Archive for November, 2005

Kwa mara ya Kwanza………!!

Si kwamba nimekuwa mshairi….la, bali najaribu kuangalia tu kuwa ni mambo mangapi ambayo yametokea ama kujiri Kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa mwaka huu.

Na kwa hakika, hii itakuwa Kwa mara ya kwanza naandika kitu katika mfumo wa mashairi utadhani nimekuwa msanii wa muziki wa kizazi kipya, ingawa kwa hakika ikitokea nikapata nafasi ya kuimba mahali huenda nikaimba Kwa mara ya kwanza

Naam, zoezi au mchakato (kama wenyewe wanavyopenda kuita) la uchaguzi mkuu wa Tanzania mwaka huu wa 2005, kama lilivyotarajiwa limeshuhudia mambo mengi sana lakini yapo yale ambayo yalijiri Kwa mara ya kwanza, ikiwa ni pamoja na msiba wa mmoja wa wagombea wa nafasi za juu kabisa za uongozi wa nchi.

Na hili likapelekea Kwa mara ya kwanza, katika historia ya nchi hii, uchaguzi mkuu kuahirishwa, jambo ambalo hatimaye Kwa mara ya kwanza, limeibua mjadala wa kweli kweli juu ya sheria ya Uchaguzi ya mwaka 1985 yenye kuruhusu uchaguzi kusogezwa ikiwa mmoja wa wagombea anaaga(?) dunia.

Mjadala huo ukawa mkubwa kwasababu Kwa mara ya kwanza, Watanzania waliweza kuelezwa waziwazi kuwa gharama za uchaguzi ni kiasi gani (bilioni 93?), hali ambayo inaonyesha wazi kuwa kuahirishwa kwake ni mzigo usiomithilika kwa Walalahoi, ingawa ni afadhali kwa baadhi ya Walalahai.

Lakini katika hali ya kushangaza sana (kwangu mimi), Watanzania tumeweza kushuhudia Kwa mara ya kwanza kuwa kumbe utawala wa sheria unawezekana kabisa kwasababu Kwa mara ya kwanza, Tume ya taifa ya Uchaguzi, iliweza kuahirisha uchaguzi huo kwasababu ya kufuata sheria, ingawa pia Kwa mara ya kwanza nilishuhudia mmoja wa wanasiasa wetu ambao wanasifika kwa kuwa ‘Wasanii” akiuweka usanii kando na kuwa muwazi.

Ndio; si mlimsikia (haikuwa mara ya kwanza lakini kumsikia ila kwa kauli yake), huyu jamaa wa (CHADEMA) Chama cha Demokrasia na Maendeleo (potelea mbali hata kama demokrasia hizo sio makini), akisema kuwa kuahirishwa kwa uchaguzi huo kulikuwa mzigo mkubwa sana na kuwa hata wao hawakushirikishwa maana huenda wangesikilizwa, uchaguzi usingeweza kuahirishwa Kwa mara ya kwanza ?

Achilia mbali michakato ile wanaiita ya MCHUJO au KURA ZA MAONI (nashangaa kwanini hazikuwa kura za maono), ambazo Kwa mara ya kwanza ziliweza kuanika waziwazi jinsi gani Watanzania wameanza kuonyesha kuwa huenda Kwa mara ya kwanza wakakubaliana na matumizi ya RUSHWA kama sehemu ya maisha yao ya kila siku.

Kulikuwa pia na tofauti kubwa sana baina ya wagombea wetu, kuanzia ngazi za chini hadi zile za juu kabisa, na ndio maana haikushangaza sana yule mwanamama ambaye ameweka rekodi ya kuwa mgombea wa nafasi ya Uraisi (sijui alijua ni U-Rahisi au vipi?) mwanamke Kwa mara ya kwanza akianza kupiga miayo ya njaa mapema sana huku wagombea wengine Kwa mara ya kwanza, wakiwa wanafanya kampeni kwa kupitia angani.

Ni bahati mbaya sana tu kuwa kuahirishwa huko Kwa mara ya kwanza kwa uchaguzi, kulitokea tu kwa upande wa Tanzania bara na hili likipelekea (sina hakika kama ni Kwa mara ya kwanza) chaguzi za pande hizi mbili kutofanyika pamoja toka Nchi hizi zilipoungana Kwa mara ya kwanza miaka mingi iliyopita.

