Kikwete…Lowassa…Wana-Mtandao

January 9, 2006 at 6:31 pm 3 comments

HATIMAYE Rais mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bw. Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye alichaguliwa kufuatia uchaguzi mkuu wa Tanzania, uliofanyika Disemba 14, 2005, alianza rasmi utekelezaji wa majukumu yake baada ya kuapishwa rasmi kushika wadhifa huo mnamo Disemba 21, 2005.

Alianza kwa kuwaapisha (maana nasikia walishateuliwa tayari kabla yake), Mwanasheria mkuu mpya wa serikali, (AG) Bw. Johnson Mwanyika, na hatimaye Mkurugenzi mpya wa kituo cha Uwekezaji, ambaye anachukua nafasi ya Bw. Samwel Sitta a.k.a Mzee wa Standard and Speed, ambaye amechaguliwa kuwa spika mpya wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akichukua nafasi ya Bw. Pius Msekwa.

Baada ya hapo, Rais Mpya, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alifanya uteuzi wa mtendaji mkuu wa serikali yake, ambapo alimteua swahiba wake wa karibu, Bw. Edward Lowassa, kuwa Waziri mkuu katika serikali ya awamu ya nne, uteuzi ambao aliutetea kwa kiasi kikubwa mno, alipokuwa akisoma risala yake ya kwanza akiwa rais, kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwa pia ni ishara ya kulizindua rasmi Bunge hilo.

Na katika kuhitimisha hayo yote, akakutana na waandishi wa habari katika makazi yake mapya ya pale Magogoni, jijini Dar es salaam, nikimaanisha Ikulu ya Tanzania, akatangaza Baraza lake la Mawaziri, akiwa kaongeza wizara kadhaa katika utitiri wa zile za awali tulizokuwa nazo huku pia zingine kadhaa akizifanyia marekebisho ya hapa na pale.

Sina hakika kama kweli ameanza kwa Kasi ile ile, Nguvu zile zile na Ari ile ile, nikimaanisha Mpya, ambayo alitamba nayo wakati wa kampeni, lakini ninaamini kuwa ameanza kwa kishindo. Kishindo kwa maana amewabwaga baadhi ya waliokuwa vigogo wa miaka nenda miaka rudi wa cheo cha Uwaziri, ameunda Wizara zake Mpya (ndio, ataacha chata gani kama asipofanya hivyo), na mengine kadhaa.

Hata hivyo, kuwa ameanza kwa kasi ipi kwangu mie sio mjadala mkubwa sana, na bilashaka hata kwa wengineo (maana najua siwezi kuwa pekeyangu mwenye ugonjwa wa kuona mambo kinyume). Kubwa ambalo limenifanya nizungumzie ‘Sirikali’ hii ya awamu ya nne, ni mambo na vijambo vyake.

‘Sirikali’ hii, imenipa maswali kadhaa toka siku ya kwanza kabisa, kamanda wake alipokuwa akiwashukuru sana wananchi wa Tanzania, kwa kumchagua na kumpatia ushindi wa Kimbunga cha Tsunami (kama wenyewe wanavyouita), na miongoni mwa maswali hayo ni haya:-

Hivi chama tawala nchini Tanzania, namaanisha CCM, kimekuwa na Jumuiya mpya na iliundwa lini? Maana kuna kitu kiliibuka wakati wa kampeni (kama mzaha) na kikashika kasi na hatimaye baada ya uchaguzi kumalizika, kamanda wa Sirikali ya awamu hii ya sasa, akakizungumzia na kukishukuru kwa kufanikisha ushindi wake. Nazungumzia hiki kinachoitwa Wana-Mtandao.

Nilishazoea (na kwasababu pia nilifundishwa hata wakati niko shuleni), kuzisikia Jumuiya za Wazazi, Jumuiya za Wanawake, Umoja wa Vijana wa CCM na zinginezo kadhaa. Lakini hii ya wana-Mtandao? Sikuwahi kuisikia kabla ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2005. Sikuwahi hata kuisikia kuzungumzwa kuwa imeanzishwa rasmi au kuzinduliwa rasmi na nani, lini na wapi.

