Bongo Flava, Itikadi Finyu na Mitizamo haba….1

November 13, 2005 at 4:35 pm 19 comments

Kizazi kipya, maisha mapya na Umbumbu Mpya
=============================================

Niliwahi kuandika wakati fulani nikiuliza Muziki wa Kizazi Kipya unakua kwa vigezo gani? Ingawa sikupata majibu ya kutosheleza lakini nadhani kuwa somo liliwafikia wadau na nafurahi kuwa katika sehemu kadhaa mjadala umekuwa mzito kiasi sasa, na ndio maana nikaona nami niingie tena leo kwa machache.

Ukiwasikiliza wakati wanaimba, wanavyoshughulika jukwaani na hata wanavyouita muziki wenyewe, kwa hakika ni lazima ujiulize maswali kadhaa kichwani mwako, kuhusu hiki wenyewe wanakiita Bongo Flava, Muziki wa Kizazi Kipya, na vyovyote vile wanavyoweza kuuita.

Ukisikiliza mashairi wanayoimba, maneno yanavyowatoka, tambo wanazotoa wahojiwapo maredioni, aina ya mavazi wanayovaa, majina wanayojipa, tembea yao mitaani, ITIKADI zao, na utaratibu mzima wa maisha wanaoutumia, kwa hakika unazidi kujiuliza maswali kibao kuhusu hiki kizazi.

Hata hivyo, matatizo ya muziki huu hayakuanza leo hii, na wala hayajaanzishwa kwa kiasi kikubwa na vijana wa sasa wanaouendeleza kwa nguvu zao zote, bali waasisi wa muziki huo nchini, ingawa pia sina hakika kama wenyewe walidhamiria kuwa uje kuwa hivi.

Simaanishi kuwalaumu bali kwakuwa inabidi kuelezana ukweli basi sio mbaya tukaelezana ukweli huo kuwa waasisi wa muziki huu wanaouita Bongo Flava, hivi sasa hawakuwa wameweka misingi ya kuufanya uwe Muziki wa Ki-Bongo kwelikweli, na ndio maana tunaona matokeo yake hivi sasa.

Hivi Tanzania ina utamaduni wa Wine ulioanzishwa na nani hadi wawe ndio wanaziimba sana kwenye nyimbo zao? Utamaduni wa Mtanzania si ule wa Kangala, Kachaso, Kangala, Kibuku, Ulanzi, Mnazi, Chimputu, na nyinginezo nyingi zinazopatikana hata kule kwa akina- Nyegerawaitu? Watanzania utamaduni wa Wine wapi na wapi?

Wanaacha kuvaa hata Shanga, wenyewe wanakazania hizi wanaita Cheni, Mikufu sijui Vikuku vya dhahabu, almasi na hata shaba, hivi Mtanzania wa kweli, ambaye kwa mtazamo wao ndio Mbongo, ana utamaduni wa wapi na vitu hivi? Mtanzania wa kweli asiyejua kuvaa kaniki ambayo haina shida hata katika uvaaji wake anayeweza hata kufunga na katani ikiwa inapwaya, utamaduni wa suruali za mlegezo umeanzia wapi?

Tulijengwa katika mazingira kuwa muziki huu ni lazima uwe na masuala hayo na ndio maana hadi leo hii vijana wetu wakitoka na rekodi basi utakuta imerekodiwa kwenye vijihoteli vyetu uchwara ambavyo wanaona wamemaliza mchezo, vijihoteli ambavyo mmarekani mwenyewe ambaye wanataka anunue muziki wao anaviona kama vibanda vya …….

Wanaacha kurekodia kwenye vijumba vyao vya Msonge kule madongoporomoka, na kuutangaza utalii wetu, kisha wanakueleza kuwa nia yao ni kupasua anga kwa kuuza nakala kibao, kwa kitu cha kuiga? kwa maana huyo ulomuiga hawezi kukinunua kamwe sasa utamuuzia nani? Hatukuwa na misingi imara ya huu muziki wetu na ndio maana hadi sasa wanazidi kuibuka tu vijana wakihanikiza Itikadi zao za kusaka mishiko hata kwa kufyeka watu…Mtanzania huyo…ni kijana wa Kitanzania huyo

Yapo mapungufu mengi sana kuhusiana na huu muziki wetu lakini nadhani pia kuwa tunaweza kabisa kurekebisha hali hii, ikiwa mimi nawe tutaamua kulifanyia kazi kwa kuanza kukitaka hiki kizazi kubadilika…Tayari alishaanza Jeff Msangi, akizungumzia juu ya huu Muziki wa Kizazi Kipya na wakajitokeza watu kujadili na wakajadili zaidi na hadi sasa mjadala haujaisha nadhani. Hivi karibuni Ndesanjo naye ambaye nadhani hakuwa amekusudia alilazimika kuanzisha mjadala baada ya kupelekewa waraka fulani na balozi mmoja wa Kitanzania, lakini uzao wa hiki hiki Kizazi kipya…Mnasemaje Watanzania?

