Archive for October 26, 2005

Siku ya Wambeya Duniani

Kaka yangu mmoja wanamuita Chesi Mpilipili, katika moja ya kazi zake za hivi karibuni alizozifanya wakati wa maadhimisho ya SIKU YAKE, ambayo kwa kawaida huadhimiswa kila Jumapili kwenye ukumbi wa Majira, aliniacha hoi alipoelezea kushangazwa kwake na huu utitiri wa SIKU, hamaanishi kuwa zimeongezeka katika kuunda wiki, mwezi au mwaka, bali anamaanisha hizi SIKU za kuadhimisha matukio fulani fulani.

Anasema yeye enzi zake wakati anakua kulikuwa na SIKU chache sana, anasema mbili tatu hivi, zikizidi sana ni tano na ambazo zilikuwa zikihanikizwa kwenye vyombo vya habari kiasi kwamba haikuwa taabu hata kujulikana kwake. Enzi hizo, anasema kuwa ilikuwa jambo la kawaida sana kusikia vyombo vya habari vikihanikiza “Wiki ijayo kutakuwa na maadhimisho ya SIKU Fulani na mwezi ujao ni maadhimisho ya SIKU Fulani. Na anasema zilikuwa chache sana kiasi kwamba si ajabu ilikuwa rahisi sana kwa mtu kuweza kuweka kwenye kumbukumbu za ubongo wake kuwa mwaka una SIKU ngapi.

Lakini sasa…. imekuwa nongwa, sio tu kuwa vyombo vya habari vimeamua kuzichunia hizo SIKU, bali pia nazo zimekuwa nyingi mno kiasi kwamba inakuwa vigumu sana hata kuweza kuzijua na zingine anahisi zinabuniwa tu na baadhi ya watu wakilala na wake zao majumbani mwao wakishauriana kuwa kesho iwe SIKU YA KULA PIZZA, basi itakuwa na kesho yake mtu ukiamka utasikia (kupitia mabalozi wao, wakiongea na waandishi wa habari pale jijini Dar), kuwa Leo ni maadhimisho ya SIKU ya ula Pizza Ulimwenguni, na hata Wabongo wataadhimisha siku hiyo ingawa wanazisoma kwenye matangazo au kuziona kwenye picha za kihindi.

Ndio, kwani hujui kuwa kuna SIKU za Kutoana Ngeu, Siku za Wanaovaa Magauni, Siku za Walalahoi (?) Siku za Watembea peku, Siku za Kadhaa na Kadhaa. na kwa Ushauri wa kakangu Chesi mwenye nywele za Kipilipili, anaona ni aheri basi Wadanganyika nao wakapendelewa na hao Watunga siku wakapewa vijisiku kadhaa hizi kama SIKU ya Hafla za Jikoni (Kitchen Party?), Siku ya Kufumuana Magumi (Boxing Day?), Siku ya Unyago, Siku ya Kusasambua, Siku za Miduara, Siku ya Ndoa za Mkeka, Siku ya Kufukuzana (Sendoff?), Siku ya Waezekaji (Wawekezaji?), Siku ya nanihii…..na Siku ya nahinii pia.

Na hizo bado ni chache sana kwa maana hujagusa Siku ya Wanaodaiwa na ile ya Wadai, hujazungumzia kabisa Siku ya Mvua na ile ya Kiangazi, na wala hujazungumzia Siku ya Wambeya kule Uswahilini na ile ya Wastaarabu kule Uzunguni na zingine nyingi ambazo hata wewe unazijua.

Hakika bilashaka naamini kwa Utitiri huu wa SIKU, utafika wakati tutakuwa na SIKU ya Ndesanjo, SIKU ya Reginald na hata SIKU YA SIKU ZOTE au SIKU YA KILA SIKU…..

Alamsiki ngoja nami niwahi nyumbani maana leo ni SIKU YANGU !!

October 26, 2005 at 4:07 pm 6 comments


Blog Stats

  • 34,787 hits
October 2005
M T W T F S S
 12
3456789
10111213141516
17181920212223
24252627282930
31