake wanafanya nini Dar es salaam?” Swali ambalo naamini si tu kuwa limedumu katika vichwa vya Watanzania, bali pia kuwa linaulizwa kwa muda wa miaka nenda rudi sasa.

Pengine tu nami naweza kuongeza maswali kadhaa kwa Serikali zilizotangulia na hii ya Ari, Nguvu na Kasi mpya, kwamba “Mlichaguliwa kwa ajili ya kuwaongoza waliowachagua au kwa ajili ya kupata uhalali wa kusimamia biashara zenu na vitega uchumi vyenu vilivyoko ndani ya Mji Mkuu wa biashara na uchumi?”

Nimalizie tu kwa kumwambia Prof. Bwenge kuwa, ukumbi wa majadiliano katika magazeti yetu bado ungali finyu sana, na hili linasababisha maswali ya muhimu kama hayo kutokuwa na uwanja mpana wa kujadiliwa kwa uwazi (sana sana watu watajadili vichwani mwao na kwenye vikao vya stuli ndefu), lakini ukija huku kwenye Blogi, utakuwa umewatendea haki zaidi wasomaji wako kwa maana utawapa mwanya wa kujimwaga kwa kadiri watakavyo kujadili miswada muhimu kama hiyo.

June 9, 2006 at 10:36 am 3 comments


Blog Stats

  • 34,787 hits
June 2006
M T W T F S S
 1234
567891011
12131415161718
19202122232425
2627282930