Najiuliza swali hili kutokana na ukweli kuwa kampeni za uchaguzi huo, ziligubikwa na mambo ambayo yalikuwa yakifanyika kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania. Ikiwa ni pamoja na baadhi ya wagombea wa chama dume, kuzomewa waziwazi mbele ya huyu aliyekuja kuwa kamanda mkuu wa mapambano ya umasikini unaowakabili wananchi wa Tanzania.

Nakumbuka kuwa wakati fulani, vigogo wa CCM, walipokuwa wakisukumana na ‘Tumilioni Twao’ pale ‘Idodomya’, kwa ajili ya kuchukua (sio kununua jamani mkumbuke maana u-rahisi wa Tanzania hauna thamani ya kamilioni kamoja), kulizuka makundi ndani ya chama hicho, kutokana na watu kuwa na watu wao wanaowaunga mkono. Hata hivyo baada ya heka heka zote za pale kwisha, iliamuriwa kuwa makundi hayo yavunjwe.

Nakumbuka pia kuwa nilisikia kauli hii ikitamkwa na Bw. Kikwete, wakati wa baadhi ya mikutano yake, sanjari na viongozi wengine wakuu wa ngazi mbalimbali katika chama hicho, walipokuwa wakishiriki katika kampeni za chama chao kusaka ushindi wa kishindo.

Nakumbuka zaidi kuwa kuna wakati niliandika nikisema kuwa, kinachosemwa kuhusu makundi ndani ya CCM, ni nadharia tu, bali kimatendo hakiwezekani. Sio tu kuwa kulikuwa na makundi, bali kulikuwa na kitu kikubwa zaidi ya makundi ndani ya CCM, na niliandika kuwa sio rahisi kuyaondoa kivitendo, kama wanavyosema au kudhania wao, maana kwa hakika hata wao wenyewe ndani ya nafsi zao hawajui kitu umoja ni nini na faida zake.

Na, nakumbuka pia kuwa wapo watu walinitolea macho kuwa nilikuwa sina nia nzuri na chama chao, nilikuwa mpika majungu na mambo kama hayo. Nilishusha pumzi, nikasema kuwa ni suala la muda tu, haya mambo yatajionyesha waziwazi punde, nyie endeleeni kunitolea macho, msinisikilize, halafu mtashangaa kitakachowatokea.

Mnanitolea macho? Hivi ni nani alisema kuwa makundi ndani ya CCM, yalivunjwa au kuvunjika baada ya kumpata mgombea wao wa nafasi ya urais wakati wa mchakato ule mwaka jana? Waliokuwa wanawazomea wagombea wao wa ubunge katika kampeni walikuwa ni akina nani? Waliokuwa wakisema kuwa watahakikisha wanapiga kura za maruhani ni akina nani kama sio wana-CCM?

Hivi wale vijana wa kata zaidi ya 20, waliotishia kuinyima CCM ushindi mjini Mbeya, hadi wakaitwa kwenye kikao cha kutwa nzima, wakabembelezwa kwa kupewa T-shirt na kofia za CCM, wakiahidiwa kuwa wamalize kwanza uchaguzi ndio waanze kumsaka mchawi wao walikuwa ni akina nani? Hawakuwa wana-CCM kweli wale.

Hawa wana-Mtandao ni akina nani? Wametoka wapi? Kwa ridhaa ya akina nani ndani ya chama? Kwa kuidhinsihwa na vikao vipi vya kichama? Kwa manufaa ya akina nani? Wanachama au Watanzania, ambao chama hiki kinawaongoza? Au kundi la watu fulani walioamua kujianzishia ‘Kajumuiya kao” kwa ajili ya kuusaka ushindi wa Ikulu? Kana tofauti gai na vile “Vijumuiya’ vya baadhi ya wazee enzi hizo, walivyovianzisha ndani ya Bunge, vile vya G7, G5 nk, na vikapigwa dafrao, kwa misingi ile ile ya kuwa ni vya kuleta utengano?