Entry filed under: maskani.

Suala la Zanzibar…TUZUNGUMZE tuache KUSEMA Mtanzania mwingine (sio mswahili) ajiunga kwenye Blogi

19 Comments Add your own

 • 1. yakub nyembo  |  November 13, 2005 at 5:57 pm

  mh!hapa suala ni asili,itikadi,utamaduni,historia na pengine ujio wa fikra za umbumbu katika maisha ya muziki wa ushetani mpya wa kizazi hiki.hapa hakuna muziki wa kizazi kipya wala kizazi chenyewe nionavyo mimi anayezaliwa sekunde hii ndio kizazi kipya tena sio hii ninayoandika tu bali ile unayosoma mawazo haya,nae hawezi kutunga wala kuandika acha kuimba na kutia voco kabla ya kuvaa sarawili za masurumbwete na buga ili kukamilisha ushetani wa kina mkono wa damu tena usio na usahihi kamilifu,bado kuna haja katika midahahalo na majadiliano haya kuwahusisha waandishi wanaofanya uchambuzi wa muziki huu pamoja na wale wanaoitwa waasisi wa bongo beats,bongo flava,kizao kipya chenye uwendawazimu mpya!

 • 2. Indya Nkya  |  November 14, 2005 at 12:02 pm

  Yakubu ameongea kitu kizuri kwenye huu mjadala. Ni nini Mchango wa waandishi wa habari katika kuchambua muziki huu. Kwanza ni nani alianzisha hilo jina la kizazi kipya na kulikuza?

 • 3. msangimdogo  |  November 14, 2005 at 6:09 pm

  @Idya Nkya
  sinashaka wadau watajadili suala hili kwa undani kwa maana huu ndio uwanja wao wa kufanya hivyo….majadiliano yanaendelea

 • 4. james  |  November 16, 2005 at 3:07 pm

  Napingana na ndugu yangu Idya hapo juu, inawezekana kweli kuwa vyombo vya habari vimeshiriki sana katika upotoshaji huu lakini nadhani vyombo vya habari kazi yake ni KUANDIKA na sio KUTENGENEZA habari nikimaanisha kuwa waliona hayo mambo wakawa wanaandika, kwahiyo sio wao walioyakuza ila tu hawakujua kuwa nao ni sehemu ya jamii na kwamba wangeweza kuondosha hali hiyo kwa kuikemea

 • 5. abdallah salum  |  November 16, 2005 at 3:14 pm

  Kama kuna mtu ambaye alinishangaza sana ni Joseph Haule, huyu bwana wakati alipotoa wimbo wake wa Bongo dar es salaam, alikandia sana hulka ya baadhi ya wasanii kujipachika majina yasiyo ya kwao……” bitozi nyangema anataka aitwe 2pac…” kilikuwa kipande cha sehemu ya wimbo wake huo, lakini naye sasa duh…..the heavy weight mc, daddy, nk…ni baadhi tu ya majina ambayo amejipa badala ya kuutangaza uafrika wake

  Kwakweli hakuna juhudi ambazo zimekuwa zikifanywa na wasanii wenyewe katika kuhakikisha kuwa wanautangaza na kujivunia Utanzania wao, yaani msanii anajikuza kimarekani, anaimba kimarekani, anavaa kimarekani, anaongea kimarekani anatamani hata kulala na kucheka pia iwe kimarekani….yaani kaaazi kweli kweli

 • 6. mtutukutu  |  November 16, 2005 at 3:20 pm

  sir nature, y-dash, jd,ray c, crazy gk, mzee wa commerial,….nk….kaka hapa kazi ipo tena sio ndogo, ya kutosha tu sijui kuwa itakuwaje huko mbele lakini kazi tunayo babake

 • 7. msangimdogo  |  November 16, 2005 at 3:27 pm

  kwa hali inavyoelekea nadhani kuna umuhimu wa kujaribu kumwona au kuwaona baadhi ya wasanii wanaotamba hapa nchini wazungumzie hali hii……….mnasemaje wasomaji wangu? itakuwa vipi kama nikimpata mr. II, Baba Ubaya, Juna nature, Crazy GK…..si itakuwa safi tu mazee? Basi msikonde

 • 8. Indya Nkya  |  November 19, 2005 at 11:54 am

  @James
  Ndugu yangu kazi ya waandishi si kukusanya habari tuu. Nadhani waandishi wanakusanya habari wanaziandika na kuzisambaza. Lakini kubwa zaidi, mwandishi ana wajibu mkubwa sana wa kuchambua habari na jamii nzima. Pili siwalahumu kwamba wameshiriki kukuza hiyo dhana ya muziki wa kizazi kipya.

