Archive for October 13, 2005

Mashujaa daima Hawafi – 2Pac Shakur

Rafiki yangu mmoja kwa jina la Akiey & kaka yangu Ndesanjo, bilashaka ni wanazi wakubwa sana wa msanii huyu, na kwa upande wa Akiey, hakika ilinishangaza kiasi kuona kuwa hakuwa na lolote alilozungumzia juu ya shujaa huyu kama kumbukumbu ya siku alipofariki na hata siku alipozikwa. hata hivyo naamini kabisa kuwa ni msongamano wa majukumu bilashaka ndio maana ikawa hivi.
Namzungumzia mwanamuziki aliyekuwa kioo cha muziki wa Hip Hop bilashaka, na ambaye kwangu mimi naamini kabisa kuwa maendeleo ya muziki huo kwa wakati huu yalitokana na kiasi kikubwa sana na mchango wake katika muziki huo. Na hapa namzungumzia hayati Tupac Amaru Shakur .
2pack 1
Ikiwa ni takriban miaka tisa sasa toka alipotutoka katika tukio lililokuwa na utata wa hali ya juu lililobatizwa jina la Mkasa wa Las Vegas, bado kumekuwa na mjadala ambao licha ya kuwa umekuwa ukizidi kufifia siku hadi siku, bado kuna baadhi ya nyakati huibuka na kuibua mgongano mkubwa wa mawazo hasa kwa mashabiki wake, na huu ni mjadala wa kuwa; Je, 2Pac alikufa kweli au bado yu hai?
Licha ya mapungufu ya kawaida kabisa ya kibinaadamu ambayo hata mimi na wewe tunayo, msanii huyu ambaye alikuwa amejijengea kundi kubwa la maadui, pengine na bila shaka hasa kutokana na mafanikio yake, bado alikuwa ni mtu mwenye upendo, na msanii ambaye alikuwa kweli kioo kwa wasanii waliokuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha masuala ya ubaguzi wa rangi yanatokomezwa.
Hayati 2Pac, ambaye alizaliwa June 16, 1971 ikiwa ni mwezi mmoja tu na siku kadhaa toka mama yake Afeni Shakur, atoke gerezani, alifariki dunia mwaka 1996, kutokana na tukio la kusikitisha kabisa la kupigwa risasi kadhaa na watu waliokuwa wanasadikiwa kuwa maadui zake. Tukio hilo lilikuwa la pili kumkumba baada ya kukumbwa na mkasa wa awali wa kupigwa risasi katika jiji la New York.
Katika enzi za uhai wake, hayati 2Pac, ambaye alikuwa rafiki kipenzi wa msanii mwingine wa muziki na mwigizaji mashuhuri duniani hivi sasa, Jada Pinkett, aliwahi kutamba na tungo mbalimbali zilizokuwa zikigusa kwa undani hisia na fikra za waafrika walio wengi hususan wale walioko katika harakati za kujikomboa na Ubaguzi wa Rangi.
Na hata alipofariki dunia kutokana na mkasa huo, gwiji huyo wa musiki wa kufoka foka, aliacha nyimbo nyingi sana ambazo hatimaye zilianza kurushwa moja baada ya nyingine kiasi kwamba zikawa ndio zinachochea mjadala wa kuwa amekufa kweli au laa. Pia alikuwa ni mtu wa kutoa maneno yenye maana kali kali sana kihisia na karibu kila neno alilokuwa akilitamka lilikuwa likimgusa kila mpenda haki humu duniani. Soma hapa baadhi ya mistari ambayo hadi leo imeendelea kuwagusa wapigania haki za binadamu duniani
Alifariki Septemba 6, baada ya kukaa kwa muda hospitali akiuguzwa majeraha ya risasi alizokuwa amepigwa, na alizikwa baadae Septemba 13 mwaka huo huo wa 1996, baada ya mabishano makali baina ya waliokuwa wakimpenda, wengi wakiamini hajafa wengi pia wakiamini amekufa. na Leo hii wakati ikiwa ni miaka tisa na mwezi mmoja toka aliporejea kwa Udongo, bado tunamkumbuka na kumhitaji sana.
Lakini kwakuwa hatuwezi kuwa naye kimwili, bado tutaendelea na hakika Daima, tutaendelea kuwa naye katika maisha yetu ya kuusaka uhuru wa kweli kwa Waafrika popote pale walipo Ulimwenguni. Hakika tulikupenda, Lakini Mungu alikupenda zaidi.