Na wakati uchaguzi wa kule visiwani ukiwa unaendelea, kulikuwa na mambo mengi sana pia ambayo ingawa mengine hayakuwa yakitokea Kwa mara ya kwanza, lakini pia yapo ambayo yalikuwa yakitokea Kwa mara ya kwanza.

Hivi ni nani alijua kuwa Zanzibar inaweza kuwa sawa sawa na Iraq, kuwa inaweza kushehenezwa vikosi vya askari na mibunduki yao na bado uchaguzi ukawa salama, kama sio rais wetu anayemaliza muda wake, Bw. Benjamin Mkapa, kuzifananisha sehemu hizi mbili Kwa mara ya kwanza wakati alipokuwa akitetea hoja yake ya kulundika wanajeshi kule?

Hivi ni nani ambaye alikuwa anajua kuwa Vikosi vyetu vya kulinda usalama vina magari yenye kubeba maji yaloyochanganywa na upupu kama sio baada ya kuyaona kule visiwani Kwa mara ya kwanza ?.

Kimsingi nadhani kuwa haikuwa Mara ya kwanza kwa wana-CUF kulalamikia kuporwa kura (zao?), lakini hii ilikuwa Mara ya kwanza kwao kutuambia kuwa wataingia Barazani na kuapa lakini hawatatoa ushirikiano.

Lakini hawa jamaa ambao nashindwa kuwaunga au kuwavunja kabisa mkono kuna jambo moja ambalo kwa hakika wangelifanya ndio ingekuwa kwa Kwa mara ya kwanza kuwahi kufanywa hapa nchini, nalo ni kukataa mshiko (ita vyovyote unavyopenda weye lakini ndio hizo hizo).

Ndio, wanaweza kabisa kuwa mabubu ndani ya vikao vya Baraza la Wawakilishi ingawa wengi wao hali ya kuwa bubu ndio watakuwa wakiishiriki Kwa mara ya kwanza, lakini hili la kuifanya mifuko yao nayo iwe bubu Kwa mara ya kwanza, wakati ambapo wengi wao ndio wameingia Barazani Kwa mara ya kwanza ili wakaonje MATUNDA ya uongozi baada ya kuhangaika muda mrefu katika MATUNDU ya Ulalahoi?

Duh! Sijui kuwa hali hii itaendelea hadi lini lakini najua ipo siku tu Kwa mara ya kwanza hawa jamaa wataufyata na kuanza kufungua mdomo yao, na kama hamuamini subirini mtaona kama hivi karibuni hamtashuhudia mikutano na vikao vya muafaka vikianza kufanyika, ingawa haitokuwa Kwa mara ya kwanza kwa vikao hivyo kufanyika.

Yapo mengi sana ambayo hakika yalijiri Kwa mara ya kwanza na ambayo kimsingi siwezi kuyaorodhesha hapa yote, lakini isichukuliwe kuwa nimeishiwa sera, kwa maana kama ikijatokea hivyo basi kwangu mimi hii itakuwa Kwa mara ya kwanza.

Kaka yangu mmoja huwa anapenda kujiita JK (sio yule mgombea kuingia jumba jeupe la Magogoni) bali yule Mlalahoi wa Mtaa wa Majira Jumapili, ananikumbusha kuwa eti uchaguzi huu pia umetukumbusha umuhimu wa kuchagua majina ya kuwapa watoto wetu kama hilo la JK au lile la Anna, kwa maana majina haya kwa mara ya kwanza yameonekana kuwa dili, kwahiyo kwa hakika sijaishiwa kichwani.

Ila nadhani kuwa mtakuwa nayi Kwa mara ya kwanza mmepata kitu kipya kidogo leo na si ajabu hata wale ambao walikuwa wasomaji wasiokuwa na la kuchagia leo hii wakachangia kazi hii Kwa mara ya kwanza kwasababu naamini kuwa nao Kwa mara ya kwanza watakuwa wameshuhudia mengi ambayo waliweza kuyaona Kwa mara ya kwanza na haitokuwa jambo la ajabu ikiwa nao wataniushirikisha katika yale walioyaona Kwa mara ya kwanza

Na kwa hakika leo siwaagi Kwa mara ya kwanza, sababu najua hii pia itakuwa Kwa mara ya kwanza, mimi kutokuwa muungwana kwa wasomaji wangu hivyo watanisamehekwakuwa kosa hili nalifanya Kwa mara ya kwanza
**********

