Archive for October, 2005

Ama hakika huku nini Kufa Kufaana

KWA hakika ni mtikisiko, sio tu katika medani ya siasa nchini Tanzania, bali pia kwa Watanzania kwa ujumla. Nazungumzia kifo cha mwanasiasa mkongwe, hayati Jumbe Rajab, aliyekuwa mgombea mwenza wa kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).Mgombea kiongozi ni Bw. Freeman Mbowe aka Mzee wa Helikopta
jumbe Hayati Rajab Jumbe (kushoto) na Bwana Freeman Mbowe

Msiba huu ambao ulitokea Oktoba 26, umesababisha uchaguzi mkuu wa Tanzania ambao ulikuwa ufanyike Oktoba 30
kusogezwa mbele hadi Disemba 18 ya mwaka huu huu (zaidi ya siku 50 mbele). Hatua hii imewezekana kutokana na sheria zilizopo nchini hasa ile ya kwanza ya uchaguzi ya mwaka 1985.
Kwa wana-SIHASA wetu, ambao kimsingi karibu siku zote wao ni WALALA-HAI, najua tukio hili la kusikitisha sana limedhihirisha kwa vitendo ule usemi wa wahenga “Kufa Kufaana” sababu kusogezwa kwa muda kunamaanisha wao kuongezewa tena muda wa kuendelea kutudanganya kupitia MIVUTANO (mikutano?) yao ya kampeni.
Lakini hata kwa upande huu pia sio kuwa ni kwa wana-SIHASA wote ambao watakuwa wamefurahia msiba huo kimoyomoyo, (kama huamini kuwa wapo wanaochekelea msiba huo, weka kumbukumbu zako siku nawe ukifa ukaombe kuona nyoyo zao zilivyokuwa siku hiyo ya msiba), maana wapo ambao tayari walikuwa Choka Mbaya kifedha.
kifo cha jumbe Bw. Freeman Mbowe wa CHADEMA na Bw. Jakaya Kikwete wa CCM, walipokutana msibani
Yaani wapo wale ambao kama ni kuupepeta uongo walishamaliza mbinu zao zoooote hadi zile za ucvunguni na walikuwa wakitarajia kuwa kwavile bado uongo wao ungalikuwa bado wa moto moto vichwani mwa Wadanganyika, basi huenda wangeambulia chochote kitu, lakini hadi Disemba 18…? Utakuwa umeshayeyushwa na Takrima nono nono za wapinzani wao.
Lakini hali ni mbaya zaidi kwa wenye NJI hii wenyewe, (ndio si wako zaidi ya asilimia 90 bwana?) na hapa namaanisha WALALA-HOI, ambao kwa mara nyingine tena watajikuta wakibeba mzigo wa Jeneza la Gharama za UCHAGUZI mwingine baada ya huu wa sasa kufanyiwa UCHAFUZI, na baadhi ya watu ambao vichwa vyao ni vizito wakati wa kutafsiri na kutekeleza sheria.
Hivi kweli Watanzania walikuwa tayari kusubiri hadi Disemba 18 kwasababu ya kifo cha mgombea mmoja? Hivi ni Watanzania wangapi ambao wangeenda kupiga kura siku hiyo wakiwa wametoka kulala na maiti za ndugu zao, ilimradi tu wamesisitiziwa kuwa kura zao zina thamani sana. Kwa mara nyingine tena yanakuja yale yale masimulizi ya kina hayati fulani, marehemu fulani na vibudu au mizoga fulani.
Hivi karibuni, hayati fulani alipofariki alisafirishwa kwa ndege tena ya SIRIKALI wakati siku hiyoi hiyo kuna mamia kama sio maelfu ya Wadanganyika walipiga teke ndoo lakini wakaambulia kusafirishwa kwenye vipanya vya kukodi tena vingine vikilazimika kusimama barabarani kwa zaidi ya masaa kadhaa eti kikikaguliwa breki na askari wa usalama barabarani.
Buriani Jumbe, buriani mzee wetu najua ipoo siku tutakutana huko lakini nitangulizie salamu zangu kwa hayati baba wa taifa Mwl. Nyerere, mwabie mjukuu wake bado nina kazi kweli kweli. Bado naendelea kupigika kwa tusiku kadhaa hadi tena Disemba 18, huenda nami ndio nikapiga.
Kweli Binadamu wote ni SAWA lakini sio SAWASAWA

