Archive for March 8, 2006

Kizazi chetu kipya, Dini zetu za kisasa na Hatma yetu

“Naambiwa kuwa Mbeya pekee, kuna madhehebu ya dini zaidi ya 280, kuna eneo idadi ya makanisa ni sawa na idadi ya wakazi wa eneo hilo, lakini Mbeya, watu wanachunana ngozi, Mbeya hiyo hiyo inaongoza kwa UKIMWI!!”
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
SINA uhakika kama marehemu Vivian Tillya, aliwaona hawa wakati alipokuwa akitunga wimbo wake wa SIWAELEWI, kwasababu hawa nao hivi sasa wamekuwa katika kundi hili hili la hawa wasioeleweka. Nawazungumzia watumishi wa Mungu, wa madhehebu mbalimbali, nchini Tanzania na bilashaka duniani kwa ujumla.
Nakumbuka zama zile wakati naanza kujifunza masuala ya dini, nilikuwa naambiwa kuwa, zamani za kale, kulikuwa na watu alikuwa wakiitwa Manabii na Mitume. Kwamba hawa walikuwa wateule wa Mungu, katika kuufikishia umma wa Wana-dunia, ujumbe, maamrisho, malekezo na utashi wa Mungu, katika wajawake.
Kwamba, walikuwa watu ambao waliagizwa kuja duniani kutupatia na kutuelkekeza namna ya kuyafuatisha maandiko matakatifu, ambayo yalikuwa ni maagizo au malekezo ya kutoka kwa Mungu, kwenda kwa kiumbe alichokiumba, akikiusia namna bora ya kuishi humu duniani. Kwamba walikuwa wakizunguka sehemu mbalimbali duniani kutoa maelekezo hayo kwa kadiri Mungu, huyo huyo alivyowajaalia.
Kwamba watu hawa ambao walikuwa katika baadhi ya nyakati wakiwasiliana na Mungu, kwa namna moja ama nyingine, akiwapa miongozo na ujumbe wa kuwaletea waja wake. Kwamba katika baadhi ya nyakati walikuwa wakikumbana na majaribu mbalimbali kiasi cha kumwomba Mungu, awaepushe na majaribu ya namna hiyo.
Kwamba katika baadhi ya nyakati walikuwa wakikutana na waja wa Mwenezi Mungu, wenye matatizo na kisha wakamwomba Mungu awashushie baraka zake na hakika hali ikawa hivyo kwa walioshushiwa baraka hizo wakapona, au kuondokana na matatizo yaliyokuwa yakiwakabili kwa namna moja ama nyingine.
Sikumbuki kama niliwahi kuambiwa kuwa watu hawa walikuwa na uwezo wa kutenda miujiza, sikumbuki kama niliwahi kufundishwa au kuelezwa kuwa walikuwa wameletwa duniani ili wawe matabibu, wapiga ramli, waganga wa kienyeji au madaktari wa miujiza.
Hawa ndio waliokuwa Mitume au Manabii, wa enzi hizo, ambao walitumwa na Mungu, na ambao kwakuwa kanuni ya Mungu ni kuwa binadamu hatoishi milele humu duniani, kila ilipokuwa inakaribia wakati wao wa kurejea kwa udongo, basi walijitahidi kuona wanaacha watu ambao watakuwa viongozi katika mwendelezo wa yale waliyokuwa wametumwa na Mungu kuja kuyafanya duniani.
Ni katika utaratibu huo huo, ambapo viongozi mbalimbali wa kidini walikuwa wakipatikana, lengo likiwa ni kwa watu hao kuja kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa maandiko, maamrisho na miongozo mbalimbali ambayo Mungu alitaka iwe, inakuwa hivyo kama alivyotaka yeye.
Ni kupitia utaratibu huo huo, hivi sasa tuna Masheikh, maimamu, ma-Ustaadh na kadhalika. Ni katika mfumo huo huo ambapo tuna Wachungaji, Mapadre, ‘Masister’, ‘Mafather’ na wengineo wengi kulingana na imani ya watu fulani katika jamii husika.
Hawa ndio ambao kwa mujibu wa maandiko matakatifu, walitakiwa kuwa watetezi wa nguzo kuu za imani, wasimamizi wakuu wa kuhakikisha maamrisho ya Mungu yanatekelezwa, viongozi wa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa wanairekebisha jamii pale inapoonyesha kuanza kupotoka, wanaharakati wakubwa wa kupenyeza imani za kidini katika mioyo ya watu, ili kuwafanya wahusika kuishi na imani hizo na kumshinda shetani.