 • 9. Ndesanjo Macha  |  November 20, 2005 at 2:40 am

  Ramadhani: nimekubaliana nawe kwenye dhana uliyoiita: umbumbumbu mpya. Pia nakubaliana kuwa ukiweza kuwapata hawa jamaa, tupatie tuzungumze (natumia hoja yako ile ya kuzungumza na sio kusema) nao. Asante kwa kuendeleza mjadala huu muhimu sana.

  @James:
  Nakubaliana nawe kuwa kazi ya waandishi wa habari (kama lilivyo jina lao) ni kukusanya habari na kuandika. Lakini sitakubaliana nawe ukitaka tukubali kuwa kazi waliyonayo ni hiyo tu. Ndio, wanatakiwa kutupasha habari, ila wanapaswa pia kutuelimisha, kutupa changamoto, kutufikirisha, kukosoa, kuonyesha njia, n.k. Sababu kubwa wengine tumeanzisha blogu ni kutokana na mtazamo huo kuwa waandishi kazi yao ni kupasha tu habari. Wengi tunaamini kuwa siku na miaka inavyokwenda (kama inavyotokea kwenye nchi nyingine) blogu zetu zitakuja kuwa vyanzo vya habari vya kuheshimiwa na pia viwanja vya maarifa. Wanablogu duniani hivi sasa wanafanya kile ambacho vyombo vya habari (napenda kuviita vyombo vya uongo) havitaki kufanya.

  @Mtutukutu:
  Kweli kazi tunayo babake.

 • 10. msangimdogo  |  November 20, 2005 at 8:03 am

  Nilijua kuwa suala hili LINAZUNGUMZIKA:

  @ James:
  Binafsi siwezi kukulaumu sababu hukuwa umekosea sana kwa imani yako, kwa maana hilo kweli ndio jukumu la waandishi, lakini ni kweli pia kuwa wana jukumu kubwa sana katika kuhakikisha maadili yanakuwepo, na ndio maana kuna suala la UHARIRI. Hawawezi (na wenyewe wanajua) kuandika kila kitu kama kilivyo. Hata hivyo, huenda hii ikawa changamoto nyingine ambayo inatakiwa kuchukuliwa na waandishi kama udhaifu walionao, kiasi cha hata jamii kushindwa kujua umuhimu wake. Tuendelee Kuzungumza

 • 11. ZAY ALLY  |  November 20, 2005 at 7:31 pm

  Bongo FLEVA ni jina ambalo kwa mara ya kwanza lilinipa utata na baadea kuamua kuliacha kama lilivyo. HII BONGO FLEVA kwa kiswahili tumesikia vituo vya Radio Vikisema LADHA ZA BONGONA hii BONGO sijui ni DAR au ni Tanzania au ni Africa mashariki. Mwanzoni walikuwa wakiziita Hip hop, African hip hop mwisho ndiyo BONGO fleva ikashika hatamu. Sijui hii BONGO FLEVA kuitwa mziki wa kizazi kipya ni kwa kwamba ni muziki wa vijana au ni miziki ya hii karne mpya au vipi Labda kwa nyie waandishi ambao mara kwa mara mnafanya interview na wasanii pamoja na kuperuzi kwenu mnaweza kutupa jibu kama sio jipu. Cha kushangza ni hivi, unakuta kanda( Tapes) CD’s zimeandikwa TOP TEN BONGO FLEVAS, sijui hata hizi zinatengenezewa kichochoroni au vipi, unakuta kuna waimbaji wa Uganda, Kenya, Tanzania, wanamuziki wakongwe sasa sijui. Nyingine zina majina ya Kizungu, mahadhi ya kizungu sasa sijui huo u-bongo fleva unakuwaje?

