Siku 100 za staili ya MBWA (Management By Walking Around)

April 3, 2006 at 3:39 pm 11 comments

” Nionavyo mimi kama hakuna sababu ya kuyajua mabaya ya marehemu, pia hakuna sababu ya kuyajua mazuri yake” – R.S Miruko, akichangia Kumbukumbu ya Kionambali, kwenye kibaraza cha Boniphace Makene
*********************************

Nianze kwa kushusha pumzi kwanza kwasababu Tamthilia ile ilinichosha mno. Uhhhh!!!

Ilikuwa kama tamthilia ya kusadikika kwa hakika, tamthilia ambayo ingekufanya uamini kuwa, hatimaye maandiko yametimia juu ya ujio wa Yesu wa Nazareth ama Nabii Issa kama wengine wanavyomwita. Tena basi amefufukia nchini Tanzania.

Machi 30 mwaka huu, vyombo vya habari nchini Tanzania (sina uhakika na vile vya nje kwa maana sikuviona), vilichukulia siku hiyo kama siku ya aina yake (Sijui kwanini wale waheshimiwa fulani fulani hawakuomba iwe siku ya mapumziko). Kisa? Kutimia kwa siku 100 toka Jakaya Kikwete, aingie rasmi madarakani katika nafasi ya Urais wa Tanzania.

Mambo yaliyokuwa yameandikwa na namna yalivyokuwa yameandikwa au kutangazwa na vyombo hivyo vya habari, yalinikumbusha alichoandika Ndesanjo Macha juu ya vyombo vya habari vya hapa Tanzania. Soma alichoandika hapa. Na yalikuwa ni mambo ambayo yalinifanya nikumbuke masimulizi ya Tamthilia ya Kusadikika, kwa maana siamini kama yalikuwa na ukweli kwa asilimia 100 kama yalivyokuwa yameelezewa katika vyombo hivyo.

Magazeti, Redio na hata Luninga za nchi hii ambayo pia inaitwa Bongo, siku hiyo kwa pamoja vilikuwa na simulizi ya aina moja tu, kuzielezea siku hizo 100 kama siku za kipekee kuwahi kutokea Tanzania. Haiyumkiniki kuwa, watu kama akina Ndesanjo, makene, Damija, na wengineo ambao hawajakuwepo Tanzania katika kipindi hicho, ilikuwa ni rahisi sana kwao kuamini Yesu (Nabii Mussa) amefufuka. tena amefufukia nchini kwao na tayari ana siku 100 toka kufufukia kwake.

Nashindwa kusema kuwa yalikuwa ni masimulizi yaliyojaa unafiki (kwa mujibu wa maadili ya uandishi na umuhimu wa vyombo hivyo katika nyanja ya siasa kwa ujumla), kwasababu kilichokuwemo kilikuwa zaidi ya unafiki na ….. ndio, kwa kiasi kikubwa uongo pia. Vilizalisha makubaliano ya aina yake, kiasi cha kumfanya mtu wa nje aamini kuwa huenda siku hiyo, mamilioni ya Watanzania, walifurika mitaani kusherehekea siku 100 za miujiza ya aina yake.

Kwa bahati mbaya sana ni watu wachache wanaowezakiri kuwa Serikali hii imeweka mianya ya ya kuwezesha unafiki, kwa kuwaaminisha baadhi ya wananchi (na hususan walioko katika nafasi za kuzalisha makubaliano feki), kushika nyadhifa fulani fulani wakati wowote ule fulani akivurunda, hivyo kuasisi (japo sio rasmi) mashindano ya unafiki kila mmoja akitarajia kushinda na kuteuliwa miongoni mwa wateule siku yoyote

“Lakini bahati mbaya zaidi ni kuwa moja kati ya mitaji ya uhakika kabisa katika mradi wa siasa sehemu yoyote Duniani ni pamoja na Unafiki, na yeyote mwenye malengo ya kuwekeza katika biashara hiyo shuruti awe na mtaji huo. Usiseme ukweli daima, kuwa msanii daima ili kuwafurahisha watazamaji wako na hasa mmoja wapo anapokuwa ameahidi kuinua vipaji wakati wowote ili aweze kukuona na kukufikiria”