Hivi Kikwete, akiwa mtu ambaye anatarajiwa kuwa mwenyekiti wa chama baada ya mwaka huu, (kwakuwa ndio utaratibu ambao tumezoeshwa kuuona) alifanya busara kuwashukuru (kwa maana ya kuwataja hadharani na kukiri kuwa walifanikisha ushindi wake) hawa wana-Mtandao?

Hivi alijua kuwa kuna watu ambao wamekunywa maji ya bendera za chama chake, ambao walikesha wakiimba, wakiingia nyumba hadi nyumba, kitanda hadi kitanda, uvungu hadi uvungu, wakitafuta kula, ambazo zilikuwa zimefichwa kwenye vungu za vitanda vya Watanzania, na akajiuliza kuwa hili litawafanya wajisikieje kuona kuwa hawakuwa sehemu ya wana-Mtandao waliofanikisha ushindi wao, kiasi cha kushukuriwa?

Maana hili kundi la Wana-Mtandao, halihusishi wana-CCM wote, lina baadhi tu ya watu na ambao kwa bahati mbaya sana wengi (kama sio wote), wanajulikana. Wanaweza kutudanganya kuwa wana-CCM wote, walikuwa wana-Mtandao, lakini huo utakuwa uongo wa hali ya juu mno, ambao itawabidi hata wasijaribu kuutamka. Kwanini hawakusema wana-CCM, kote nchini basi, na badala yake wakatamka wana-Mtandao?

Na bado. Mambo hayaishii hapo, kwasababu shukrani za wana-Mtandao siamini kabisa kuwa ziliishia pale jukwaani, wakati alipokuwa akiwashukuru, na bilashaka (kwa imani yangu mimi) kukiri kwa mara ya kwanza kuwepo kwao na ikiwa ni ishara ya wazi pia (kwa imani na mtizamo wangu pia) kuwa ndani ya chama chake kuna makundi, tena si ajabu makundi kuliko hata neno lenyewe linavyoweza kumaanisha.

Hapana..…hapana. Sitaki kabisa kusadiki na kuamini hivyo. Naamini kuwa zitaendelea zaidi ya hapo. Kuandaliwa hafla maalum Ikulu, pale kwenye jumba jeupe lililoko Magogoni, jijini Dar es salaam, kwa lengo la kupongezana, na hatimaye kesho yake mkasikia mheshimiwa saaaaaaana (naye kakataa kuitwa mtukufu), aliyejuu kuliko waheshimiwa wooooote humu nchini Tanzania, kafanya uteuzi wa wakuu wapya wa wilaya na mikoa, sanjari na kugawanya wilaya kadhaa (si ajabu na mikoa pia) ili kupeleka huduma karibu kabisa na wananchi, kwakuwa sehemu husika zilikuwa kubwa sana, kiasi cha masuala ya kiutendaji kuwa magumu. Ptuh!! (kinyaa)

Ndio, unadhani watapelekwa wapi? Ikiwa hawana nafasi nyingine ya ulaji? Maana zilizopo haziwatoshi kurejesha nguvu zao walizotumia katika kuhakikisha ushindi unapatikana? Sikatai kuwa baadhi yao, au hata wote wanaweza kuwa na uwezo wa kufanya kazi zao watakazopangiwa, lakini tatizo moja kubwa ni kuwa katika siasa, unafiki ni moja ya sifa kuu za kuweza kuwa mtu wa kutizamwa sana.