 • 12. Jumaa  |  November 21, 2005 at 10:21 am

  kwanza mr. msangi naomba nikubaliane nawe kuwa MUZIKI wa KIZAZI KIPYA, ni neno ambalo tayari limeshakuwa tata. Maana sio tu hiyo Hip Hop, ambayo wameigeuza kuwa muziki wa kizazi kipya, maana hata huu muziki wa dansi pia wameugeuza kuwa wa kizazi kipya. Ukisikiliza Taarabu za kisasa, Muziki wa dansi wa kisasa, miduara ya kisasa na hata ngoma zetu za kisasa, utaona dhahiri zimepoteza vionjo vya uasili wa Mtanzania…na huu wote bilashaka ni muziki wa kizazi kipya. Kwa maana nyingine ni kuwa kuna Ngoma za kizazi kipya, Taarabu za Kizazi kipya na kila kitu cha kizazi kipya…..hebu tuzungumze katika muktadha huu

 • 13. Anonymous  |  November 21, 2005 at 2:39 pm

  nashukuru kwa kunipa nafasi ya kusema chochote juu ya suala hili la huu muziki wa hapa nyumbani wanaouita “muziki wa kizazi kipya au bongo fleva”. kwakweli ukisikiliza vionjo vyao wanavyotumia utapenda, sio siri ni vizuri lakini sasa kinachokuja kukera huu muziki umejaa sana makasumba ya nchi za magharibi. ukiangalia kuanzia mavazi, shooting zao na mazingira wanayotumia kutengeneza muziki wneyewe. zipo kazi za baadhi ya wasanii kwa kweli zinakubalika na zina kila sifa ya kuiwa muziki wa bongo, kwani ukiangalia mazingira waliyofanyia kazi zao yanakubalika kuitwa mazingira ya mtanzania halisi sio yale ya kuigizia. napenda sana kuangalia kazi ya msanii Renee, katika “ngoma za kwetu”, halafu kuna wale jamaa wanajiita Solid ground family katika “Bush party”. halafu tena hata AY nae katika Binadamu nae kajitahidi sana nimeipenda kazi yake, angalau wasanii hawa wamejaribu kuonyesha mazingira kamili ya mtanzania. sasa wewe msanii utakuta anaishi vingunguti lakini anataka afanye shooting ya wimbo wake kama mmarekani anataka aonyeshe kuwa yeye hana tofauti na wasanii wa nchi magharibi. sasa hii kasumba ya kuiga umagharibi itaisha lini? kwa maana hiyo kazi za wasanii wetu wa hapa bongo kupata mafanikio katika soko la kimataifa ni ndoto za alinacha. kwani wanaiga umagharibi hivyo zikienda sokoni zinaonekana zipo chini ya kiwango kinachotakiwa katika soko la kimataifa. hivyo wao wataishia kuuzia kazi zao hapahapa nyumbani. thanks tchaoo!!

 • 14. Anonymous  |  November 21, 2005 at 6:46 pm

  Haya tena msela. Hivi maana ya BONGO Fleva ni nini? Namuunga mkono Zena hapo juu jinsi walivyoua jina hip hop kwa style ya mende. Bongo ni Tanznia au? na kama ni hivyo je hizo nyimbo ziko katika hali ya kitanzania? Na je wabongo wan asili ya wanume kuvaa hereni, kusuka nywele, au wanawake kutoboa vitovu, au wanamuziki hawa wanojiita wa kizazi kipya wakishaanza kupata umaarufu ndo wanaanza kula steers,best bites, Florida pub,mara kuchora miili yao(tatoo) Kariakoo hawaendi tena mambo ni shoprite

 • 15. Jeff Msangi  |  November 23, 2005 at 11:51 pm

  Mjadala mkali na wakati ni muafaka kabisa.Namaanisha kabla merikebu haijazama.Nadhani wakati umefika sasa kwa kuwauliza wahusika hasa(wanamuziki wenyewe)Msangi mwenzangu utatusaidia kwa hili(ahsante sana).

 • 16. kivale  |  November 25, 2005 at 8:54 pm

  Babuuu najua siyo niyayako kumtafuta mchawi wa upotoshaji wa jina la huo muziki wala mavazi yao tenbea yao maisha yao wala kwa sisi tunao changia. ila nikuwekana sawa kwa hili ambalo linatokea na linaloendelea kutokea nahisi mjadala huu unaendelea kuwa mkubwa na kutofikia muafaka bila kutizama upande wa pili na upande huu. watu wengi wamekuwa hawaujui hatimae wamewaingiza watu wangine kuhusika kuchochea,kukuza,na kuhamasisha ambao wanaitwa waandishi. lakini siyo kweli hakuna kitu kama hicho japo wapo watu fulani ambao wapo kwenye kitengo hichocho cha uandishi lakini baadhi yao ukiwachukua na kuwapeleka sehemu wakachukue hiyo habari si ajabu akakwambia sijui niandikaje maana hajui lolote zaidi ya kile alicho somea kutangaza tu. na hao ndio mameneja wa hao vijana na ndio wanaotangaza kwa nguvu zote jina la muziki wa kizazi kipya hivyo wamekuwa wakitumia vibaya vituo vya utangazaji kwa masrai yao kwa kupanga wimbo ulio shika chati na kuludia ludia kupiga kwa kisingizio wimbo mpya na umeombwa na watu wengi wakati yeye ndio meneja wa vikundi hivyo hivyo husababisha watu kulazimika kusikiliza na kuuzalau nyimbo zenye utanzania kwa kusahau kutokana na kutokuzisikia mara kwa mara jamani hawa hamfahamu kuwa wanachangia kuwaharibu hao vijana kwa kuwatangaza kwa majina ya a.k.a na kufanya wavimbekicha na kujikuta wanabadilisha hata mavazi na mwendo wao?

