Archive for November 7, 2005

Suala la Zanzibar…TUZUNGUMZE tuache KUSEMA

Kuna KUSEMA na KUZUNGUMZA.
Mambo mengi YAMESEMWA, baada ya Bw. (mh.?) Aman Abeid Karume, kufanikiwa kutetea nafasi ya urais wa Visiwa vya Zanzibar, akimbwaga mpinzani wake mkuu, Bw. Seif Shariff Hamad, kufuatia uchaguzi wa hivi karibuni visiwani humo.
Sinashaka pia wenye hamu na shauku ya kufungua midomo yao kuiruhusu itoe chochote kuhusu uchaguzi huo, wangali wapo, lakini, wote hao watafanya hivyo kwa dhamira ya KUSEMA.
Hili ndilo lililonivuta kufungua mdomo, fikra na mawazo yangu, kuruhusu mtizamo wangu kuhusu uchaguzi huo utoke, ingawa niko tofauti na wenzangu ambao wameshanitangulia. Tofauti tuliyonayo ni kuwa walionitangulia wamekuwa WAKISEMA lakini mimi napenda KUZUNGUMZA.
Ndio, nataka KUZUNGUMZIA uchaguzi wa Visiwa hivyo ambavyo viliwahi kuvuma kwa a.k.a ya ‘Visiwa vya Marashi ya Karafuu’, ingawa hivi sasa vinaelekea kuwa ‘Visiwa vya Machafuko na Umwagikaji damu’
Kwa mujibu wa moja ya Kamusi za Kiswahili Fasaha (kati ya nyingi), nilizowahi kusoma, ‘KUZUNGUMZA‘ huchukuliwa kama mbadilishano wa mawazo, kutoa mawazo katika mkutano, kutoa hoja, kujadili na mengine ya uelekeo huo. Kifupi MAZUNGUMZO ni lazima yahusishe pande mbili ili yawe na sifa ya kuitwa MAZUNGUMZO.
KUSEMA‘, kwa upande wake ni kutamka, kusengenya kupaza sauti na mengine yenye uelekeo kama huo. Kifupi KUSEMA sio lazima kuwa na pande mbili, sio lazima watu wa kukusikiliza wawepo, sio lazima watu wa kujali unachosema wawepo, sio lazima wawepo watu wa kukujibu na mambo kama hayo.
Naam, nimerejea maneno hayo kutokana na mtizamo wangu juu ya Uchaguzi huo ulivyokuwa, toka zama za mchakato wa kuuelekea hadi kufanyika kwake, na mapokeo yake kwa Wazanzibar wenyewe, Watanzania na Dunia kwa ujumla.
Kabla sijaendelea zaidi, kwanza pengine nitapenda kuwa wazi (haijalishi kuwa watanichukia baadhi ya watu), kwa kusema kuwa “Katika zama hizi, kuzungumzia siasa za Visiwani humo, unahitajika kuwa na akili zisizotosheleza kichwani mwako, ama ziwe zimepungua au zimezidi sana.
Kwa wale wenzangu ambao wamekuwa wakifuatilia mwenendo wa siasa za Visiwani humo, ni wazi kabisa kuwa watakubaliana nami kuwa Zanzibar hakuna siasa zenye misingi ya halisi ya kisiasa, bali siasa za Uhasama, Chuki, Visasi na kwa hakika Uchu wa Madaraka, kwa baadhi ya wadau wa siasa hizo.
Hali hii imekuwa ikijionyesha wazi nyakati mbalimbali, iwe wakati wa mikutano ya kawaida ya wafuasi wa vyama mbalimbali vilivyopo visiwani humo, au nyakati za kampeni au uchaguzi kama ilivyo sasa. Siasa za Zanzibar ni ‘KUSEMA’ sana na sio KUZUNGUMZA, hali ambayo imeambukizwa hadi kwa waandishi wa habari na wachambuzi wa masuala mbalimbali kuhusiana na mwenendo wa siasa za eneo hilo.
Hivi ni nani anaweza kuniambia kuwa Bw. Karume au mpinzani wake waliwahi KUZUNGUMZA, iwe wakati wa kampeni zao au wakati wa mikutano yao mbalimbali wakati wa kuelekea uchaguzi huo, zaidi ya kuwa wote walikuwa mahodari wa KUSEMA?
Ni katika KUSEMA tu ambako hata hiki tunachokiita hali tete iliyoenea eneo hilo kimewezekana. Ni katika KUSEMA tu ambako chama fulani kinaweza kuwa na MATOKEO yake kinyume na yale ya tume. Ni katika kusema tu ambako mtu mmoja anaweza kutishia kulala barabarani na mwingine naye akasema ataenda kulala kwenye nyumba yake.