October 13, 2005 at 5:19 pm 3 comments

Mkapa; Hivi huku sio kujitega wenyewe?


Niko hapa kwenye kompyuta yangu, nikiwa nasikiliza muziki mmojawapo kati ya hii mingi tuliyonayo hapa nchini inayoitwa ya kizazi kipya. Hapa nasikiliza wimbo wa ‘SIWAELEWI’ ulioimbwa na marehemu Vivian Tillya (Mungu amlaze mahali pema peponi) enzi za uhai wake.

Nawakumbuka pia hawa jamaa zetu ‘Wanasi-hasa’, ambao baadhi yao mishipa yao ya shingoni inakaribia kupasuka, kila mmoja akijitahidi kuhanikiza uongo na uwezo wake alionao (hivi sasa lakini) wa kuweza kuondoa matatizo ya “Wadanganyika” katika muda mfupi sana tu, kila mmoja kwa staili ya aina yake.

Wengine wana ile staili ya majiko ya kizamani ya mafiga matatu; “Ari mpya, Nguvu mpya na Kasi mpya,” japo sijui ni ya kuelekea wapi maana kukimbia sio lazima iwe kwenda mbele tu.
Wapi pia wanaotumia staili ambazo hazitofautiani sana na zile za ‘Vidume’ vyetu vya pale TMK; “Hakuna kulala Mpaka kieleweke” nadhani kweli hawawezi kulala maana walilala miaka yote mitano iliyopita unadhani watashindwa kukesha siku 70 za kuhanikiza usanii wao majukwaani?

Lakini wakati jamaa hao wakiendelea huko, kwa upande mwingine kaka yetu Ben, ambaye amejijengea umaarufu wa aina yake duniani kwa sera zake za kutaka “Kuupiga teke Ukapa uliokithiri miongoni mwa Wadanganyika” yeye anaendelea na yake huku. Anaendelea kusaka wadau wa kuhakikisha sera yake hiyo inatekelezeka kwa “Uwazi na Ukweli” na hivi karibuni eti aliteketeza milioni 100 hivi za Kibongo kumnunulia Papa Benedicto wa 16, vinyago kadhaa vya kutokea ukanda wa Lupaso na kumpelekea kule kwenye maskani yake Vatican.
Wapo wapinzani wake ambao wameshaanza kuchonga kuhusu hili lakini hawa bilashaka hawajui kuwa huu ni aina ya ukarimu ambao unatumika kwa ajili ya kumvutia Papa ili naye siku moja afikirie kuja “Kuezeka”… naambiwa ni “Kuwekeza” kumbe…hapa hapa Bongo (potelea mbali hata kama uwekezaji wenyewe utakuwa wa kiroho tu), ili “Wadanganyik”a wapate nafasi ya kujiajiri.
Wakati hayo yakiendelea, nakumbuka pia kuwa kuna hawa jamaa zetu wapatao 600, ambao kimsingi wanawakilisha wenzao karibu au zaidi kidogo ya milioni 2 kote nchini, ambao kwa bahati mbaya sana walipitiwa na hili Pepo linaloitwa Ukimwi, ambao wamesema kuwa Nnjuluku, mshiko au Ngawira” zao zilizotolewa na “Sirikali” zisipowafikia hadi mwishoni mwa Novemba ya mwaka huu, watatuonyesha kwa kiasi gani walivyo wakarimu kwa kuanza kutugawia bure bure virusi vyao licha ya uchoyo wetu kwa fedha zetu.
Unashangaa? Ndio hali ilivyo hivyo. Kaka Ben anateketeza milioni 100 kutafuta wawekezaji ambao watakuja kufanya kazi kwa nchi ambayo wananchi wake wamegawiana virusi bila hiayana tena kwa kasi mpya, nguvu mpya na ari mpya. Tena basi hawa jamaa wamepania kuonyesha ukarimu wao kwa utaratibu wa Hakuna Kulala hadi Kieleweke. Je huku sio ndio KUJITEGEA mabomu sisi wenyewe lakini?
oohhh Dada yangu Vivian, kaka yako huku baaado SIWAELEWI Wadanganyika

October 13, 2005 at 2:34 pm 7 comments


Blog Stats

  • 35,058 hits
October 2005
M T W T F S S
 12
3456789
10111213141516
17181920212223
24252627282930
31