October 28, 2005 at 1:32 pm 4 comments

Siku ya Wambeya Duniani

Kaka yangu mmoja wanamuita Chesi Mpilipili, katika moja ya kazi zake za hivi karibuni alizozifanya wakati wa maadhimisho ya SIKU YAKE, ambayo kwa kawaida huadhimiswa kila Jumapili kwenye ukumbi wa Majira, aliniacha hoi alipoelezea kushangazwa kwake na huu utitiri wa SIKU, hamaanishi kuwa zimeongezeka katika kuunda wiki, mwezi au mwaka, bali anamaanisha hizi SIKU za kuadhimisha matukio fulani fulani.

Anasema yeye enzi zake wakati anakua kulikuwa na SIKU chache sana, anasema mbili tatu hivi, zikizidi sana ni tano na ambazo zilikuwa zikihanikizwa kwenye vyombo vya habari kiasi kwamba haikuwa taabu hata kujulikana kwake. Enzi hizo, anasema kuwa ilikuwa jambo la kawaida sana kusikia vyombo vya habari vikihanikiza “Wiki ijayo kutakuwa na maadhimisho ya SIKU Fulani na mwezi ujao ni maadhimisho ya SIKU Fulani. Na anasema zilikuwa chache sana kiasi kwamba si ajabu ilikuwa rahisi sana kwa mtu kuweza kuweka kwenye kumbukumbu za ubongo wake kuwa mwaka una SIKU ngapi.

Lakini sasa…. imekuwa nongwa, sio tu kuwa vyombo vya habari vimeamua kuzichunia hizo SIKU, bali pia nazo zimekuwa nyingi mno kiasi kwamba inakuwa vigumu sana hata kuweza kuzijua na zingine anahisi zinabuniwa tu na baadhi ya watu wakilala na wake zao majumbani mwao wakishauriana kuwa kesho iwe SIKU YA KULA PIZZA, basi itakuwa na kesho yake mtu ukiamka utasikia (kupitia mabalozi wao, wakiongea na waandishi wa habari pale jijini Dar), kuwa Leo ni maadhimisho ya SIKU ya ula Pizza Ulimwenguni, na hata Wabongo wataadhimisha siku hiyo ingawa wanazisoma kwenye matangazo au kuziona kwenye picha za kihindi.

Ndio, kwani hujui kuwa kuna SIKU za Kutoana Ngeu, Siku za Wanaovaa Magauni, Siku za Walalahoi (?) Siku za Watembea peku, Siku za Kadhaa na Kadhaa. na kwa Ushauri wa kakangu Chesi mwenye nywele za Kipilipili, anaona ni aheri basi Wadanganyika nao wakapendelewa na hao Watunga siku wakapewa vijisiku kadhaa hizi kama SIKU ya Hafla za Jikoni (Kitchen Party?), Siku ya Kufumuana Magumi (Boxing Day?), Siku ya Unyago, Siku ya Kusasambua, Siku za Miduara, Siku ya Ndoa za Mkeka, Siku ya Kufukuzana (Sendoff?), Siku ya Waezekaji (Wawekezaji?), Siku ya nanihii…..na Siku ya nahinii pia.

Na hizo bado ni chache sana kwa maana hujagusa Siku ya Wanaodaiwa na ile ya Wadai, hujazungumzia kabisa Siku ya Mvua na ile ya Kiangazi, na wala hujazungumzia Siku ya Wambeya kule Uswahilini na ile ya Wastaarabu kule Uzunguni na zingine nyingi ambazo hata wewe unazijua.