Hata hivyo, licha ya ukweli huo (mwa mtazamo wangu lakini), hali imekuwa kinyume na hivyo, kinyume na inavyotakiwa, kinyume na Mungu alivyotaka, kinyume na walivyokuwa wakifanya Mitume na Manabii, kinyume na maandiko wanayoyatumia katika kutuhubiria makanisani na misikitini, na kwa hakika kinyume hata na jinsi nafsi zao zilivyotakiwa kufanya.
Katika miaka ya karibuni, dunia ikiwa inashuhudia mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia, hasa katika upande wa mawasiliano, wafuatiliaji wa masuala mbalimbali ya kijamii katika vyombo mbalimbali vya mawasiliano, watakubaliana nami kuwa masuala ya dini ni miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakipewa uzito wa aina yake katika vyombo mbalimbali vya habari, bila kujali kuwa ni kwa ubaya au uzuri wake.
Ni kupitia njia hii hii ambako nami nimekuwa nikifuatilia kwa ukaribu makongamano mbalimbali ya kidini, ingawa nimekuwa nikiona baadhi ya mambo yanayofanyika huko ni kinyume kabisa na maandiko yale yale ambayo sote tunajua kuwa yametoka kwa Mungu.
Limekuwa ni jambo la kawaida kabisa hivi sasa, na kimsingi hata wengi wanaoyahudhuria ndio wanalokuwa wakilitarajia, kuwa makongamano mengi yamekuwa makongamano ambayo sio kwa ajili ya mafundisho ya neno la Mungu, bali makongamano kwa ajili ya mchungaji au mhubiri fulani kuonyesha miujiza ya uponyaji wa watu wenye matatizo lukuki.
Nadiriki kusema kuwa ndio maana hata idadi ya watu wanaohudhuria makanisani au misikitini imepungua kwasababu ndani ya majumba hayo naamini bila ya Yesu, miujiza haiwezi kutokea. Bila ya usafi wa nafsi ya mhubiri hakuna muujiza unaoweza kutokea, bila ya imani ya kweli kwa anayemjua na kumjali Muumba wake, hakuna miujiza inayoweza kutokea.
Kinyume chake, makongamano ndio ambayo yamekuwa yakijaza watu kupita kiwango, bilashaka kutokana na ukweli tu kuwa ni katika makongamano hayo tu ndio miujiza huweza kufanywa na wahusi,a ambao hata katika mabango ya matangazo kuhusu semina, makongamano au warsha zao za neno la bwana, huhanikizwa kwa ukubwa wa maajabu na miujiza itakayojiri.
Si jambo la kushangaza hivi sasa, kumwona mtu ameandaa kongamano la neno la bwana, lakini akifika pale, hata kabla ya kusalimia waliohudhuria katika jina la anayemwamini, anaanza kwa kuwahitaji wale wote wenye matatizo kujitokeza mbele. Cha ajabu unaweza kukuta waliojitokeza wote ni watu ambao hata hapo mtaani kwenu hamuwajui, na hata ukifuatilia mitaa ya jirani inayowazunguka pia hamna aliye mkazi wa eneo hilo.
Wala sio jambo la kushangaza kabisa, kusikia wahubiri hao hao baadhi yao wakihanikiza kuwa wana uwezo wa kuponya hata UKIMWI, lakini hakuna ambaye anaweza kutuonyesha takwimu halisi za kisayansi kuwa ameshawahi kuwaponya watu wangapi ugonjwa huo, na uthibitisho juu ya hilo.
Ndio huku huku katika makongamano hayo ambako watu hutolewa majini, hutolewa mashetani, hutolewa mapepo wabaya, huponywa kwa miujiza ya kuombewa dua ambazo hata hao wanaozitoa, ukiwaambia wazirejee tena wanashindwa maana hazijulikani kuwa ziko katika lugha gani. Ndio wapo hawa, ambao inafkia hatua ambapo lugha wanayoongea inakuwa haieleweki nadhani hata kwao binafsi.