Je, ikitokea kuwa hao watu wakajakuwa wanafiki kivitendo ndani ya uongozi tayari, (maana sisadiki kuwa waliuhangaikia tu ushindi bila kujali maslahi yao wakiukwaa ushindi) Watanzania tutakuwa wapi, maana kwakuwa ni wana-Mtandao, basi itakuwa ngumu kuwawajibisha kwasababu huenda wakageuka na kuhakikisha kunapatikana mwanguko wa kishindo, kwa wakati huo?

Tayari baadhi ya Watanzania, wameshaanza kuhoji juu ya uteuzi na uhalalishwaji wa Bw. Lowassa, kuwa waziri mkuu. Hawa ni wale wanaosema kuwa, huyu alikuwa mmoja kati ya viongozi waandamizi wa kundi la wana-Mtandao, na sio ajabu kuwa hata nafasi hiyo ni sehemu ya shukrani za mwasisi wa Uana-Mtandao.

Binafsi, sina wasiwasi wala shaka juu ya utendaji wa Bw. Lowassa, katika sehemu takriban zote ambazo aliwahi kufanya kazi, ikiwa ni pamoja na Wizara ya Maji na Maendeleo ya Mifugo, ambayo alikuwa Waziri wake katika serikali ya awamu ya tatu. Na wala sina mashaka yoyote yale na utendaji wake katika nafasi mpya aliyopewa hivi sasa, na komredi mwenzake, huyo ambaye inajulikana wazi kuwa ni maswahiba wa zama.

Ni kweli kabisa kuwa Bw. Lowassa, ni mchapakazi asiyeweza kutiliwa mashaka na yeyote anayemfahamu, na ndio maana hata rais wake, Bw. Kikwete, wakati wa risala yake iliyosifiwa hata na wapinzani (sio wapingaji na wapinganaji?), pia alimsifia, akisema kuwa uteuzi wake haukuzingatia uswahiba wao bali uchapa kazi wake, lakini pia hili halitoshi kutuainishia kuwa hii si ishara ya wazi juu ya kuwashukuru wale wanaojiita au walioitwa Wanamtandao. (Sio rushwa hata hivyo, nadhani hii itakuwa ni takrima bilashaka).

Hebu tuangalie mfano huu. Tuchukulie wewe ni mtu ambaye una malalamiko dhidi ya jambo fulani, kisha unaenda kumwona Waziri mkuu, ambaye ni Bw. Lowassa, unaona kuwa hutendewi haki hapo. Je, katika mazingira ya kawaida unaweza kwenda kumlalamikia huyu mtu kwa rais wake, ambaye wakati huo ni Bw. Kikwete, ukitarajia kile unachokiona kama haki yako kutendeka dhidi yako?

Tuseme kuwa kwa bahati mbaya sana mheshimiwa Waziri mkuu amekuwa mtu wa kwanza kutajwa tajwa katika tuhuma fulani, (kama ilivyomtokea Waziri mkuu wa ‘Sirikali’ ya awamu ya tatu) iwe na wananchi wenyewe, au iwe na vyombo vya habari. Hivi itakuwa rahisi sana kwa mtu huyu kuwajibishwa, tena kwa haraka iwezekanavyo ili kukidhi matakwa ya wananchi, ikiwa mwajibishaji wake ni huyu huyu rais wake wa sasa, ambaye ni swahiba wake, na mwajibishwaji alikuwa kiongozi wa kundi lililoleta ushindi wake?

Tukiachana na suala hilo, pengine na kulitizama lile la wanamtandao kwa ujumla wao. Itakumbukwa kuwa Siasa, (na hasa hizi za kibongo, ambazo zimekuwa Si-Hasa), ni mchezo ambao siku zote umekuwa hautabiriki hata siku moja. Hata kama u-mganga wa kienyeji, mtabiri wa nyota, mtaalamu wa kusoma alama, mchawi au mwanga, bado siasa ni miongoni mwa vitu ambavyo ukiamua kuwekeza kwavyo, utaishia kuadhirika na kudhalilika tu kwa maana ni mchezo ambao umejaa wanafiki wengi zaidi kuliko wakweli.

