Kizazi chetu kipya, Dini zetu za kisasa na Hatma yetu

March 8, 2006 at 4:41 pm 15 comments

“Naambiwa kuwa Mbeya pekee, kuna madhehebu ya dini zaidi ya 280, kuna eneo idadi ya makanisa ni sawa na idadi ya wakazi wa eneo hilo, lakini Mbeya, watu wanachunana ngozi, Mbeya hiyo hiyo inaongoza kwa UKIMWI!!”
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
SINA uhakika kama marehemu Vivian Tillya, aliwaona hawa wakati alipokuwa akitunga wimbo wake wa SIWAELEWI, kwasababu hawa nao hivi sasa wamekuwa katika kundi hili hili la hawa wasioeleweka. Nawazungumzia watumishi wa Mungu, wa madhehebu mbalimbali, nchini Tanzania na bilashaka duniani kwa ujumla.
Nakumbuka zama zile wakati naanza kujifunza masuala ya dini, nilikuwa naambiwa kuwa, zamani za kale, kulikuwa na watu alikuwa wakiitwa Manabii na Mitume. Kwamba hawa walikuwa wateule wa Mungu, katika kuufikishia umma wa Wana-dunia, ujumbe, maamrisho, malekezo na utashi wa Mungu, katika wajawake.
Kwamba, walikuwa watu ambao waliagizwa kuja duniani kutupatia na kutuelkekeza namna ya kuyafuatisha maandiko matakatifu, ambayo yalikuwa ni maagizo au malekezo ya kutoka kwa Mungu, kwenda kwa kiumbe alichokiumba, akikiusia namna bora ya kuishi humu duniani. Kwamba walikuwa wakizunguka sehemu mbalimbali duniani kutoa maelekezo hayo kwa kadiri Mungu, huyo huyo alivyowajaalia.
Kwamba watu hawa ambao walikuwa katika baadhi ya nyakati wakiwasiliana na Mungu, kwa namna moja ama nyingine, akiwapa miongozo na ujumbe wa kuwaletea waja wake. Kwamba katika baadhi ya nyakati walikuwa wakikumbana na majaribu mbalimbali kiasi cha kumwomba Mungu, awaepushe na majaribu ya namna hiyo.
Kwamba katika baadhi ya nyakati walikuwa wakikutana na waja wa Mwenezi Mungu, wenye matatizo na kisha wakamwomba Mungu awashushie baraka zake na hakika hali ikawa hivyo kwa walioshushiwa baraka hizo wakapona, au kuondokana na matatizo yaliyokuwa yakiwakabili kwa namna moja ama nyingine.
Sikumbuki kama niliwahi kuambiwa kuwa watu hawa walikuwa na uwezo wa kutenda miujiza, sikumbuki kama niliwahi kufundishwa au kuelezwa kuwa walikuwa wameletwa duniani ili wawe matabibu, wapiga ramli, waganga wa kienyeji au madaktari wa miujiza.
Hawa ndio waliokuwa Mitume au Manabii, wa enzi hizo, ambao walitumwa na Mungu, na ambao kwakuwa kanuni ya Mungu ni kuwa binadamu hatoishi milele humu duniani, kila ilipokuwa inakaribia wakati wao wa kurejea kwa udongo, basi walijitahidi kuona wanaacha watu ambao watakuwa viongozi katika mwendelezo wa yale waliyokuwa wametumwa na Mungu kuja kuyafanya duniani.
Ni katika utaratibu huo huo, ambapo viongozi mbalimbali wa kidini walikuwa wakipatikana, lengo likiwa ni kwa watu hao kuja kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa maandiko, maamrisho na miongozo mbalimbali ambayo Mungu alitaka iwe, inakuwa hivyo kama alivyotaka yeye.
Ni kupitia utaratibu huo huo, hivi sasa tuna Masheikh, maimamu, ma-Ustaadh na kadhalika. Ni katika mfumo huo huo ambapo tuna Wachungaji, Mapadre, ‘Masister’, ‘Mafather’ na wengineo wengi kulingana na imani ya watu fulani katika jamii husika.