Kama utataka kupitia japo vichwa vya habari tu vya magazeti ya Tanzania siku hiyo, unaweza kushikwa na mshangao wa aina yake. – “Siku 100 za matumaini na mwanga mpya, siku 100 za mwelekeo wa matumaini, siku 100 za ukombozi, JK aitwa Nyerere” – Hivyo ni baadhi tu ya vichwa vya habari vya Habari siku hiyo, vichwa ambavyo kwa mara nyingine vilidhihirisha taaluma ya habari inavyokabiliwa na kirusi cha kujikomba, tena kwa watu ambao mwisho wa siku huidhalilisha taaluma hii kwa kuiponda na kuitupia kila aina ya kashfa. Ndio, wataachaje ilhali hata akitukana kesho bado atakuta mmemuandika kwa mazuri yake?

Kuna mambo mengi ya kimsingi yalizungumzwa siku hiyo ambayo naamini yalikuwa na ukweli ndani yake (kwasababu watu tunatofautiana katika kuchambua ukweli wa jambo), lakini pia kulikuwa na unafiki wa hali ya juu katika masimulizi hayo kwa kuacha kuchambua uhalisia wa mambo (sio ukweli). Kilichozungumzwa au kuandikwa kilikuwa kweli lakini sio halisi kwa mantiki ya hali halisi ilivyo hapa nchini.

Binafsi nilitarajia katika zama hizi ambapo vyombo vyetu vinajinadi kuwa vimepania kuleta mabadiliko ya kimaendeleo, kutuelezea mambo hayo kwa mchanganuo unaotuwezesha sisi wananchi kufahamu kama kweli siku hizo zimekuwa za ukombozi au laa.

Nilitarajia waandishi wa habari siku hiyo kutulinganishia idadi ya matukio ya ujambazi na uporaji katika siku hizi 100 na idadi matukio kama hayo wakati wa awamu7 zilizotangulia. Kwanza huu utamaduni wa kumpima mtu kwa siku 100 za awali ulianza lini kama sio ushabiki na unafiki wa kiwango cha juu ambao baadae utamalizikia kwa kusababisha maanguko? Kwanini hakupimwa katika siku 50 za mwanzo, kwanini zisiwe siku 150, 200 au hata 500?

Mbaya zaidi, habari nyingi ziliandikwa kutokea jijini Dar es salaam. Kama ilizidi hapo basi kulikuwa na Zanzibar labda na Mbeya. Hivi Wakazi wa dar es salaam na mikoa hiyo mingine miwili ndio wanatosha kuwa kielelezo cha Watanzania wanaokadiriwa kufikia milioni 40 kwa sasa? na je, ni kweli kuwa ulikuwa msimamo wa wakazi hao wa Dar es salaam, au ndugu zetu tunaoishi nao au maongezi ya kwenye vijiwe vya kahawa na stuli ndefu?

Kwa mtu aliyesoma kwa umakini habari zile, kuna baadhi ya nyakati atakubaliana nami kuwa maoni, mitizamo na mawazo yaliyokuwepo katika masimulizi yale hayakuwa ya Watanzania hawa walioko katika ukanda huu wa Afrika Mashariki. Hawakuwa Watanzania hawa ambao nchi yao ni miongoni mwa zinazounda hiki tunakiita Dunia, bali Wadanganyika ambao wanaishi katika Jamhuri moja iliyoko katika sayari ya Bongo na mitizamo ya Waandika habari”

Hivi ni kweli kulikuwa na matumaini kwa serikali iliyoahidi kutimiza ndoto ya makao makuu ya Nchi kwenda Dodoma, kwa kasi mpya, nguvu mpya na ari mpya, kuwajengea mawaziri wake nyumba za kuishi Dar? Za nini sasa wakati wanatakiwa kuhamia Dodoma? Au mwanga wa matumaini hapo uko katika ukweli kuwa licha ya kutumia mabilioni ya fedha za walalahoi wa Tanzania kujengea nyumba hizo, bado watatumia zingine tena kujenga mahekalu mengine Dodoma muda mfupi ujao?

