Archive for November 24, 2005

Kwa mara ya Kwanza………!!

Si kwamba nimekuwa mshairi….la, bali najaribu kuangalia tu kuwa ni mambo mangapi ambayo yametokea ama kujiri Kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa mwaka huu.

Na kwa hakika, hii itakuwa Kwa mara ya kwanza naandika kitu katika mfumo wa mashairi utadhani nimekuwa msanii wa muziki wa kizazi kipya, ingawa kwa hakika ikitokea nikapata nafasi ya kuimba mahali huenda nikaimba Kwa mara ya kwanza

Naam, zoezi au mchakato (kama wenyewe wanavyopenda kuita) la uchaguzi mkuu wa Tanzania mwaka huu wa 2005, kama lilivyotarajiwa limeshuhudia mambo mengi sana lakini yapo yale ambayo yalijiri Kwa mara ya kwanza, ikiwa ni pamoja na msiba wa mmoja wa wagombea wa nafasi za juu kabisa za uongozi wa nchi.

Na hili likapelekea Kwa mara ya kwanza, katika historia ya nchi hii, uchaguzi mkuu kuahirishwa, jambo ambalo hatimaye Kwa mara ya kwanza, limeibua mjadala wa kweli kweli juu ya sheria ya Uchaguzi ya mwaka 1985 yenye kuruhusu uchaguzi kusogezwa ikiwa mmoja wa wagombea anaaga(?) dunia.

Mjadala huo ukawa mkubwa kwasababu Kwa mara ya kwanza, Watanzania waliweza kuelezwa waziwazi kuwa gharama za uchaguzi ni kiasi gani (bilioni 93?), hali ambayo inaonyesha wazi kuwa kuahirishwa kwake ni mzigo usiomithilika kwa Walalahoi, ingawa ni afadhali kwa baadhi ya Walalahai.

Lakini katika hali ya kushangaza sana (kwangu mimi), Watanzania tumeweza kushuhudia Kwa mara ya kwanza kuwa kumbe utawala wa sheria unawezekana kabisa kwasababu Kwa mara ya kwanza, Tume ya taifa ya Uchaguzi, iliweza kuahirisha uchaguzi huo kwasababu ya kufuata sheria, ingawa pia Kwa mara ya kwanza nilishuhudia mmoja wa wanasiasa wetu ambao wanasifika kwa kuwa ‘Wasanii” akiuweka usanii kando na kuwa muwazi.

Ndio; si mlimsikia (haikuwa mara ya kwanza lakini kumsikia ila kwa kauli yake), huyu jamaa wa (CHADEMA) Chama cha Demokrasia na Maendeleo (potelea mbali hata kama demokrasia hizo sio makini), akisema kuwa kuahirishwa kwa uchaguzi huo kulikuwa mzigo mkubwa sana na kuwa hata wao hawakushirikishwa maana huenda wangesikilizwa, uchaguzi usingeweza kuahirishwa Kwa mara ya kwanza ?

Achilia mbali michakato ile wanaiita ya MCHUJO au KURA ZA MAONI (nashangaa kwanini hazikuwa kura za maono), ambazo Kwa mara ya kwanza ziliweza kuanika waziwazi jinsi gani Watanzania wameanza kuonyesha kuwa huenda Kwa mara ya kwanza wakakubaliana na matumizi ya RUSHWA kama sehemu ya maisha yao ya kila siku.

Kulikuwa pia na tofauti kubwa sana baina ya wagombea wetu, kuanzia ngazi za chini hadi zile za juu kabisa, na ndio maana haikushangaza sana yule mwanamama ambaye ameweka rekodi ya kuwa mgombea wa nafasi ya Uraisi (sijui alijua ni U-Rahisi au vipi?) mwanamke Kwa mara ya kwanza akianza kupiga miayo ya njaa mapema sana huku wagombea wengine Kwa mara ya kwanza, wakiwa wanafanya kampeni kwa kupitia angani.

Ni bahati mbaya sana tu kuwa kuahirishwa huko Kwa mara ya kwanza kwa uchaguzi, kulitokea tu kwa upande wa Tanzania bara na hili likipelekea (sina hakika kama ni Kwa mara ya kwanza) chaguzi za pande hizi mbili kutofanyika pamoja toka Nchi hizi zilipoungana Kwa mara ya kwanza miaka mingi iliyopita.