November 24, 2005 at 5:54 pm 6 comments

Mtanzania mwingine (sio mswahili) ajiunga kwenye Blogi

Kwa muda wa siku kadhaa sasa nimekuwa nikifuatilia zaidi masuala ya siasa, na hili likinifanya niwe mchoyo katika kuwakaribisha baadhi ya wadau wanaozidi kujisajili katika ulimwengu wa Blogi, lakini leo hii nimeona si vyema nikaendelea kukaa kimya baada ya kupata ujumbe toka kwa rafiki yangu mmoja wa karibu, ambaye pia amekuwa miongoni mwa wachangiaji wazuri sana wa mijadala yangu. Msome hapa Bw. Nyembo, japo kaingia na utamaduni ule ule wa kuleweshwa na lugha za wenzetu sijui anaamini kuwa kiswahili hakitoshi au vipi. karibu Bw. Nyembo.

November 14, 2005 at 5:47 pm 1 comment

Bongo Flava, Itikadi Finyu na Mitizamo haba….1

Kizazi kipya, maisha mapya na Umbumbu Mpya
=============================================

Niliwahi kuandika wakati fulani nikiuliza Muziki wa Kizazi Kipya unakua kwa vigezo gani? Ingawa sikupata majibu ya kutosheleza lakini nadhani kuwa somo liliwafikia wadau na nafurahi kuwa katika sehemu kadhaa mjadala umekuwa mzito kiasi sasa, na ndio maana nikaona nami niingie tena leo kwa machache.

Ukiwasikiliza wakati wanaimba, wanavyoshughulika jukwaani na hata wanavyouita muziki wenyewe, kwa hakika ni lazima ujiulize maswali kadhaa kichwani mwako, kuhusu hiki wenyewe wanakiita Bongo Flava, Muziki wa Kizazi Kipya, na vyovyote vile wanavyoweza kuuita.

Ukisikiliza mashairi wanayoimba, maneno yanavyowatoka, tambo wanazotoa wahojiwapo maredioni, aina ya mavazi wanayovaa, majina wanayojipa, tembea yao mitaani, ITIKADI zao, na utaratibu mzima wa maisha wanaoutumia, kwa hakika unazidi kujiuliza maswali kibao kuhusu hiki kizazi.

Hata hivyo, matatizo ya muziki huu hayakuanza leo hii, na wala hayajaanzishwa kwa kiasi kikubwa na vijana wa sasa wanaouendeleza kwa nguvu zao zote, bali waasisi wa muziki huo nchini, ingawa pia sina hakika kama wenyewe walidhamiria kuwa uje kuwa hivi.

Simaanishi kuwalaumu bali kwakuwa inabidi kuelezana ukweli basi sio mbaya tukaelezana ukweli huo kuwa waasisi wa muziki huu wanaouita Bongo Flava, hivi sasa hawakuwa wameweka misingi ya kuufanya uwe Muziki wa Ki-Bongo kwelikweli, na ndio maana tunaona matokeo yake hivi sasa.

Hivi Tanzania ina utamaduni wa Wine ulioanzishwa na nani hadi wawe ndio wanaziimba sana kwenye nyimbo zao? Utamaduni wa Mtanzania si ule wa Kangala, Kachaso, Kangala, Kibuku, Ulanzi, Mnazi, Chimputu, na nyinginezo nyingi zinazopatikana hata kule kwa akina- Nyegerawaitu? Watanzania utamaduni wa Wine wapi na wapi?

Wanaacha kuvaa hata Shanga, wenyewe wanakazania hizi wanaita Cheni, Mikufu sijui Vikuku vya dhahabu, almasi na hata shaba, hivi Mtanzania wa kweli, ambaye kwa mtazamo wao ndio Mbongo, ana utamaduni wa wapi na vitu hivi? Mtanzania wa kweli asiyejua kuvaa kaniki ambayo haina shida hata katika uvaaji wake anayeweza hata kufunga na katani ikiwa inapwaya, utamaduni wa suruali za mlegezo umeanzia wapi?

Tulijengwa katika mazingira kuwa muziki huu ni lazima uwe na masuala hayo na ndio maana hadi leo hii vijana wetu wakitoka na rekodi basi utakuta imerekodiwa kwenye vijihoteli vyetu uchwara ambavyo wanaona wamemaliza mchezo, vijihoteli ambavyo mmarekani mwenyewe ambaye wanataka anunue muziki wao anaviona kama vibanda vya …….