Hawa ndio ambao kwa mujibu wa maandiko matakatifu, walitakiwa kuwa watetezi wa nguzo kuu za imani, wasimamizi wakuu wa kuhakikisha maamrisho ya Mungu yanatekelezwa, viongozi wa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa wanairekebisha jamii pale inapoonyesha kuanza kupotoka, wanaharakati wakubwa wa kupenyeza imani za kidini katika mioyo ya watu, ili kuwafanya wahusika kuishi na imani hizo na kumshinda shetani.
Hata hivyo, licha ya ukweli huo (mwa mtazamo wangu lakini), hali imekuwa kinyume na hivyo, kinyume na inavyotakiwa, kinyume na Mungu alivyotaka, kinyume na walivyokuwa wakifanya Mitume na Manabii, kinyume na maandiko wanayoyatumia katika kutuhubiria makanisani na misikitini, na kwa hakika kinyume hata na jinsi nafsi zao zilivyotakiwa kufanya.
Katika miaka ya karibuni, dunia ikiwa inashuhudia mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia, hasa katika upande wa mawasiliano, wafuatiliaji wa masuala mbalimbali ya kijamii katika vyombo mbalimbali vya mawasiliano, watakubaliana nami kuwa masuala ya dini ni miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakipewa uzito wa aina yake katika vyombo mbalimbali vya habari, bila kujali kuwa ni kwa ubaya au uzuri wake.
Ni kupitia njia hii hii ambako nami nimekuwa nikifuatilia kwa ukaribu makongamano mbalimbali ya kidini, ingawa nimekuwa nikiona baadhi ya mambo yanayofanyika huko ni kinyume kabisa na maandiko yale yale ambayo sote tunajua kuwa yametoka kwa Mungu.
Limekuwa ni jambo la kawaida kabisa hivi sasa, na kimsingi hata wengi wanaoyahudhuria ndio wanalokuwa wakilitarajia, kuwa makongamano mengi yamekuwa makongamano ambayo sio kwa ajili ya mafundisho ya neno la Mungu, bali makongamano kwa ajili ya mchungaji au mhubiri fulani kuonyesha miujiza ya uponyaji wa watu wenye matatizo lukuki.
Nadiriki kusema kuwa ndio maana hata idadi ya watu wanaohudhuria makanisani au misikitini imepungua kwasababu ndani ya majumba hayo naamini bila ya Yesu, miujiza haiwezi kutokea. Bila ya usafi wa nafsi ya mhubiri hakuna muujiza unaoweza kutokea, bila ya imani ya kweli kwa anayemjua na kumjali Muumba wake, hakuna miujiza inayoweza kutokea.
Kinyume chake, makongamano ndio ambayo yamekuwa yakijaza watu kupita kiwango, bilashaka kutokana na ukweli tu kuwa ni katika makongamano hayo tu ndio miujiza huweza kufanywa na wahusi,a ambao hata katika mabango ya matangazo kuhusu semina, makongamano au warsha zao za neno la bwana, huhanikizwa kwa ukubwa wa maajabu na miujiza itakayojiri.
Si jambo la kushangaza hivi sasa, kumwona mtu ameandaa kongamano la neno la bwana, lakini akifika pale, hata kabla ya kusalimia waliohudhuria katika jina la anayemwamini, anaanza kwa kuwahitaji wale wote wenye matatizo kujitokeza mbele. Cha ajabu unaweza kukuta waliojitokeza wote ni watu ambao hata hapo mtaani kwenu hamuwajui, na hata ukifuatilia mitaa ya jirani inayowazunguka pia hamna aliye mkazi wa eneo hilo.
Wala sio jambo la kushangaza kabisa, kusikia wahubiri hao hao baadhi yao wakihanikiza kuwa wana uwezo wa kuponya hata UKIMWI, lakini hakuna ambaye anaweza kutuonyesha takwimu halisi za kisayansi kuwa ameshawahi kuwaponya watu wangapi ugonjwa huo, na uthibitisho juu ya hilo.
Ndio huku huku katika makongamano hayo ambako watu hutolewa majini, hutolewa mashetani, hutolewa mapepo wabaya, huponywa kwa miujiza ya kuombewa dua ambazo hata hao wanaozitoa, ukiwaambia wazirejee tena wanashindwa maana hazijulikani kuwa ziko katika lugha gani. Ndio wapo hawa, ambao inafkia hatua ambapo lugha wanayoongea inakuwa haieleweki nadhani hata kwao binafsi.