Naambiwa kuwa hadi sasa kuna mawaziri ambao wakiwa Dar, wanakuwa wako nje ya vituo vyao vya kazi, kwahiyo wanalipwa marupurupu ya kuwa nje ya vituo vyao vya kazi. Je, matumaini yaliyopatikana katika hizi siku 100, ni kujua kuwa serikali itakuwa inamlipa waziri wake posho na marupurupu ya safari kwakuwa yuko nyumbani kwake? Tena katika nyumba ambayo amejengewa na serikali hiyo hiyo? na akija Dodoma kikao cha Bunge alale hoteli ya kifahari?

Mbona hamjatueleza gharama za utengenezaji wa nafasi milioni 1 za ajira alizoahidi kuwa hadi sasa zimekuwa kiasi gani, na walioajiriwa wameingiza kiasi gani? Ndio, si alianza kwa kuongeza mawaziri 15 katika baraza lake. Hawa walisababisha vitegemezi vingine kadhaa navyo kukwaa ajira katika ofisi nzuri nzuri walizotengewa, mafundi gereji nao bilashaka walijua kuongezeka kwa tenda feki za utengenezaji wa magari nao wakafikiria kutengeneza risiti hewa, wenye maduka ya “Stationeries” nao wakanufaika, wenye sheli wakaanza kunufaika nakadhalika. nafasi hizo zimegharimu kiasi gani kuzitengeneza?

Hivi ni kweli kuwa kiinimacho kilichopewa jina la “Mabadilioko ndani ya Jeshi” kimeleta mwanga huo wa matumaini ilhali kuna virusi kibao vya rushwa, uzembe kazini na tamaa ambayo vimesalia katika jeshi hilo? Na sisi sote tunajua wazi kuwa virusi hivi huwa vina nguvu kubwa kiasi cha kuweza kueneza sumu yake kwa muda mfupi sana, ikimaanisha baada ya muda huenda hali ikarejea pale pale ilipokuwa japo kwa staili nyingine lakini yenye ari mpya nguvu mpya na kasi mpya?

Nani alijadili hivi vitu vinaitwa semina au warsha elekezi ambavyo vilikuwa vikifanyika katika mahoteli ya kifahari, yenye kulipiwa mamilioni ya shilingi sanjari na mamilioni mengine kwa posho za wana warsha, ilhali serikali ina ukumbi mzuri tu wa pale Chimwaga Dodoma? Nani alihoji vikao vya wakubwa ambavyo walikuwa wanalipana posho za zaidi ya laki nne kwa siku huku vikifanyika katika hoteli za kifahari za mamilioni kwa siku ilhali wakubwa hao wana ukumbi wao na ofisi ambazo zimetumia mabilioni ya Watanzania katika kuziandaa?

Kwanini tusiwe kama Ndesanjo kuamini kuwa wametufanya sisi kama wanyama fulani katika mbuga ya wanyama na wao wamekuja kutuona, kwa jinsi wanavyoendesha mambo yao? Kuishi hoteli ya kifahari, kazi hoteli ya kifahari, usafiri wa kifahari, kuongea nako kwa ufahari, madai nayo ya kifahari….yaani kila kitu cha kifahari na haya yote yamejiri ndani ya hizo siku 100. hakuna aliyetueleza kuwa yamewagharimu Watanzania kiasi gani na kutuingizia faida ya kiasi gani.

Ndio, yote haya yametokea ndani ya siku 100 za sirikali ya awamu mpya, lakini nani kahoji? Ni nani amehoji mapato (makusanyo) ya sirikali ya awamu ya nne katika siku hizi 100 akalinganisha na hali ilivyokuwa katika sirikali zilizotangulia kisha akatuacha sisi tukakubali kuwa kweli tuko katika mwanga na tumaini jipya? Au mwanga wa matumaini ni kutembelea Kariakoo, kushikana mikono na wachuuzi kisha dakika tano baada ya yeye kuondoka bei za bidhaa zinapanda?