Na wakati uchaguzi wa kule visiwani ukiwa unaendelea, kulikuwa na mambo mengi sana pia ambayo ingawa mengine hayakuwa yakitokea Kwa mara ya kwanza, lakini pia yapo ambayo yalikuwa yakitokea Kwa mara ya kwanza.

Hivi ni nani alijua kuwa Zanzibar inaweza kuwa sawa sawa na Iraq, kuwa inaweza kushehenezwa vikosi vya askari na mibunduki yao na bado uchaguzi ukawa salama, kama sio rais wetu anayemaliza muda wake, Bw. Benjamin Mkapa, kuzifananisha sehemu hizi mbili Kwa mara ya kwanza wakati alipokuwa akitetea hoja yake ya kulundika wanajeshi kule?

Hivi ni nani ambaye alikuwa anajua kuwa Vikosi vyetu vya kulinda usalama vina magari yenye kubeba maji yaloyochanganywa na upupu kama sio baada ya kuyaona kule visiwani Kwa mara ya kwanza ?.

Kimsingi nadhani kuwa haikuwa Mara ya kwanza kwa wana-CUF kulalamikia kuporwa kura (zao?), lakini hii ilikuwa Mara ya kwanza kwao kutuambia kuwa wataingia Barazani na kuapa lakini hawatatoa ushirikiano.

Lakini hawa jamaa ambao nashindwa kuwaunga au kuwavunja kabisa mkono kuna jambo moja ambalo kwa hakika wangelifanya ndio ingekuwa kwa Kwa mara ya kwanza kuwahi kufanywa hapa nchini, nalo ni kukataa mshiko (ita vyovyote unavyopenda weye lakini ndio hizo hizo).

Ndio, wanaweza kabisa kuwa mabubu ndani ya vikao vya Baraza la Wawakilishi ingawa wengi wao hali ya kuwa bubu ndio watakuwa wakiishiriki Kwa mara ya kwanza, lakini hili la kuifanya mifuko yao nayo iwe bubu Kwa mara ya kwanza, wakati ambapo wengi wao ndio wameingia Barazani Kwa mara ya kwanza ili wakaonje MATUNDA ya uongozi baada ya kuhangaika muda mrefu katika MATUNDU ya Ulalahoi?

Duh! Sijui kuwa hali hii itaendelea hadi lini lakini najua ipo siku tu Kwa mara ya kwanza hawa jamaa wataufyata na kuanza kufungua mdomo yao, na kama hamuamini subirini mtaona kama hivi karibuni hamtashuhudia mikutano na vikao vya muafaka vikianza kufanyika, ingawa haitokuwa Kwa mara ya kwanza kwa vikao hivyo kufanyika.

Yapo mengi sana ambayo hakika yalijiri Kwa mara ya kwanza na ambayo kimsingi siwezi kuyaorodhesha hapa yote, lakini isichukuliwe kuwa nimeishiwa sera, kwa maana kama ikijatokea hivyo basi kwangu mimi hii itakuwa Kwa mara ya kwanza.

Kaka yangu mmoja huwa anapenda kujiita JK (sio yule mgombea kuingia jumba jeupe la Magogoni) bali yule Mlalahoi wa Mtaa wa Majira Jumapili, ananikumbusha kuwa eti uchaguzi huu pia umetukumbusha umuhimu wa kuchagua majina ya kuwapa watoto wetu kama hilo la JK au lile la Anna, kwa maana majina haya kwa mara ya kwanza yameonekana kuwa dili, kwahiyo kwa hakika sijaishiwa kichwani.

Ila nadhani kuwa mtakuwa nayi Kwa mara ya kwanza mmepata kitu kipya kidogo leo na si ajabu hata wale ambao walikuwa wasomaji wasiokuwa na la kuchagia leo hii wakachangia kazi hii Kwa mara ya kwanza kwasababu naamini kuwa nao Kwa mara ya kwanza watakuwa wameshuhudia mengi ambayo waliweza kuyaona Kwa mara ya kwanza na haitokuwa jambo la ajabu ikiwa nao wataniushirikisha katika yale walioyaona Kwa mara ya kwanza

Na kwa hakika leo siwaagi Kwa mara ya kwanza, sababu najua hii pia itakuwa Kwa mara ya kwanza, mimi kutokuwa muungwana kwa wasomaji wangu hivyo watanisamehekwakuwa kosa hili nalifanya Kwa mara ya kwanza
**********

November 24, 2005 at 5:54 pm 6 comments


Blog Stats

  • 35,058 hits
November 2005
M T W T F S S
 123456
78910111213
14151617181920
21222324252627
282930