Hivi bila kuongea kilatino, kijerumani, kizungu, kiholanzi au hata kimarekani kama kipo, dua haliwezi kusikilizwa? Hivi ni nani alisema kuwa maombezi ya Kiswahili hayawezi kusikilizwa na Mungu? Na Kwanini basi watumie lugha ambayo hata wenyewe baadhi ya nyakati wanakuwa hawawezi kuyarudia maneno hayo kuyatamka ikiwa utawataka wafanye hivyo? Katika hilo nani anayehitaji kuombewa kati ya wawili wa aina hiyo?
Na kizuri zaidi ni kuwa siku hizi imeshakuwa kanuni. Kwamba siku hizi maombezi, warsha, semina na makongamano yote ya dini hayawezi kuitwa hivyo ikiwa hayatakuwa na kipengele cha miujiza, kipengele cha watu kuitwa na kugaragara kwenye mavumbi kama hawana akili nzuri vile (ingawa baadhi ya nyakati naamini kweli hawanazo), wakililia maumivu wanayoyapata wakati mapepo mabaya yakiwatoka. Hivi ni nani anaweza kututhibitishia kisayansi kuwa hayo madudu wakati yanatoka tendo hilo linaambatana na maumivu ya mtu kutaka kulia machozi ya damu?
Wahubiri mbalimbali siku hizi wamegeuka waganga wa kienyeji, na ninasema kwa makusudi kabisa kuwa ni waganga wa kienyeji kwasababu ni vitu vya kienyeji tu ambavyo huwa haviwezi kuwa na uthibitisho wa kueleweka wa kitaalamu, wanachokifanya ni kitu ambacho hata wao wenyewe hawawezi kukithibitisha kisayansi, isipokuwa kwa nguvu za ki-giza giza tu. Ndio, kuna tofauti gani kati ya watu hawa?
Lakini haiyumkiniki kuwa katika baadhi ya nyakati, watu wamekuwa wakifanyiwa hivyo na kisha baadae wakakutwa tena wako katika hali yao ile ile iliyokuwa ikiwakabili na kisha mkimuuliza aliyemfanyia maombezi atawajibu “HUYO HAKUAMINI KATIKA JINA LA BWANA”. Sasa swali la kujiuliza hapa ni kuwa, je, kilitakiwa kwanza kipi kati ya haya mawili? Kumpandikiza imani ya kumwamini Mungu, au kumpandikiza miujiza ya muda ambayo naamini ni kwa ajili ya kumuogofya na hali fulani?
Wengi wamekuwa wakitumia nguvu za giza katika kutenda haya, nadhani wengi wetu tungali tunakumbuka suala la yule mchungaji mkenya kule Uingereza na nyingine kama hizo ambazo sizikumbuki mimi. Wengi wamekuwa ni watu ambao wanajenga mazingira ya kuwafanya wanaowasilikiza kuwa waoga dhidi yao na sio dhidi ya Mungu wao, matokeo yake ni kuwa kila wanalowaamrisha ndilo wanalifanya…..ndio si wameshapandikizwa mazingira hayo?
Kila kukicha wamekuwa wakizidi kujenga hofu mpya dhidi ya wanaowapandikiza woga huo, na kujijengea majeshi yao ambayo hatimaye huanza malumbano kuwa mimi ni bora zaidi kuliko fulani. Ndio, tumeyaona haya na wala hawawezi kutubishia. Je, hivi Mungu ndio aliagiza kuwa watu wawe wanatengwa kwa makundi fulani fulani? Mbona alisema kuwa tupendane daima na tuwapende hata maadui zetu? Mbona nyie mnawakataza hata waumini wenu kuwatembelea waumini wa madhehebu mengine?
Katika masuala ya Muziki, hasa nchini Tanzania, kuna kitu wanakiita MUZIKI WA KIZAZI KIPYA. Na bilashaka kuwa hata katika upande huu wa masuala ya dini, muda si mrefu tutaanza kusikia kuwa kuna DINI YA KIZAZI KIPYA. Dini ya watenda miujiza, dini ya waponyaji, wajenga hofu, wasambaratishaji wa umoja wa mwanadamu. Naam, dini ya MATABIBU WA MIUJIZA, dini ya MASHAHIDI WA SHETANI NA MIUJIZA
Ni Mtazamo Tu
…..Alamsiki…..

