Archive for April 12, 2006

Azimio la Dodoma na ujio wa Teknolojia mpya


Miongoni mwa mambo ambayo yamezungumzwa katika Azimio la Dodoma, ni pamoja na kupeana taarifa mbalimbali kuhusiana na teknolojia rahisi ambazo zitakuwa zikituwezesha kuzidi kusukuma mbele gurudumu la uandishi wa mtandaoni, na bilashaka kuzidi kutuunganisha. Nina furaha kuwaletea malezo kidogo juu ya mambo mapya ambayo naamini yanaweza kwa namna moja ama nyingine kuleta chachu ya kazi zetu.

SURA YA KITANZANIA:
Kwa kipindi kirefu kidogo (nadhani Ndesanjo na Mike, wanakumbuka hili), nimekuwa nikihangaika kujaribu kuona ni namna gani ambavyo sisi Watanzania ambao tunamiliki Blogi, au Magazeti Tando, tunakuwa walau na kitu ambacho kinatutambulisha na kutubainisha miongoni mwa wenzetu. Tuwe na Magazeti Tando ambayo yatakuwa na sura ya Rasilimali mbalimbali za Kitanzania. Nimekuwa na ndoto ya namna hii kwa muda mrefu sana, na nilishaijadili sana na Mike Mushi, na akaniahidi kuwa angeliifanyia kazi. Hata hivyo kabla Mike hajafikia hatua hiyo, napenda kuwaelezeni kuwa nimefikia ndoto hii tayari kwa msaada wa ndugu yetu MK, wa vijimambo.

Kupitia hali hii, ndio maana kwa wale wanaoingia kwangu hivi sasa na waliokuwa wakijua awali Jumba langu lilikuwa na sura gani, wataona mabadiliko, kadhaa ikiwa ni pamoja na picha za wanyama wetu, mlima wetu wa Kilimanjaro na ndugu zetu wa Kimasai wakisherehesha sura ya Jumba langu. (Makene, mshahara wangu naongeza kwa kuuza vitafunwa na barafu wakati wangu wa ziada). Kuna mengi ambayo yanaweza kufanyika kupitia hili na kwa wale ambao watakuwa na uhitaji wa kufanyia ukarabati majumba yao, naomba wasisite kuniandikia kwa anwani yangu hapo kulia, au wakawasiliana na MK, kwa anwani hii.

TAARIFA ZA UJIO WA KAZI MPYA:
Hii huduma niliibaini kupitia kwa ndugu yetu Ndesanjo, katika maskani yake mpya. Ni huduma ambayo inawawezesha wasomaji wako, kujiandikisha na kisha wakawa wanatumiwa taarifa juu ya wewe kupandisha kazi mpya katika Gazeti lako, kila mara unapofanya hivyo. Huduma hii inayowezeshwa na Mtandao wa FeedBlitz, ni huduma ambayo ingetufaa sote, hasa kwa kuzingatia ukweli kuwa katika mazingira ya kawaida, wengi wetu bado hatujawa na uwezo wa kuingia kwenye mikahawa ya Intaneti, na kuwa na muda wa kupitia Magazeti Tando yote ambayo tunayajua, kwa lengo la kujua kuna lipi jipya. Ni gharama kwakuwa huduma hiyo hutolewa kwa kulipiwa, na pia huduma zinazopatikana katika mikahawa mingi ni za kasi ya chini mno, hivyo itakuhitaji muda mrefu sana.

Kupitia huduma hii, ikiwa kila mwana-Mtandao wa Magazeti Tando, (ndio hata sisi tuna wanamtandao bwana, kwani wao wameweza wana nini hata sisi tushindwe tuna nini!!), atajiandikisha kwa huduma hii, na kisha akaweka kiungo chake katika Gazeti lake, itawawezesha wasomaji wetu kujiandikisha kwa ajili ya kujulishwa kila tuandikapo kazi mpya, na hivyo wasomaji watakuwa na urahisi wa kutembelea magazeti yale yatakayokuwa na habari mpya baada ya kujulishwa.

UKUMBI HURU WA MAJADILIANO:
Sina uhakika kama huduma hii inaweza kuwa ya manufaa saaana kwa kila mmoja wetu, ila naamini hivyo. Ni huduma ambayo inawezeshwa na mtandao wa TagBoard. Ni huduma ambayo inakuwezesha wewe kuwa na sehemu ambayo itawawezesha wasomaji wako kuweka maoni yao mpya au tuseme kubadilishana mawazo na wasomaji wengine kwa uhuru, kwa kujiandikisha tu majina yao na anwani zao.

Kuna jambo moja ambalo linanifanya niamini kuwa huduma hii pia ina umuhimu wa aina yake. Kuna baadhi ya nyakati mtu anaweza kuwa ama na salamu za kukutumia na akipenda wasomaji wengine wazione, lakini akakosa sehemu muafaka, matokeo yake analazimika kuingiza salamu zake kwenye maoni ya kazi fulani ambayo wala haihusiano na alichodhamiria kukisema. Kuna vitu kama makaribisho ya wageni wapya, ambao wengi hawaanzi na kazi za kuomba kukaribishwa, huanza na mambo mazito moja kwa moja, sasa tunawakaribishia wapi kama sio kupitia kazi zao hizo? Hili pekee ndilo linanifanya nione umuhimu pia wa huduma hizi.

HITIMISHO:
Kuna ugumu fulani katika kukamilisha huduma hizi, sio katika hatua za kujiorodhesha, bali katika hatua ya kuingiza vile viungo vya huduma hizo katika Gazeti Tando lako, ili kuiwezesha huduma hiyo kufanya kazi. Hata hivyo, kama ambavyo Azimio la Dodoma, linavyobainisha, ushirikiano ni kitu cha msingi kabisa, na ninawahakikishia wazi kuwa wapo watu ambao bilashaka wanafahamu kuhusu mambo haya zaidi yangu, ambao watakuwa tayari kuwapa mwongozo mzuri. Unaweza kuniandikia mimi kupitia anwani yangu hii, au kumwandikia Ndesanjo au Waziri Mteule wa sayansi na Teknolojia, ndugu yetu MK, ambaye anaweza kuongoza haya yote.

Makene na Miruko, kazi kwenu sasa.

April 12, 2006 at 10:18 am 6 comments


Blog Stats

  • 35,058 hits
April 2006
M T W T F S S
 12
3456789
10111213141516
17181920212223
24252627282930