Ni mchezo ambao beki anaweza kuamua, wakati wowote ule kuwa msaliti na kuamua kuifungisha timu, ilimradi labda anataka siku hiyo aandikwe sana magazetini na kuonyeshwa luningani au vyovyote ajuavyo. Kama hamuamini haya muulizeni Bw. Kibaki kule Kenya.

Kwani wanaomwadhiri hivi sasa, kumpelekesha puta na hata kumfanya aonekane hafai ni akina nani zaidi ya waliokuwa wana-Mtandao wake? Walewale ambao walikihakikisha anaibuka na ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa mwaka 2002, dhidi ya kilichokuwa chama tawala nchini humo enzi hizo cha KANU, ambao hivi sasa wako katika kila aina ya harakati kuhakikisha anaanguka kwa kishindo?

Hivi mnadhani kinachotokea kule kilisababishwa na nini hasa kama sio tofauti baina ya wana-Mtandao, wa NARC, na hususan kwa upande wa maslahi, na mnadhani jambo hilo linawezekana kweli kutotokea Tanzania, ikiwa wana-Mtandao wanasalitiana kwa upande wa maslahi? Sijui, labda akina Sheikh Yahya na akina Profesa Maji Marefu, wanaweza kulitizama hili kwa mapana zaidi (kwa maana baada ya miaka kadhaa ijayo) wakatuhakikishia lililo la ukweli kuhusu suala hili.

Inawezekana kabisa watu wakaona kuwa kilichojiri huko, hakiwezi kutokea Tanzania, lakini hizi zitakuwa ni fikra za kinadharia zaidi, kuliko ukweli wenyewe ulivyo. Kwangu mimi, kilichojiri kwa jirani zetu kinastahili kabisa kuchukuliwa kama tahadhari ya juu mno na tukakitumia katika kutahadharishana ili kuhakikisha kuwa tunakikwepa.

Na tahadhari kubwa kabisa ambayo kwa hakika Watanzania, hatuna budi kuhakikisha kuwa tunaichukua, ni pamoja na kukemea kwa ngvu zetu zote hivi Vijumuiya vinavyoanza kuibuka katika vyama vyetu, bila ridhaa ya wananchi, wanachama na vikao vyenye mamlaka ya kuviibua, kwa maana hivi ndivyo vyanzo vya migawanyiko ambayo Watanzania hatutaki hata kuiskia achilia mbali kuiona.

Simaanishi kuwa nimekuwa mganga wa kienyeji, mtabiri wa nyota, msoma alama, au vyovyote viule, ila kinachoonekana mbele yangu ni ishara za nyakati tu. Huu ni mtizamo tu kwakweli, tena mtizamo wangu mimi, sijui wewe, na yule mna mitizamo gani, lakini kwa hakika, bila kujali mitizamo yenu, bado najiuliza hili la Kikwete, Lowassa na Wana-Mtandao, lina ishara zipi katika hatma ya Tanzania?

Mungu Ibariki Afrika,
Mungu Ibariki Tanzania,
Mungu Zibariki FIKRA SAHIHI za VIONGOZI WALIO SAHIHI,
Mungu Tubariki sisi sote tunaokuomba kwa nia njema kutoka nafsini mwentu,
Mungu Uwabariki na hata wale wenye mtazamo wa kutuangamiza,
Mungu Wabariki, kwa maana ubarikio wako utawabadilisha,

Entry filed under: maskani.