Entry filed under: maskani.

Ndugu zangu Wapendwa… Kwanza Tujipongeze

15 Comments Add your own

 • 1. John Mwaipopo  |  March 9, 2006 at 5:53 am

  Msangi unatibua dili. Mie nataka nikirejea Mbeya nianzishe kakanisa pale Makungulu. Vipi uko tayari uaskofu msaidizi?

  Mbeya kuna vituko ati. Kuna kanisa moja linaendeshwa kwa kingereza tu (lipo lililokuwa jumba la sinema zamani)

  Swali langu kule Mbeya kuna haja gani ya kizungu kama sio kuchanganyana. Waumini wake nawajua karibu wa kutosha. Wote wanajua Kiswahili vizuri tu.

  Nitachangia zaidi badaye umeme umekatika na huu wa kwenye hifadhi ya hii laptop ya ‘my friend wangu’ umekaribia kuisha

 • 2. msangimdogo  |  March 9, 2006 at 10:03 am

  @Mwaipopo

  Nadhani tatizo sio wingi au aina ya makanisa, na wala sio wapi yalipo au akina nani ndio viongozi wake. Hoja hapa ni kuwa yana kazi gani? Kama hayajaweza kumbadili mwanadamu na kuwa mchamungu, ni ya nini? yanatufundisha nini kama sio masuala ya ushirikina, nguvu za giza, na kumwasi Mungu? Imefikia hatua makanisa nayo yanapewa ‘a.k.a’ kama hilo unalolisema. Kanisa! aka! wapi na wapi mambo haya?

 • 3. nyembo  |  March 9, 2006 at 2:09 pm

  Mh! Mwaipopo umenichekesha sana mshikaji unajua hilo kanisa lililopo katika jengo la sinema la zamani lina jina mbadala hapa kwa sasa A.K.A Winners Chapel, nimeanza kujitafutia kakitabu kangu ka azimio la arusha pengine ndio itakuwa kitabu muhimu katika kanisa lako la kule makunguru ingawa sijui nalo litakuwa la miujiza ama vipi?
  Msangi nae kanikumbusha Kakobe maana yeye siku hizi tukitaka kufanya ibada ya maponyo ni kuangalia katika TV yako hata kama uko kasulu kule kigoma unachannel tu yupo nawe anakuuliza kama unawashwa mwili mzima ama una ugonjwa sugu kama vile nanihii vile ule ugonjwa wa kurivasi ndani, nje ule( ukimwi) basi anakwambia weka mkono wako mahala kisha taja jina la mkombozi wa ulimwengu wetu.yesu yesu yesu! akisema yatosha basi umepona!
  hii ndio ibada yetu mpya maana hata mtoto wa jirani yangu mama theophil, bahati mbaya hamumfahamu naye alitolewa mapepo tayari anasali(gi) kwenye tv tu!sasa mwaipopo wewe itakuwaje utaendesha kanisani, katika ngwangwa yako, radioni,katika mabango, na pia redioni?

 • 4. ndesanjo  |  March 10, 2006 at 5:46 am

  Msangi, umetibua moja ya mada ninazopenda sana. Nimepita kwa Msaki nikakuta ameshusha aya ndefu kwa utamu, nikaja nikakuta uzi huo huo. Maswali uliyoibua wengine huogopa kuuliza. Tukijenga utamaduni wa kuhoji mambo fulani na mambo fulani kuyaacha kwa hofu ya kuwa tutamuudhi mungu itakuwa akili na ufahamu tunao kwa kazi gani?
  Nimependa jina hili la Mashahidi wa shetani.

 • 5. Martha Mtangoo  |  March 10, 2006 at 2:29 pm

  Hayo yote uliyoandika wala sijayaona ila nimeona picha yako uliyoweka katika blog yako aisee kakangu ee imetulia sana.