Au mwanga wa matumaini ni kufanya ziara za ghafla na za kushtukiza kwenye Wizara, kujua matatizo yaliyopo na siku chache baadae akinamama wakaandamana kwa mkuu wa mkoa kupinga kitendo cha wao kudhalilishwa katika hospitali fulani kana kwamba wao sio wakazi wa eneo ilipo hospitali hiyo na hawastahili kupata huduma mahali hapo? Eti ghafla na kushtukiza, kweli? Mlijuaje nyie kama ilikuwa ghafla? Hawakuwa wamendaa bahasha za khaki mlizokabidhiwa baada ya kumaliza safari hiyo ya ghafla? Huo ughafla ulitoka wapi hapo?

Mwanga wa matumaini unapatikana kwa bwana mkubwa kutumia siku moja kwa kuhudhuria kikao Dodoma, kisha mazishi Zanzibar na akarejea tena Dodoma kuhudhuria kikao na kupumzika Ikulu kwake pale Chamwino? Safari hiyo imezalisha na kutafuna kiasi gani cha fedha? nani alitueleza hili tukajua kweli tupo katika mawio ya matumaini? Hivi ni kweli kuwa wafanyibiashara walimpongeza jamaa alipokuwa akifanya bomoa bomoa pale jijini? Kwanini Mr. Edo (Waziri Mkuu), akasimamisha zoezi hilo kama lilikuwa linachekelewa?

Hivi uamuzi wa kuanza kutizama mikataba ile tuliyoambiwa ina utata uliishia wapi? Kwa maana tulitarajia kuwa masuala kama hayo yangepewa uzito katika hizi siku 100 za awali. Bado tunazidi kuumia kwa ule mkataba wa IPTL tena basi baadhi ya nyakati magazeti yakichelewa mitamboni sababu ya mgao wa umeme. nani kahoji mgao huu ilhaliu serikali ina mkataba wa mamilioni ya fedha na IPTL?

Au hatuyaoni haya kuwa yanazidi kutuumiza tena kwa kasi mpya, nguvu mpya na ari mpya? Hapana, tunayaona ila nani atathubutu kuhoji ilhali wengi wetu bado tunasubiria ukurugenzi wa halimashauri kadhaa ambazo tunazikodolea macho? Nani atahoji wakati mkubwa hajatangaza bado wakuu wa wilaya nasi huenda tunatarajia kuwa miongoni mwa wateule?

Lakini cha kufurahisha zaidi ni kuwa siku zote waandishi hatukosi cha kuandika. Tumefumbia macho masuala yote hayo, na badala yake tumeona hoja ya Mkapa kutangaza mali zake baada ya kutoka Ikulu kama ajenda muhimu sana. na hili limevaliwa njuga kweli kweli, tukimtaka jamaa JK amchunguze kaka Beni.

Wakati tunahangaikia mavi ya kale, huku yanaibuka mapyaaaaaaa!! Jamaa wanasaini mkataba wa aina yake wa kuleta wataalamu wa kufanya mvua zinyeshe, na baada ya miaka miwili tunakumbuka, he!! kumbe ule mkataba ulikuwa hauna maslahi yoyote.zaidi ya kuwa umeongeza donda katika kumbukumbu zetu.

Anyway, Hongera sana JK kwa kufikisha siku 100 na ushee toka uingie madarakani japo mimi sitarajii ipo siku tutashikana mikono maana nadhani kampeni yako huwa ni kuongea na Watanzania kupitia Wazee wetu walioko pale Daa-salamu au kule Idodomya.

Ni mtizamo tu…..Mnisamehe kama nimegusa Pabaya
Alamsiki

Entry filed under: maskani.