Wanaacha kurekodia kwenye vijumba vyao vya Msonge kule madongoporomoka, na kuutangaza utalii wetu, kisha wanakueleza kuwa nia yao ni kupasua anga kwa kuuza nakala kibao, kwa kitu cha kuiga? kwa maana huyo ulomuiga hawezi kukinunua kamwe sasa utamuuzia nani? Hatukuwa na misingi imara ya huu muziki wetu na ndio maana hadi sasa wanazidi kuibuka tu vijana wakihanikiza Itikadi zao za kusaka mishiko hata kwa kufyeka watu…Mtanzania huyo…ni kijana wa Kitanzania huyo

Yapo mapungufu mengi sana kuhusiana na huu muziki wetu lakini nadhani pia kuwa tunaweza kabisa kurekebisha hali hii, ikiwa mimi nawe tutaamua kulifanyia kazi kwa kuanza kukitaka hiki kizazi kubadilika…Tayari alishaanza Jeff Msangi, akizungumzia juu ya huu Muziki wa Kizazi Kipya na wakajitokeza watu kujadili na wakajadili zaidi na hadi sasa mjadala haujaisha nadhani. Hivi karibuni Ndesanjo naye ambaye nadhani hakuwa amekusudia alilazimika kuanzisha mjadala baada ya kupelekewa waraka fulani na balozi mmoja wa Kitanzania, lakini uzao wa hiki hiki Kizazi kipya…Mnasemaje Watanzania?