 • 6. Reginald S. Miruko  |  March 11, 2006 at 6:23 pm

  msimuogope mungu, ni uhakika yeye hasomi blogu, hivyo shusheni na kuhoji kila jambo, Mungu ana mahali pake. Huko Mbeya anapatikana katika makanisa hayo 280, na kwenye misikiti, na masinagogi. leteni mambo bila kupita jwenye chujio

 • 7. msangimdogo  |  March 13, 2006 at 11:37 am

  Jumapili asubuhi, nilikuwa naangalia ibada moja inaendeshwa katika kanisa moja huko ‘Bondeni” wanakotoka hawa Wawekezaji wetu, nikafurahishwa sana na kipande kimoja alichokielezea mchungaji aliyekuwa akiendesha ibada hiyo (sio ya kutibu lakini), akisema kuwa “Waliotuletea neno walitujenga katika imani ya kuishi wa HOFU, lakini daima hofu haina matokeo yaliyo chanya katika maisha ya mwanadamu. Imani, utiifu na uchamungu ndio nguzi za mafanikio alizozielezea Mungu, pengine hili nalo tunaweza kuliangalia kwa mapana yake wakati tunajadili muswada wangu. Je, waliotuletea na kutulisha hilo neno la Mungu, Je, wanaotulisha neno hilo katika zama za sasa, wanatujenga kiimani ya kumcha, kumtii na kumwabudu Mungu, au wanatulisha hofu?

 • 8. frankj  |  March 23, 2006 at 6:23 pm

  umesahau na iringa mbona?.umenikumbusha vivian msangi mdogo mungu ailaze roho yake mapema.
  haya msangi mdogo naomba orodhesha tovuti yangu ambayo ni http://www.fglukwaro.blogspot.com

 • 9. akiey  |  March 25, 2006 at 12:12 am

  Nyakati kweli zimebadilika na jukumu la kuongoza waumini limekamatwa na watu wengi wasiostahili kuwa viongozi wa imani za kidini.

  Inasikitisha mno kuona kuwa dini imekuwa biashara na/au fursa ya kujipa uwezo wa kutawala “kondoo waliopotea”.

  Wangapi tumeshuhudia walipokuwa jamaa tu wa kawaida wa kubangaiza huku na kule kutafuta riziki maisha hugeuka na ghafla si mapajero, mabenzi na masuti ya bei?!
  Dini zote zimeeingiwa na kunguni hawa walaghai, si Uislamu, Ukristo wala Uyahudi, tunakanywa kutenda dhambi na wenye kusambaza dhambi, ni yapi tena haya?!?

  PS: Asante kwa kunipitia kule maskani kwangu…Nimekuchorea kibarua pepe…tuendelee kuwasiliana Kaka.

 • 10. ndesanjo  |  April 2, 2006 at 6:39 am

  Msangi, nimerudia kusoma tena waraka wako huu. Napenda tuendelee kuandika kwa undani masuala kama haya maana yanasaidia kujenga utamaduni wa kuhoji mambo ya msingi na mambo ambayo wakati mwingine huwa tunaogopa kuhoji. Tabia hii ya watu “wanaoponyeshwa” kuwa hawajulikani imeandikiwa vitabu vingi na kufanyiwa utafiti. Jiulize, katika maisha yako yote umewahi kujua mtu asiye na mkono, mguu, au asiyeona kijijini au mtaani kwenu ambaye ghafla siku moja unakutana naye akiwa ana mguu au mkono kwakuwa eti kaombewa na sijui Kakobe, Bonke, Egon Falk na wengine…