Kwanza Tujipongeze Azimio la Dodoma na ujio wa Teknolojia mpya

11 Comments Add your own

 • 1. Boniphace Makene  |  April 3, 2006 at 4:57 pm

  Msangi nimesoma hadi mwisho. Nimesoma kwa umakini sana. Nimetoka machozi kiasi hapa. Wakati nasoma nasikiliza maelezo ya maisha ya Pope John Paul, kiongozi ninayeamini alizidi mipaka ya dini. Kuna sababu ya kuandika hivi, tumepoteza dira kama tutaenda kwa mwendo huu. Swali lingine, je ni nani anamiliki magazeti na vyombo vua habari hapo nyumbani? Kuna kazi katika safari yetu.

 • 2. Rashid Mkwinda  |  April 3, 2006 at 6:12 pm

  Unajua Bw.Msangi hii imetokana na Ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya bila kuwa na fikra mpya, naamini iwapo huyu mwana wa Pakaya aka JAKAYA aka ‘wa nyumbani’ falsafa yake ingeenda kwa kunasibisha fikra mpya haya yote yasingekuwepo.

  Hii nndio hatari tunaweza kujiikuta tukitumbukia baharini kwa kasi,nguvu na ari tukashindwa kujiokoa kwa kukosa fikra mpya, haiingii akilini mtu akasifiwa kwa siku alfu moja na mo… ooh samahani kwa siku mia moja,maana siku hizi si za kumsifia mtu kiasi hiki mimi nadhani kutokana na ridhaa ya kura zetu siku ile ya Desemba 14 ni wajibu wake kutuwajibikia kama kiongozi wa nchi.

  Nakumbuka siku ile ya dhifa ya Rais wa visiwa vya Ngazija Azzari mwana wa Asuoman nikiwa karibu na kilonga longa changu watu wakitafuna mapaja ya kuku Ikulu, jirani yangu vitegemezi vyake vilikuwa vikilia njaa, alikosa Sh.1000 ya kununulia kilo ya sembe, hivyo ilibidi wife aongeze maji katika sufuria ya ugali ili angalau majirani wapate kuwatuliza watoto kwa njaa, niketi chini na kutafakari hali ile nusura nimwage machozi lakini nilijikaza kiume, nikatafakari na kusema kuwa hivi huyu mwana wa Kikwere anayajua haya yanayowakumba wapiga kura wake waliomfikisha pale alipo kwa kasi, nguvu na ari mpya bila fikra mpya?

  Moyoni niliumia lakini nilikubaliana na yaliyopo kutokana na wakati tulionao hatuna budi kukubaliana nao.

  Wakatabahu

 • 3. Martha Mtangoo  |  April 4, 2006 at 2:03 pm

  kaka wee acha tu, hii kasi mpya ya kurudi nyuma ya Dogo Jakaya inatisha unajua hizo siku 100 na ushee zinatia kinyaa na hasa ukiangali kwa undani unajua nini, kitu kimoja kinanikera sana aliwaahidi watanzanai hususan ni Vijana kuwa akipata hiyo fursa ya kuwaongoza ajira milioni 1 zitakuwa nje nje lakini cha kushangaza ajira hakuna na wale walionazo bado wananyang’anywa, vijana wanapigwa na kufukuzwa sehemu zao ambazo wanafanyia biashara zao ndogondogo halafu mbaya zaidi inaendeshwa oparesheni ya kuwatokomeza majambazi hivi mtu anajitafutia kula kwa njia ya halali unamfukuza sasa akitoka hapo na hasira zake aende wapi? matokeo yake ndio hao majambazi ambao wao wanajifanya wanayasaka inanitia kichefuchefu tena kikali mno aah mbona unaniziba mdomo niache niache unajua nimekasirika sana!

 • 4. Mwavizo  |  April 6, 2006 at 3:49 pm

  Kusema kweli kasi ya Raisi Kikwete Inatisha lakini kabla hatujaketi na kuanza kumchambua raisi na kazi aliyoifanya hebu kwanza tumpe nafasi angalau afanye kazi mwaka mmoja au miwili ili tuweze kuona mwelekeo wake vizuri zaidi.

  Wazungu walisema Roma haikujengwa kwa siku moja. Hata hivyo, kama kweli kateleza inabidi aelezewe ili arekebishe. Haya ndo maoni yangu.