Hakika bilashaka naamini kwa Utitiri huu wa SIKU, utafika wakati tutakuwa na SIKU ya Ndesanjo, SIKU ya Reginald na hata SIKU YA SIKU ZOTE au SIKU YA KILA SIKU…..

Alamsiki ngoja nami niwahi nyumbani maana leo ni SIKU YANGU !!

October 26, 2005 at 4:07 pm 6 comments

Mbona Uchaguzi wetu mnaufanyia Uchafuzi?

Acha kelele zoote zinazopigwa mitaani, kutoka kwa wagombea wa vyama mbalimbali ambao kila mmoja amekuwa akijitahidi kumchafua mwenzake ili yeye aonekane bora (japo sijui ni yupi sasa kati yao maana kila mmoja ni mchafu). Na wala hapo hujazungumzia juu ya mitusi (ikiwemo ile ya nguoni), ambayo wagombea hao wamekuwa wakiiporomosha kwa wenzao, bado kuna hali kama hiyo baina ya chama na chama, kambi na kambi na makundi kwa makundi.

Nadhani kimsingi siwezi kuwapinga wale ambao walikuwa na nia yao nzuri kabisa (maana kila mtu hufanya jambo kwa nia nzuri hata kama litawadhuru wengine), kwasababu hakika walikuwa wakijitahidi kujipalilia njia ya kuelekea madarakani. Lakini kinachonipa wasiwasi ni kubaini kuwa hawakuwa wameweka utaratibu bayana wa mipaka ya hayo makambi, sijui na vingine vinaitwa Vikundi vya Uhamasishaji.

Matokeo ya hili, ingawa kwa hakika huko waliko waliounda kambi hizi hawawezi kuona kwa urahisi au kujua na kukubali kwa urahisi, ni kuwa hali ni mbaya sana huku chini. Ni mbaya kwasababu hivyo vinavyoitwa Vikundi vya Uhamasishaji, hivi sasa vimegeuka kuwa Vikundi vya Uhasamishaji (kujenga uhasama).

Najua wenyewe watakataa, kwasababu kukataa ndio jadi yao lakini ukweli ndio huo kuwa hali imekuwa mbaya huku chini kiasi kwamba katika baadhi ya maeneo ndio hivyo hivyo vilivyokuwa vikundi vyao vya uhamasishaji, viulijizatiti kujenga mazingira kama sio ya kuzomea mgombea, basi ni kuhakikisha kuwa hatapata kura, na ilivyo ni kuwa wagombea wengi wako katika hali mbaya kwasababu wanakumbana na upinzani toka ndani yao kabisa.

Hii sio dalili nzuri kabisa kwasababu itakuja fikia hatua ya baadhi yao kuamua kulipa kisasi, ambacho hatujui kitakuwa kwa njia gani, na hapo ndipo tutakapoanza kuona madhara ya haya mambo ya kipuuzi yanayofanywa nyakati hizi za kuelekea uchaguzi wowote ule.

Jamani, uchaguzi ni sehemu ya kuonyesha uimara wa Utaifa wetu, demokrasia ya kweli na kila lililo zuri katika maendeleo ya nchi hii. Hivi ni kwanini Uchaguzi tunaufanyia Uchafuzi??

