Archive for October 28, 2005

Ama hakika huku nini Kufa Kufaana

KWA hakika ni mtikisiko, sio tu katika medani ya siasa nchini Tanzania, bali pia kwa Watanzania kwa ujumla. Nazungumzia kifo cha mwanasiasa mkongwe, hayati Jumbe Rajab, aliyekuwa mgombea mwenza wa kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).Mgombea kiongozi ni Bw. Freeman Mbowe aka Mzee wa Helikopta
jumbe Hayati Rajab Jumbe (kushoto) na Bwana Freeman Mbowe

Msiba huu ambao ulitokea Oktoba 26, umesababisha uchaguzi mkuu wa Tanzania ambao ulikuwa ufanyike Oktoba 30
kusogezwa mbele hadi Disemba 18 ya mwaka huu huu (zaidi ya siku 50 mbele). Hatua hii imewezekana kutokana na sheria zilizopo nchini hasa ile ya kwanza ya uchaguzi ya mwaka 1985.
Kwa wana-SIHASA wetu, ambao kimsingi karibu siku zote wao ni WALALA-HAI, najua tukio hili la kusikitisha sana limedhihirisha kwa vitendo ule usemi wa wahenga “Kufa Kufaana” sababu kusogezwa kwa muda kunamaanisha wao kuongezewa tena muda wa kuendelea kutudanganya kupitia MIVUTANO (mikutano?) yao ya kampeni.
Lakini hata kwa upande huu pia sio kuwa ni kwa wana-SIHASA wote ambao watakuwa wamefurahia msiba huo kimoyomoyo, (kama huamini kuwa wapo wanaochekelea msiba huo, weka kumbukumbu zako siku nawe ukifa ukaombe kuona nyoyo zao zilivyokuwa siku hiyo ya msiba), maana wapo ambao tayari walikuwa Choka Mbaya kifedha.
kifo cha jumbe Bw. Freeman Mbowe wa CHADEMA na Bw. Jakaya Kikwete wa CCM, walipokutana msibani
Yaani wapo wale ambao kama ni kuupepeta uongo walishamaliza mbinu zao zoooote hadi zile za ucvunguni na walikuwa wakitarajia kuwa kwavile bado uongo wao ungalikuwa bado wa moto moto vichwani mwa Wadanganyika, basi huenda wangeambulia chochote kitu, lakini hadi Disemba 18…? Utakuwa umeshayeyushwa na Takrima nono nono za wapinzani wao.
Lakini hali ni mbaya zaidi kwa wenye NJI hii wenyewe, (ndio si wako zaidi ya asilimia 90 bwana?) na hapa namaanisha WALALA-HOI, ambao kwa mara nyingine tena watajikuta wakibeba mzigo wa Jeneza la Gharama za UCHAGUZI mwingine baada ya huu wa sasa kufanyiwa UCHAFUZI, na baadhi ya watu ambao vichwa vyao ni vizito wakati wa kutafsiri na kutekeleza sheria.
Hivi kweli Watanzania walikuwa tayari kusubiri hadi Disemba 18 kwasababu ya kifo cha mgombea mmoja? Hivi ni Watanzania wangapi ambao wangeenda kupiga kura siku hiyo wakiwa wametoka kulala na maiti za ndugu zao, ilimradi tu wamesisitiziwa kuwa kura zao zina thamani sana. Kwa mara nyingine tena yanakuja yale yale masimulizi ya kina hayati fulani, marehemu fulani na vibudu au mizoga fulani.
Hivi karibuni, hayati fulani alipofariki alisafirishwa kwa ndege tena ya SIRIKALI wakati siku hiyoi hiyo kuna mamia kama sio maelfu ya Wadanganyika walipiga teke ndoo lakini wakaambulia kusafirishwa kwenye vipanya vya kukodi tena vingine vikilazimika kusimama barabarani kwa zaidi ya masaa kadhaa eti kikikaguliwa breki na askari wa usalama barabarani.
Buriani Jumbe, buriani mzee wetu najua ipoo siku tutakutana huko lakini nitangulizie salamu zangu kwa hayati baba wa taifa Mwl. Nyerere, mwabie mjukuu wake bado nina kazi kweli kweli. Bado naendelea kupigika kwa tusiku kadhaa hadi tena Disemba 18, huenda nami ndio nikapiga.
Kweli Binadamu wote ni SAWA lakini sio SAWASAWA

October 28, 2005 at 1:32 pm 4 comments


Blog Stats

  • 34,787 hits
October 2005
M T W T F S S
 12
3456789
10111213141516
17181920212223
24252627282930
31