 • 5. Reginald S. Miruko  |  April 7, 2006 at 10:15 am

  Nakupongeza Rama kwa riwaya yako tamu, yenye uchambuzi wa kutosha na wa kina. JK nimeanza kumpenda, lakini bado nina wasiwasi kwa utekelezaji wa ‘Hizi ahadi zinazokuja baada ya uchaguzi’. nadhani tunachotaka sasa ni utekelezaji, si ahadi. Ngoja tuone

 • 6. Hudson Eliah Kazonta  |  April 7, 2006 at 6:41 pm

  Ni sawa lakini tumpatie muda zaidi ili tuone kasi anayokwenda nayo itafikia wapi kwani najua kuwa sio rahisi kiasi hicho katika siku 100 tu akaweza kutekeleza ahadi zake ikiwa ni pamoja na kuwapatia vijana ajira milioni 1 kama alivyochangia Martha.

  Nafikiri kuwa anahitaji muda zaidi ili aweze kutimiza yale aliyo ahidi katika kampeni zake na kweli kasi aliyoanza nayo inatisha lakini nina wasiwasi ni bomu ambalo siku moja litalipuka kwani wale wote wanaofukuzwa ama kuadabishwa kwa kasi yake na kutolewa kwenye system nao hawakupenda kufukuzwa kwa hiyo hao hao kwa kutumia mitandao yao wanaweza lipua bomu siku zijazo dhidi yake.

 • 7. Boniphace Makene  |  April 7, 2006 at 6:57 pm

  walahi Msangi hivi haya ni mashindano ya kujenga makasri. Mbona hamtuambii mnapata wapi pesa za kujengea makasri yenu hivi wakati vipato vyenu twavijua. Natania kaka hapa jumba lako linapendeza sana nitumie taarifa mshikaji nami nilipandishe chati Kasri langu

 • 8. Anonymous  |  April 8, 2006 at 3:02 pm

  Leo nilikuwa naongea na mdogo wangu mmoja aliyepo nyumbani TZ. Maoja ya tuliyoongelea ni sifa za serikali ya awamu ya nne. Mojawapo ya sifa zake ni kutake advantage ya makosa ya serikali ya awamu ya tatu. Kati ya makosa ya awamu ya tatu ambayo awamu ya nne imeyachukulia advantage na kujipatia sifa kedekede ni usitishwaji wa uuzaji wa nyumba za umma, mageuzi ndani ya jeshi la polisi, na marekebisho ya mitaala. Kwa kufanya hivyo wanajipatia sifa kibao. Watanzania yawapasa waelewe wazi kwamba haya yote yanayofanyiwa marekebisho yalikuwepo wakati wengi wa wanaounda serikali ya awamu ya nne waliokuwemo kwenye serikali ya aamu ya tatu. Kwa maana nyingine pana unafiki na kujijenga kwa kutumia makosa ya serikali ya tatu.

  F MtiMkubwa Tungaraza.

 • 9. Absalom Kibanda  |  April 20, 2006 at 6:10 pm

  Katika hili umetafakari sawa sawa. Huyu Kikwete ni Rais wa Watanzania wote, waliomuunga mkono wakati akitafuta urais na waliomkataa, wanamtandao na wasio wanamtandao, wana CCM na wasio wana CCM. Jambo la ajabu ni kwamba, kumekuwa na kundi dogo la Watanzania ambalo limeamua kumbinafsisha na kumfanya rais wao peke yao na hivyo kufikia hatua ya kutumia hadi njia za chini chini za kutuzuia japo kumkosoa rais wetu.

 • 10. siliakus felician  |  November 8, 2008 at 2:11 pm

  nimewapata hasa Bonne Maken.

 • 11. siliakus felician  |  November 8, 2008 at 2:12 pm

  siku nyingine.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Trackback this post  |  Subscribe to the comments via RSS Feed


Blog Stats

 • 35,061 hits
April 2006
M T W T F S S
 12
3456789
10111213141516
17181920212223
24252627282930