Ndio, ni katika KUSEMA tu ambako mtu anaweza kukurupuka na kusema hakuna serikali ya mseto wakati nguvu za madaraka kwa wanaowakilisha wananchi zimegawanywa karibu sawa. Ni katika KUSEMA tu ambako mtu anaweza kuja na tishio la kushusha Gharika ikiwa hatarejeshewa kura zake(?) alizoibiwa.
Naam, ni katika KUSEMA tu ambako hata Mmarekani, ana haki ya kuingilia madaraka ya Wazanzibar, ni katika KUSEMA tu ambako hata asilimia kubwa yetu waandishi tumejikuta tukiamini kuwa kulikuwa na wizi wa kura kule visiwani, na ni katika KUSEMA tu ambako demokrasia ya kweli haimaanishi lolote lile zaidi ya kushinda URAIS wa nchi. Hii ni hatari, tena hatari kubwa sana.
Wakati mchakato wa kupata serikali mpya kwa upande wa Tanzania nzima kwa ujumla na Visiwani kwa upande wao, nilibahatika kuwa mmoja wa waliokuwa wakifuatilia kwa ukaribu mkubwa sana mwenendo mzima wa mchakato huo, na hasa katika kile kipindi cha KUTUPIANA MADONGO, wenyewe walikuwa wanakiita kipindi cha KAMPENI (sijui hata walikuwa wakijua maana ya KAMPENI kweli kweli au walikuwa waki-SEMA tu.
Kwa wafuatiliaji wenzangu, ni wazi watakubaliana nami kuwa kilichokuwa kikijiri wakati wa zoezi hilo, kwa wenzetu wa huko Visiwani, hakikuwa kampeni ambazo wananchi walikuwa wakizihitaji (nazungumzia mwananchi makini, maana wasiokuwa makini pia wanakuwa hawafai, wameshapandikizwa mbegu za ku-SEMA), zaidi ya kupokezana mizigo ya lawama, vitisho na ubabe wakinamna ndani yake.
Tanzania ikiwa kama moja ya nchi ambazo zinakabiliwa na umasikini mkubwa, imekuwa ikijitahidi sana kuandaa sera karibu kila kukicha ili kuupiga teke huo umasikini, laini imekuwa ikishindikana sababu ya ubovu ama wa sera zenyewe au watekelezaji wa sera hizo, na hasa wale viongozi.
Ni vyema pia ikaeleweka kuwa sio hao CUF wala chama kingine chochote ambacho kingeweza kuingia madarakani na kisha kuweka mpaka wa mstari mwekundu pale serikali iliyopita ilipokuwa imeishia na kisha wao wakaanza na yao mapya kabisa. Ni wazi kabisa kuwa kuna mambo mengi ambayo wangeyakuta na wangelazimika kuyaendeleza, ikiwa ni pamoja na baadhi ya sera ambazo zimeshaandaliwa, sababu sio zote ni mbovu.
Ni katika mustakabali huu basi ambapo nilitarajia kampeni zingelilenga kufafanua mchakato wa kutekeleza sera fulani, utaanzaje hadi kumaliza namna gani na sio atatufanyia nini…ataanzisha huduma gani au kitu gani, ilhali hata hizo zilizopo wanashindwa kuzitekeleza. Haukuwa wakati wa ku-SEMA ilimradi mtu anajisikia ku-SEMA bali ulikuwa wakati wa KUZUNGUMZA.
Ulikuwa wakati wa wagombea kuwasikiliza wananchi wanasemaje, na kushauriwa pale ambapo wagombea wakiwa kama viongozi, wangeona kuna mapungufu katika hoja au matakwa ya wananchi. Ulikuwa wakati wa KUZUNGUMZA na wala sio KUSEMA
Lakini hali haikuwa hivyo tu safari hii kwani baada ya jamaa zetu kuona kuwa wamedanganya vya kutosha miaka iliyopita na wakashindwa, wakaona kuwa safari hii uongo hautawasaidia na badala yake kuongeza juhudi katika kupandikiza mbegu za chuki, uhasama na uonevu dhidi ya watu fulani. Badala yake wakaelekeza juhudi zao katika kujidai “Maripota wa Udaku”. kucha kutwa wakifuatiliana siri zao za ndani ili kila mmoja aje mmbomoa mwenzake akipata wasaa wa kupanda jukwaani.