November 13, 2005 at 4:35 pm 19 comments

Suala la Zanzibar…TUZUNGUMZE tuache KUSEMA

Kuna KUSEMA na KUZUNGUMZA.
Mambo mengi YAMESEMWA, baada ya Bw. (mh.?) Aman Abeid Karume, kufanikiwa kutetea nafasi ya urais wa Visiwa vya Zanzibar, akimbwaga mpinzani wake mkuu, Bw. Seif Shariff Hamad, kufuatia uchaguzi wa hivi karibuni visiwani humo.
Sinashaka pia wenye hamu na shauku ya kufungua midomo yao kuiruhusu itoe chochote kuhusu uchaguzi huo, wangali wapo, lakini, wote hao watafanya hivyo kwa dhamira ya KUSEMA.
Hili ndilo lililonivuta kufungua mdomo, fikra na mawazo yangu, kuruhusu mtizamo wangu kuhusu uchaguzi huo utoke, ingawa niko tofauti na wenzangu ambao wameshanitangulia. Tofauti tuliyonayo ni kuwa walionitangulia wamekuwa WAKISEMA lakini mimi napenda KUZUNGUMZA.
Ndio, nataka KUZUNGUMZIA uchaguzi wa Visiwa hivyo ambavyo viliwahi kuvuma kwa a.k.a ya ‘Visiwa vya Marashi ya Karafuu’, ingawa hivi sasa vinaelekea kuwa ‘Visiwa vya Machafuko na Umwagikaji damu’
Kwa mujibu wa moja ya Kamusi za Kiswahili Fasaha (kati ya nyingi), nilizowahi kusoma, ‘KUZUNGUMZA‘ huchukuliwa kama mbadilishano wa mawazo, kutoa mawazo katika mkutano, kutoa hoja, kujadili na mengine ya uelekeo huo. Kifupi MAZUNGUMZO ni lazima yahusishe pande mbili ili yawe na sifa ya kuitwa MAZUNGUMZO.
KUSEMA‘, kwa upande wake ni kutamka, kusengenya kupaza sauti na mengine yenye uelekeo kama huo. Kifupi KUSEMA sio lazima kuwa na pande mbili, sio lazima watu wa kukusikiliza wawepo, sio lazima watu wa kujali unachosema wawepo, sio lazima wawepo watu wa kukujibu na mambo kama hayo.
Naam, nimerejea maneno hayo kutokana na mtizamo wangu juu ya Uchaguzi huo ulivyokuwa, toka zama za mchakato wa kuuelekea hadi kufanyika kwake, na mapokeo yake kwa Wazanzibar wenyewe, Watanzania na Dunia kwa ujumla.
Kabla sijaendelea zaidi, kwanza pengine nitapenda kuwa wazi (haijalishi kuwa watanichukia baadhi ya watu), kwa kusema kuwa “Katika zama hizi, kuzungumzia siasa za Visiwani humo, unahitajika kuwa na akili zisizotosheleza kichwani mwako, ama ziwe zimepungua au zimezidi sana.
Kwa wale wenzangu ambao wamekuwa wakifuatilia mwenendo wa siasa za Visiwani humo, ni wazi kabisa kuwa watakubaliana nami kuwa Zanzibar hakuna siasa zenye misingi ya halisi ya kisiasa, bali siasa za Uhasama, Chuki, Visasi na kwa hakika Uchu wa Madaraka, kwa baadhi ya wadau wa siasa hizo.
Hali hii imekuwa ikijionyesha wazi nyakati mbalimbali, iwe wakati wa mikutano ya kawaida ya wafuasi wa vyama mbalimbali vilivyopo visiwani humo, au nyakati za kampeni au uchaguzi kama ilivyo sasa. Siasa za Zanzibar ni ‘KUSEMA’ sana na sio KUZUNGUMZA, hali ambayo imeambukizwa hadi kwa waandishi wa habari na wachambuzi wa masuala mbalimbali kuhusiana na mwenendo wa siasa za eneo hilo.
Hivi ni nani anaweza kuniambia kuwa Bw. Karume au mpinzani wake waliwahi KUZUNGUMZA, iwe wakati wa kampeni zao au wakati wa mikutano yao mbalimbali wakati wa kuelekea uchaguzi huo, zaidi ya kuwa wote walikuwa mahodari wa KUSEMA?
Ni katika KUSEMA tu ambako hata hiki tunachokiita hali tete iliyoenea eneo hilo kimewezekana. Ni katika KUSEMA tu ambako chama fulani kinaweza kuwa na MATOKEO yake kinyume na yale ya tume. Ni katika kusema tu ambako mtu mmoja anaweza kutishia kulala barabarani na mwingine naye akasema ataenda kulala kwenye nyumba yake.
Ndio, ni katika KUSEMA tu ambako mtu anaweza kukurupuka na kusema hakuna serikali ya mseto wakati nguvu za madaraka kwa wanaowakilisha wananchi zimegawanywa karibu sawa. Ni katika KUSEMA tu ambako mtu anaweza kuja na tishio la kushusha Gharika ikiwa hatarejeshewa kura zake(?) alizoibiwa.
Naam, ni katika KUSEMA tu ambako hata Mmarekani, ana haki ya kuingilia madaraka ya Wazanzibar, ni katika KUSEMA tu ambako hata asilimia kubwa yetu waandishi tumejikuta tukiamini kuwa kulikuwa na wizi wa kura kule visiwani, na ni katika KUSEMA tu ambako demokrasia ya kweli haimaanishi lolote lile zaidi ya kushinda URAIS wa nchi. Hii ni hatari, tena hatari kubwa sana.
Wakati mchakato wa kupata serikali mpya kwa upande wa Tanzania nzima kwa ujumla na Visiwani kwa upande wao, nilibahatika kuwa mmoja wa waliokuwa wakifuatilia kwa ukaribu mkubwa sana mwenendo mzima wa mchakato huo, na hasa katika kile kipindi cha KUTUPIANA MADONGO, wenyewe walikuwa wanakiita kipindi cha KAMPENI (sijui hata walikuwa wakijua maana ya KAMPENI kweli kweli au walikuwa waki-SEMA tu.