October 17, 2005 at 6:00 pm 3 comments

Mashujaa daima Hawafi – 2Pac Shakur

Rafiki yangu mmoja kwa jina la Akiey & kaka yangu Ndesanjo, bilashaka ni wanazi wakubwa sana wa msanii huyu, na kwa upande wa Akiey, hakika ilinishangaza kiasi kuona kuwa hakuwa na lolote alilozungumzia juu ya shujaa huyu kama kumbukumbu ya siku alipofariki na hata siku alipozikwa. hata hivyo naamini kabisa kuwa ni msongamano wa majukumu bilashaka ndio maana ikawa hivi.
Namzungumzia mwanamuziki aliyekuwa kioo cha muziki wa Hip Hop bilashaka, na ambaye kwangu mimi naamini kabisa kuwa maendeleo ya muziki huo kwa wakati huu yalitokana na kiasi kikubwa sana na mchango wake katika muziki huo. Na hapa namzungumzia hayati Tupac Amaru Shakur .
2pack 1
Ikiwa ni takriban miaka tisa sasa toka alipotutoka katika tukio lililokuwa na utata wa hali ya juu lililobatizwa jina la Mkasa wa Las Vegas, bado kumekuwa na mjadala ambao licha ya kuwa umekuwa ukizidi kufifia siku hadi siku, bado kuna baadhi ya nyakati huibuka na kuibua mgongano mkubwa wa mawazo hasa kwa mashabiki wake, na huu ni mjadala wa kuwa; Je, 2Pac alikufa kweli au bado yu hai?
Licha ya mapungufu ya kawaida kabisa ya kibinaadamu ambayo hata mimi na wewe tunayo, msanii huyu ambaye alikuwa amejijengea kundi kubwa la maadui, pengine na bila shaka hasa kutokana na mafanikio yake, bado alikuwa ni mtu mwenye upendo, na msanii ambaye alikuwa kweli kioo kwa wasanii waliokuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha masuala ya ubaguzi wa rangi yanatokomezwa.
Hayati 2Pac, ambaye alizaliwa June 16, 1971 ikiwa ni mwezi mmoja tu na siku kadhaa toka mama yake Afeni Shakur, atoke gerezani, alifariki dunia mwaka 1996, kutokana na tukio la kusikitisha kabisa la kupigwa risasi kadhaa na watu waliokuwa wanasadikiwa kuwa maadui zake. Tukio hilo lilikuwa la pili kumkumba baada ya kukumbwa na mkasa wa awali wa kupigwa risasi katika jiji la New York.
Katika enzi za uhai wake, hayati 2Pac, ambaye alikuwa rafiki kipenzi wa msanii mwingine wa muziki na mwigizaji mashuhuri duniani hivi sasa, Jada Pinkett, aliwahi kutamba na tungo mbalimbali zilizokuwa zikigusa kwa undani hisia na fikra za waafrika walio wengi hususan wale walioko katika harakati za kujikomboa na Ubaguzi wa Rangi.
Na hata alipofariki dunia kutokana na mkasa huo, gwiji huyo wa musiki wa kufoka foka, aliacha nyimbo nyingi sana ambazo hatimaye zilianza kurushwa moja baada ya nyingine kiasi kwamba zikawa ndio zinachochea mjadala wa kuwa amekufa kweli au laa. Pia alikuwa ni mtu wa kutoa maneno yenye maana kali kali sana kihisia na karibu kila neno alilokuwa akilitamka lilikuwa likimgusa kila mpenda haki humu duniani. Soma hapa baadhi ya mistari ambayo hadi leo imeendelea kuwagusa wapigania haki za binadamu duniani
Alifariki Septemba 6, baada ya kukaa kwa muda hospitali akiuguzwa majeraha ya risasi alizokuwa amepigwa, na alizikwa baadae Septemba 13 mwaka huo huo wa 1996, baada ya mabishano makali baina ya waliokuwa wakimpenda, wengi wakiamini hajafa wengi pia wakiamini amekufa. na Leo hii wakati ikiwa ni miaka tisa na mwezi mmoja toka aliporejea kwa Udongo, bado tunamkumbuka na kumhitaji sana.
Lakini kwakuwa hatuwezi kuwa naye kimwili, bado tutaendelea na hakika Daima, tutaendelea kuwa naye katika maisha yetu ya kuusaka uhuru wa kweli kwa Waafrika popote pale walipo Ulimwenguni. Hakika tulikupenda, Lakini Mungu alikupenda zaidi.

October 13, 2005 at 5:19 pm 3 comments

Mkapa; Hivi huku sio kujitega wenyewe?


Niko hapa kwenye kompyuta yangu, nikiwa nasikiliza muziki mmojawapo kati ya hii mingi tuliyonayo hapa nchini inayoitwa ya kizazi kipya. Hapa nasikiliza wimbo wa ‘SIWAELEWI’ ulioimbwa na marehemu Vivian Tillya (Mungu amlaze mahali pema peponi) enzi za uhai wake.