 • 11. Bwaya  |  April 3, 2006 at 10:09 pm

  Msangi,
  Nimesoma waraka wako kwa makini sana. Kazi yako ni nzuri.
  Nakubaliana na wewe kwamba wako wababaishaji wengi sana katika mambo haya ya kiimani. Ninakubaliana na wewe kwamba siku hizi watu wanasisitiza zaidi “ibada za uponyaji” kuliko mafundisho ya imani zao. Hilo ni kweli.
  Suala la ubabaishaji haliko katika dini peke yake. Limeeenea katika nyanja karibu zote. Ndio maana wapo walimu wababaishaji. Waandishi wababaishaji. Mainjinia wababaishaji n.k Maana ubababishaji umeshika nafasi katika jamii yetu. Sio dini peke yake.
  Lakini pia tujiulize: Hivi ni kweli hakuna kitu kinachoitwa muujiza? Hivi ni kweli mambo ya uponyaji hayapo?
  Kuhusu suala la lugha zisizoeleweka, ni kweli sababu yake haieleweki. Maana nijuavyo mimi si lugha tunazozifahamu. Si kihispaniola wala kireno. si Kiaarabu kama kinavyotumia na baadhi ya waumini. Maana hata msemaji mwenyewe hawezi kuelewa anaongea nini. Kuna kitu cha tofauti nadhani kuhusu lugha hizi. Ninafuatilia.

 • 12. Indya Nkya  |  April 4, 2006 at 8:32 pm

  Msangi angalia vizuri takwimu za idadi ya makanisa. Inawezekana hiyo ni Mbeya Mjini tuu. Mbeya ni mji wa pili kwa idadi ya makanisa Afrika baada ya Lagos!! Kuna wakani Nilikutana na kiongozi mmoja wa Serikali hapo Mbeya mjini akaniambia Manispaa yake peke yake ilikuwa na idadi ya makanisa 230 nahisi. Hilo si kubwa sana. Vyovyote itakavyokuwa namba hiyo ni kubwa sana. Cha msingi kama wanavyohoji wachangiiaji wengine: Yanasaidia yale matatizo ya kila siku? UKIMWI na mengineyo?

 • 13. Rashid Mkwinda  |  April 17, 2006 at 12:17 pm

  MWAIPOPO UNAJUA LILE KANISA PALE UKUMBI WA SINEMA WA ZAMANI ENTERPRISE WANAOSALI NI WENYE NAZO NA AKINA DADA NI WALE WALIOJAZIA JAZI SI UNAJUA TENA DADA ZAKO WALIVYOJAALIWA MAKALIO AFANAALEKH, HALAFU WANAVALIA VIJINGUO HIVYO MHUUU!!! MIE SISEMI.

  MWAIPOPO ULE UKUMBI NASIKIA ENZZZI ZENU MLIKUWA MKIANGALIA PICHJA ZA AKINA BRUCE LEE NA AKINA AMITABH BACCHAN AU ULIKUWA HAUJAZALIWA(NATANIA)
  ILA JAMBO MOJA TUJIULIZE HIZI DINI NGENI ZINA MASLAHI GANI KWETU

 • 14. Rashid Mkwinda  |  April 17, 2006 at 12:21 pm

  TUFIKE MAHALI TUJIULIULIZE NI KWELI DINI WALIZOTULETEA NI SAHIHI MBONA BASI WALIKUWA WAKIWATESA BABU ZETU NA KUWAPIGANISHA VITA NA KUUANA WENYEWE KWA WENYEWE, KWALI IMANI ZAO ZA DINI NI SAHIHI HAWA WAGENI?MIE NINA MASHAKA NA HILI, MABABU ZETU WALIKUWA WAKIOMBA MVUA ZINANYESHA LEO PAMOJA NA DINI HIZI MPYA OMBA MVUA KAMA ITANYESHA NG’O, NA HEBU BASI TUJIULIZE NI IPI DINI SAHIHI ITAKAYOMUONGOA MWANADAMU ILHALI MADHEHEBU LUKUKI YAKIANZZISHWA KILA UCHAO, HILI LINALETA MASHAKLA MAKUBWA KATIKA KUFUATILIA MAMBO YA IMANI,

 • 15. fadhili  |  April 23, 2010 at 4:55 pm

  Ni kweli kabisa yanayozungumzwa kuhusu Mbeya na Lagos yanafanana sana na bila shaka ni yale yale. Mbeya ni mji wa pili Africa kwa wingi wa madhehebu baada ya Lagos. Angalia yanayotekea Mbeya na sawa ama yanafanana sana na yanayotekea Lagos.