Kwa wafuatiliaji wenzangu, ni wazi watakubaliana nami kuwa kilichokuwa kikijiri wakati wa zoezi hilo, kwa wenzetu wa huko Visiwani, hakikuwa kampeni ambazo wananchi walikuwa wakizihitaji (nazungumzia mwananchi makini, maana wasiokuwa makini pia wanakuwa hawafai, wameshapandikizwa mbegu za ku-SEMA), zaidi ya kupokezana mizigo ya lawama, vitisho na ubabe wakinamna ndani yake.
Tanzania ikiwa kama moja ya nchi ambazo zinakabiliwa na umasikini mkubwa, imekuwa ikijitahidi sana kuandaa sera karibu kila kukicha ili kuupiga teke huo umasikini, laini imekuwa ikishindikana sababu ya ubovu ama wa sera zenyewe au watekelezaji wa sera hizo, na hasa wale viongozi.
Ni vyema pia ikaeleweka kuwa sio hao CUF wala chama kingine chochote ambacho kingeweza kuingia madarakani na kisha kuweka mpaka wa mstari mwekundu pale serikali iliyopita ilipokuwa imeishia na kisha wao wakaanza na yao mapya kabisa. Ni wazi kabisa kuwa kuna mambo mengi ambayo wangeyakuta na wangelazimika kuyaendeleza, ikiwa ni pamoja na baadhi ya sera ambazo zimeshaandaliwa, sababu sio zote ni mbovu.
Ni katika mustakabali huu basi ambapo nilitarajia kampeni zingelilenga kufafanua mchakato wa kutekeleza sera fulani, utaanzaje hadi kumaliza namna gani na sio atatufanyia nini…ataanzisha huduma gani au kitu gani, ilhali hata hizo zilizopo wanashindwa kuzitekeleza. Haukuwa wakati wa ku-SEMA ilimradi mtu anajisikia ku-SEMA bali ulikuwa wakati wa KUZUNGUMZA.
Ulikuwa wakati wa wagombea kuwasikiliza wananchi wanasemaje, na kushauriwa pale ambapo wagombea wakiwa kama viongozi, wangeona kuna mapungufu katika hoja au matakwa ya wananchi. Ulikuwa wakati wa KUZUNGUMZA na wala sio KUSEMA
Lakini hali haikuwa hivyo tu safari hii kwani baada ya jamaa zetu kuona kuwa wamedanganya vya kutosha miaka iliyopita na wakashindwa, wakaona kuwa safari hii uongo hautawasaidia na badala yake kuongeza juhudi katika kupandikiza mbegu za chuki, uhasama na uonevu dhidi ya watu fulani. Badala yake wakaelekeza juhudi zao katika kujidai “Maripota wa Udaku”. kucha kutwa wakifuatiliana siri zao za ndani ili kila mmoja aje mmbomoa mwenzake akipata wasaa wa kupanda jukwaani.
Na wakati haya yakiendelea, kimsingi yakiendelea kushika kasi na kila mmoja akijua kuwa yanatupeleka pabaya, na wananchi wakijua kabisa kuwa sio mambo wanayoyahitaji, bado wengi wetu tuliendelea KUSEMA badala ya KUZUNGUMZA. Hatukuweza kuona haja ya kuwakutanisha hawa watu na kuwabana kwanini wanazidi kutupeleka pabaya kwa tambo na kauli zao, hatukuwahi kuwakalisha na kuwaonya, hatukuwahi hata kuwanyooshea kidole, na badala yake, nasi kwa upande wetu kila mmoja alikuwa AKISEMA lile aonalo kuwa linamridhisha.
Hebu tugusie mchakato wa Uchaguzi huo na Uchaguzi wenyewe na baadhi ya Vijimambo vilivyojiri baada ya uchaguzi wenyewe..
Kuna suala la malalamiko dhidi ya Tume ya Uchaguzi ya Visiwa vya Zanzibar,(ZEC), malalamiko ambayo yanatolewa zaidi na waliokuwa wagombea kutoka chama cha CUF pamoja na wanachama na washabiki wao. Hivi ni lini Seif Shariff Hamad aliikatia rufaa ya kisheria Tume ya Uchaguzi huko Visiwani, lakini pingamizi lake likatupwa?
Hivi ni nani aliiambia serikali kuwa Wazanzibar hawataenda kupiga kura siku hiyo ila kufanya fujo kwahiyo wawapelekee misururu ya Polisi na magari yaliyojaa maji yenye Upupu sijui wa kutoka wapi, wakati magari ya namna hiyo yamekuwa hayaonekani wakati wananchi wanapounguliwa na nyumba zao ili yasaidie kuzima moto?
Hivi ni nani aliyewapa mamlaka mawakala (naambiwa eti walikula viapo, bilashaka kwa ku-SEMA tu viapo hivyo midomoni mwao na sio KUZUNGUMZA na nafsi zao), kuwa na nyaraka zao za matokeo wakati hizo ni nyaraka za tume? na zaidi ya yote madaraka ya kuwa Watangaza matokeo?
Hivi ni nani amemwambia Karume kuwa akiunda serikali ya mseto kule Visiwani atakuwa ametenda dhambi ya kuhukumiwa kwenda Jehanam siku ya kiama, ni nani aliyemwambia kuwa Viongozi wazuri ni lazima watoke chama cha CCM, mbona sehemu zingine waliangushwa kama kweli kila mwana-CCM ni mtu safi?
Kwa hakika hakuna. Hakuna aliepinga tume, hakuna aliyesema serikali ya mseto visiwani ni sawa na Nguruwe kupelekwa ndani ya Msikiti, hakuna aliyekuwa na ushahidi kuwa Wazanzibar walikuwa wamejiandaa kufanya fujo na wala hakuna ambaye ana uhakika na hicho wanachodai kuwa ni matokeo yao sababu hakuna ambaye anaweza kushuhudia mbele ya Mungu wake kuwa anajua kilichoko ndani ya nafsi ya Karume au ndani ya Seif ni kitu fulani na ni cha ukweli kabisa.