Nawakumbuka pia hawa jamaa zetu ‘Wanasi-hasa’, ambao baadhi yao mishipa yao ya shingoni inakaribia kupasuka, kila mmoja akijitahidi kuhanikiza uongo na uwezo wake alionao (hivi sasa lakini) wa kuweza kuondoa matatizo ya “Wadanganyika” katika muda mfupi sana tu, kila mmoja kwa staili ya aina yake.

Wengine wana ile staili ya majiko ya kizamani ya mafiga matatu; “Ari mpya, Nguvu mpya na Kasi mpya,” japo sijui ni ya kuelekea wapi maana kukimbia sio lazima iwe kwenda mbele tu.
Wapi pia wanaotumia staili ambazo hazitofautiani sana na zile za ‘Vidume’ vyetu vya pale TMK; “Hakuna kulala Mpaka kieleweke” nadhani kweli hawawezi kulala maana walilala miaka yote mitano iliyopita unadhani watashindwa kukesha siku 70 za kuhanikiza usanii wao majukwaani?

Lakini wakati jamaa hao wakiendelea huko, kwa upande mwingine kaka yetu Ben, ambaye amejijengea umaarufu wa aina yake duniani kwa sera zake za kutaka “Kuupiga teke Ukapa uliokithiri miongoni mwa Wadanganyika” yeye anaendelea na yake huku. Anaendelea kusaka wadau wa kuhakikisha sera yake hiyo inatekelezeka kwa “Uwazi na Ukweli” na hivi karibuni eti aliteketeza milioni 100 hivi za Kibongo kumnunulia Papa Benedicto wa 16, vinyago kadhaa vya kutokea ukanda wa Lupaso na kumpelekea kule kwenye maskani yake Vatican.
Wapo wapinzani wake ambao wameshaanza kuchonga kuhusu hili lakini hawa bilashaka hawajui kuwa huu ni aina ya ukarimu ambao unatumika kwa ajili ya kumvutia Papa ili naye siku moja afikirie kuja “Kuezeka”… naambiwa ni “Kuwekeza” kumbe…hapa hapa Bongo (potelea mbali hata kama uwekezaji wenyewe utakuwa wa kiroho tu), ili “Wadanganyik”a wapate nafasi ya kujiajiri.
Wakati hayo yakiendelea, nakumbuka pia kuwa kuna hawa jamaa zetu wapatao 600, ambao kimsingi wanawakilisha wenzao karibu au zaidi kidogo ya milioni 2 kote nchini, ambao kwa bahati mbaya sana walipitiwa na hili Pepo linaloitwa Ukimwi, ambao wamesema kuwa Nnjuluku, mshiko au Ngawira” zao zilizotolewa na “Sirikali” zisipowafikia hadi mwishoni mwa Novemba ya mwaka huu, watatuonyesha kwa kiasi gani walivyo wakarimu kwa kuanza kutugawia bure bure virusi vyao licha ya uchoyo wetu kwa fedha zetu.
Unashangaa? Ndio hali ilivyo hivyo. Kaka Ben anateketeza milioni 100 kutafuta wawekezaji ambao watakuja kufanya kazi kwa nchi ambayo wananchi wake wamegawiana virusi bila hiayana tena kwa kasi mpya, nguvu mpya na ari mpya. Tena basi hawa jamaa wamepania kuonyesha ukarimu wao kwa utaratibu wa Hakuna Kulala hadi Kieleweke. Je huku sio ndio KUJITEGEA mabomu sisi wenyewe lakini?
oohhh Dada yangu Vivian, kaka yako huku baaado SIWAELEWI Wadanganyika

October 13, 2005 at 2:34 pm 7 comments

Older Posts


Blog Stats

  • 35,058 hits
October 2005
M T W T F S S
 12
3456789
10111213141516
17181920212223
24252627282930
31