Archive for April 23, 2006

Mafanikio ya China na Azimio lililotelekezwa Tanzania

Nyerere once more opened his Arusha Declaration booklet, shook his head and muttered; “There is nothing wrong with this manifesto, why did the Tanzanian chose to trash it? Soon they will all be talking like Banana, Mobutu and Idi Amin ……….How I weep for the country!” – {Mtandao wa NTZ}
******************************
Kama kuna vitu ambavyo naamini kabisa kutoka sakafuni mwa moyo wangu, kuwa vingali vikimuumiza Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, moyoni mwake, huko mahali pema peponi tunakoamini yupo, ni lile la Azimio la Arusha. Na ninaamini kabisa kuwa, angalikuwa hai hadi leo hii angalikuwa akilipigia chapuo Azimio hilo, tena basi akiwa na mifano hai.
Hivi karibuni, nilivutiwa na taarifa moja kuhusu ziara ya rais wa China, Hu Jintao, nchini Marekani. Pamoja na mambo mengine mengi aliyoyafanya rais huyo katika ziara hiyo, kama ilivyo ada, alilazimika kukutana na mwenyeji wake, ambaye ni rais wa Marekani, George .W. Bush, ambaye eti alimwomba Bw. Tao, kuangalia uwezekano wa nchi yake kupunguza baadhi ya bidhaa zake zilizoko katika soko nchini Marekani, (bilashaka na kwingine Duniani), kwakuwa eti zinadhoofisha ushindani wa kibiashara.
Awali nilicheka sana niliposikia taarifa hiyo, lakini baadae nililazimika kuitafakari kwa undani zaidi, kutokana na maswali kadhaa ambayo yalinijia kichwani. Marekani?, kuitaka China ipunguze bidhaa zake katika soko? Kwani waasisi wa sera ya soko huria walikuwa akina nani hasa humu duniani?
Kumbukumbu zangu (zinaweza kuwa finyu, hivyo wengine mnisaidie), zinaniambia kuwa, Wamarekani, kupitia viongozi wao ambao wanaamini kabisa kuwa waliletwa kuitawala Dunia, ndio walioasisi sera ya soko huria kwa minajili ya kuliteka somo la Dunia. kwa bidhaa zao ambazo kimsingi bei yake ni rahisi sana kwakuwa wanawapatia Wajasiriamali wao ruzuku. Ndesanjo, nadhani anaweza kulieleza hili zaidi. Inakuwaje leo hii wamezidiwa tena hadi kuanza kuwataka watu watoe bidhaa zao sokoni kwakuwa zinaua ushindani wa kibiashara?
Lakini swali kubwa zaidi ambalo lilinikuna kichwa ni kuhusu nguvu za Uchina katika soko la dunia hivi sasa, hadi kufikia kuwa Taifa linaloogopwa kiasi cha kuombwa kuanza kupunguza bidhaa zake sokoni (japo najua wakijitetea kuwa ni soko huria, Wamarekani hawatakosa ufa wa kuwabana kwa lengo la kuwadhoofisha, {washindwe na walegee}).
Enzi za uhai na uongozi wake, hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere, alikuwa mtu ambaye alipenda sana kuwajasirisha Watanzania, kwa kila mbinu ambayo aliona inafaa. Alipenda waungane, alipenda wawe na uhuru, alipenda wawe na maisha bora, ambayo msingi wake ulikuwa ni nguvu na umoja baina yao. Alifanya hivi kwasababu (naamini), alikuwa anajua wazi kuwa Watanzania wanaweza.
Kwa wote waliowahi kulipitia, kulichambua na kulichanganua Azimio la Arusha, naamini kabisa kuwa wataendelea kuwa upande wake kuwa Azimio lile lilikuwa na kila kitu kumwezesha Mtanzania kutembea kifua mbele sehemu yoyote duniani na akijivunia Utanzania wake. Naamini wote hao watakubaliana na ukweli kuwa endapo Azimio lile lingetekelezwa kikamilifu, leo hii Watanzania wangekuwa ‘wanakula sahani moja’ na Wachina katika nyanja mbalimbali.