Lakini kwa bahati mbaya zaidi, au kibaya zaidi ni kuwa hakuna ambaye amethubutu KUZUNGUMZA kuhusu hali hii na badala yake kila mmoja anakazana KUSEMA. Inanishangaza hata baadhi ya vyombo vya habari na baadhi ya waandishi pia tumo katika mkumbo huu.
Hivi kuna mmoja kati yetu aliwahi kuingia ndani ya moyo wa mfuasi aliyebahatika kuongea naye akajua kuwa alichoelezwa ni kweli tupu? Kwasababu Siasa kwa misingi hasa ya Siasa na hasa Siasa zenyewe zinapokuwa zinahusisha Wanasiasa wa hapa Tanzania na hususan Visiwani, zimejengwa katika misingi ya Uongo, Unafiki, Uzandiki, Ufisadi, Majungu, Tamaa na Uchu wa Madaraka.
Ni rahisi sana kwa mtu aliyekulia katika ‘madhehebu’ ya namna hiyo kutokuwa mkweli daima dumu, kutokuwa mkweli kwa maisha yake yote, na haya sio ya kuyajadili kwa maana wapo watu wa namna hii. Wapo wanasiasa ambao wamezikana hata nafsi zao kwa ajili tu ya madaraka, wapo wale ambao wamediriki kudanganya nafsi zao wenyewe ilimradi kupata kitu fulani. Ndio, wapo watu wa aina hii, sasa kwanini basi tuamini kuwa wanachoki-SEMA wao ni ukweli?
Kwangu mimi bado naona kuwa suala la Zanzibar, sio la Wamarekani, sio la waandishi, sio la tume ya uchaguzi visiwani humo, sio la waangalizi wa uchaguzi, sio la polisi na wala sio suala la kila mtu kujitahidi kujiaminisha kuwa ndio lilivyo. Suala la Zanzibar ni suala la KUZUNGUMZA badala ya KUSEMA.
Nasema la KUZUNGUMZA kwasababu ninaamini kabisa kuwa wadau wa siasa za visiwani humo ni watu wenye nguvu sana. na hili linanipa matumaini kuwa wote ni watu walioiva katika siasa (bila kujali ni za aina gani maana ndio walizojichagulia). Hii ikimaanisha kuwa ni watu ambao wanaweza kukaa meza moja na kujadili masuala hayo na yakaenda sawasawa kabisa na kuzimwa kwa hizi chokochoko zilizopo hivi sasa.
Kwa nguvu walizonazo wana-CUF, wanaweza kabisa kuwashinikiza viongozi wao kukaa na wale wapinzani wao na kujadili hatma yao ikiwa kweli wanataka Maendeleo, na ikiwa kweli walidhamiria kufanya uchaguzi ili kupata viongozi watakaoleta changamoto mpya katika kuharakisha maendeleo.
Kwa nguvu walizonazo wana-CCM visiwani humo, ninaamini kabisa kuwa wanaweza kumshinikiza Karume na akakaa meza moja na Maalim Seif kujadili hatma yao ikiwa kweli bado wana ndoto zao za kuigeuza Zanzibar kuwa Rome, kama kweli bado wana ndoto za kumfanya kila Mzanzibar kusahau kitu Umasikini. Ndio, haya yanawezekana, ikiwa tu kila upande utaacha Unafiki na Uongo.
Binafsi bado naamini kabisa kuwa Bw. Karume anaweza kabisa kukutana na mwenzake Seif, wakakaa na wakajadili juu ya mustakabali wa visiwa hivyo. Kwa maana ya KUZUNGUMZA na sio KUSEMA.
Akisimama huyu jukwaani anasema…’eee, ndio lazima serikali ya mseto…..” Serikali ya mseto jukwaani?…akisimama huyu naye sababu anaona aibu kuambiwa kaogopa, anaanza……’andikeni mmeumia serikali ya mseto’. Kaumia yeye au mmeumia Wazanzibar wote ambao mtaishia kulumbana badala ya kujiletea maendeleo?
Kwa hulka ya wanasiasa, huwa sio watu wa kufikia muafaka katika majukwaa hata siku moja, maana Majukwaa yetu hayatumiki kwa ajili ya Siasa bali Kuonyeshana uhodari wa Kupondana na kutangaziana ubabe. Ila pale wanapokaa pamoja na kuweza KUZUNGUMZA, na hili naamini kabisa linawezekana Zanzibar. Kwanini ishindikane?
Haiwezi kushindikana kabisa sababu kama kila mmoja akiwa na lengo la kujenga basi hatimaye tutajenga ila tu kwa kukaa pamoja na TUKAZUNGUMZA haya mambo jinsi yalivyo kwa maana YANAZUNGUMZIKA.
Huu ushabiki wa kuwa fulani kaniibia kura…fulani alidhamiria kuniletea fujo…huu ni ufinyu wa mawazo ambao hautuelekezi sehemu ya kuhakikisha kuwa siasa za visiwani humo zinakuwa za kuweka mazingira ya kupata serikali zenye kuingizwa madarakani kidemokrasia na zikiwa na changamoto za kuwakomboa wananchi.
Poleni sana mlioshindwa, sababu mmeshindwa kufikia ndoto zenu za kuingia IKULU (na sio kutawala maana mmevuna viti vya kutosha lakini hamtaki kujivunia kuwa hayo ni mafanikio makubwa)
Poleni mlioshinda, kwa maana nyie mna kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa mbegu zenu za chuki mlizopandikiza na ambazo zimesha mea, mnazinyunyiza dawa haraka ili zife kusudi muweze kuendeleza gurudumu la maendeoe ya Visiwani kwenu.
Poleni nyote ambao mtakuwa mmekerwa na maandiko haya kwa maana huu ni mtizamo wangu hata mkisema vipi siwezi kuubadilisha. Ila tu ninawafariji kuwa kwangu mimi. kila kitu KINAZUNGUMZIKA na atakayetaka tuzungumze tutazungumza..ila atakayetaka KUSEMA basi nitamwacha aendelee KUSEMA kwa maana Mdomo ni mali yake.