  Lagos kuna madhehebu karibu elfu na kila mtu anataka kuanzisha kanisa lake. Lakini Lagosi kuna ushirikina wa kutisha, biashara ya viungo vya watu, vikundi vyenye imani za siri (cults), mauaji ya vikongwe, watoto wadogo, waabudu shetani, waganga wa kienyeji wa kutosha na yanayofanana na hayo. Mambo haya mtakubadiliana na mimi kwamba ndio yaliyopo Mbeya pia.

  Kama wewe ni mtu unayejiuliza maswali basi utajiuliza maswali mengi sana kutokana na jambo hili. Hivi ni kwanini mahali ambapo panatajwa kuwa na makanisa kila kona ya mji na karibu kila nyumba ya nne au ya tano kuna mchungaji kunakuwa ndio mahali penye vitendo vingi zaidi vya kishetani kuliko sehemu nyingine?? Lazima kuna uhusiano kati ya haya madhehebu na vitendo hivi. Huwezi kupata picha ni kwa vipi uhusiano huo kuwepo ili hali tunavyojua mahali penye madhehebu ya kikristo kama yanafanya kazi yake kama yanavyotakiwa hali inatarajiwa kuwa kinyume kabisa ni ilivyo Mbeya na Lagos.

  Sasa swali kubwa hapa ni kwa jinsi gani vitendo hivi vya kishetani vinabobea zaidi katika miji yenye madhehebu mangi sana? Ni vigumu kuamini jambo hili kwa wengi wetu kwani baadhi yetu tumesha haribiwa vibaya sana uwezo wetu wa kuona na kuchambua mambo. Nasema kwamba viongozi wa madhehebu haya ndio wanaohusika na vitendo vya kishirikina vilivyopo katika maeneo husika. Njia wanazotumia ni za kijanja sana kiasi kwanmba itamgarimu mtu MWANGA wa MBINGUNI kuweza kuona ni kwa vipi inawezekana.

  Kama Biblia ilivyosema watakuja manabii wa uongo, watu wanaosema Bwana bwana lakini sio watu wa Kristo. Ukiangalia kwa makini na kwa msaada wa MWANGA namaanisha ROHO MTAKATIFU, utaona kweli utabiri ule wa Biblia umetimia. Wamejitokeza watu wengi kwa majina mbali mbali manabii( wa uongo), mitume (wa nafsi zao), waalimu ( wa oungo), wazee wa upako ( upako wa ulafi wa fedha na heshima), mitume wa fedha (na kweli ni watumwa wa fedha) n.k, lakini watu hawa lao ni moja tu, FEDHA.

  Njia ambayo watu hawa wantumia ni kunzisha makanisa ambayo wanayamililki kama makampuni binafsi na kutumia nguvu za giza ambazo ama wamerithi kwa wazazi au wamezipaka kwa njia nyingine ili kufanya udanganyifu kwa watu wenye shida mbalimbali.

  Hawa ni mbwa, wezi, washirika wakubwa wa shetani, maagenti wa uovu. Wapo wengi sana hasa katika miji mikubwa na yenye fedha. Wao huubiri Injili mijiji tu ma mahali ambapo watu wanakipato kizuri.

  Watu hawa kwa kweli sio wachungaji au manabii au mitume kama wanavyojiita bali ni wachawi na washirikina wakubwa na hatari sana. Huwezi kuamini wahubiri na wachungaji wengi wa makanisa yanayojiita ya “kisasa au kiroho” ndio wanaoongoza kwa vitendo vya kuingiza uchawi kwenye makanisa.

  Wanachofanya ni kutumia nguvu za giza kufanya “miujiza” ili kuvuta watu kwa wingi na mwisho wa yote kubwa zaidi kwao ni michango ambayo wanaitumia kuishi maisha ya kifahari sana huku waumini wao wakizidi kuangamia kwenye umasikini.

  Inatubidi wapendwa tuwe macho sana na kuhoji lakini kwa msaada wa ROHO MTAKATIFU kila roho na unabii na utume vinginevyo tutaingia kweli huu undanganyifu na uharibifu wa kisasa.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Trackback this post  |  Subscribe to the comments via RSS Feed


Blog Stats

 • 34,944 hits
March 2006
M T W T F S S
 12345
6789101112
13141516171819
20212223242526
2728293031