 • 17. msangimdogo  |  November 26, 2005 at 8:04 am

  Bado jitihada za kuwasaka baadhi ya wasanii zinaendelea, japo nimekuwa pia nikijitahidi kuwasiliana na baadhi ya wachambuzi wa masuala ya muziki hapa nchini kutoka vyombo kadhaa vya habari ili wanipe mtazamo wao kuhusu wao kuchangia kwa kiasi kikubwa katika upotoshaji huu.

  @Twaha Kivale.
  Mzeeumeleta hoja ya maana sana hapo, ni kweli kabisa kuwa asilimia kubwa ya wale wanaoitwa mameneja wa wasanii wetu ama ni waandishi wa habari hasa za burudani, au watangazaji katika vituo fulani fulani vya Radio au Luninga, na hakika wamekuwa wakiyafanya hayo…kufanya machaguo yao wakidai ni maombi ya wapenzi wengine. Labda hili nalo tutalizungumza na mmoja kati ya wadau ninaojitahidi kuwatafuta.
  TUENDELEE KUZUNGUMZA

 • 18. Tabu Sudi  |  December 8, 2005 at 12:19 pm

  Mimi niko tofauti kidogo na wachangiaji wa mada hii, mimi kwa mtazamo wangu ni kwamba mziki wa kizazi kipya lazima kiende na wakati uliopo, kwanza ukiangalia mziki wa kizazi cha zamani utaona tofauti kuanzia mavazi (bugaluu na mashati ya slimfit na viatu vya platform)hadi uchezaji wake ni tofauti na sasa. kitu cha muhimu ni kuangalia maudhui ya wimbo yanawafikiaje wananchi? kuna baadhi ya maeneneo ndio yanatakiwa kufanyiwa marekebisho hasa wakina dada kuhusu kuvaa nguo nusu uchi.

 • 19. mwalyoyo  |  November 22, 2006 at 3:39 pm

  Nakubaliana na watoa maoni walio wengi kuwa kuna mushkeli katika muziki wetu.Kumekuwa na lawama sana toka kwa watu wazima kuwa muziki huu ni wa kihuni sana! Kwa upande fulani naona kuna ukweli wa suala hili. Hebu kwanza angalia majina ya wanamuziki wetu wa Muziki wa kizazi kipya. (rejea maoni ya mtutukutu hapo juu) Utakuta wanajiita, Soggy Doggy, Mb Dog, King Crazy,Misifa, Commando, Dudubaya, Zimwi nk. Sasa ktk muktadha huu, unafikiri ni mtu gani na heshima zake atanunua albamu ambayo ina jina mojawapo kati ya hayo? Thubutu! Kwa ufupi atafikiri kuwa ndani ya albamu hizo hakuna nyimbo za maana, kutokana na jina tu! Hali kadhalika, video za wasanii wetu zina walakini, kwani maudhui ya video hizo haziendani na mazingira halisi ya Mtanzania. Hali kadhalika, Afande Sele alijaribu kukemea tabia ya wanamuziki wa Tanzania kutumia lugha za kigeni ktk muziki ambao walengwa wake ni Watanzania. Ukiangalia hii ni kweli, kuna wasanii wengi sana kwa sasa ambao huchanganya Kiingereza na Kiswahili, sasa sijui huu ni utamaduni wa wapi! Wazo langu ni kwamba, tujaribu kuweka makongamano na warsha ili kuwaelimisha hawa watu vile ambavyo sisi kama hadhira tunataka wawe. Nahisi kuwa hili linawezekana, hata kwa kuanzia na mwanamuziki mmoja mmoja! Inawezekana, tutimize wajibu wetu!

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Trackback this post  |  Subscribe to the comments via RSS Feed


Blog Stats

 • 35,058 hits
November 2005
M T W T F S S
 123456
78910111213
14151617181920
21222324252627
282930