Archive for August, 2005

Yaliyojiri kikao cha 1 cha Bunge la awamu ijayo!!

Ni bahati mbaya sana na mtanisamehe sana kwasababu nimeshindwa hadi sasa kujua kuwa nilikuwa katika nchi gani vile, ila nina uhakika ni nchi moja wapo iliyopo hapa hapa Guniani, .. ah, kuna jamaa yangu hapa jirani ananibonyeza kuwa ni Duniani kumbe.
Enewei, kilichojiri ni kwamba, kupitia kazi hii hii ya Upapara-wa-zii, basi nilialikwa kwenda huko katika hiyo nchi, kwa ajili ya kuripoti yaliyokuwa yakijiri katika kikao cha kwanza kabisa cha Bunge la nchi hiyo, ambacho kilikuwa kinafanyika baada.. …….sijui ni Uchambuzi au Uchaguzi vile, lakini tuendelee, ambao ulishuhudia kuingia kwa sirikali ya awamu mpya.
Basi bwana, kwakuwa kikao hicho kilikuwa cha kwanza chini ya Sirikali hiyo, na kikiwa na sura nyiiiingi ngeni za wajumbe, ambazo nyingi zao zilikuwa za makinda ambayo bado ndio kwanza yanadai na damu inachemka, na ambao pia walikuwa ni mseto toka karibu kila kada, ilibidi mwongoza kikao hicho, ambaye walimwita pia Spika, atoe nafasi kwa ajili ya wajumbe hao kujitambulisha ili watambuane, kujuana na kufahamiana pia.
Kilichonifurahisha sana kwanza labda ulikuwa ni mpangilio wa wajumbe katika ukumbi wao ambao ndio kwanza walikuwa wakiuzindua kama sio kuuzingua, ambapo kulikuwa na usawa baina ya kujipanga kwa maana mwanaume hapa, anayefuata ni mwanamke hivyo hivyo hadi ukumbi wote ulipojaa. Basi bwana, utambulisho ambao ulianza kulie kwetu (tulipokuwa tumekaa sisi Mapapara-wa-zii), ulikuwa kama ifuatavyo:

Mimi wahishimiwa sana, naitwa Bibi Nanihii a.k.a The first Lady 2b
Mimi ndugu zangu naitwa Baba Nanihino a.k.a Mzee wa Mitulinga
Mimi kwa upande wangu najulikana zaidi kwa jina la Madame Nanihii a.k.a Watajiju
Na mimi naitwa mhishimiwa Fulani a.k.a Chizi Kapewa Rungu
Mimi naitwa Mama Watakoma Kuringa a.k.a Kujisifu jadi yangu
Mimi wananiita Mzee wa Mbumba a.k.a Msanii
Mimi naitwa……………………………………………

Dah, huyu hata hakuweza kumalizia maana mwenye rungu la kuongoza na kuendesha kikao hicho, alisimama ghafla na kutoa agizo lifuatalo:
“Wahishimiwa saana nawaomba utambulisho kwa wakati huu Usimamie hapo kwanza maana kama mjuavyo mambo haya inabidi yaende kwa Kasi sana kulingana na Hila zetu za Uchaguzi, hivyo nawaomba wajumbe mkapumzike kwanza hapo nje na kupunga jua pamoja na kuvuta sigara, ili tutakaporejea ndani tuwe na Nguvu mpya, na Hali mpya za Kujitambulisha kwa Wananchi wetu kabla hatujaanza rasmi mambo mengine”

Kisha anaendelea “Sisi kwa sisi oyeeeee……. oyeeeee. Kigumu Chama chetu”………. mara wajumbe nao wanaitikia “Chidumu Chitendekunu” Muulizeni Martha Mtangoo yuajua maana yake
Mara ghafla nikajikuta nakurupuka na kuangaza huku na kule, He Kutahamaki kumbe nilikuwa Kitandani mwangu nimelala na hiyo ilikuwa ndoto tu???
Tuonane siku ijayo

August 11, 2005 at 12:51 pm Leave a comment

Walahi Tunajenga dunia ndani ya Tanzania

Ungeliwaona ungewaonea huruma sana kwa jinsi walivyokuwa wakihangaika kila kukicha. Kulikuwa na vikao vya kila mara na kila mahali, kulikuwa na hujuma za kila aina, kulikuwa na ubabe wa hapa na pale, lakini kubwa zaidi ni kuwepo kwa matendo yaliyokithiri ya Rushwa.