Uelewa wangu katika kitabu kile, unaniambia kuwa, maandiko yaliyokuwemo ndani yake, yalikuwa yamelenga miaka mingi sana ya mbeleni, na bilashaka kutokuwa na mtazamo wa mbali ndio kilikuwa chanzo cha kulisaliti Azimio lile, ambalo daima Mwl Nyerere, alitembea nalo mkononi sanjari na kitabu chake cha dini. Alilifananisha na maandiko mengine matakatifu, kwakuwa tu alikuwa na uhakika kuwa, kilikuwa na uwezo wa kumfanya kila Mtanzania aishi maisha bora, kwa namna anayotaka na sio kwa masharti ya fulani.
Sina shaka kabisa kuwa, Azimio lile, licha ya kuwa lilitoka enzi zile bado tuko katika ukoloni uliotopea kwa uonevu, bado lilikuwa na kila mazingira ya kumwezesha Mtanzania aingie katika utandawazi na soko huria kwa hiari yake mwenyewe, sio kwa kulazimishwa au kutishiwa huku akinung’unika.
Wakati taifa hili linapata uhuru wake, waliokuwepo enzi hizo wanashuhudia kuwa China, ilikuwa miongoni mwa nchi masikini kabisa duniani, ikilinganishwa na yaliyokuwa mataifa makubwa kiuchumi enzi hizo, lakini China, ilijua kuwa yenyewe ni nchi, ina utamaduni wake, ina maamuzi yake, ina uwezo wake na zaidi ya yote iliamini katika uwezo wa kile ilichokuwa nacho.
Wachina, hawakuwahi kuitukuza lugha yoyote ya kigeni duniani, na hata bidhaa zao zote zina lugha ya kikwao, lakini Tanzania, naambiwa eti Kiswahili bado ni finyu sana kuweza kuifanya Tanzania kushindana na mataifa mengine kimaendeleo. Wachina (licha ya misukosuko yote iliyowakumba), bado ni nchi ambayo pamoja na mapungufu ya hapa na pale, walisimama kwa dhati kabisa kujenga uwezo wa watu wao na kuegemea katika ujamaa, kwa maana walijua hiyo ndio njia pekee ya kujenga, kudumisha na kuimarisha utaifa wao. Kwanini Tanzania tulishindwa?
Hivi sasa, wakati China ni miongoni mwa nchi zilizokuwa masikini ambazo zimeliona soko huria kama mkombozi kwao, kwakuwa wanazalisha bidhaa nyingi na kwa teknolojia rahisi, wakitumia Wajasiriamali wazalendo, Tanzania, ambayo hata utamaduni wake unaendelea kubomoka kwa kasi mpya, nguvu mpya na ari mpya, wanaendelea kusononeshwa na sera hizi za kidunia.
Hayati mwalimu Nyerere, aliwahi kunukuliwa akisema kuwa, dhambi ya kuua ni dhambi endelevu, ukiua leo kesho utajisikia tena kuua na keshokutwa na daima, lakini dhambi hiyo pia ni dhambi ambayo itakuhukumu daima dumu. Tulipolikataa Azimio la Arusha (ni kweli lilikuwa na mapungufu, lakini tulitakiwa kuliboresha sio kulizika), hatukuwa na tofauti ya mtu ambaye aliukataa utu wake, utamaduni wake, uwezo wake na kwa ujumla kujikataa mwenyewe.
Na kwa hakika, ikiwa hatatokea kiongozi wa kukubali kuugua mafua kwa kukisaka kile kijitabu kilikokuwa na akakikung’uta mavumbi, na akajitoa mhanga kuanza kukipenyeza katika fikra za Watanzania, tutaendelea kuamini kuwa tulizaliwa ili tuwe tunasaidiwa daima dumu. Hata Rwanda, Burundi, Somalia, Sudan, Kongo Kinshasa nk, ambako vita ni sehemu ya majukumu ya kila siku ya wakazi wake, tutawasuluhisha na kisha wageuke wafadhili wetu.
“Oh…..how I weep for my country!”

April 23, 2006 at 5:30 pm Leave a comment


Blog Stats

  • 35,061 hits
April 2006
M T W T F S S
 12
3456789
10111213141516
17181920212223
24252627282930