Hivi bila kuongea kilatino, kijerumani, kizungu, kiholanzi au hata kimarekani kama kipo, dua haliwezi kusikilizwa? Hivi ni nani alisema kuwa maombezi ya Kiswahili hayawezi kusikilizwa na Mungu? Na Kwanini basi watumie lugha ambayo hata wenyewe baadhi ya nyakati wanakuwa hawawezi kuyarudia maneno hayo kuyatamka ikiwa utawataka wafanye hivyo? Katika hilo nani anayehitaji kuombewa kati ya wawili wa aina hiyo?
Na kizuri zaidi ni kuwa siku hizi imeshakuwa kanuni. Kwamba siku hizi maombezi, warsha, semina na makongamano yote ya dini hayawezi kuitwa hivyo ikiwa hayatakuwa na kipengele cha miujiza, kipengele cha watu kuitwa na kugaragara kwenye mavumbi kama hawana akili nzuri vile (ingawa baadhi ya nyakati naamini kweli hawanazo), wakililia maumivu wanayoyapata wakati mapepo mabaya yakiwatoka. Hivi ni nani anaweza kututhibitishia kisayansi kuwa hayo madudu wakati yanatoka tendo hilo linaambatana na maumivu ya mtu kutaka kulia machozi ya damu?
Wahubiri mbalimbali siku hizi wamegeuka waganga wa kienyeji, na ninasema kwa makusudi kabisa kuwa ni waganga wa kienyeji kwasababu ni vitu vya kienyeji tu ambavyo huwa haviwezi kuwa na uthibitisho wa kueleweka wa kitaalamu, wanachokifanya ni kitu ambacho hata wao wenyewe hawawezi kukithibitisha kisayansi, isipokuwa kwa nguvu za ki-giza giza tu. Ndio, kuna tofauti gani kati ya watu hawa?
Lakini haiyumkiniki kuwa katika baadhi ya nyakati, watu wamekuwa wakifanyiwa hivyo na kisha baadae wakakutwa tena wako katika hali yao ile ile iliyokuwa ikiwakabili na kisha mkimuuliza aliyemfanyia maombezi atawajibu “HUYO HAKUAMINI KATIKA JINA LA BWANA”. Sasa swali la kujiuliza hapa ni kuwa, je, kilitakiwa kwanza kipi kati ya haya mawili? Kumpandikiza imani ya kumwamini Mungu, au kumpandikiza miujiza ya muda ambayo naamini ni kwa ajili ya kumuogofya na hali fulani?
Wengi wamekuwa wakitumia nguvu za giza katika kutenda haya, nadhani wengi wetu tungali tunakumbuka suala la yule mchungaji mkenya kule Uingereza na nyingine kama hizo ambazo sizikumbuki mimi. Wengi wamekuwa ni watu ambao wanajenga mazingira ya kuwafanya wanaowasilikiza kuwa waoga dhidi yao na sio dhidi ya Mungu wao, matokeo yake ni kuwa kila wanalowaamrisha ndilo wanalifanya…..ndio si wameshapandikizwa mazingira hayo?
Kila kukicha wamekuwa wakizidi kujenga hofu mpya dhidi ya wanaowapandikiza woga huo, na kujijengea majeshi yao ambayo hatimaye huanza malumbano kuwa mimi ni bora zaidi kuliko fulani. Ndio, tumeyaona haya na wala hawawezi kutubishia. Je, hivi Mungu ndio aliagiza kuwa watu wawe wanatengwa kwa makundi fulani fulani? Mbona alisema kuwa tupendane daima na tuwapende hata maadui zetu? Mbona nyie mnawakataza hata waumini wenu kuwatembelea waumini wa madhehebu mengine?
Katika masuala ya Muziki, hasa nchini Tanzania, kuna kitu wanakiita MUZIKI WA KIZAZI KIPYA. Na bilashaka kuwa hata katika upande huu wa masuala ya dini, muda si mrefu tutaanza kusikia kuwa kuna DINI YA KIZAZI KIPYA. Dini ya watenda miujiza, dini ya waponyaji, wajenga hofu, wasambaratishaji wa umoja wa mwanadamu. Naam, dini ya MATABIBU WA MIUJIZA, dini ya MASHAHIDI WA SHETANI NA MIUJIZA
Ni Mtazamo Tu
…..Alamsiki…..

March 8, 2006 at 4:41 pm 15 comments


Blog Stats

  • 35,058 hits
March 2006
M T W T F S S
 12345
6789101112
13141516171819
20212223242526
2728293031