Hureeeeeeeeee!! Blog Tanzania….blog.co.tz….na Ndoto za Mike za kila Mwandishi kuwa na Blogi yake

3 Comments Add your own

 • 1. mark msaki  |  January 12, 2006 at 2:50 pm

  kha bwana msangi hapa kweli umechambua! ni vizuri pia kujua lengo la mtandao. mimi ukiniuliza kwa haraka haraka nitakueleza kuwa ninahisi kuwa wanamtandao ni kikundi fulani kilichomua na bila hivyo isingewezekana kuchukua utawala wa nchi pembeni ya utamaduni wa kimakunyanzi uliozoeleka.- kwamba ikulu ni sehemu ya kwenda kustaafia! na kama niko sahihi basi mimi hilo naliona ni jema. cha mshingi basi ni kuwa kikundi hicho kisipate kwa namna yoyote ushawishi wa kujilimbikizia nguvu yasije kuwageuka kama yale ya ndizi za kibaki.

  cheers

 • 2. nyembo  |  January 12, 2006 at 7:59 pm

  bado kaka naufuatilia Uchambuzi wako kwa kina zaidi,nahisi hawa wana mtandao kwa mara ya kwanza walikuwa nchini Congo kwa Laurent Kabila walimsaidia kuingia pale kutoka Msituni na jina lao maarufu kweli wanaitwa wanyamlenge*banyamlenge*kutoka rwanda,unajua kilichotokea ni kudai Takrima tu,sasa TIZI tunao,lakini hawa sio wageni kutoka nje,naona ni wa hapahapa pengine ndio mabosi wale Janjawidi,naona Mangula atakuwa na ukweli zaidi!

 • 3. mark msaki  |  March 5, 2006 at 12:50 pm

  Msangi nimerudi tena na kusoma makala hii. wewe kweli ukitulia ni mwandishi mzuri sana na unakipa kichwa chako matumizi stahili!! unakusanya mrejesho nyuma, unasema tulipo na unahisi kitachofuatia. majibu ya wanamtandao nadhani tumeendelea kuyaona. mfano huu uchaguzi mpya wa mabosi wa polisi. tunaona kuwa labda wanamtandao ni kikundi cha watu wanaotaka nchi iendeshwa kitaalamu zaidi na uteuzi utokane na merits na sio tu kwa kuwa ukikulia mitaa ya ostabei kama ilivyokuwa imezoeleka!

  naona kabisa wanamtandao ni wanaCCM waliosema inatosha. nadhani iko wazi kuwa upinzani kwa maana ya vyama bado hauko Tanzania, na pia ni ukweli kuwa process ya upinzani ilifanyika nadni ya CCM na kumuibua Kikwete. kimsingi vijumuiya ulivyovisemelea hapa makalani ndio vyama ndani ya vyama… na hili hata wale wanamazoea ndani ya CCM walililiona. hakukuwa na hatari ya CCM kushuka chati kama wangedhubutu kumwacha JK nje! ilikuwa pia ni hatua kunusuru chama… nadhani vijikundi kama hivi ni muhimu hasa kwa kipindi hiki na hasa ndani ya CCM ambacho CCM ni chama chenye influence zaidi ili kucheck watu wasionewe na maamuzi sahihi yachukuliwe mara zote!!! hebu angalia NHC yetu iliyokuwa inakufa wakati kuna watu wamekalia rasilimali za shirika kwa mgongo wa kadi za CCM!! na hivyo hata ndoto za nyerere kuhakikisha watu wanaendelea kupatiwa makazi bora zikafa…nina uhakika kama mitandao hii ingekuwapo tangu enzi za mchonga mambo yangekuwa sawa zaidi!

  kwa upande wa upinzani, nao wanahitaji mitandao itakayogeuza vyama vyao kutoka kwenye sura ya NGO na kuwa vyama vya siasa vyenye lengo la kukamata uongozi wa nchi!! wanahitaji sana mtandao pia!!

  nadhani vijumuiya hadi sasa naona mwendo mzuri, tuone itavyokuwa mbeleni!

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Trackback this post  |  Subscribe to the comments via RSS Feed


Blog Stats

 • 35,058 hits
January 2006
M T W T F S S
 1
2345678
9101112131415
16171819202122
23242526272829
3031