Na wakati haya yakiendelea, kimsingi yakiendelea kushika kasi na kila mmoja akijua kuwa yanatupeleka pabaya, na wananchi wakijua kabisa kuwa sio mambo wanayoyahitaji, bado wengi wetu tuliendelea KUSEMA badala ya KUZUNGUMZA. Hatukuweza kuona haja ya kuwakutanisha hawa watu na kuwabana kwanini wanazidi kutupeleka pabaya kwa tambo na kauli zao, hatukuwahi kuwakalisha na kuwaonya, hatukuwahi hata kuwanyooshea kidole, na badala yake, nasi kwa upande wetu kila mmoja alikuwa AKISEMA lile aonalo kuwa linamridhisha.
Hebu tugusie mchakato wa Uchaguzi huo na Uchaguzi wenyewe na baadhi ya Vijimambo vilivyojiri baada ya uchaguzi wenyewe..
Kuna suala la malalamiko dhidi ya Tume ya Uchaguzi ya Visiwa vya Zanzibar,(ZEC), malalamiko ambayo yanatolewa zaidi na waliokuwa wagombea kutoka chama cha CUF pamoja na wanachama na washabiki wao. Hivi ni lini Seif Shariff Hamad aliikatia rufaa ya kisheria Tume ya Uchaguzi huko Visiwani, lakini pingamizi lake likatupwa?
Hivi ni nani aliiambia serikali kuwa Wazanzibar hawataenda kupiga kura siku hiyo ila kufanya fujo kwahiyo wawapelekee misururu ya Polisi na magari yaliyojaa maji yenye Upupu sijui wa kutoka wapi, wakati magari ya namna hiyo yamekuwa hayaonekani wakati wananchi wanapounguliwa na nyumba zao ili yasaidie kuzima moto?
Hivi ni nani aliyewapa mamlaka mawakala (naambiwa eti walikula viapo, bilashaka kwa ku-SEMA tu viapo hivyo midomoni mwao na sio KUZUNGUMZA na nafsi zao), kuwa na nyaraka zao za matokeo wakati hizo ni nyaraka za tume? na zaidi ya yote madaraka ya kuwa Watangaza matokeo?
Hivi ni nani amemwambia Karume kuwa akiunda serikali ya mseto kule Visiwani atakuwa ametenda dhambi ya kuhukumiwa kwenda Jehanam siku ya kiama, ni nani aliyemwambia kuwa Viongozi wazuri ni lazima watoke chama cha CCM, mbona sehemu zingine waliangushwa kama kweli kila mwana-CCM ni mtu safi?
Kwa hakika hakuna. Hakuna aliepinga tume, hakuna aliyesema serikali ya mseto visiwani ni sawa na Nguruwe kupelekwa ndani ya Msikiti, hakuna aliyekuwa na ushahidi kuwa Wazanzibar walikuwa wamejiandaa kufanya fujo na wala hakuna ambaye ana uhakika na hicho wanachodai kuwa ni matokeo yao sababu hakuna ambaye anaweza kushuhudia mbele ya Mungu wake kuwa anajua kilichoko ndani ya nafsi ya Karume au ndani ya Seif ni kitu fulani na ni cha ukweli kabisa.
Lakini kwa bahati mbaya zaidi, au kibaya zaidi ni kuwa hakuna ambaye amethubutu KUZUNGUMZA kuhusu hali hii na badala yake kila mmoja anakazana KUSEMA. Inanishangaza hata baadhi ya vyombo vya habari na baadhi ya waandishi pia tumo katika mkumbo huu.
Hivi kuna mmoja kati yetu aliwahi kuingia ndani ya moyo wa mfuasi aliyebahatika kuongea naye akajua kuwa alichoelezwa ni kweli tupu? Kwasababu Siasa kwa misingi hasa ya Siasa na hasa Siasa zenyewe zinapokuwa zinahusisha Wanasiasa wa hapa Tanzania na hususan Visiwani, zimejengwa katika misingi ya Uongo, Unafiki, Uzandiki, Ufisadi, Majungu, Tamaa na Uchu wa Madaraka.
Ni rahisi sana kwa mtu aliyekulia katika ‘madhehebu’ ya namna hiyo kutokuwa mkweli daima dumu, kutokuwa mkweli kwa maisha yake yote, na haya sio ya kuyajadili kwa maana wapo watu wa namna hii. Wapo wanasiasa ambao wamezikana hata nafsi zao kwa ajili tu ya madaraka, wapo wale ambao wamediriki kudanganya nafsi zao wenyewe ilimradi kupata kitu fulani. Ndio, wapo watu wa aina hii, sasa kwanini basi tuamini kuwa wanachoki-SEMA wao ni ukweli?