Nazungumzia zoezi la kuwasaka “WAGOMBEA” <em>(na hakika waligombea) wa nafasi za ubunge kupitia CCM. Zoezi ambalo limedhihirisha wazi ni kwa kiasi gani ndani ya CCM yenyewe kulivyojaa Wanafiki, Waongo, Wasaliti na Mafisadi wa aina yake. Ndio najua kuwa wapo ambao wakisoma hapa wataanza kunitolea macho lakini sijali kusema ukweli.

Ni nani ambaye hakushuhudia umwagwaji wa fedha kwa wananchi ulivyokuwa ukifanywa na mabingwa hawa wa kupambana na Rushwa, ambaye kwamba anaweza kuniambia nisiwaite wanafiki na waongo waliopitiliza?

Ni nani ambaye hajui kuwa baadhi ya vigogo walitumika katika kuwapepelea njia baadhi ya waliokuwa wameshayakoroga ilimradi warejee tena katika nafasi zao kwa ajili ya kuendelea kutoa harufu zinazowachefua wananchi wao za uvundo wa mawazo, fikra na hata mitizamo?

Potelea mbali bwana, atakayethubutu kuninyooshea kidole aninyooshee tu na wala sitojali kwasababu baadhi ya matukio haya nimeyashuhudia kwa macho yangu, yakiwemo pia ya baadhi yao kuiba wapiga kura na kuwahamisha maeneo yao ili wenzao wasiwakute na kuwarubuni.

Lakini sasa wakati tukiendelea na hali hii kuna mambo ambayo kwahakika yanastahili kabisa kukaa vichwani mwetu kuwa, kinachojiri sasa ni kuunda Ulimwengu uliooza kwa kila aina ya uozo unaoweza kuujua wewe, humu humu ndani ya Tanzania hii.

Tunajenga tabaka la Wamarekani wetu, ambao watatumia mabavu na vijisenti vyao katika kutunyanyasa sisi akina yakhe wa ulimwengu wa tatu, ambao pia kimsingi tunaishi nao humuhumu ndani ya Bongo hii hii ya Wadanganyika. Astakafirulahi walahi.

Sijui ndio dalili za kukata tamaa, kutojua kile kitakachokuja mbeleni mwetu au nini lakini hakika tumejitia msambweni, kwa kuwa Tanzania inaelekea sasa kuwa na tabaka la Viongozi matajiri, watakaokuwa wakiongoza masikini wa kutupwa ambao kimsingi watageuka kuwa wakutumikishwa, kuburuzwa na …………, dah ngoja niishie hapa maana wajameni, hali ni mbaya

Tutaendelea kuichambua hali hii kwa kipindi kiasi kwahiyo tuzidi kuwa karibu katika darasa hili.

August 9, 2005 at 1:42 pm 1 comment

Hivi kukimbia ni kwenda mbele tu????

Ingawa bado Chama tawala nchini Tanzania hakijatangaza rasmi kile watakachokiita ilani yao ya Uchaguzi mkuu kwa mwaka huu wa 2005, kuna jambo mojambalo limejitokeza wazi, nalo ni kuwa tayari wameshakuwa na kitu wanachokiita KAULI MBIU YAO ambayo ni Ari mpya, Nguvu mpya na Kasi mpya. Jambo moja tu ambalo bado linanitatizo hapa ni kuwa hivi hiyo kasi ni ya kuelekea wapi maana hawajatueleza kuhusu hilo?

Hivi tunajua kuwa kukimbia sio lazima kuwe ni kwa kwenda mbele, bali hata nyuma na kama ni hivyo kwanini hawa jamaa zetu wasituwekee hili wazi kuwa ni kasi ya kuelekea wapi???

August 6, 2005 at 10:53 am 2 comments

Newer Posts


Blog Stats

  • 34,491 hits
August 2005
M T W T F S S
« Jul   Sep »
1234567
891011121314
15161718192021
22232425262728
293031