November 7, 2005 at 1:36 pm 8 comments

…na sasa ni siku ya Wayahudi, ya waafrika wenye njaa ni lini?

Wakati fulani fulani huwa navunja utamaduni wetu sisi Watanzania, ule utamaduni ambao umekuwa ukihanikizwa sana na watu kuwa Watanzania hatupendi Kusoma (kujisomea?) na katika moja ya nyakati ambazo nilipokuwa natekeleza kuvunja utamaduni huu, nilipokuwa napitia taarifa ya Umoja wa Mataifa nilivutiwa sana na taarifa moja aliyoitoa Katibu Mkuu wa Umoja huo, Bw. Koffi Annan, kuhusiana na Bara la Afrika.

Katika chapishi lake moja ambalo aliwahi kulitoa, katibu huyo alisema kuwa AFRIKA HAIWEZI KUWA HURU AU KUENDELEA IKIWA NA NJAA. Lakini cha ajabu hawa jamaa hawakuamua hata kuweka siku ya kutokomeza hiyo njaa inayolikabili Bara la Afrika, na badala yake nikakutana tena na chapisho jingine la Umoja huo eti Umoja huo umeamua kuwa Januari 27 ya kila mwaka, sasa itakuwa Siku ya Wayahudi, kuwakumbuka maelfu ya Wayahudi walioteketezwa enzi hizo za utawala wa jamaa mmoja ambaye alidhani kuwa Dunia yote inaweza kuwa mikononi mwake.

Je Waafrika tulio na njaa na bara letu, tuna umuhimu wa kuwa na siku kama hii kweli?

November 2, 2005 at 6:31 pm 4 comments

Unaijua TUKALEWAPI.Com….?

Ndio…mnataka tukale wapi sasa kama sio kuchakura chakura humo katikati? haijalishi ni kati kati ya Mistari ya uchafu, ukarimu, umaarufu, unyama, uonevu au nini lakini ni katikati ya Mistari na huko ndio tunakotaka tukachakurechakure….Karibuni sana Tukalewapi.Com

November 2, 2005 at 8:52 am Leave a comment


Blog Stats

  • 34,786 hits
November 2005
M T W T F S S
 123456
78910111213
14151617181920
21222324252627
282930