Kwangu mimi bado naona kuwa suala la Zanzibar, sio la Wamarekani, sio la waandishi, sio la tume ya uchaguzi visiwani humo, sio la waangalizi wa uchaguzi, sio la polisi na wala sio suala la kila mtu kujitahidi kujiaminisha kuwa ndio lilivyo. Suala la Zanzibar ni suala la KUZUNGUMZA badala ya KUSEMA.
Nasema la KUZUNGUMZA kwasababu ninaamini kabisa kuwa wadau wa siasa za visiwani humo ni watu wenye nguvu sana. na hili linanipa matumaini kuwa wote ni watu walioiva katika siasa (bila kujali ni za aina gani maana ndio walizojichagulia). Hii ikimaanisha kuwa ni watu ambao wanaweza kukaa meza moja na kujadili masuala hayo na yakaenda sawasawa kabisa na kuzimwa kwa hizi chokochoko zilizopo hivi sasa.
Kwa nguvu walizonazo wana-CUF, wanaweza kabisa kuwashinikiza viongozi wao kukaa na wale wapinzani wao na kujadili hatma yao ikiwa kweli wanataka Maendeleo, na ikiwa kweli walidhamiria kufanya uchaguzi ili kupata viongozi watakaoleta changamoto mpya katika kuharakisha maendeleo.
Kwa nguvu walizonazo wana-CCM visiwani humo, ninaamini kabisa kuwa wanaweza kumshinikiza Karume na akakaa meza moja na Maalim Seif kujadili hatma yao ikiwa kweli bado wana ndoto zao za kuigeuza Zanzibar kuwa Rome, kama kweli bado wana ndoto za kumfanya kila Mzanzibar kusahau kitu Umasikini. Ndio, haya yanawezekana, ikiwa tu kila upande utaacha Unafiki na Uongo.
Binafsi bado naamini kabisa kuwa Bw. Karume anaweza kabisa kukutana na mwenzake Seif, wakakaa na wakajadili juu ya mustakabali wa visiwa hivyo. Kwa maana ya KUZUNGUMZA na sio KUSEMA.
Akisimama huyu jukwaani anasema…’eee, ndio lazima serikali ya mseto…..” Serikali ya mseto jukwaani?…akisimama huyu naye sababu anaona aibu kuambiwa kaogopa, anaanza……’andikeni mmeumia serikali ya mseto’. Kaumia yeye au mmeumia Wazanzibar wote ambao mtaishia kulumbana badala ya kujiletea maendeleo?
Kwa hulka ya wanasiasa, huwa sio watu wa kufikia muafaka katika majukwaa hata siku moja, maana Majukwaa yetu hayatumiki kwa ajili ya Siasa bali Kuonyeshana uhodari wa Kupondana na kutangaziana ubabe. Ila pale wanapokaa pamoja na kuweza KUZUNGUMZA, na hili naamini kabisa linawezekana Zanzibar. Kwanini ishindikane?
Haiwezi kushindikana kabisa sababu kama kila mmoja akiwa na lengo la kujenga basi hatimaye tutajenga ila tu kwa kukaa pamoja na TUKAZUNGUMZA haya mambo jinsi yalivyo kwa maana YANAZUNGUMZIKA.
Huu ushabiki wa kuwa fulani kaniibia kura…fulani alidhamiria kuniletea fujo…huu ni ufinyu wa mawazo ambao hautuelekezi sehemu ya kuhakikisha kuwa siasa za visiwani humo zinakuwa za kuweka mazingira ya kupata serikali zenye kuingizwa madarakani kidemokrasia na zikiwa na changamoto za kuwakomboa wananchi.
Poleni sana mlioshindwa, sababu mmeshindwa kufikia ndoto zenu za kuingia IKULU (na sio kutawala maana mmevuna viti vya kutosha lakini hamtaki kujivunia kuwa hayo ni mafanikio makubwa)
Poleni mlioshinda, kwa maana nyie mna kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa mbegu zenu za chuki mlizopandikiza na ambazo zimesha mea, mnazinyunyiza dawa haraka ili zife kusudi muweze kuendeleza gurudumu la maendeoe ya Visiwani kwenu.
Poleni nyote ambao mtakuwa mmekerwa na maandiko haya kwa maana huu ni mtizamo wangu hata mkisema vipi siwezi kuubadilisha. Ila tu ninawafariji kuwa kwangu mimi. kila kitu KINAZUNGUMZIKA na atakayetaka tuzungumze tutazungumza..ila atakayetaka KUSEMA basi nitamwacha aendelee KUSEMA kwa maana Mdomo ni mali yake.

November 7, 2005 at 1:36 pm 8 comments


Blog Stats

  • 35,058 hits
November 2005
M T W T F S S
 123456
78910111213
14151617181920
21222324252627
282930